Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akimjulia hali mmoja wa majeruhi wa moto aliyelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro. |
Waziri Ummy akizungumza na baadhi ya wananchi waliojitokeza katika chumba cha kuhifadhia maiti ili kutambua miili ya ndugu zao. |
Na.WAMJW - Morogoro
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu (Mb), leo ameshiriki katika zoezi la utambuzi na uhifadhi wa miili ya marehemu wa ajali ya lori la mafuta lilioanguka na kuwaka moto katika eneo la Msamvu Itigi mjini Morogoro.
Pamoja na shughuli hizo, Mhe.Waziri Ummy Mwalimu amewatembelea majeruhi na kuwajulia hali, kuwapa pole na kuona mwendelezo wa huduma za matibabu wanazopata na kuwatakia kheri ya kupona haraka na kurejea katika shughuli za ujenzi wa Taifa majeruhi wote ambao bado wanapata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Aidha, mara baada ya kuwajulia hali alizungumza na ndugu, jamaa na rafiki wa walioathirika na ajali hii iliyopoteza maisha wa wananchi 69 na kusababisha majeruhi 65 ambao maziko ya awamu ya kwanza yanafanyika leo katika makaburi ya Mlima Kolla mjini Morogoro huku majeruhi wakiendelea na tiba Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Morogoro.
Aidha, amezidi kuwasihi na kuwahimiza wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu katika hali ya kawaida kibinaadamu na kuwahakikishia kuwa Serikali inazidi kuweka nguvu zaidi katika kuokoa maisha ya majeruhi wote katika Hospitali walizopo ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar Es Salaam.
"Naomba kuwathibitishia wataalamu wetu kwa pamoja wameunganisha nguvu kutoka Kitengo cha Dharura Muhimbili, Amana, Mwananyamala, Benjamin Mkapa Dodoma, wote wako hapa ili kuokoa maisha ya ndugu zetu. Na wenzetu wa MSD pamoja na wadau wengine hapa mkoani wamehakikisha kila kinachohitajika kwa waathirika wetu kimepatika na kiko hapa ili huduma muafaka itolewe kwa wakati kulingana na mahitaji ya aina ya janga lenyewe," amesema Waziri Ummy.
Ajali hii ilitokea siku ya Jumamosi Agosti 10, 2019 mida ya saa 2 asubuhi baada ya lori la mafuta lililokua limebeba shehema ya mafuta aina ya petrol na dizeli likielekea Mafinga mkoani Iringa kumkwepa mwendesha pikipiki aliyekatisha ghafla barabarani hivyo gari kupoteza uelekeo na kuanguka kisha kuwaka moto.
Mwisho.
0 on: "WAZIRI UMMY ASHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA ZOEZI LA KUTAMBUA MAITI NA KUJULIA HALI MAJERUHI"