Na WAMJW- Brazzaville
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Mhe. Ummy Mwalimu amelipongeza Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kushirikiana
na Serikali ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo kwa juhudi inazofanya kwa pamoja
katika kudhibiti ugonjwa wa Ebola.
Waziri Ummy amesema hayo leo wakati akiwasilisha taarifa ya
mkakati wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola katika mkutano wa 69 wa Shirika la
Afya Duniani (WHO) unaojumuisha Mawaziri wa Afya kutoka nchi mbalimbali za
Afrika unaoendelea jijini Brazzaville nchini Jamhuri ya Kongo.
Aidha, Waziri Ummy amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt.
Tedros Adhanom kwa kutangaza Ebola kuwa janga la Kimataifa, na kuongeza kuwa
Tanzania imefaidika na msaada wa WHO ambao umeiwezesha nchi kujenga uwezo wa
utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo iwapo utaingia nchini.
Waziri Ummy amesema kumekua na uboreshaji wa mpango mkakati wa
Ebola uliofanyika Mwezi Machi Mwaka 2019 ambao umelenga kuimarisha ufuatiliaji
wa mgonjwa maeneo ya mipakani, kujenga uwezo wa watumishi wa afya kumtambua
mgonjwa na kutoa matibabu, kununua vifaa vya kujikinga (PPE) na uratibu huu wa
kukabiliana na Ebola umeshirikisha sekta mbalimbali zaidi ya Afya.
Pamoja na hayo, Waziri Ummy ametaja maeneo ambayo WHO
isaidie ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza
mpango mkakati wa kukabiliana na Ebola, kuimarisha ufuatiliaji katika ngazi ya
jamii na kufanya mazoezi zaidi ya kupima utayari wa nchi.
Pia Waziri Ummy alitaka kujua chanjo ya ugonjwa Ebola inachukua
muda gani kuanza kufanya kazi baada ya mtu kuchanjwa ambapo majibu yalitolewa
kuwa chanjo hiyo inaanza kufanya kazi baada ya siku kumi huku muda wake wa
kumkinga mtu ukiwa bado katika utafiti.
Vile vile Waziri Ummy alitaka kupata ufafanuzi kuwa chanjo hiyo
ni kwa ajili ya aina gani ya virusi vya Ebola na ufafanuzi ulitolewa kuwa chanjo
hiyo ni kwa ajili ya kirusi cha Zaire ambacho kwa sasa ndicho kinachosababisha
mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.
MWISHO
0 on: "WAZIRI UMMY AIPONGEZA WHO KWA KUSAIDIA KUDHIBITI EBOLA NCHINI KONGO"