Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa lengo namba tatu (AFYA BORA NA USTAWI) la Malengo Endelevu ya Maendeleo SDG"s kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Huduma na Maendeleo ya Jamii.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Huduma na Maendeleo ya Jamii wakipitia taarifa ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu leo katika ukumbi wa mikutano Bungeni Jijini Dodoma.
Wataalam kutoka taasisi mbalimbali katika Sekta ya Afya wakisikiliza uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa lengo namba tatu (AFYA BORA NA USTAWI) la Malengo Endelevu ya Maendeleo SDG"s kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Huduma na Maendeleo ya Jamii leo katika ukumbi wa mikutano Bungeni Jijini Dodoma.
Na Englibert Kayombo, WAMJW - Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara nchini TANROADS iko mbioni kuanzisha mfumo wa huduma za dharura na uokoaji katika barabara kuu nchini.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Ummy Mwalimu alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa lengo namba tatu (AFYA BORA NA USTAWI) kati ya malengo 17 ya Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDG’s) kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kwenye ukumbi wa mikutano bungeni Jijini Dodoma.
Waziri Ummy Mwalimu amesema “mfumo huu una lengo la kusaidia kupambana na dharura au maafa pindi yanapotokea na kuweza kusaidia upatikanaji wa huduma kwa haraka na tutaanza na vituo 7 vya huduma za dharura katika barabara kuu toka Mkoa wa Dar Es Salaam mpaka Ruaha Mbuyuni Mkoa wa Iringa.
Amevitaja vituo vya huduma za dharura ambayo vitaanzishwa kuwa ni Kituo cha Afya Kimara (DSM), Hospitali ya Tumbi, Kituo cha Afya Chalinze (PWANI), Zahanati ya Fulwe (Mikese Morogoro), Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Hospitali ya St. Kizito (Mikumi, Morogoro) pamoja na Zahanati ya Ruaha Mbuyuni Darajani (Iringa)
“Tumeweza kununua gari za kubebea wagonjwa (Ambulance) 12 ambazo tutazisamba katika vituo vya huduma za dharura” amesema Waziri Ummy na kuendelea “bado tuna lengo la kuongeza magari matatu ya uzimaji moto yenye uwezo wa kuinua na kukata vyuma ili kuwaokoa majeruhi na kuwapatia huduma eneo la tukio”
Aidha Waziri Ummy amesema kuwa tayari watoa huduma 272 wamehitimu mafunzo ya huduma za dharura na uokoaji yaliyotolewa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi ambao kati yao, 1212 ni “basic provider” huku 160 ni watoa huduma ngazi ya Vijiji.
Akitoa maoni yake juu ya mfumo huo, Mbunge wa Jimbo la Ludewa Mhe. Deo Ngalawa ameipongeza Wizara ya Afya kwa kuja na mfumo huo ambao utaokoa maisha ya watanzania wengi huku akitumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuhakikisha kuwa mfumo huo unasambaa maeneo yote ya barabara kuu ili kusaidia upatikanaji wa huduma za uokozi kwa haraka zaidi.
Waziri Ummy amesema kuwa wameanza na eneo hilo kwanza kwakuwa limekuwa na athari za kutokea kwa ajali nyingi kulinganisha na maeneo mengine huku akisema kuwa huo ni mpango endelevu na wataendelea maeneo yote ya barabara kuu nchini huku akisema kuwa mfumo huo utazinduliwa mwishoni wa Mwaka 2019.
MWISHO
0 on: "WIZARA YA AFYA YAJA NA MFUMO WA DHARURA NA UOKOZI"