Na WAJMW-Brazzaville
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Mhe. Ummy Mwalimu amekutana na Waziri wa Afya wa Marekani Admiral Brett Giroir
na kufanya mazungumzo na kuona namna gani nchi hizo mbili zinavyoweza
kushirikiana katika kupambana na ugonjwa wa Sickle Cell (Seli Mundu) hasa kwa
watoto wachanga na wale walio chini ya miaka mitano.
Waziri Ummy amemueleza Waziri huyo kuwa watoto wapatao 11,000
wanazaliwa na ugonjwa huo Tanzania na wengi hupoteza maisha kwa sababu ya
kuchelewa kufanyiwa vipimo na kugundulika mapema.
Waziri Ummy amemueleza kuwa muelekeo wa nchi sasa ni
kuhakikisha kuwa kila mtoto anayezaliwa anapimwa Sickle Cell na
watakaogundulika matibabu yaanze mapema ili kupunguza vifo vinavyotokana na
ugonjwa huo.
Mawaziri hao wamekubaliana kwa pamoja kushirikiana katika
kudhibiti vifo vinavyoweza kutokea kwa sababu ya ugonjwa huo huku Waziri Brett akiahidi kuimarisha upatikanaji wa vipimo, pamoja na matibabu kwa watoto
wanaozaliwa na ugonjwa huo kuanzia ngazi ya zahanati na vituo vyote vya kutoa
huduma za afya ya msingi nchini.
“Ni muhimu huduma hizi zikatolewa katika ngazi ya afya ya msingi
mpaka taifa ili kuwapa huduma stahiki wananchi, hii ikiwa ni utekelezaji wa
afya kwa wote. Suala la upimaji wa Seli Mundu, elimu kwa jamii na pia suala la
matibabu katika ngazi zote za utoaji huduma ni muhimu vikapewa kipaumbele”.
Aliongeza Waziri Ummy.
Hivi sasa huduma hii hapa nchini inapatikana katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali za Rufa za Mikoa za Amana na Temeke pekee kwa
nchi nzima.
Kwa upande wake Waziri Brett amepongeza juhudi zinazofanywa
na Serikali ya Tanzania kwa kujenga viwanda vya dawa nchini ikiwa ni pamoja na
za Sickle Cell. Pia ameahidi kutembelea Tanzania kuona na kujadiliana zaidi
namna nchi hizi mbili zitavyoshirikiana katika kushughulikia ugonjwa huu
nchini.
Mawaziri hao wanahudhuria mkutano wa 69 wa Shirika la Afya
Duniani (WHO) unaojumuisha Mawaziri wa Afya toka nchi mbalimbali za Afrika unaoendelea
jijini Brazzaville nchini Jamhuri ya Kongo.
0 on: " SERIKALI YA MAREKANI YAAHIDI KUSAIDIA MAPAMBANO DHIDI YA UGONJWA WA SELI MUNDU (SICKLE CELL) NCHINI"