NA WAMJW-DAR ES SALAAM
TAASISI ya Mifupa nchini MOI sasa
itafanya upasuaji wa mifupa kwa wagonjwa wapatao 1000 kwa mwezi kutoka wagonjwa
500 mpaka 700 baada ya kupokea msaada wa chumba cha upasuaji na vifaa vyake
kutoka kwa Serikali ya Kuwait .
Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa kuzindua na
kupokea msaada wa chumba cha upasuaji na vifaa vyake vyenye thamani ya
shilinigi milioni 186 leo katika Taasisi ya mifupa MOI leo jijini Dar es
salaam.
“Hii ni faraja kubwa sana kwa Serikali
kwani uboreshwaji wa huduma katika hospitali zetu za kibingwa kubwa kama MOI
itaweza kuhudumia wagonjwa wengi Zaidi kutoka wagonjwa 700 kwa mwezi mpaka
kufikia 1000 kwa mwezi” alisema Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Aidha Makamu wa Rais Samia Suluhu
amesema kuwa anaishukuru Serikali ya Kuwait kupitia Balozi wake Jasem Al Najem
kwa msaada huo kwani utaisaidia kwa kiasi kikubwa MOI katika kuboresha utoaji
huduma hasa katika fani ya upasuaji kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo
wazi hapa nchini.
Kwa uapnde wake Naibu Waziri wa
Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema
kuwa kukamilika
kwa vyumba hivi viwili vya upasuaji, kutaiwezesha Taasisi ya MOI kuwa na jumla
ya vyumba vya upasuaji 8 kutoka 6 vilivyopo sasa na miongoni mwa vyumba
hivi vya upasuaji kimoja kitakuwa maalumu kwa ajili ya watoto tu.
“MOI imeshatoa matibabu ya upasuaji kwa wagonjwa
1,670 ikiwemo upasuaji mifupa (wagonjwa 1,228), kubadilisha nyonga (wagonjwa
84), kubadilisha goti (wagonjwa 72), upasuaji wa uti wa mgongo (wagonjwa 109),
ubongo (wagonjwa 64), na watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi (wagonjwa
113” alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha Dkt. Ndugulile
amesema kuwa katika kuimarisha na kuboresha afya za Watanzania jengo hilo pia
litakuwa na vitanda 16 vya ICU (Intensive Care Unit) na 16 vya HDU (High
Dependency Unit), hivyo kuimarisha huduma za tiba kwa wagonjwa wanaohitaji
uangalizi maalumu.
Naye Balozi wa Kuwait Nchini Balozi
Jasem Al Najem amesema kuwa Nchi ya Kuwait ipo mstari wa mbele katika
kuhakikisha Hospitali na Vituo vya afya
nchini Tanzania vinatoa huduma bora za Afya kwa kutumia Taaluma na ujuzi
wa kisasa ikiwemo vifaa na vifaa tiba .
“Serikali ya Kuwait itakuwa mstari wa
mbele katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuimarisha afya
za wananchi kwa kuendelea kutoa misaada mbalimbali ikiwemo vifaa,vifaa tiba na
wataalamu wa afya na kutochoka katika hilo” alisema Balozi Najem.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya
MOI Bi. Zakia Mejhi amesema kuwa Taasisi yake imeokoa Bilioni 3 za kufanyia
upasuaji kwani kwa sasa huduma hizo za kibingwa zinafanyika nchini kwa Shilingi
Bilioni 12 kutoka Bilioni 15 za rufaa ya kwenda kutibiwa nje.
0 on: "MOI SASA KUFANYA UPASUAJI KWA WAGONJWA 1000 KWA MWEZI ASEMA MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN."