|
Meneja wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kanda ya nyanda za juu kusini, Gaspar Gerald akizungumza na waandishi wa habari walioambatana na Maofisa habari wa Wizara na taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Afya katika kampeni ya 'Tunaboresha sekta ya afya". |
|
Baadhi ya Wakemia wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kanda ya Nyanda za juu kusini wakionesha namna vifaa vya maabara vinavyofanya kazi na baadhi ya sampuli wanazopata kwa ajili ya kufanyia uchunguzi. |
MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali(GCLA) kanda ya nyanda za juu kusini, imekusanya sampuli mbalimbali 2589 na kuzifanyia uchunguzi na kutoka ushahidi mahakamani katika kesi 68.
Aidha, kati ya sampuli hizo 221 zilikuwa za Vinasaba(DNA) ambazo zililenga masuala kibinadamu ya utambuzi.
Kauli hiyo imetolewa leo na Meneja wa kanda hiyo, Gaspar Gerald alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari walioambatana na Maofisa habari wa taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Afya katika kampeni ya 'Tunaboresha sekta ya afya' inayolenga kuangalia mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli.
Meneja huyo sampuli hizo 2580 ni za kimazingira,makosa ya jinai, vinasaba na chakula na dawa ndio zinazopokelewa.
Aidha alisema kanda hiyo kwa kipindi cha miaka minne wametoa ushahidi kwenye kesi 68 na kwamba sio kila sampuli zinazopimwa zinatolewa ushahidi bali ni zile zinazohitajika kutolewa ushahidi mahakamani.
"Huu ushahidi ni pale mahakama inapohitaji ushahidi ndo tunaenda kutoa na ushahidi tunaotoa ni kile tulichokiona kwenye sampuli iliyoletwa kama vile dawa za kulevya hivyo mkemia anatoa ripoti yake,"alisema
Akizungumzia kuhusu mafanikio mengine, Gerald alisema wamefanikiwa kujenga ofisi yao kwa gharama ya Sh.Milioni 300, kukagua na kudhibiti kemikali, kuongezeka wafanyakazi kutoka watatu hadi 18 na kufanikiwa kupima sampuli 2580.
"Mwaka 2017 wafanyakazi waliongezeka kwa asilimia 80 na inatokana na juhudi za Rais Magufuli kuhakikisha anatekeleza sera ya serikali ya kufikisha huduma kwa wananchi, kanda hii kijiografia ina mikoa sita lakini kiutawala kwa mujibu wa mkemia wa serikali ni mikoa mitano Njombe, Songwe, Mbeya, Katavi na Rukwa,"alisema
Alisema huduma zinazotolewa ni pamoja na uchunguzi wa kimaabara, utekelezaji wa sheria za mamlaka ikiwemo ya kemikali za majumbani na viwandani, Vinasaba vya binadamu na sheria ya Mkemia Mkuu.
Alieleza ofisi hiyo imefanikiwa kusimamia kemikali na kudhibiti zinazoingia mipakani kwenye mpaka wa Tunduma na Kasumulu na kutoa elimu kwa watu zaidi ya 150 wanaojihusisha na kemikali na watu 140 wanaotoka jeshi la polisi kwa ajili ya usimamizi wa sampuli za jinai.
Kadhalika, Gerald alisema udhibiti wa kemikali awali hakuwa mzuri lakini baada ya mamlaka hiyo kuanzishwa udhibiti umekuwa mkubwa na wasafirishaji wamepewa elimu ili kufuata taratibu za kulinda mazingira na afya za watu.
Kuhusu DNA, Meneja huyo alisema vinasaba vinapimwa kwa maana mbili ya utambuzi na masuala ya jamii au ya ndoa.
"Kwenye sheria ya DNA imeanisha mamlaka inayoomba kupimiwa DNA, ile mamlaka ndio zinazoleta maombi kwa mkemia kuomba kupimiwa DNA, hakuna uoga watu wanafuata taratibu, kwenye suala la utambuzi kwa mfano tukio la moto Morogoro pale mkemia aliingia kujua huyu ni nani,"alisema.
Alisema mpaka sasa sampuli 221 za DNA kwa kipindi cha miaka minne na mamlaka zingine zilizowasilisha maombi ya kupimiwa kwa Mkemia ndio zenye majibu ya vinasaba hivyo.
Mwisho.