Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatano, 20 Juni 2018

PICHA ZA MATUKIO ZA VIONGOZI WA SERIKALI WAKITEMBELEA BANDA LA HJFMRI NA NIMRI-MBEYA

- Hakuna maoni

Waziri wa Afya Maendeleo ya jamii , Jinsia , Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu (wa katikati) akishuka kutoka kwenye gari lenye Clinic inayotoa huduma za TB (Kifua Kikuu) liliopo kwenye banda la HJFMRI kwa kushirikana na NIMR –Mbeya, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Furaha yangu , iliyozinduliwa na Waziri Mkuu, mheshimiwa Kassim Majaliwa, mjini Dodoma.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akiingia kuangalia huduma za TB (Kifua Kikuu) zinazotolewa na HJFMRI kwa kushirikiana na NIMR-Mbeya , wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Furaha Yangu iliyozinduliwa mjini Dodoma.


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akipata maelekezo kutoka kwa mtaalamu katika Banada la HJFMRI kwa kushirikana na NIMR –Mbeya, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Furaha yangu.

Ijumaa, 15 Juni 2018

TAARIFA KWA UMMA


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, 
WAZEE NA WATOTO

TAHADHARI KWA UMMA KUHUSU UGONJWA WA HOMA YA BONDE LA UFA (RVF) HAPA NCHINI, ILIYOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU (MB); WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, TAREHE 14 JUNI 2018 

Ndugu Wanahabari,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, inatoa tahadhari ya ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever) kufuatia uwepo wa taarifa juu ya ugonjwa huo nchini Kenya. Mpaka sasa jumla ya wagonjwa 19 na vifo 6 (CFR 31.6%) vilivyosababishwa na ugonjwa huu vimeripotiwa na Wizara ya Afya nchini Kenya. Ugonjwa ulianzia katika Kaunti ya Wajir, Kaskazini mwa Kenya na hadi sasa ugonjwa huu umeripotiwa kuenea kwenye Kaunti za Marsabit na Tana River. 

Homa ya Bonde la Ufa ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyoitwa Phlebovirus unaoathiri wanyama na binadamu ambapo wanyama wanaoathirika zaidi ni pamoja na Ng’ombe, Kondoo, Mbuzi na Ngamia. Virusi vya ugonjwa wa homa ya bonde la ufa husambazwa kwa mnyama baada ya kuumwa na mbu aliyeambukizwa ugonjwa huu. Mbu aenezae ugonjwa huu ni wa aina ya Aedes ambao ni weusi na wana madoadoa meupe ya kung’aa.

Kwa binadamu ugonjwa huu huambukizwa kwa  kuumwa na mbu aina ya Aedes aliyeambukizwa na virusi hivi au kugusa damu,majimaji au mzoga wa  mnyamaaliyeathirika na ugonjwa huu. Binadamu anaweza kugusa damu au maji maji ya mnyama kwa njia ya Kuchinja, kula nyama, kuchuna ngozi au kunywa maziwa yasiochemshwa kutoka kwa mnyama aliyeambukizwa.

Ndugu Wanahabari,
Dalili za ugonjwa huu kwa wanyama ni pamoja na kuharibu mimba; kuwa na homa kali na kuzubaa; vifo vya ndama, watoto wa mbuzi na watoto wa kondoo; kuharisha na kutapika na wakati mwingine matapishi au kinyesi huchanganyika na damu. 

Kwa binadamu dalili za ugonjwa huu huanza kuonekana kati ya siku 2 hadi 5 baada ya maambukizi. Dalili za awali ni; homa kali, kuumwa na kichwa, maumivu ya mwili, kichefuchefu au kutapika, kizunguzungu na kupungua uzito. Aidha, kama mgonjwa hatapata matibabu ya haraka, mgonjwa anaweza kupata dalili za  kutokwa damu mdomoni, puani, masikioni na  kwenye ngozi.Vilevile mgonjwa anaweza kupata dalili za kutapika au  kuharisha damu, uvimbe wa ubongo au uvimbe kwenye macho na hatimaye kupoteza maisha. Endapo mgonjwa akiwahi kutibiwa,  wengi hupona wiki moja baada ya kuonyesha dalili za awali.  Watu wote wanaweza kuambukizwa ugonjwa huu lakini  watu ambao wako katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa ni wanaojishughulisha na kuchinja wanyama, wachungaji wa mifugo pamoja na;  madaktari wa wanyama. .

Ndugu Wanahabari, 
Wizara inaendelea kusisitiza jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anajilinda dhidi ya kupata maambukizi ya ugonjwa huu wa Homa ya Bonde la Ufa. Aidha Wizara inawasihi wananchi kushirikiana  na Halmashauri pamoja na Mikoa yote ya Tanzania katika juhudi za kupambana na kuzuia ugonjwa huu ili usiingie  kwenye maeneo yao kwa kufanya  yafuatayo; 
Kutokugusa damu, majimaji kutoka mwilini au mzoga wa mnyamaanayehisiwa  kuwa na ugonjwa huu.
Kutochinja mnyama ambaye anahisiwa kuwa na ugonjwa huu. 
Kutokunywa maziwa na kula nyama ya mnyama ambaye anahisiwa kuwa na ugonjwa huu.
Kutokulala na wanyama kwenye nyumba moja, wanyama watengwe sehemu mbali na makazi ya watu.
Ikiwa mtu yeyote yule atalazimika kushika mizoga pengine kutokana na taaluma au kazi yake, anatakiwa avae vifaa kinga kama vile glovu (gloves), mabuti na mask.
Kunawa mikono kwa sabuni na maji safi.
Wahudumu wa afya na wafanyakazi wa machinjioni wanashauriwa kuchuku hatua za tahadhari dhidi ya maambukizi kwa kuvaa vifaakinga. 
Jamii hasa za wafugaji au zinazojishughulisha na shughuli za mifugo na uchinjaji wa mifugo watoe taarifa mapema kwa mamlaka husika pale waonapo dalili za ugonjwa huu katika mifugo yao.
Kuzuia mazalia ya mbu  kwa kufunika maji yaliyotuama, kufukia  madimbwi,  kufyeka vichaka na kuondoa takataka zinazosabisha maji kutuama ikiwemo vifuu vya nazi, makopo na matari ya gari.
Kuchukua hatua za kujilinda  kuumwa na mbu kwa kutumia chandarua, kuvaa nguo ndefu na kutumia dawa za kujipaka ili kuzuia kuumwa na mbu.   

Ndugu Wanahabari,
Wizara yangu imechukua hatua zifuatazo kufuatia tishio la mlipuko wa ugonjwa huu wa Homa ya Bonde la Ufa nchini;  

Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara kupitia Makatibu Tawala na Wakurugenzi wa Halmashauri. 
Kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa nchini kwa kutumia mfumo wa Integrated Diseases Surveillance and Response IDSR ambapo tunaendelea kupata taarifa za kila siku juu ya mwenendo wa ugonjwa huu na mkazo umewekwa zaidi katika maeneo ya mipakani.
Wizara ipo katika hatua za mwisho kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji wa ugonjwa wa RVF kwa kuanzisha vituo maalum ‘Sentinel Surveillance Sites’ katika Mikoa ya Arusha, Manyara, Tanga na Kilimanjaro 
Kufanya mkutano wa pamoja wa kisekta (Afya ya binadamu na  wanyama) kuhusu ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa "Cross border Surveillance” kwa Mikoa ya Arusha, Manyara, Dodoma na Kilimanjaro
Kuimarisha Utambuzi wa ugonjwa katika maabara  ambapo sasa, tuna uwezo wa kupima na kuthibitisha ugonjwa huu hapa nchini 

 Hitimisho
Wizara inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa ugonjwa huu wa Homa ya Bonde la Ufa nchini Kenya. Aidha, wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kwani hadi sasa hakuna mgonjwa aliyegundulika kuugua ugonjwa huu hapa nchini. Juhudi zinaendelea kuchukuliwa kuimarisha mawasiliano ya sekta husika ili kubaini kwa haraka ugonjwa huu pale utakapotokea. 

Wizara yangu inashauri wananchi kuwahi kwenda katika kituo cha kutolea huduma za afya mara moja pale waonapo dalili za awali za ugonjwa huu. Aidha, Wizara inaendelea kushirikiana na wadau wa sekta na mashirika mbalimbali kufuatilia na kujiandaa kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huu endapo utatokea.

HOTUBA YA MHESHIMIWA UMMY A. MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KWENYE SHEREHE YA MAADHIMISHO YA SIKU YA WACHANGIA DAMU DUNIANI MKOANI DODOMA

- Hakuna maoni

Waziri wa Afya akiongea na Kanali Ramson Mwaisaka ambaye alishiriki uchangiaji wa damuwakati wa zoezi la uchangiaji damu linalofanyika Nyerere Square katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kuchangia damu Duniani.

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akisoma kadi ya mchangiaji damu kutoka JKT Dodoma wakati wa zoezi la uchangiaji damu linalofanyika Nyerere Square katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kuchangia damu Duniani





Waziri Ummy Mwalimu akiongea na mmoja wa wanawake waliofika kuchangia damu. Damu salama ni nguzo muhimu katika kuokoa vifo vitokanavyo na uzazi kwa akina mama wajawazito nchini wakati wa zoezi la uchangiaji damu linalofanyika Nyerere Square katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kuchangia damu Duniani.


HOTUBA YA MHESHIMIWA UMMY A. MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KWENYE SHEREHE YA MAADHIMISHO YA SIKU YA WACHANGIA DAMU DUNIANI MKOANI DODOMA TAREHE 14-6-2018


Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
Mheshimiwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma,
Mkurugenzi wa Tiba-MOHCDGEC,
Mganga Mkuu wa Mkoa-Dodoma,
Meneja wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama,
Waheshimiwa Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa,
Viongozi wa Dini,
Mwakilishi wa CDC,
Mwakilishi Shirika la Afya Duniani,
Mwakilishi KOICA,
Ndugu  Wachangia Damu, 
Wanahabari,
Wasanii mbalimbali,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.

Ndugu Wananchi,
Leo tarehe 14 Juni, 2018 tunaungana na Dunia Kuadhimisha Siku ya Wachangia Damu Duniani.  Hivyo, ninayo furaha kuungana na Watanzania na wananchi wa Dodoma  katika siku hii muhimu  kuwashukuru na  kuwaenzi Wachangia  Damu  wote ambao wamekuwa wakichangia damu, ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya kuongezewa damu. Pamoja na hayo pia ninayo furaha kuona kuwa leo tunazindua Kikundi cha Wachangia Damu Wenye Kundi Adimu la Damu (Rare Blood Group Donor Club) hapa Mkoani Dodoma.
Ndugu Wananchi,
Ni kweli kwamba uchangiaji damu wa hiari bila malipo, ndiyo msingi wa upatikanaji wa damu iliyo salama. Wachangiaji damu wa hiari wanaorudia kuchangia mara kwa mara wapo salama na wanahusishwa na viwango vya chini vya magonjwa ambayo yanaweza kuambukizwa kwa njia ya damu kama virusi vya UKIMWI, homa ya ini na kaswende.  Naomba nitumie fursa hii kwa niaba ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusema “ASANTENI SANA KWA WOTE AMBAO MMEKUWA MKICHANGIA DAMU KWA HIARI KUOKOA MAISHA YA WATANZANIA WENZETU”.
Ndugu Wananchi,
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni "Jitoe kwa ajili ya mwingine. Changia damu. Okoa Maisha ya mwenzio" (Be there for someone else. Give blood. Share life).  Kauli mbiu ya mwaka huu inalenga kuonyesha mshikamano katika uchangiaji damu, inalenga mambo muhimu ambayo yanaonyesha thamani ya mwanadamu kama heshima, huruma, wema na kuwajali wengine ambavyo ndio msingi wa kuendeleza uchangiaji damu wa hiari bila malipo yoyote.

Ndugu Wananchi,
Huduma za Damu Salama Tanzania Bara zilianza mwaka 1946 kwa utaratibu wa ndugu wa mgonjwa kujitolea damu ya kumuongezea mgonjwa (Family Replacement). Hata hivyo mfumo huu wa kutoa damu kwa utaratibu wa ndugu wa mgonjwa kujitolea damu ulifanya damu kuwa adimu hasa panapotokea dharura.

Tokea kuanzishwa kwa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, kumekuwa na ongezeko la ukusanyaji wa chupa za damu kutoka 52,000 (2006) hadi 233,593 (2017). Hata hivyo, ongezeko hili bado halijakidhi mahitaji ya nchi ambayo ni sawa na chupa 520,000 (asilimia moja ya wananchi; kwa takwimu za mwaka 2017 au chupa 10 kwa kila wananchi 1000). Kwa taarifa za Mpango za 2017, Mikoa iliyoongoza kwenye makusanyo ya damu ni Katavi (94% ya malengo), Lindi (79% ya malengo), Pwani (66% ya malengo). Mikoa ambayo haikufanya vizuri ni Songwe (16% ya malengo), Mbeya (20% ya malengo) na Tabora (22% ya malengo). 

Aidha, ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano, Mpango wa Taifa wa Damu Salama wakishirikiana na Mikoa na Halmashauri za Wilaya, pamoja na Jeshi la Wananchi Tanzania wameweka lengo la kuongeza ukusanyaji damu kufikia chupa 375,000 mwaka 2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia 72.  Vile vile, nimetoa maelekezo kwa Mpango wa Taifa wa Damu Salama kuweka mikakati na kuhakikisha wanakusanya chupa za damu 540,000 (asilimia moja ya wananchi kwa takwimu za mwaka 2018 ambapo inakadiriwa kuwa watanzania watakuwa 54,000,000) ambayo ndio mahitaji ya halisi ya chupa za damu nchini.  Uboreshaji wa huduma za damu salama nchini ni utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2015, ambayo imelenga kuboresha na kuimarisha huduma ya Afya ya uzazi na mtoto nchini; na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ifikapo mwaka 2020.

Ili kuweza kufikia malengo haya kwa muda huu mfupi na kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano, napenda kutoa maelekezo kwa Mpango wa Taifa wa Damu Salama kuimarisha na kuboresha mifumo na utendaji kazi, ikiwa ni pamoja kufanya kazi kwa ukaribu na timu za kukusanya damu za Mikoa na Halmashauri, Timu za Kanda ya Jeshi (TPDF) na Chama cha Msalaba Mwekundu (TRCS).

Aidha, Wizara kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI imeanzisha utaratibu wa kuwa na vituo vya benki za damu kwenye ngazi ya Mikoa ili visaidiane na Benki za damu za Kanda katika kuboresha upatikanaji wa damu salama hususani kwa akina mama wajawazito. Hadi sasa Vituo Vidogo vya Damu Salama za Mikoa 9 zimeanzishwa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Morogoro, Dodoma, Iringa, Kigoma, Shinyanga, Kagera na Mara. Lengo ni kuhakikisha kila Mkoa una Benki ya damu; na kuwa na uwezo wa kutoa huduma ya damu salama kwa kila anayehitaji ndani ya Mkoa. Hii ikiwa ni mojawapo ya jitihada za kuboresha huduma za afya pamoja na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi. Katika bajeti ya mwaka 2018/2019, Wizara imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Vituo Vidogo vya Damu Salama za Mikoa 5, ikiwemo Mkoa wa Tanga, Ruvuma, Rukwa, Katavi na Geita.

Ndugu Wananchi,
Tumeshuhudia hospitali zetu za rufaa kama Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali ya Mifupa MOI, Hospitali ya Mloganzila na nyinginezo zinavyoboresha na kupanua wigo wa huduma za kitaalamu zinazopatikana nchini, kama vile kufanya operesheni za moyo, na kupandikiza figo.  Kuongezeka kwa operesheni hizi kunahitaji damu pamoja na mazao ya damu iliyo salama na ya kutosha, na yenye makundi mbalimbali. Hivyo jitihada zinazofanyika za kuongeza makusanyo ya damu zinaendana na azima ya Serikali kuhakikisha na kufanikisha huduma zote za kibingwa zinatolewa hapa hapa nchini. Kipaumbele kwa Wizara ni kuendelea kuboresha na kuimarisha huduma za kibingwa zitolewazo nchini katika kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa ya matibabu nje ya nchi ili kupunguza gharama kubwa ambazo serikali inaingia katika kupeleka wagonjwa nje ya nchi. 

Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Wizara itaboresha upimaji wa kuhakiki usalama wa damu kwa kununua mashine za kisasa kupitia MSD na kusimikwa katika vituo vyetu vya Kanda . Mashine hizi ‘full automated machines’ zitakuwa na uwezo wa kupima sampuli nyingi kwa wakati mmoja. Hii itaongeza ufanisi katika upimaji wa maambukizi ya ukimwi, homa ya ini na kaswende na zitarahisisha upatikanaji wa damu salama kwa wakati katika vituo vya kutolea huduma. 

Vile vile, Wizara itanunua mashine za Apheresis nne (4), ambazo ni maalum na kisasa zinazotumika kukusanya damu na kutengeneza mazao ya damu. Faida za mfumo huu wa kutengeneza mazao ya damu kwa kutumia ‘Apheresis Machine’ utasaidia mchangiaji damu mmoja kuchangia kati ya dozi 2 hadi 3 za chembe sahani “platelets” zilizo katika viwango vya ubora wa juu. Tofauti na mfumo wa sasa ambao unahitaji wachangiaji 6 ili kupata dozi moja ya chembe sahani. Aidha, mashine hizi za apheresis zitawezesha upatikanaji wa mazao ya damu maalum yanayohitajika kutumiwa na madaktari katika kutoa huduma za kibingwa mfano matibabu ya cancer, upasuaji wa mishipa ya fahamu, moyo na upandikizaji wa figo.

Ndugu Wananchi,
Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) umekuwa ukitekeleza mikakati mbalimbali katika usimamizi wa viwango na ubora katika huduma ya damu,  mkakati mmojawapo ni  kusajili Vituo Vyote vya Damu Salama vya Kanda kwenye mchakato wa utambuzi wa Ithibati (Accreditation) kwa kutumia viwango vya Shirika la Kimataifa la “Africa Society for Blood Transfusion” (AfSBT). Mpaka sasa nina taarifa kanda mbili za Kaskazini-Kilimanjaro, Mashariki-Dar-es-salaam, pamoja na Mpango wa Damu Salama Zanzibar, zimefanikiwa kupata vyeti vya utambuzi rasmi kwa kufika daraja la pili la Ithibati inayotolewa na “African Society for Blood Transfusion” (AfSBT) yaani ‘’Step II Certification’’. Nachukua fursa hii kupongeza Menejimenti na Wafanyakazi wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama kwa hatua hii. 
Ninatambua kupata cheti kuna manufaa yafuatayo; ni uthibitisho kuwa serikali kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama sio tu unaongeza juhudi katika kukusanya damu lakini pia unaendelea kuboresha ubora wa huduma ya damu salama. Kupata vyeti vya utambuzi wa Ithibati utawezesha pia Huduma za Mpango wa Taifa wa Damu Salama kutambulika Kitaifa na Kimataifa; lakini pia utawezesha wananchi kupata huduma bora na kujenga imani kuwa Damu Salama inatoa huduma zinazokidhi viwango vya hali ya juu.
Maelekezo yangu kwa uongozi wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama; ni kuweka mikakati na kuhakikisha vituo vinne (4) vilivyobaki; Kanda ya Ziwa-Mwanza, Nyanda za Juu Kusini-Mbeya, Magharibi-Tabora na Kusini-Mtwara vinapata utambuzi wa Ithibati daraja la pili pia, na hatimaye kupata cheti cha Idhibati kwa huduma zote zinazotolewa na Mpango kwa maana ya kufikia ‘’Full Accreditation’’
Ndugu Wananchi,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama umeanzisha Kikundi cha Wachangia Damu Wenye Kundi Adimu la Damu  (Rare Blood Group Donor Club) kama 0-negative, A-negative, B-negative na AB-negative katika kila Mkoa . Lengo ni kuweka msukumo na kuwakutanisha watu wenye kundi adimu la damu na kuwahamasisha wawe wanachangia damu mara kwa mara ili Taifa liwe na akiba ya kutosha ya damu. 

Tunataka kuhakikisha kuwa wagonjwa wenye kundi adimu la damu wanapata huduma za matibabu sawa na wagonjwa wengine na kuhakikisha vifo vyinavyosababishwa na ukosefu wa kundi adimu la damu vinapungua au havitokei kabisa. Hivyo basi nitoe rai kwa wananchi ambao wana kundi adimu la damu watuunge mkono na kujiunga katika klabu hizi. Vile vile, niwaombe Mashirika, Taasisi mbalimbali na vyombo vya habari kuwaelimisha wananchi wote wenye makundi adimu ya damu juu ya umuhimu wa kujiunga katika klabu hizi.

Ndugu Wananchi,
Kabla sijahitimisha napenda kutoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Centres for Disease Control and Prevention (CDC), Mfuko wa Dunia wa Magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund), Shirika la Maendeleo ya Korea Kusini (KOICA) kwa kuendelea kugharimia uimarishaji wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama hapa nchini katika masuala ya mfumo wa TEHAMA, viwango na ubora na mchakato wa Ithibati (Accreditation), upatikanaji wa vifaa tiba (equipments and reagents) na mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi. Pia nawashukuru wahisani na wadau wengine ambao kwa njia moja au nyingine wanaendelea kusaidiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama katika kuhakikisha damu inapatikana nchini.

Pia napenda kutambua jukumu na umuhimu wa vyombo vya habari katika juhudi zetu za pamoja za kuelimisha, kuhamasisha na kuongeza idadi ya wachangia damu wa hiari bila malipo.

Napenda kuvisihi vyombo vya habari kuendelea kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama, kujenga ufahamu wa umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari, ili wananchi ambao wamekuwa na imani potofu kuhusu kuchangia damu wabadili imani zao na tabia, ili nao waanze kuchangia damu kwa hiari.

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
CHANGIA DAMU, OKOA MAISHA

Alhamisi, 14 Juni 2018

DKT. NDUGULILE HAIMIZA UTUNZAJI MZURI WA DAWA.

- Hakuna maoni
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiongea na Wafamasia hawapo pichani wakati wa maadhimisho ya wiki ya Famasia yaliyofanyika leo jijini Dar es salaam.

Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wa kwanza kushoto akipata maelezo juu ya dawa aliyoishika kutoka kwa Mkurugenzi wa kiwanda cha kutengeneza dawa Gullin Bw. Ashok Pandey kulia wakati wa maadhimisho ya wiki ya Famasia yaliyofanyika leo jijini Dar es salaam.

Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile kushoto akionesha juu Bango Kitita la famasia baada ya kulizindua wakati  wa maadhimisho ya wiki ya Famasia yaliyofanyika leo jijini Dar es salaam. Kulia ni Msajili wa Baraza la Famasia Bi. Elizabeth Shekirego 



Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiwakabidhi zawadi baadhi ya wadau wa Famasi kwa mchango wao katika sekta hiyo wakati wa maadhimisho ya wiki ya Famasia yaliyofanyika leo jijini Dar es salaam.


NA WAMJW-DAR ES SALAAM


NAIBU Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amewaagiza wafamasia wa Hospitali za serikali kutunza dawa vizuri na mahali panapostahili ili kuweza kuepuka uharibifu wa dawa hizo.
Hayo ameyazungumza wakati wa maadhimisho ya wiki ya Famasia duniani yaliyofanyika leo jijini Dar es salaam yakiwa na lengo la kuimarisha na kuboresha fani hiyo nchini.
“Licha ya kutunza dawa  mahali salama wafamasia wanapaswa kutunza kumbukumbu za dawa hizo zinapoingia,zinapopokelewa ,zinapotolewa kwa wagonjwa na matumizi ili kuondoa uhaba wa dawa na kuthibitisha matumizi yake” alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha Dkt. Ndugulile amesema kuwa wafamasia wanatakiwa kuwa waaminifu kazini kwani kuna badhi ya wafamasia wana tabia ya kuiba dawa  kwenye  vituo vyao vya kazi na kwenda kuuza nje ya kituo cha kutolea huduma za afya.
Mbali na hayo Dkt. Ndugulile amewaagiza Mganga Mkuu wa Serikali na Mfamasia Mkuu wa serikali kukaa pamoja na kujadili na kuwatengenezea mazingira wezeshi wazalishaji wa Dawa nchini ili waweze kutengeneza dawa kwa kuzingatia ubora na usalama wa mtumiaji .
“Asilimia 90 ya dawa zinanunuliwa nje ya nchi hivyo lazima tukae na kutengeneza mazingira wezeshi kwa wazalishaji wa ndani ili kuweza kutengeneza dawa hapa nchini na tuweze kuokoa fedha nyingi zinazokwenda nje ya nchi” alisema dkt. Ndugulile.
Kwa upande wake Msajili wa Baraza la wafamasia Bi. Elizabeth Shekirego amewasisitiza wanawake kujiunga na fani hiyo kwani wapo wachache ambapo ni asilimia 30 kuliko wanaume.
Aidha Bi. Shekirego amesema Baraza la wafamasia wamejidhatiti kuleta matokeo chanya kwa kuhakikisha dawa zinazotengenezwa nchini zinaboreshwa kwa mahitaji ya watanzania.
Wiki ya Famasia nchini imeadhimishwa leo jijini Dar es salaam ambapo imebeba kauli mbiu isemayo “TAALUMA YA FAMASI KUELEKEA TANZANIA YA UCHUMI WA VIWANDA” ambapo ulienda na uzinduzi wa bango kitita kitakachotumika kutoa elimu na wajibu wa mfamasia.

Jumatano, 13 Juni 2018

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA KUZINDUA KAMPENI YA FURAHA YANGU JUNI 19 DODOMA

- Hakuna maoni
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya Dkt. Angera Ramadhan akihutubia mbele ya Wadau wa masuala mbali mbali ya VVU, ikiwa ni kuelekea katika uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya Furaha yangu,mkoani Dodoma Juni 19 mwaka huu,inayohusisha upimaji wa VVU na kuanza kutumia ARV

Wadau mbali mbali wa wa masuala mbali mbali ya VVU wakifuatilia kwa makini hotuba ya mgeni rasmi ambae ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya Dkt. Angera Ramadhan ikiwa ni kuelekea katika uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya Furaha yangu,mkoani Dodoma Juni 19 mwaka huu,inayohusisha upimaji wa VVU na kuanza kutumia ARV.


NA WAMJW-DAR ES SALAAM 

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa,anatarajiwa kuzindua kampeni ya kitaifa ya Furaha yangu,mkoani Dodoma Juni 19 mwaka huu,inayohusisha upimaji wa VVU na kuanza kutumia ARV

Hayo yamezungumzwa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya Dkt. Angera Ramadhan,
Kampeni hiyo imetajwa kuhamasisha mkakati wa serikali wa upimaji wa VVU na kuanza kutumia ARV mapema kwa wale watakaokutwa na maambukizi.


"Asilimia 45 ya wanaume wanajijua kuwa wanaishi na maambukizi ya VVU na asilimia 55 hawajijui huku wanawake waliokuwa wanajijua kuwa wanamaambukizi  ni asilimia 56 na 44 bado hawako tayari" alisema Dkt. Angera

Dkt. Angera amesema kuwa Kuanza ARV mapema kutapunguza wingi wa  VVU  mwilini na kuimarisha kinga kwa wagonjwa,hivyo kampeni hii kwa wanaume itakuwa chachu ya kujua afya zao na wengi kuwa tayari kwa kuimarisha afya na kupunguza hatari ya kuambukiza wenza wao. 

Aidha Dkt. Angera amesema kuwa serikali itaendelea kubuni mbinu mbadala ili kufikia malengo ya dira ya taifa ya kutokomeza maambukizi ya Ukimwi iliyoridhia malengo ya UNAIDS ya 90-90-90 ambayo ni kuhakikisha asilimia 90 ya watu wote wanaoishi na VVU  wanatambua afya zao,wanaanza dawa na kupunguza maambukizi mapya.

Naye Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI TACAIDS, Dkt. Leornad Maboko,alisema uzinduzi wa kampeni hiyo utakuwa na siku tano za kutoa huduma za afya bila malipo,ikiwemo upimaji wa VVU  na magonjwa sugu.

Aidha Dkt.  Maboko alisema kuwa  lengo la kuhamasisha kwa kauli ya Furaha yangu  Pima,Jitambur ,Ishi na mwanaume njoo kwenye huduma ni kutokana na kubaini kundi hilo kubwa halifikiwi na ili kumaliza maambukizi ni lazima kupewa hamasa.

"Hivyo tunatoa wito wakazi wa Dodoma,mikoa ya jirani na mikoa sita ambayo ipo katika awamu ya kwanza ya uzinduzi ikiwemo Njombe,Iringa na Mwanza kumuunga mkono Waziri Mkuu kwa kujitokeza kwa wingi kujua afya zao na ikigundulika kutumia dawa mapema ili kuiamrisha afya na kupunguza nguvu ya VVU," alisema Dkt.  Maboko. 

Jumatatu, 11 Juni 2018

WAZIRI UMMY AKUTANA NA BALOZI WA JAMHURI YA NCHI YA UTURUKI NA WAKURUGENZI WA TAASISI ZA SERIKALI ZINAZOHUSIANA NA AFYA.

- Hakuna maoni
WAZIRI wa afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiongea na wakurugenzi wa Wakurugenzi Tasisi za Serikali zinazojihusisha na maswala ya afya hapa nchini  hawapo pichani wakati alipokutana na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Uturuki nchini, Mhe.Ali Dovutoglu hayupo pichani 

WAZIRI wa afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu mwenye kiremba cha rangi ya bluu bahari akipitia muongozo wa Sera ya afya wakati alipokutana na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Uturuki nchini, Mhe.Ali Dovutoglu kushoto kwake ni Naibu Waziri wa afya Dkt. Faustine Ndugulile .

WAZIRI wa afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akijadili jambo na Naibu wake Dkt. Faustine Ndugulile  wakati alipokutana na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Uturuki nchini, Mhe.Ali Dovutoglu .

NA WAMJW
WAZIRI wa afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amekutanana Balozi Mteule wa Jamhuri ya Uturuki nchini, Mhe.Ali Dovutoglu kujadili maswala mbalimbali ya kuboresha sekta ya afya nchini ikiwemo kubadilishana wataalam pamoja na Wakurugenzi Tasisi za Serikali zinazojihusisha na maswala ya afya hapa nchini  leo jijini Dar es salaam.

MAKAMU WA RAIS AHAIDI MILIONI 600 KUPAMBANA NA CHANGAMOTO ZA DAWA MLOGANZILA.

- Hakuna maoni
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan akizungumza na wafanyakazi wa hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi shirikishi Muhimbili (MAMC), Kampasi ya Mloganzila wakati wa ziara yake iliyofanyika leo.

Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza kutolea machache ufafanuzi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan  (mwenye kilemba cha bluu) akipata maelezo kutoka kwa Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kulia) wakati wa ziara yake katika hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MAMC), Kampasi ya Mloganzila jijini Dar es Salaam. Pembeni kushoto ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Huduma za Hospitali, Prof. Said Aboud.

NA WAMJW-MLOGANZILA

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Bi. Samia Suluhu Hassan amehaidi  kuiongezea fedha za dawa hospitali Mloganzila Sh. milioni 600 mpaka kufikia Sh. milioni 900 ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa dawa hospitalini hapo.

Hayo ameyasema wakati alipofanya ziara yake ya kuangalia hali ya utoaji huduma katika Hospitali ya Mloganzila iliyopo nje kidogo ya jiji la Dar es salaam leo alipoambatana na Waziri wa Afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.

“Tatizo hata fedha mliyopewa awali mkichukua dawa MSD hamrudishi tena fedha kule, hakikisheni hizi fedha tunazowaongeza mlipe bili MSD ili iweze kuleta dawa nyingi zaidi angalau nusu ya fedha muirejeshe tena huko,” alisema.Mhe. Samia.

Aidha Mhe. Samia ameiagiza pia hospitali hiyo kufungua duka la dawa ili kuweza kuweka aina ya dawa ambazo wamekuwa wakizikosa Bohari ya Dawa.

Mbali na hayo Mhe.  Samia alikagua na kushangazwa na Wakala wa Ujenzi Tanzania (TBA kwa kitendo cha kusuasua ujenzi wa mabweni katika Hospitali ya Taaluma na Tiba Mloganzila.

Kwa upande wake  Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu  aliwataka  wananchi kuchangia huduma za matibabu kupitia bima za afya ili waweze kupata matibabu ya kibingwa ngazi za juu bila vikwazo vya kifedha 


“ Mloganzila ni miongoni mwa Hospitali saba  zinazomilikiwa na serikali zinazotoa matibabu ya kibingwa ngazi ya juu na uwepo wake umeleta unafuu katika kuongeza wigo wa huduma na mafunzo kwa wataalamu wa afya” alisema Mhe. Ummy.
Naye, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo huduma za hospitali, Profesa Said Abood, alisema wamekuwa wakipata asilimia 24 pekee ya dawa wanazozihitaji kutoka MSD na dawa zingine wamekuwa wakizinunua kupitia wakala mbalimbali.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya ameongoza mkutano wa robo mwaka wa kitaalam katika sekta ya Afya.

- Hakuna maoni
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya akiongea na baadhi wadau wa maendeleo,wadau wa sekta ya afya wa Serikali na Binafisi na Wakurugenzi wa vitengo mbalimbali kutoka Wizara ya Afya hawapo pichani wakatri wa Mkutano wa robo mwaka wa kitaalam katika sekta ya afya uliofanyika leo jijini Dar es salaam.




Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya akiwakabidhi vyeti watumishi watatu wa Sekretarieti ya pamoja kwa kutambua michango yao kwa kipindi chote cha utumishi wao wakati wa Mkutano wa robo mwaka wa kitaalam katika sekta ya afya uliofanyika leo jijini Dar es salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya katikati akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi wadau wa maendeleo,wadau wa sekta ya afya wa Serikali na Binafisi na Wakurugenzi wa vitengo mbalimbali kutoka Wizara ya Afya hawapo pichani wakatri wa Mkutano wa robo mwaka wa kitaalam katika sekta ya afya uliofanyika leo jijini Dar es salaam.



Baadhi wadau wa maendeleo,wadau wa sekta ya afya wa Serikali na Binafsi na Wakurugenzi wa vitengo mbalimbali kutoka Wizara ya Afya wakifuatilia kwa makini maelekezo kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya hayupo pichani wakati wa Mkutano wa robo mwaka wa kitaalam katika sekta ya afya uliofanyika leo jijini Dar es salaam.

NA WAMJW


Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya ameongoza mkutano wa robo mwaka wa kitaalam katika sekta ya Afya unaowaleta pamoja Serikali ,wadau wa maendeleo,Sekta binafsi na Asasi za kiraia.
Leongo la mkutano huo ni kuangalia utekelezaji wa maazimio ya pamoja na kuandaa mipango mipya ya utekelezaji wa mpango mkakati wa sekta ya afya wanne 2015-2020 kupitia vikundi kazi 11 vya kilaam.
Pia watumishi watatu wa Sekretarieti ya pamoja wametunukiwa vyeti kwa kutambua michango yao kwa kipindi chote cha utumishi wao ambao ni Dkt. Oberlin Kisanga ,Dkt. Anna Nswila na Dkt. Didace Mutagwaba.

Ijumaa, 8 Juni 2018

TAARIFA KWA UMMA

- Hakuna maoni


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO

  
TAARIFA KWA UMMA

 WATUMISHI WA AFYA 200 KUPATIWA MAFUNZO YA UTOAJI WA DAWA ZA USINGIZI (ANAESTHESIA) KWENYE VITUO VYA AFYA VYA UPASUAJI WA DHARURA KWA WAJAWAZITO

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI inatekeleza mkakati wa kuhakikisha kwamba huduma za Afya kwa akina mama wajawazito zinakuwa za uhakika na salama kwa kuandaa rasilimali watu, miundombinu ya majengo na vifaa vitakavyowezesha kutoa huduma hizi ikiwemo huduma za upasuaji wa dharura   kwa akina mama wajawazito wakati wa kujifungua.

Mkakati huu una lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi kufikia 290 mwaka 2020. Takribani, vituo vya afya (Health Centres) 288 vinavyomilikiwa na Serikali vilivyopo katika Halmashauri za Wilaya, Miji na Manispaa kote nchini vinaboreshwa ili kuviwezesha kutoa huduma za uzazi za dharura kwa akina mama wajawazito.
Uwepo wa Wataalam wa afya ikiwemo wataalam wa utoaji huduma ya dawa za usingizi (Anaesthesia) ni mojawapo ya mahitaji ya lazima katika utoaji wa huduma  hizi.

Ili kutimiza azma ya kupata wataalam wa utoaji wa huduma ya dawa za usingizi wakati wa upasuaji, Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wa Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health Basket Fund) imepata fedha kiasi cha shilingi 1,079,200,000.00 kwa ajili ya kuwasomesha watumishi wa afya wa Serikali (Wauguzi na Matabibu) katika fani ya utoaji huduma ya dawa za usingizi (Anaesthesia). Fedha hizi zitasomesha watumishi wapatao 200, kati ya watumishi hao 100 watafanya mafunzo yao katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na MOI, Watumishi 50 watafanya mafunzo katika Hospitali ya KCMC na 50 watafanya mafunzo hayo katika Hospitali ya Bugando. Mafunzo haya yataanza kutolewa tarehe 15 Juni, 2018. MAJINA WA WATUMISHI WALIOCHAGULIWA KUFANYA MAFUNZO HAYA YANAPATIKANA KWENYE TOVUTI YA WIZARA YA AFYA (www.moh.go.tz) NA YA OFISI YA RAIS-TAMISEMI (www.tamisemi.go.tz)

Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2019 na kabla ya Mwaka 2020 vituo vyote vya afya vinavyomilikiwa na Serikali vinakuwa na watumishi maalum wa kutoa Huduma ya dawa ya Usingizi kwa ajili ya upasuaji wasiopungua wawili (2) kwa kila kituo. Aidha, watumishi wa afya wapatao 85 wamekwishahitimu mafunzo haya katika Hospitali ya KCMC na Bugando na tayari watumishi hao wako kwenye vituo vya afya vilivyokwisha kamilika kuanza kutoa huduma hizo za dharura kwa akina mama wajawazito.

Mafunzo haya ya mwaka mmoja ni ya mpito wakati Serikali ikiendelea kurasimisha mafunzo ya Shahada ya kwanza ya kutoa dawa ya usingizi kwa wauguzi yatakayotolewa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kuanzia mwaka huu wa masomo 2018/19.


Imetolewa na


Nsachris Mwamwaja
MKUU KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI-AFYA
08 Juni, 2018

Alhamisi, 7 Juni 2018

MKUTANO WA MWAKA WA KUPITIA,KUJADILI NA KUPANGA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA TAIFA WA KUDHIBITI MAGONJWA YALIYOKUWA HAYAPEWI KIPAUMBELE YAFIKIA TAMATI LEO.

- Hakuna maoni
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi akiongea na wadau mbalimbali wa sekta ya afya hawapo pichani kuhusu kinga tiba za magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele wakati wa kufunga mkutano wa mwaka wa kupitia,kujadili na kupanga utekelezaji wa mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa hay oleo jijini Dar es salaam.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi kulia akifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinatolewa na wadau mbalimbali wa sekta ya afya hawapo pichani wakati wa kufunga mkutano wa mwaka wa kupitia,kujadili na kupanga utekelezaji wa mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mratibu wa Taifa wa mpango wa kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele nchini Dkt. Upendo Mwingira.

Mratibu wa Taifa wa mpango wa kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele nchini Dkt. Upendo Mwingira akiongea na wadau mbalimbali wa sekta ya afya hawapo pichani kuhusu kinga tiba za magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele wakati wa kufunga mkutano wa mwaka wa kupitia,kujadili na kupanga utekelezaji wa mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa hay oleo jijini Dar es salaam.



Wadau mbalimbali wa sekta ya afya kwa upande wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele wakifuatilia kwa makini hotuba ya  Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi hayupo pichani wakati wa kufunga mkutano wa mwaka wa kupitia,kujadili na kupanga utekelezaji wa mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa hayo leo jijini Dar es salaam.

 Na WAMJW-DSM
Mkutano wa mwaka wa kupitia,kujadili na kupanga utekelezaji wa mpango wa taifa wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele yamefikia tamati leo jijini Dar es salaam ambapo wadau mbalimbali wa sekta ya afya wanaoshughulika na magonjwa hayo wamekutana na kutoka na njia mbalimbali za kupambana na magonjwa hayo ambapo tamati yake itafikia Juni 8 mwaka huu kwa kutembelea Kambi ya kufanyia upasuaji wa matende na mabusha iliyopo Kisarawe Mkoani Pwani.