JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO
YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TAARIFA
KWA UMMA
WATUMISHI WA AFYA 200 KUPATIWA MAFUNZO YA
UTOAJI WA DAWA ZA USINGIZI (ANAESTHESIA) KWENYE VITUO VYA AFYA VYA UPASUAJI WA
DHARURA KWA WAJAWAZITO
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Ofisi
ya Rais-TAMISEMI inatekeleza mkakati wa kuhakikisha kwamba huduma za Afya kwa
akina mama wajawazito zinakuwa za uhakika na salama kwa kuandaa rasilimali
watu, miundombinu ya majengo na vifaa vitakavyowezesha kutoa huduma hizi
ikiwemo huduma za upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito wakati wa
kujifungua.
Mkakati
huu una lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka 556 kwa kila vizazi
hai 100,000 hadi kufikia 290 mwaka 2020. Takribani, vituo vya afya (Health
Centres) 288 vinavyomilikiwa na Serikali vilivyopo katika Halmashauri za
Wilaya, Miji na Manispaa kote nchini
vinaboreshwa ili kuviwezesha kutoa huduma za uzazi za dharura kwa akina mama
wajawazito.
Uwepo wa Wataalam wa afya
ikiwemo wataalam wa utoaji huduma ya dawa za usingizi (Anaesthesia) ni mojawapo
ya mahitaji ya lazima katika utoaji wa huduma
hizi.
Ili
kutimiza azma ya kupata wataalam wa utoaji wa huduma ya dawa za usingizi wakati
wa upasuaji, Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wa Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health Basket
Fund) imepata fedha kiasi cha shilingi 1,079,200,000.00
kwa ajili ya kuwasomesha watumishi wa afya wa Serikali (Wauguzi na Matabibu)
katika fani ya utoaji huduma ya dawa za usingizi (Anaesthesia). Fedha hizi zitasomesha watumishi wapatao 200, kati ya watumishi hao 100
watafanya mafunzo yao katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na MOI, Watumishi 50
watafanya mafunzo katika Hospitali ya KCMC na 50 watafanya mafunzo hayo katika
Hospitali ya Bugando. Mafunzo haya yataanza kutolewa tarehe 15 Juni, 2018. MAJINA WA WATUMISHI
WALIOCHAGULIWA KUFANYA MAFUNZO HAYA YANAPATIKANA KWENYE TOVUTI YA WIZARA YA
AFYA (www.moh.go.tz) NA YA OFISI YA RAIS-TAMISEMI
(www.tamisemi.go.tz)
Lengo
la Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2019 na kabla ya Mwaka 2020 vituo
vyote vya afya vinavyomilikiwa na Serikali vinakuwa na watumishi maalum wa
kutoa Huduma ya dawa ya Usingizi kwa ajili ya upasuaji wasiopungua wawili (2) kwa kila kituo. Aidha,
watumishi wa afya wapatao 85
wamekwishahitimu mafunzo haya katika Hospitali ya KCMC na Bugando na tayari
watumishi hao wako kwenye vituo vya afya vilivyokwisha kamilika kuanza kutoa huduma
hizo za dharura kwa akina mama wajawazito.
Mafunzo
haya ya mwaka mmoja ni ya mpito wakati Serikali ikiendelea kurasimisha mafunzo
ya Shahada ya kwanza ya kutoa dawa ya usingizi kwa wauguzi yatakayotolewa na
Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kuanzia mwaka huu
wa masomo 2018/19.
Imetolewa na
Nsachris Mwamwaja
MKUU KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI-AFYA
08 Juni, 2018
0 on: "TAARIFA KWA UMMA"