Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatano, 20 Juni 2018

SALAMU ZA MHE. UMMY. A MWALIMU (MB) KATIKA KAMPENI YA FURAHA YANGU.

 
SALAMU ZA MHE. UMMY. A MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, KATIKA UZINDUZI WA KITAIFA WA KAMPENI YA KUPIMA VVU NA KUANZA DAWA MAPEMA KWA WENYE MAAMBUKIZI MKOA WA DODOMA, VIWANJA VYA JAMHURI TAREHE 19 JUNI 2018

Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 
Mheshimiwa Suleiman Jafo (Mb) - Waziri wa Nchi - Ofisi ya Rais, TAMISEMI,
Mheshimiwa Jenister Mhagama - Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu,
Waheshimiwa Mawaziri wote mliopo hapa,
Mheshimiwa Dkt. Bilinith Mahenge - Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, 
Mkurugenzi Mkazi wa USAID,
Manaibu Waziri wote mlioko hapa,
Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM - Mkoa wa Dodoma,
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,
Waheshimiwa Wabunge,
Waheshimiwa Mabalozi,
Makatibu Wakuu Wote Mlioko hapa,
Viongozi wa Madhehebu ya Dini,
Dkt. Leonard Maboko - Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, 
Ndugu Justine Mwinuka Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI,
Wadau wa Maendeleo katika Mapambano dhidi ya UKIMWI. 
Viongozi wa Vyama vya siasa,
Waandaaji wa kampeni ya Furaha Yangu,
Wanahabari,
Wageni Waalikwa, 
Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote, Napenda kumshukuru Mungu kwa kuwezesha na kutuweka salama kuifikia siku hii ya leo ambayo ni muhimu sana kwa ajili ya Afya ya watanzania katika uhamasishaji wa kupima VVU na kuanza ARV mapema maarufu kama Furaya Yangu - Pima, Jitambue, Ishi. Zaidi ya yote, napenda kukushukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiwa mgeni rasmi na balozi wa Kampeni hii. 
Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuupongeza kwa dhati, uongozi wa Mkoa wa Dodoma chini ya Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Dkt. Belinith Mahenge kwa kuwa mwenyeji wa uzinduzi huu na kwa ushirikiano mkubwa uliotuonyesha kwa kamati ya maandalizi ya Kitaifa na ile ya Mkoa, pongezi sana.

Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Kampeni hii inawalenga watanzania wote watambue hali zao za maambukizi ya VVU, hususani wanaume na makundi mengine ambayo ni Wasichana walio katika umri wa balehe, Wanawake vijana wenye umri wa miaka 15-24, akinamama wajawazito na wanaonyonyesha pamoja na watoto wao.
Napenda kutoa ufafanuzi kwa nini tunawalenga wanaume zaidi na makundi tajwa hapo juu katika kampeni hii, ni kwa sababu takwimu za utafiti wa Viashia vya VVU na UKIMWI nchini wa mwaka 2016-2017 umeonyesha kuwepo na kiwango cha chini cha upimaji wa VVU kwa wanaume ukilinganisha na wanawake. Katika utafiti huo, inakadiriwa kuwa asilimia 48 ya watu wanaoishi na VVU Tanzania hawajui kuwa wana maambukizi ya VVU. Hali hii ni hatari kwa afya ya watu hao, familia, kaya na Taifa kwa ujumla, kwa kuwa inadhoofisha mapambano dhidi ya UKIMWI nchini na kulifanya Taifa letu kutofikia malengo ya kutokomeza ugonjwa huu hivyo kuendelea kuwa kikwazo katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. 

Mheshimiwa Waziri Mkuu, 
Katika kukabiliana na VVU na UKIMWI, nchi yetu mnamo mwaka 2015 iliridhia malengo ya kidunia ya tisini tatu ifikapo mwaka 2020 ambapo asilimia 90 ya watu wanaoishi na VVU wawe wanajua hali zao za maambukizi ya VVU na asilimia 90 kati yao wawe wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU, na kati yao wanaotumia dawa asilimia 90 Virusi vya ukimwi viwe vimefubaa. 
Tanzania imekuwa kati ya nchi zinazoonyesha mafanikio katika kupambana na maambukizi ya VVU kwa kiwango kikubwa. Tunajivunia kuweza kushusha kiwangocha maambulkizi kutoka asilimia 7 mwaka 2003 kufikia asilimia 4.7 mwaka 2017/2018 (THIS report). Haya ni matokeo mazuri ya miaka 30 ya mapambano dhidi ya ugonjwa huu hatari wa UKIMWI nchini
Hali ilivyo kwa mujibu wa takwimu za Utafiti wa Viashiria vya VVU na UKIMWI THIS 2016/2017 ni kwamba kwa 

Tisini ya Kwanza: waliopimwa na kugundulika na maambukizi ya VVU ni asilimia 52.2 kati ya watu wanaokadiriwa kuwa 1,400, 000 wanaoishi na VVU nchini wenye umri wa miaka 15 - 64 ambao wanajua hali zao za maambukizi ya VVU ambapo Wanawake ni asilimia 55.9 na Wanaume ni asilimia 45.3

Kuhusu Tisini ya Pili: Wanaotumia dawa Kati ya watu wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15 - 64 ambao wanajua hali zao za maambukizi, asilimia 90.9 walitoa taarifa kuwa wanatumia ARV, Wanawake ni asilimia 92.9. na Wanaume ni asilimia 86.1. kwa takwimu hizi inaonyesha tumepiga hatua nzuri na hata kuvuka lengo kwa ujumla wake kitaifa na kwa kundi la wanawake.

Aidha kwa upande wa Tisini ya Tatu: Kushuka kwa kiwango cha VVU mwilini, inaonyesha kuwa kati ya watu wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15 - 64 ambao wametoa taarifa kuwa wanatumia ARV, asilimia 87.7 ya watu hao inaonyesha kiasi cha VVU kimeshuka mwilini. Wanawake ni asilimia 89.2 na Wanaume ni asilimia 84. Natoa wito kwa wanaotumia ARV kuzingatia masharti na kuwa na ufuasi endelevu wa kutumia ARV.

Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Kampeni hii imepewa jina la Furaha yangu - Pima, Jitambue, Ishi kutokana na ukweli kwamba Kampeni hii tofauti na kampeni zilizopita kwani inatoa ujumbe wa furaha kwa wote watakaopima na kujua hali zao za maambikizi. Kwa wale watakaokutwa na VVU sasa wanaanzishiwa matibabu mara moja tofauti na ilivyokuwa zamani walipokuwa wanalazimika kusubiri kuanza dawa mpaka CD4 zishuke au kufikia hatua fulani ya ugonjwa. Kuanza ARV mapema na kuzitumia kama inavyotakiwa, hukata makali ya VVU haraka na kumfanya mtu anayeishi na VVU kuepuka kushuka kwa kinga ya mwili na hivyo kuishi maisha ya kawaida na kupunguza uwezekano wa kuwaambukiza watu wengine. Hivyo basi, kampeni hii inaleta furaha na amani kwa watu hata kama unaishi na VVU. 

Tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na wadau wetu wa maendeleo wakiwemo PEPFAR, Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua kikuu na Malaria na Jumuiya za Umoja wa Mataifa kwa kuwezesha uwepo wa vitendanishi na dawa za kutosha kwa wote wanaohitaji huduma hizi. Wizara yangu imefanikiwa kupima VVU kwa watu milioni 7.4 hadi kufikia Disemba, 2017 ambao ni sawa na ongezeko la watu milioni 2.4 ikilinganishwa na watu waliopima mwaka 2016 ambao ni milioni 5. Aidha, vituo vya kutolea huduma za upimaji wa VVU na ushauri nasaha vimeongezeka kutoka vituo 5,700 mwaka 2015 hadi kufikia vituo 6,005 hadi Machi, 2018. Pia, hadi sasa kuna jumla ya vituo 1,868 vinayotoa huduma za CTC na vituo 4,365 vinavyotoa huduma za PMTCT. Katika kuboresha utoaji wa huduma hizi tunatarajia kuongeza vituo vya kutoa huduma za Tiba na Matunzo (CTC), hadi kufikia jumla ya vituo 4,050 ifikapo mwaka 2018/19.  

Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Napenda kuchukua fursa hii pia kuwataarifu watu wanaoishi na VVU na wanaotumia ARV na watanzania wote kwa ujumla kuwa hivi sasa tumeanza kwa majaribio kutoa ARV kwa wateja wetu kwa miezi mitatu mitatu hasa wale ambao mwenendo wao wa tiba unaridhishwa kwa kuwa kiwango cha VVU mwilini kimeshuka na wanazingatia umezaji wa ARV na mahudhurio kiliniki, Aidha utaratibu huu hautawahusu wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, walio kwenye dawa za mstari wa pili na wale ambao hawatakidhi vigezo vya kitaalamu vilivyoweka.

Mpango huu utasaidia kupunguza muda kwa walengwa kusubiri huduma vituoni hivyo kwaongezea muda wa kufanya shughuli za ujenzi wa taifa letu katika kujenga Tanzania ya Viwanda na kuelekea uchumi wa kati. Aidha nitoe wito kwa wataalamu wetu kufuatilia kwa karibu mwenendo wa huduma za tiba kwa wagonjwa na kuchukua hatua pale inapojitokeza kuna tatizo lolote la kitaalamu au kiafya.

Aidha, 2019 Wizara itaanza kutoa dawa zenye ufanisi zaidi na zenye maudhi kidogo ukilinganisha na hizi za sasa. Hii ni kutokana na tafiti za kisayansi zinazoendelea kufanyika chini ya WHO.

Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Napenda kukutaarifu kuwa Jumla ya mashine 35 zenye uwezo wa kupima Wingi wa Virusi vya UKIMWI (HIV Viral Load) Hospitali za Mikoa 17 na Hospitali za Wilaya 18 na hivi sasa tuna mashine za Genexpert 191 zinazopima wagonjwa wa TB na zina uwezo wa kupima wingi wa Virusi vya UKIMWI ambapo zimesambazwa katika Hospital za Mikoa na Wilaya ili kuboresha huduma ya upimaji wa wingi wa VVU katika vituo vya kutolea huduma za afya. Aidha hadi Mwezi Machi 2018 watu 1, 022,745 walikuwa wameandikishwa katika huduma za tiba na Matunzo, kati ya hao 1,007,026 wanatumia ARV.

Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Maambukizi ya VVU yanaenezwa kwa kiasi kikubwa na ngono zisizo salama. Aidha, watu wanaotumia dawa ya kulevya kwa kujidunga, wanawake wanaofanya biashara ya ngono, wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao, Wasichana wadogo wa umri balehe (miaka 15 -19) ,wasichana wa umri kati ya miaka 20 - 24, vijana wa kiume miaka 15 - 24 ambao ndio nguvu kazi ya taifa letu wako katika hatari zaidi ya maambuzi ya ugonjwa huu. Hivyo nitoe wito wa watanzania kujitambua na kuchukua hatua.  kwa kulitambua hilo Wizara imekuwa ikitoa huduma kwa makundi haya ambayo yapo katika hatari zaidi ya kuambukiza au kuambukizwa VVU. 

Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Pamoja na mkakati wa kupima na kuanza ARV mapema, Wizara yangu, tukishirikiana kwa karibu na TACAIDS, OR TAMISEMI na Wadau wa maendeleo, inaendelea kutekeleza mikakati mingine ikiwemo huduma za tohara kwa wanaume, Elimu ya matumizi sahihi na endelevu ya kondomu, Utoaji wa damu salama, kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na Elimu ya kubadili tabia. 

Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Katika kutekeleza mikakati mbalimbali tunaweza kufanikiwa zaidi iwapo kila mmoja wetu atachukua hatua aidha kwa kutumia huduma za afya, kubadili tabia hatarishi, kuacha unyanyapaa na kuchangia rasilimali fedha pale ambapo Serikali na wadau wameishia. Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wadau ambao baadhi yao ni: 
Serikali ya Marekani kupitia mradi wa PEPFAR,
Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua kikuu na Malaria, 
Shirika la Maendeleo la Marekani USAID kupitia mradi wa Tulonge Afya, 
Shirika la Kimataifa la Kazi Duniani (ILO),
Asasi za Kiraia za mapambano dhidi ya UKIMWI wakiwemo Jhpiego, MDH, TAYOA, WRP, Pharm Access, Benjamin Mkapa Fondation, THPS, 
Viongozi wa Dini na Vyama vya Siasa.

Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Kwa heshima nikuombe ukabidhi vyeti vya shukrani kwa mabalozi wanne wa Kampeni ya Furaha yangu, mabalozi hao ni baadhi ya watu wanaoishi na VVU ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha umma kujua hali zao za maambukizi ya VVU na kuanza dawa za ARV mapema bila uwoga wowote na hivyo kuwa mstari wa mbele katika kutokomeza unyanyapaa. 
(Majina ya watu hao yatatajwa).
FURAHA YANGU - PIMA, JITAMBUE, ISHI
Asanteni kwa kunisikiliza

0 on: "SALAMU ZA MHE. UMMY. A MWALIMU (MB) KATIKA KAMPENI YA FURAHA YANGU."