NAIBU Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee
na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amewaagiza wafamasia wa Hospitali za serikali
kutunza dawa vizuri na mahali panapostahili ili kuweza kuepuka uharibifu wa dawa
hizo.
Hayo ameyazungumza wakati wa maadhimisho ya wiki ya Famasia
duniani yaliyofanyika leo jijini Dar es salaam yakiwa na lengo la kuimarisha na
kuboresha fani hiyo nchini.
“Licha ya kutunza dawa mahali salama wafamasia wanapaswa kutunza
kumbukumbu za dawa hizo zinapoingia,zinapopokelewa ,zinapotolewa kwa wagonjwa
na matumizi ili kuondoa uhaba wa dawa na kuthibitisha matumizi yake” alisema
Dkt. Ndugulile.
Aidha Dkt. Ndugulile amesema kuwa wafamasia
wanatakiwa kuwa waaminifu kazini kwani kuna badhi ya wafamasia wana tabia ya
kuiba dawa kwenye vituo vyao vya kazi na kwenda kuuza nje ya
kituo cha kutolea huduma za afya.
Mbali na hayo Dkt. Ndugulile amewaagiza Mganga Mkuu
wa Serikali na Mfamasia Mkuu wa serikali kukaa pamoja na kujadili na kuwatengenezea
mazingira wezeshi wazalishaji wa Dawa nchini ili waweze kutengeneza dawa kwa
kuzingatia ubora na usalama wa mtumiaji .
“Asilimia 90 ya dawa zinanunuliwa nje ya nchi hivyo
lazima tukae na kutengeneza mazingira wezeshi kwa wazalishaji wa ndani ili
kuweza kutengeneza dawa hapa nchini na tuweze kuokoa fedha nyingi zinazokwenda
nje ya nchi” alisema dkt. Ndugulile.
Kwa upande wake Msajili wa Baraza la wafamasia Bi.
Elizabeth Shekirego amewasisitiza wanawake kujiunga na fani hiyo kwani wapo
wachache ambapo ni asilimia 30 kuliko wanaume.
Aidha Bi. Shekirego amesema Baraza la wafamasia
wamejidhatiti kuleta matokeo chanya kwa kuhakikisha dawa zinazotengenezwa
nchini zinaboreshwa kwa mahitaji ya watanzania.
Wiki ya Famasia nchini imeadhimishwa leo jijini Dar
es salaam ambapo imebeba kauli mbiu isemayo “TAALUMA YA FAMASI KUELEKEA
TANZANIA YA UCHUMI WA VIWANDA” ambapo ulienda na uzinduzi wa bango kitita
kitakachotumika kutoa elimu na wajibu wa mfamasia.
0 on: "DKT. NDUGULILE HAIMIZA UTUNZAJI MZURI WA DAWA."