Waziri wa Afya akiongea na Kanali Ramson Mwaisaka ambaye alishiriki uchangiaji wa damuwakati wa zoezi la uchangiaji damu linalofanyika Nyerere Square katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kuchangia damu Duniani.
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee
na Watoto Ummy Mwalimu akisoma kadi ya mchangiaji damu kutoka JKT
Dodoma wakati wa zoezi la uchangiaji damu linalofanyika Nyerere Square
katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kuchangia damu Duniani
Waziri Ummy Mwalimu akiongea na mmoja wa
wanawake waliofika kuchangia damu. Damu salama ni nguzo muhimu katika
kuokoa vifo vitokanavyo na uzazi kwa akina mama wajawazito nchini wakati wa zoezi la uchangiaji damu linalofanyika Nyerere Square
katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kuchangia damu Duniani.
HOTUBA YA MHESHIMIWA UMMY A. MWALIMU (MB) WAZIRI WA
AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KWENYE SHEREHE YA
MAADHIMISHO YA SIKU YA WACHANGIA DAMU DUNIANI MKOANI DODOMA TAREHE
14-6-2018
• Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
• Mheshimiwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma,
• Mkurugenzi wa Tiba-MOHCDGEC,
• Mganga Mkuu wa Mkoa-Dodoma,
• Meneja wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama,
• Waheshimiwa Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa,
• Viongozi wa Dini,
• Mwakilishi wa CDC,
• Mwakilishi Shirika la Afya Duniani,
• Mwakilishi KOICA,
• Ndugu Wachangia Damu,
• Wanahabari,
• Wasanii mbalimbali,
• Wageni Waalikwa,
• Mabibi na Mabwana.
Ndugu Wananchi,
Leo
tarehe 14 Juni, 2018 tunaungana na Dunia Kuadhimisha Siku ya Wachangia
Damu Duniani. Hivyo, ninayo furaha kuungana na Watanzania na wananchi
wa Dodoma katika siku hii muhimu kuwashukuru na kuwaenzi Wachangia
Damu wote ambao wamekuwa wakichangia damu, ili kuokoa maisha ya
wagonjwa wanaohitaji huduma ya kuongezewa damu. Pamoja na hayo pia
ninayo furaha kuona kuwa leo tunazindua Kikundi cha Wachangia Damu Wenye
Kundi Adimu la Damu (Rare Blood Group Donor Club) hapa Mkoani Dodoma.
Ndugu Wananchi,
Ni
kweli kwamba uchangiaji damu wa hiari bila malipo, ndiyo msingi wa
upatikanaji wa damu iliyo salama. Wachangiaji damu wa hiari wanaorudia
kuchangia mara kwa mara wapo salama na wanahusishwa na viwango vya chini
vya magonjwa ambayo yanaweza kuambukizwa kwa njia ya damu kama virusi
vya UKIMWI, homa ya ini na kaswende. Naomba nitumie fursa hii kwa niaba
ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusema
“ASANTENI SANA KWA WOTE AMBAO MMEKUWA MKICHANGIA DAMU KWA HIARI KUOKOA
MAISHA YA WATANZANIA WENZETU”.
Ndugu Wananchi,
Kauli
mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni "Jitoe kwa ajili ya mwingine.
Changia damu. Okoa Maisha ya mwenzio" (Be there for someone else. Give
blood. Share life). Kauli mbiu ya mwaka huu inalenga kuonyesha
mshikamano katika uchangiaji damu, inalenga mambo muhimu ambayo
yanaonyesha thamani ya mwanadamu kama heshima, huruma, wema na kuwajali
wengine ambavyo ndio msingi wa kuendeleza uchangiaji damu wa hiari bila
malipo yoyote.
Ndugu Wananchi,
Huduma
za Damu Salama Tanzania Bara zilianza mwaka 1946 kwa utaratibu wa ndugu
wa mgonjwa kujitolea damu ya kumuongezea mgonjwa (Family Replacement).
Hata hivyo mfumo huu wa kutoa damu kwa utaratibu wa ndugu wa mgonjwa
kujitolea damu ulifanya damu kuwa adimu hasa panapotokea dharura.
Tokea
kuanzishwa kwa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, kumekuwa na ongezeko la
ukusanyaji wa chupa za damu kutoka 52,000 (2006) hadi 233,593 (2017).
Hata hivyo, ongezeko hili bado halijakidhi mahitaji ya nchi ambayo ni
sawa na chupa 520,000 (asilimia moja ya wananchi; kwa takwimu za mwaka
2017 au chupa 10 kwa kila wananchi 1000). Kwa taarifa za Mpango za 2017,
Mikoa iliyoongoza kwenye makusanyo ya damu ni Katavi (94% ya malengo),
Lindi (79% ya malengo), Pwani (66% ya malengo). Mikoa ambayo haikufanya
vizuri ni Songwe (16% ya malengo), Mbeya (20% ya malengo) na Tabora (22%
ya malengo).
Aidha, ili
kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano, Mpango wa Taifa wa Damu
Salama wakishirikiana na Mikoa na Halmashauri za Wilaya, pamoja na Jeshi
la Wananchi Tanzania wameweka lengo la kuongeza ukusanyaji damu kufikia
chupa 375,000 mwaka 2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia 72. Vile vile,
nimetoa maelekezo kwa Mpango wa Taifa wa Damu Salama kuweka mikakati na
kuhakikisha wanakusanya chupa za damu 540,000 (asilimia moja ya wananchi
kwa takwimu za mwaka 2018 ambapo inakadiriwa kuwa watanzania watakuwa
54,000,000) ambayo ndio mahitaji ya halisi ya chupa za damu nchini.
Uboreshaji wa huduma za damu salama nchini ni utekelezaji wa ilani ya
CCM ya mwaka 2015, ambayo imelenga kuboresha na kuimarisha huduma ya
Afya ya uzazi na mtoto nchini; na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi
ifikapo mwaka 2020.
Ili
kuweza kufikia malengo haya kwa muda huu mfupi na kuendana na kasi ya
Serikali ya Awamu ya Tano, napenda kutoa maelekezo kwa Mpango wa Taifa
wa Damu Salama kuimarisha na kuboresha mifumo na utendaji kazi, ikiwa ni
pamoja kufanya kazi kwa ukaribu na timu za kukusanya damu za Mikoa na
Halmashauri, Timu za Kanda ya Jeshi (TPDF) na Chama cha Msalaba Mwekundu
(TRCS).
Aidha, Wizara
kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI imeanzisha utaratibu wa kuwa na vituo
vya benki za damu kwenye ngazi ya Mikoa ili visaidiane na Benki za damu
za Kanda katika kuboresha upatikanaji wa damu salama hususani kwa akina
mama wajawazito. Hadi sasa Vituo Vidogo vya Damu Salama za Mikoa 9
zimeanzishwa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Morogoro, Dodoma,
Iringa, Kigoma, Shinyanga, Kagera na Mara. Lengo ni kuhakikisha kila
Mkoa una Benki ya damu; na kuwa na uwezo wa kutoa huduma ya damu salama
kwa kila anayehitaji ndani ya Mkoa. Hii ikiwa ni mojawapo ya jitihada za
kuboresha huduma za afya pamoja na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Katika bajeti ya mwaka 2018/2019, Wizara imetenga fedha kwa ajili ya
ujenzi wa Vituo Vidogo vya Damu Salama za Mikoa 5, ikiwemo Mkoa wa
Tanga, Ruvuma, Rukwa, Katavi na Geita.
Ndugu Wananchi,
Tumeshuhudia
hospitali zetu za rufaa kama Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete,
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali ya Mifupa MOI, Hospitali ya
Mloganzila na nyinginezo zinavyoboresha na kupanua wigo wa huduma za
kitaalamu zinazopatikana nchini, kama vile kufanya operesheni za moyo,
na kupandikiza figo. Kuongezeka kwa operesheni hizi kunahitaji damu
pamoja na mazao ya damu iliyo salama na ya kutosha, na yenye makundi
mbalimbali. Hivyo jitihada zinazofanyika za kuongeza makusanyo ya damu
zinaendana na azima ya Serikali kuhakikisha na kufanikisha huduma zote
za kibingwa zinatolewa hapa hapa nchini. Kipaumbele kwa Wizara ni
kuendelea kuboresha na kuimarisha huduma za kibingwa zitolewazo nchini
katika kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa ya matibabu nje ya
nchi ili kupunguza gharama kubwa ambazo serikali inaingia katika
kupeleka wagonjwa nje ya nchi.
Aidha,
katika mwaka wa fedha 2018/2019, Wizara itaboresha upimaji wa kuhakiki
usalama wa damu kwa kununua mashine za kisasa kupitia MSD na kusimikwa
katika vituo vyetu vya Kanda . Mashine hizi ‘full automated machines’
zitakuwa na uwezo wa kupima sampuli nyingi kwa wakati mmoja. Hii
itaongeza ufanisi katika upimaji wa maambukizi ya ukimwi, homa ya ini na
kaswende na zitarahisisha upatikanaji wa damu salama kwa wakati katika
vituo vya kutolea huduma.
Vile
vile, Wizara itanunua mashine za Apheresis nne (4), ambazo ni maalum na
kisasa zinazotumika kukusanya damu na kutengeneza mazao ya damu. Faida
za mfumo huu wa kutengeneza mazao ya damu kwa kutumia ‘Apheresis
Machine’ utasaidia mchangiaji damu mmoja kuchangia kati ya dozi 2 hadi 3
za chembe sahani “platelets” zilizo katika viwango vya ubora wa juu.
Tofauti na mfumo wa sasa ambao unahitaji wachangiaji 6 ili kupata dozi
moja ya chembe sahani. Aidha, mashine hizi za apheresis zitawezesha
upatikanaji wa mazao ya damu maalum yanayohitajika kutumiwa na madaktari
katika kutoa huduma za kibingwa mfano matibabu ya cancer, upasuaji wa
mishipa ya fahamu, moyo na upandikizaji wa figo.
Ndugu Wananchi,
Mpango
wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) umekuwa ukitekeleza mikakati mbalimbali
katika usimamizi wa viwango na ubora katika huduma ya damu, mkakati
mmojawapo ni kusajili Vituo Vyote vya Damu Salama vya Kanda kwenye
mchakato wa utambuzi wa Ithibati (Accreditation) kwa kutumia viwango vya
Shirika la Kimataifa la “Africa Society for Blood Transfusion” (AfSBT).
Mpaka sasa nina taarifa kanda mbili za Kaskazini-Kilimanjaro,
Mashariki-Dar-es-salaam, pamoja na Mpango wa Damu Salama Zanzibar,
zimefanikiwa kupata vyeti vya utambuzi rasmi kwa kufika daraja la pili
la Ithibati inayotolewa na “African Society for Blood Transfusion”
(AfSBT) yaani ‘’Step II Certification’’. Nachukua fursa hii kupongeza
Menejimenti na Wafanyakazi wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama kwa hatua
hii.
Ninatambua kupata cheti kuna manufaa
yafuatayo; ni uthibitisho kuwa serikali kupitia Mpango wa Taifa wa Damu
Salama sio tu unaongeza juhudi katika kukusanya damu lakini pia
unaendelea kuboresha ubora wa huduma ya damu salama. Kupata vyeti vya
utambuzi wa Ithibati utawezesha pia Huduma za Mpango wa Taifa wa Damu
Salama kutambulika Kitaifa na Kimataifa; lakini pia utawezesha wananchi
kupata huduma bora na kujenga imani kuwa Damu Salama inatoa huduma
zinazokidhi viwango vya hali ya juu.
Maelekezo
yangu kwa uongozi wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama; ni kuweka mikakati
na kuhakikisha vituo vinne (4) vilivyobaki; Kanda ya Ziwa-Mwanza, Nyanda
za Juu Kusini-Mbeya, Magharibi-Tabora na Kusini-Mtwara vinapata
utambuzi wa Ithibati daraja la pili pia, na hatimaye kupata cheti cha
Idhibati kwa huduma zote zinazotolewa na Mpango kwa maana ya kufikia
‘’Full Accreditation’’
Ndugu Wananchi,
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Mpango wa
Taifa wa Damu Salama umeanzisha Kikundi cha Wachangia Damu Wenye Kundi
Adimu la Damu (Rare Blood Group Donor Club) kama 0-negative,
A-negative, B-negative na AB-negative katika kila Mkoa . Lengo ni kuweka
msukumo na kuwakutanisha watu wenye kundi adimu la damu na
kuwahamasisha wawe wanachangia damu mara kwa mara ili Taifa liwe na
akiba ya kutosha ya damu.
Tunataka
kuhakikisha kuwa wagonjwa wenye kundi adimu la damu wanapata huduma za
matibabu sawa na wagonjwa wengine na kuhakikisha vifo vyinavyosababishwa
na ukosefu wa kundi adimu la damu vinapungua au havitokei kabisa. Hivyo
basi nitoe rai kwa wananchi ambao wana kundi adimu la damu watuunge
mkono na kujiunga katika klabu hizi. Vile vile, niwaombe Mashirika,
Taasisi mbalimbali na vyombo vya habari kuwaelimisha wananchi wote wenye
makundi adimu ya damu juu ya umuhimu wa kujiunga katika klabu hizi.
Ndugu Wananchi,
Kabla
sijahitimisha napenda kutoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Marekani
kupitia Shirika la Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Centres for Disease
Control and Prevention (CDC), Mfuko wa Dunia wa Magonjwa ya UKIMWI,
Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund), Shirika la Maendeleo ya Korea
Kusini (KOICA) kwa kuendelea kugharimia uimarishaji wa Mpango wa Taifa
wa Damu Salama hapa nchini katika masuala ya mfumo wa TEHAMA, viwango na
ubora na mchakato wa Ithibati (Accreditation), upatikanaji wa vifaa
tiba (equipments and reagents) na mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi.
Pia nawashukuru wahisani na wadau wengine ambao kwa njia moja au
nyingine wanaendelea kusaidiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama katika
kuhakikisha damu inapatikana nchini.
Pia
napenda kutambua jukumu na umuhimu wa vyombo vya habari katika juhudi
zetu za pamoja za kuelimisha, kuhamasisha na kuongeza idadi ya wachangia
damu wa hiari bila malipo.
Napenda
kuvisihi vyombo vya habari kuendelea kushirikiana na Mpango wa Taifa wa
Damu Salama, kujenga ufahamu wa umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari,
ili wananchi ambao wamekuwa na imani potofu kuhusu kuchangia damu
wabadili imani zao na tabia, ili nao waanze kuchangia damu kwa hiari.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
CHANGIA DAMU, OKOA MAISHA
0 on: "HOTUBA YA MHESHIMIWA UMMY A. MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KWENYE SHEREHE YA MAADHIMISHO YA SIKU YA WACHANGIA DAMU DUNIANI MKOANI DODOMA"