Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akieleza jambo mbele ya Waandishi wa Habari (Hawapo
kwenye picha) wakati akitoa tamko kuhusu ugonjwa wa Chikungunya, Dengue na
Ebola katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es salaam. Kushoto kwake ni
Katibu mkuu wa Wizara ya Afya Idara Kuu ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya na Kulia
ni Mkurugenzi Mkazi kutoka shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Adiele Onyeze.
Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbali mbali
wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Mhe.Ummy Mwalimu kuhusu ugonjwa wa Chikungunya, Dengue na Ebola katika
ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es salaam.
SERIKALI
YATOA TAADHARI KWA WANANCHI JUU YA UWEPO WA UGONJWA WA CHIKUNGUNYA NCHINI.
Na WAMJW - DSM
Serikali kupitia Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa tahadhari kwa wananchi
juu ya kuingia kwa ugonjwa wa Chikungunya nchini baada ya watu wanne
waliotokea nchini Kenya kubainika kuwa
na dalili zinazofanana na ugonjwa huo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu mapema leo
jijini katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es salaam wakati akiongea na
waandishi wa Habari.
“Mnamo tarehe 20, Mwezi
Juni, 2018 wasafiri wanne wa familia moja waliotokea tena Mombasa nchini Kenya
walishukiwa kuwa na ugonjwa huu baada ya kuwa na dalili zinazofanana na ugonjwa
wa homa ya Chikungunya kwenye kutuo cha mpakani cha Holili kilichopo wilayani Rombo mkoani Kiliamanjaro”, alisema
Mhe. Ummy
Waziri Ummy aliwatoa hofu wananchi kuwa Ugonjwa huu si mpya katika
nchi yetu kwani hapa nchini uligundulika
katika maeneo ya Kusini mwa Tanzania, sehemu za Makonde katika mpaka wa
Tanzania na Msumbiji mnamo mwaka 1952 huku
Jina la ugonjwa likiwa na asili ya Kimakonde lenye maana ya
“kilichopinda” yaani hali ya kupinda
mwili inayotokana na maumivu makali ya viungo kunakosababishwa na ugonjwa huu.
Kwa upande mwingine Mhe.
Ummy alithibitisha juu ya kuwepo kwa ugonjwa wa Dengue nchini hususani katika
jiji la Dar es salaam huku idadi
ya wagonjwa ambao wamethibishwa kwa kipindi cha Januari hadi Mei ni 226 ambao
wanatoka katika mkoa wa Dar es Salaam.
‘Dengue ulithibitishwa kuwepo hapa nchini hususani jijini Dar es Salaam
kuanzia mwishoni mwa mwezi wa Januari 2018. Hadi kufikia sasa idadi ya wagonjwa
ambao wamethibishwa kuwa na ugonjwa huu kwa kipindi cha Januari hadi Mei ni 226
ambao wanatoka katika mkoa wa Dar es Salaam.
Vilevile ugonjwa huu si mpya hapa nchini kwani umewahi kuripotiwa katika
miaka ya 2010, 2013 na 2014” alisema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy ameeleza
dalili za ugonjwa wa Dengue zinashabihiana amabazo ni pamoja na homa ya ghafla, kuumwa kichwa, maumivu
ya viungo na uchovu. Dalili hizi huanza kujitokeza siku ya 3 hadi 14 tangu mtu
alipoambukizwa virusi vya magonjwa haya. Wakati mwingine dalili za magonjwa
haya yanaweza kufanana sana na dalili za ugonjwa wa malaria. Vilele mara
nyingine magonjwa haya yanaambatana na kutokwa na damu
sehemu za fizi, mdomoni, puani, kwenye macho na pia kwenye njia ya haja kubwa
au ndogo.
Kwa upande
mwingine Waziri Ummy amethibitisha kuwa hadi sasa nchini Tanzania
hakuna mgonjwa yoyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya Ebola,
huku kwa tathmini ilifanyika na Shirika la Afya Duniani (Regional Risk
Assessment) imesema kuwa Tanzania ipo kwenye uwezekano wa kupata ugonjwa wa
Ebola na imewekwa katika kundi la pili miongoni mwa nchi 6 zilizo katika hatari
ya kupata maambukizi zaidi, kutokana na kupakana na nchi ya DRC pamoja na mwingiliano
mkubwa wa watu wake.
Pia Mhe. Waziri amewatoa hofu Wananchi na
kuwataka kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huu kwani mpaka
sasa hakuna mtu aliyethibitishwa kuugua ugonjwa huu hapa nchini, huku akiwaonya
wanaosambaza taarifa za uzushi juu ya uwepo wa ugonjwa huu na kuwataka waache
haraka.
Aidha, Wizara itaendelea kushirikiana na
Sekta mbalimbali katika kuimarisha ufuatiliaji na kuendelea kutekeleza mikakati
ya kudhibiti ili ugonjwa huu usiingie nchini na kuendelea kutoa taarifa pamoja
na Elimu kwa Jamii kadri itakavyohitajika.
0 on: "SERIKALI YATOA TAADHARI KWA WANANCHI JUU YA UWEPO WA UGONJWA WA CHIKUNGUNYA NCHINI"