Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akielezea jambo mbele ya Wadau
wa Afya, mashirika yasiyo Yakiserikali, na Serikali katika kikao kilichofanyika
katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam.
Afisa kutoka kitengo cha
Elimu ya Afya kwa umma Wizara wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Dkt. Amalbega Kasangala akiwasilisha taarifa mbele ya mgeni rasmi Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu(hayupo
kwenye picha).
Wadau wa Afya, mashirika
yasiyo Yakiserikali, Watumishi wa Serikali na Waandishi wa Habari wakifuatilia
taarifa kutoka kwa mgeni rasmi Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu(hayupo kwenye
picha), katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu
Nyerere jijini Dar es salaam.
Na WAMJW. Dar es salaam.
SERIKALI kupitia Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatarajia kuwa na watoa
huduma wa Afya ngazi ya jamii (CHWz) Zaidi ya 30,000 ifikapo mwaka 2020 katika
vijiji Zaidi ya 15,000 nchini.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu katika
Mkutano wa Wadau wa Afya, mashirika yasiyo Yakiserikali, na Serikali katika
ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.
“Tunataka itakapofika mwaka
2020, tuwe na angalau Wahudumu wa Afya zaidi ya 30,000 katika vijiji Zaidi ya
15,000 tulivyonavyo Tanzania, Eneo hili tumeliona ni eneo muhimu kwasababu
tutapata matokeo ya haraka, ni bora kutumia Bilioni 40 kwa ajili ya kinga ya
magonjwa kwa Watanzania .” Alisema Mhe. Ummy Mwalimu.
Mhe. Ummy alisema kuwa lengo
la Mkutano huo ni kujadiliana na Wadau wa Maendeleo na Mashirika yasiyo
Yakiserikali juu ya kuimarisha huduma ya Afya ya msingi hasa katika kuwakinga
wananchi dhidi ya maradhi kupitia mikakati ambayo inakubalika kimataifa ya kuwa
na watoa huduma katika ngazi ya jamii.
“Kisera tumesema kuwa
tunataka kuwa na watu wawili ambao watakuwa wanafanya kazi kama watoa huduma za
Afya na kazi yao kubwa haitakuwa kutibu bali itakuwa ni kusisitiza masuala ya
lishe, masuala ya uzazi wa mpango, kuhimiza watu kujua hali zao hasa katika maambukizi
ya VVU na kuwaelekeza waende maeneo gani ili kupata huduma za Afya” alisema
Mhe. Ummy
Kwa upande mwingine Mhe. Ummy
Mwalimu aliwashukuru wadau wa maendeleo na Mashirika yasiyo Yakiserikali kwa
kuwa tayari kushirikiana na Serikali katika kufanikisha kuwa na watoa huduma za
Afya ngazi ya jamii kwa idadi yakuridhisha ifikapo 2020.
Hata hivyo Waziri Ummy
alisema kuwa rasilimali watu katika Sekta ya Afya nchini ni Asilimia 51, huku
kukiwa na upungufu wa watoa huduma za Afya kwa Asilimia 49, ambao ni pamoja na
Madaktari, Wauguzi, Wataalamu wa Maabara, huku mikoa ambayo inaupungufu Zaidi
ni Katavi, Rukwa, Tabora, Kigoma na Kagera.
Naye, Afisa kutoka kitengo
cha Elimu ya Afya kwa umma Wizara wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Dkt. Amalbega Kasangala alisema Serikali kuwa Serikali imejipanga katika
kukinga ugonjwa kuliko kutibu jambo ambalo litasaidia katika kupunguza gharama
kwa wananchi.
0 on: "SERIKALI YATARAJIA KUWA NA WATOA HUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII ZAIDI YA 30,000 "