Na WAMJWW. Dom
Serikali
imejipanga kutumia tiba mtandao kuboresha huduma za afya nchini kwenye
hospitali zote za ngazi ya taifa, rufaa na wilaya ili kuwawezesha
wagonjwa waishio sehemu mbali mbali nchini kupata huduma za afya kwa
wakati na kwa ufanisi.
Hayo
yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati akifungua
kongamano la ubunifu na utekelezaji wa huduma za tiba mtandao Tanzania
lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa jengo la LAPF, Dodoma.
Dkt.
Ulisubisya amesema kuwa lengo la kongamano hilo ni kuwakutanisha
watendaji wakuu wa hospitali za taifa nchini, madaktari bingwa wa sekta
ya Afya, wakuu wa taasisi zinazoshughulika na sekta ya Afya, Wizara ya
TAMISEMI, Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano; taasisi nyingine za Serikali;
sekta binafsi na wabia wa maendeleo ili kujadiliana na kuwa na uelewa
wa pamoja wa kufanikisha utekelezaji wa huduma za tiba mtandao ili
kuboresha huduma za afya nchini.
Amesema
kuwa tiba mtandao itawezesha na kuongeza ufanisi katika kufanya
uchunguzi, utoaji wa tiba na madawa kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na
magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza na yanayotokana na ajali za
barabarani.
“Hadi hivi sasa ni asilimia 37 tu ya wagonjwa wa kifua kikuu
ndio wanaotambulika na kupatiwa huduma na Wizara ya Afya katika
hospitali mbalimbali nchini. Hivyo, tiba mtandao itawezesha upatikanaji
wa wagonjwa na ufikishaji wa huduma kwao kwa wagonjwa wengine asilimia
63”, alifafanua Dkt. Ulisubisya.
Aliongeza
kuwa tiba mtandao itapunguza gharama za wagonjwa na wanaowahudumia
kusafiri kufuata madaktari. Aidha, amewataka wakuu hao wa taasisi
kuwaruhusu wataalamu wao, wa Wizara ya TAMISEMI na wa Wizara ya Afya,
kushiriki mafunzo ya tiba mtandao ili kuongeza ufanisi wao katika
kuhudumia wagonjwa.
Amewataka
wataalamu wa afya na wakuu wa taasisi zinazohusika na masuala ya afya
kununua vifaa tiba vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
vyenye viwango na ubora unaohitajika ili kuwezesha tiba mtandao na
manunuzi hayo yazingatie na kufuata ununuzi wa pamoja wa huduma na
bidhaa za Serikali.
Vifaa vya kisasa vya TEHAMA vinavyohusika na tiba
mtandao vitawawezesha wataalamu kufanya uchunguzi kwa mgonjwa, kupata
majibu ya uhakika na kumpatia mgonjwa tiba inayostahili na ya uhakika.
Aidha, amemuelekeza Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote
(UCSAF), Eng. Ulanga, ambao ndio waanadaji na waratibu wa kongamano
hilo, kushirikiana na TTCL kuhakikisha kuwa tiba mtandao inapatikana
katika hospitali zote za rufaa na hospitali ambazo zina changamoto ya
kijiografia ya kufikika kwa urahisi.
0 on: " TIBA MTANDAO KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI"