Mkurugenzi wa idara ya dharura hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt.Juma Mfinanga akipokea kitabu hicho cha mafunzo kutoka kwa Katibu Mkuu Dkt.Mpoki Mara baada ya kukizindua |
Picha ya Pamoja ya watumishi toka wizara ya Afya, hospitali, Shirika la msalaba Mwekundu, Chuo kikuu MUHAS Pamoja na majeshi ambao kwa Pamoja watatekeleza mpango huo nchini. |
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema kuwa moja ya sababu za ajali barabarani, ni uchovu wa madereva.
Dkt. Mpoki ameyasema leo Novemba 13,2018 wakati wa kufungua mafunzo ya watoa huduma za tiba, uokoaji na usafirishaji wa majeruhi wa ajali na wagonjwa wenye dharura mbalimbali nje ya Hospitali nchini.
Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, Dkt. Mpoki amelitaka jeshi la Polisi nchini kuangalia namna ya kuweka utaratibu wa madereva kubadilishana kwani suala la uchovu linachangia kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani.
Aidha,akitolea mfano suala la uchovu, dereva kutoka Mwanza au Bukoba kwenda Dar es Salaam, basi ashuke Singida ili aingie dereva mwingine kumalizia safari na hiyo itasaidia kuepusha ajali.
“Tumemuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi atusaidie kama mchango wa Polisi katika kupunguza ajali kwa kuhakikisha kwamba wanaweka utaratibu wa madereva wanaendesha kwa muda maalum. Kuliko ilivyo sasa madereva wanaweza kuendesha siku nzima, Hivyo wanakuwa wachovu na kuchangia kwa kiasi kikubwa sana ajali mbalimbali barabarani” amesema Dkt. Mpoki.
Hata hivyo ameeleza kuwa, mpango huo ni hatua ya kwanza ambayo Serikali imewekeza kuingilia kati pale watu wanapokuwa wameumia, ambapo huko nyuma maisha ya watu wengi yalikuwa yakipotea kwa sababu vifaa vilikuwa vinachelewa sana kufika mahali tukio na hivyo kushirikiana na Benki ya dunia kwa kutenga kiasi cha shilingi Bilioni 8 kwa ajili ya uwekezaji na shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kuendesha shughuli za kila siku za wataalam.
“Katika fani ya tiba, Tunazungumzia saa ya kwanza ni saa muhimu sana kusaidia mtu aliyepata changamoto ya ajali. Hawa watakuwa chachu ya kusaidia kati ya wale waliopata mafunzo.” Amesema Dkt. Mpoki
Dkt. Mpoki ameongeza kuwa katika afua hiyo,itakuwa na vituo maalum vyenye miundombinu ya kutoa huduma hizo ambapo awamu ya kwanza itaanzia Dar e Salaam hadi Ruaha Mbuyuni na kwa kila kituo kutakuwa na gari la kubebea wagonjwa, vifaa vya zima moto na kuweka utaratibu wa kusafirisha majeruhi kwa kushirikiana majeshi yakiwemo la Jeshi la Wananchi (JWTZ), Polisi, Zimamoto pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD).
Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma (MUHAS), Profesa Appolenary Kamuhabwa amesema mafunzo hayo ni muhimu sana kwani kutakuwa na mfumo thabiti wa kuwahudumia wagonjwa wa dharura watokanao na ajali na ni hatua muhimu kwani bila afya bora, wananchi hawawezi kutumikia nchi hususani ajenda ya Serikali ya viwanda.
Profesa Kamuhabwa amesema katika mpanguo huo, utakuwa na vituo mbalimbali vya Afya vitakavyokuwa vikitoa huduma za dharura ikiwemo: Vituo vya Afya vya Kimara (Dar es Salaam), Tumbi, Chalinze (Pwani), Mikese, St, Kizito, Doma-Mikumi (Morogoro) na Ruaha Mbuyuni (Iringa).
0 on: "DKT. MPOKI AELEZA UCHOVU NI SABABU ZA AJALI ZA BARABARANI"