Picha ya Pamoja ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya katika baada ya kikao cha Maafisa Afya wa Mkoa, Halmashauri pamoja na Wadau wa Mazingira kilichofanyika leo jijini Dodoma.
NA WAJMW-DODOMA
Madereva wa mabasi yaendayo mikoani na abiria wametakiwa
kuacha tabia ya kujisaidia “Kuchimba dawa” katika maeneo yasiyo rasmi ili
kutunza na kuepuka uharibifu wa mazingira unaoweza kujitokeza ikiwa ni pamoja
kusababisha magonjwa ya milipuko.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati akifungua
mkutano unaojumuisha Maafisa Afya kutoka mikoa na Halmashauri mbalimbali nchini
pamoja na wadau wa mazingira, katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.
Dkt. Mpoki amekemea tabia hiyo hatarishi kwa ustawi wa
mazingira huku akiwataka maafisa Afya na wadau wa mazingira nchini kusimamia
afua zilizowekwa zinaendelea kutekelezwa ili kulinda mazingira ambayo
yanatuzunguka.
“Kuna watu wengine nimeshawahi kuwaona kwenye basi wanatupa
taka ovyo na mabasi mengine yanasimama porini ili abiria wajisaidie, hii tabia
siyo nzuri na inatakiwa ikemewe kwa nguvu zote, Dkt. Subi na wenzake wanakuja
na mpango mkakati wa kuondoa kabisa
dhana ya watu kusimama kujisaidia porini, sisi tunatakiwa kuwa msitari wa mbele
kupiga marufuku mabasi kusafiri bila kuchafua
mazingira”.
Dkt. Mpoki amesema ni aibu kubwa kwa taifa kuona watu
hawafuati kanuni za usafi huku akiwataka Maafisa Afya kuhakikisha wanafanya
kazi kwa nguvu ili ionekane kuwa kero kwa watu wengine na watakaobainika
kuchafua mazingira wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria.
Aidha, Dkt. Mpoki ameongeza kuwa jamii inatakiwa kuzingatia
matumizi ya vyoo bora na kunawa mikono mara baada ya kujisaidia ili kuepuka
magonjwa ya milipuko yanayoweza kusababishwa na tabia ya uchafu ikiwa ni pamoja
na kuacha tabia ya kujisaidia ovyo porini ili kaulimbiu ya “Nyumba ni Choo” iweze
kutekelezwa ipasavyo kwa kujenga vyoo vya kisasa katika maeneo mbalimbali ili
huduma ipatikane mahala pote.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi amesema takwimu
zinaonesha kaya zilizokua na vyoo bora mwaka 2012 zilikua asilimia 19.5 lakini
hivi sasa nchi nzima kaya zenye vyoo bora ni asilimia 51.4.
Dkt. Subi amesema kutokana na takwimu hiyo inaonesha kuna mafanikio
katika uhamasishaji kwa jamii kutumia vyoo bora na kuacha kutumia vyoo ambavyo
havina viwango na salama kwa matumizi, na badala yake serikali inaendelea kutoa
elimu na kusisitiza jamii kutumia vyoo bora ili kuepuka magonjwa yanayoweza
kuzuilika ikiwemo kipindupindu, magonjwa ya tumbo na kuhara.
Pamoja na hayo, maafisa Afya wametakiwa kuongeza nguvu
katika kutoa elimu kwa umma, kuhamasisha usafi wa mazingira na kufukia maeneo
ya mazalia ya vimelea vya ugonjwa wa Malaria ili kutokomeza ugonjwa huo ambao
umekua hatari kwa jamii hasa kwa wanawake wajawazito na watoto.
Mkutano huo unaojumuisha Maafisa wa Afya nchi nzima una
lengo la kutoa elimu na kubadilishana uzoefu wa kufanya kazi lakini msisitizo
mkubwa ikiwa ni utunzaji wa mazingira na kuzingatia kanuni bora za afya pamoja
na usafi wa mazingira na usafi na afya ya binadamu.
|
0 on: "DKT. MPOKI AKEMEA TABIA YA ABIRIA NA MADEREVA KUCHIMBA DAWA MAENEO YASIYOHUSIKA"