Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Ijumaa, 23 Novemba 2018

WAZIRI MKUU AWAAGIZA MAAFISA TAWALA KUSIMAMIA UJENZI WA VYOO BORA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. kassim Majaliwa akifuatilia maelekezo katika banda la Hedhi salama  wakati wa mkutano wa Maafisa Afya wa Mkoa, Halmashauri na Wadau wa Usafi nchini uliofanyika leo jijini Dodoma.


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. kassim Majaliwa (wakwanza kulia) akiwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wakatikati) pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii Mhe. Peter Selukamba wakifuatilia kikundi cha ngoma cha Mpoto (hawapo kwenye picha) wakati wa mkutano wa Maafisa Afya wa Mkoa, Halmashauri na Wadau wa Usafi nchini uliofanyika leo jijini Dodoma.Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. kassim Majaliwa akimkabidhi Afisa Afya wa Mkoa wa Iringa zawadi ya Bodaboda wakati wa mkutano wa Maafisa Afya wa Mkoa, Halmashauri na Wadau wa Usafi nchini uliofanyika leo jijini Dodoma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. kassim Majaliwa akisikiliza maelezo kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu namna ya matumizi ya choo pindi walipopita katika mabanda ya maonesho, wakati wa mkutano wa Maafisa Afya wa Mkoa, Halmashauri na Wadau wa Usafi nchini uliofanyika leo jijini Dodoma.


Makatibu Tawala wa Mikoa, Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini wametakiwa  kusimamia vizuri kampeni ya ujenzi wa vyoo bora kwa kutimiza lengo la kila familia na jamii inakuwa na vyoo vya kisasa hadi kufikia Disemba 31 mwaka huu.

Hayo yamesemwa leo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati akifunga mkutano wa maofisa afya wa Mikoa, Halmashauri na Wadau wa usafi Tanzania uliyofanyika jijini hapa.

Mhe. Majaliwa amesema kwamba ujenzi wa vyoo vya kisasa katika kila kaya utasaidia kupunguza uwezekano wa magonjwa ya milipuko ambayo yanaweza kutokea kwa sababu ya kutokuwa na vyoo bora.

“Nawataka mtumie mbinu yeyote ili kuwawezesha hawa Maofisa Afya katika kutoa elimu  kwa wananchi ili suala la ujenzi wa vyoo bora liweze kutekelezeka na hata kutimiza wajibu wao wa kila siku”. Alisema Waziri Mkuu.

Hata hivyo Waziri Mkuu aliwataka wananchi  kutunza mazingira kwa kufuata kanuni bora za afya ikiwa ni pamoja na matumizi ya vyoo bora na vya kisasa ambapo alisema kutumia kampeni hiyo imewezesha kupunguza idadi ya kaya zisizokuwa na vyoo kutoka asilimia 9.5 mwaka 2015 hadi asilimia 3.8 mwaka 2018.

“Serikali ya awamu ya tano inaendelea kusisitiza juu ya uhifadhi wa mazingira na nyinyi wataalamu wa afya mnaombwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kuelimisha umma juu ya utunzaji wa mazingira ili kutekeleza dhana ya Tanzania ya viwanda kwa kutunza vyanzo vya maji na kutumia vyoo bora”. Alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Aidha, amewataka maafisa afya nchini kote kuhakikisha hakuna mfumo mbovu wa utililishaji maji kutoka viwandani na kutaka sheria ya utunzaji mazingira ya mwaka 2004 inatekelezwa ipasavyo ikiwa na kuhakikisha watumishi wa viwanda wanakua na mfumo wa utunzaji wa afya zao.

“Ninaagiza uwepo wa miundombinu ya ujenzi wa vyoo bora, sehemu ya kunawa mikono kwa maji safi na sabuni kwa taasisi zote za umma na binafsi, vituo vya afya, shule zote, vituo vya abiria na nyumba zote za ibada kabla ya Aprili 30 mwaka 2019.

Kuhusu tabia ya uchimbaji dawa wakati wa safari ambayo hivi sasa imeota mizizi, Waziri Kassim Majaliwa amesema kuwa hivi sasa serikali pamoja na watu binafsi wamejenga na kutoa huduma za vyoo katika vituo maalum, vituo vya kuuzia mafuta, hoteli pamoja na maeneo ya umbali mrefu hivyo kuwataka Maofisa Afya kuwachukulia hatua kali wale wote wanaogundulika wanachimba dawa sehemu ambazo siyo rasmi au zilizotengwa na hiyo itasaidia  kuondoa kero za uchafuzi wa mazingira kwa kuchimba dawa porini.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema katika awamu ya pili ya kampeni ya taifa ya usafi wa mazingira ya mwaka 2016/2021 wizara yake imepanga kuhakikisha asilimia 75 ya kaya nchini zinakua na vyoo bora  na kwamba kuondoa kaya ambazo hazina vyoo kabisa.

Alisema kwa upande wa shule, lengo ni kujenga miundombinu ya usafi na huduma za maji kwenye shule za msingi 3,500 na 700 za sekondari.
”Na kwa upande wa vituo vya tiba tunapanga kufikia vituo 1,000 hivyo kwa bajeti ya mwaka 2018/2019  tumejenga vyoo vipatavyo 700”. Alisistitiza Waziri Ummy.

Katika mkutano huo ambao uliambatana na maadhimisho ya wiki ya usafi wa mazingira kitaifa ambapo kulitangazwa washindi wa mashindano ya usafi na  Halmashauri ya Njombe iliibuka mabingwa kwa miaka mitatu mfululizo katika kundi la halmashauri za miji, wilaya, vijiji, shule za msingi za vijijini pamoja na shule za sekondari za bweni za  serikali na binafsi.
-Mwisho-


0 on: "WAZIRI MKUU AWAAGIZA MAAFISA TAWALA KUSIMAMIA UJENZI WA VYOO BORA"