Kaimu Meneja Kituo cha Damu Salama Bw. Richard Komanga akiwasilisha taarifa ya kituo kwa Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile (hayupo pichani)
Moshi, Kilimanjaro
Vituo vya ukusanyaji damu salama nchini vyatakiwa kuboresha
huduma zaidi katika ukusanyaji wa damu na kuwa na benki ya damu itakayowasaidia
wenye uhitaji muda wote bila kutegemea ndugu au jamaa wa mgonjwa kuchangia
damu.
Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Dkt.Faustine Ndugulile alipotembelea kituo cha
ukusanyaji damu salama kanda ya kaskazini kinachohudumia mikoa ya Kilimanjaro,
Arusha, Tanga na Manyara.
“Tangia tumeanzisha mpango huu wa ukusanyaji wa damu salama
mwaka 2004 ukuaji wake umekuwa ni wa kusuasua naona bado hatujapiga hatua sana”
alisema Dkt Ndugulile na kuendela “Zipo changamoto katika upimaji
wa damu, huku idadi ya damu salama inayokusanywa ikiwa ni ndogo kulinganisha na
uhitaji uliopo”
Dkt. Ndugulile amesema kuwa Serikali kupitia Bohari ya Dawa
(MSD) imetenga bajeti ya kununua vitendea kazi vya kisasa vitakavyosaidia vituo
vya ukusanyaji wa damu salama kukusanya kiasi kingi cha damu ndani ya muda
mfupi na kuitaka bohari ya dawa kushughulikia suala hilo haraka ili vituo hivyo
vipate vifaa hivyo haraka.
Aidha Dkt. Ndugulile amekiri kuwa kazi ya ukusanyaji wa damu
salama hugharimu muda mrefu na fedha nyingi huku damu salama inayokusanywa
ikiwa ni kidogo kulishanginsha na muda na gharama zinazotumika na kuwtaka
watendaji toka Vituo vya ukusanyaji wa damu salama kuja ma mifumo
itakayowawezesha kutumia muda na rasilimali fedha kidogo katika ukusanyaji wa
damu salama huku kiwango cha ukusanyaji kikiongezeka.
“Hiki ni kituo cha kanda, ni lazima tuongeze kasi ya
ukusanyaji wa damu. Haiwezekani kwa kituo hiki kuwa na damu uniti 70, kiwango
hiki bado ni kidogo huku gharama za ukusanyaji bado zipo juu” alisema DKt.
Ndugulile
Aidha Dkt. Ndugulile amevitaka vituo vyote vya upimaji wa
damu salama nchini kutoa majibu ya vipimo kwa haraka na kuacha mara moja
urasimu wa kuchelewesha matokeo ya vipimo vya damu. “tuhakikishe sasa tunaweka
mifumo mizuri kuhakikisha damu zinazokusanywa katika vituo vyetu vinatoa majibu
kwa haraka ili damu hizo ziweze kutumika kwa walengwa waliokusudiwa.
Hata hivyo Dkt. Ndugulile amesema kuwa zipo changamoto
katika uhifadhi wa damu salama na Serikali katika bajeti ya mwaka huu wa fedha
2018/19 imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo 10 vya uhifadhi wa damu
salama katika hospitali za rufaa za mikoa huku huku upimaji ukiwa bado
unafnayika kwa ngazi ya kanda na kuvitaka vituo vinayohusika na upimaji na
uhifadhi wa damu salama kuboresha mifumo ya usafirishaji wa damu salama ili
damu ziweze kupimwa kwa haraka na kurejeshwa haraka kwa ajili ya matumizi.
Awali akiwasilisha taarifa yake, Kaimu Meneja Kituo cha
Ukusanyaji wa Damu Salama Kanda ya Kaskazini Bw. Richard Komanga, amesema kuwa
Kituo hicho cha ukusanyaji wa damu salama huhusisha timu 36 zilizojengwa uwezo
wa ukusanyaji wa damu katika ngazi za Halmashauri na Mikoa 4 iliyopo katika
Kanda ya kaskazini ambapo wananchi huchangia damu bila malipo. Kituo hicho pia
hupima damu zenye maambukizi ambapo damu hupimwa magonjwa ya homa ya ini (b),
(c) kasendwe na Virusi Vya Ukimwi.
|
0 on: "VITUO VYA DAMU SALAMA VYATAKIWA KUBORESHA HUDUMA"