Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema serikali ina mpango madhubuti wa
kuhakikisha wamama wajawazito hawawaambukizi watoto walio tumboni Virusi vya
Ukimwi na kipindi wanapozaliwa.
Waziri Ummy amesema hayo leo wakati wa uzinduzi wa
machapisho ya uchambuzi wa bajeti katika sekta ya maendeleo ya jamii ikiwa ni
pamoja na masuala ya lishe, uliofanyika katika ukumbi wa Hazini, Jijini Dodoma.
Waziri Ummy amesema hadi hivi sasa asilimia 99 ya
wajawazito wenye maambukizi ya VVU wanapewa huduma za kumkinga mtoto asipate
maambukizi hayo huku la serikali ifikapo mwaka 2020 ni kuhakikisha hakuna mtoto atakayezaliwa na maambukizi ya VVU.
“Sasa hivi asilimia 99 ya wanawake wajawazito wote
wenye maambukizi ya VVU tumewaingiza
katika mpango wa dawa, na hiyo asilimia moja bado hatujawafikia ila kwa nguvu
na msukumo tuliouweka juzi wa kuwasainisha Wakuu wa Mikoa kwenda kufuatilia
masuala ya afya ya mama na mtoto, tunaamini hakuna mtoto yeyote Tanzania
atakayezaliwa na maambukizi ya UKIMWI”. Amesema Waziri Ummy.
Katika Uzinduzi huo, Waziri Ummy ameipongeza
Wizara ya Fedha na Mipango kupitia kwa Waziri wake Mhe. Dkt. Philipo
Mpango inavyojikita katika mipango ya
kuendeleza wanawake na watoto kwa kutoa huduma bora za afya, elimu, maji na
masuala ya maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na
Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) imefanya uchambuzi wa bajeti katika sekta
mtambuka ya jamii, hususani katika elimu, afya, Virusi vya Ukimwi, maji, usafi
wa mazingira na lishe kwa lengo la kuboresha upangaji na utekelezwaji wa
masuala ya mama na mtoto.
Pamoja na hayo, uzinduzi wa machapisho hayo
umelenga kupunguza tatizo la lishe linalosababisha udumavu kwa watoto walio
katika umri mdogo. Ambapo katika ripoti iliyotolewa katika mkutano wa IMF na
Benki ya dunia uliofanyika nchini Indonesia mwezi Oktoba mwaka 2018, inaonesha
Tanzania inashika nafasi ya 128 kati ya nchi 157 duniani katika kipimo cha
ubora wa nguvukazi katika uwekezaji wa
rasilimali watu hususani katika sekta ya afya na elimu ya lishe.
Kufuatia hali hiyo, Tanzania inaonekana kuwa na
matatizo ya udumavu, elimu ya lishe na afya kwa watoto wenye umri mdogo ambapo
serikali inafanya kazi kubwa ya kuhakikisha elimu ya lishe inawafikia wazazi na
jamii kwa ujumla ili kupambana na tatizo la udumavu. Na kufikia mwaka 2015
tatizo la udumavu limeshuka kutoka asilimia 34 kutoka asilimia 42 mwaka 2010.
Alisema Waziri huyo.
Tatizo la lishe limeonekana kupungua nchini huku
viashiria vya tatizo hilo vikipungua ambavyo ni uzito pungufu umeshuka kutoka
asilimia 16 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 14 mwaka 2015/16, pamoja na
ukondefu wa mwili kuendelea kubakia chini ya asilimia 5 kwa mwaka 2015/16.
0 on: "SERIKALI YAJIPANGA KUTOKOMEZA MAAMBUKIZI YA VVU KWA WATOTO WACHANGA."