Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumapili, 4 Novemba 2018

WANANCHI SASA KUANZA KUJICHAGULIA VIFURUSHI VYA HUDUMA YA BIMA YA AFYA NCHINI





Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari (Hawapo pichani) wakati alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Manyara kuona huduma zinazotolewa hapo. Kulia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Catherine Magali.
 
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akimkabidhi Mwenyekiti wa kamati ya mkoa wa Manyara ya kudhibiti ukatili dhidi ya watoto wa kike Bw. Anza Amen Ndosa miongozo ya utendaji wa kamati hiyo.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisalimiana na wazee wanaolelewa katika kituo cha kulelea wazee cha Sarame kilichopo wilaya ya Babati mkoani Manyara.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akimulekeza mbunge wa Babati vijijini, Jitu Son alama ambazo zimewekwa katika dawa za serikali ili kuzilinda kuuzwa katika maduka ya watu binafsi. Kulia ni mkuu wa wilaya ya Babati Elizabeth Kitundu.

WANANCHI SASA KUANZA KUJICHAGULIA VIFURUSHI VYA HUDUMA YA BIMA YA AFYA NCHINI 

Na.WAMJW-BABATI
 
Serikali imesema ina mpango wa kuanzisha huduma ya bima ya afya ambayo itamwezesha mwananchi kujichagulia “Kifurushi” kulingana na uwezo wake.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati alipokua akiongea na wafanyakazi wa kituo cha afya cha Magugu pamoja na wananchi wa kata ya Magugu iliyopo wilayani Babati katika mkoa wa Manyara, wakati alipotembelea kituo hicho cha afya.

Dkt. Ndugulile amesema, kutokana na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, serikali sasa chini  ya Wizara ya Afya,  imeamua kutengeneza mkakati mpya wa huduma za bima za afya zitakazokidhi mahitaji ya wananchi kulingana na kipato chao.

“Serikali imeanza mchakato wa mkakati mpya wa bima za afya utakaokua na vifurushi viwili, kimoja kinaitwa Jipimie na kingine Dunduliza ambavyo vitaanza hivi karibuni ambapo Vifurushi hivi vimelenga wananchi wa vipato tofauti, ambapo katika kifurushi cha Jipimie mwananchi ana uwezo wa kuchagua aina ya gharama za huduma za bima ya afya kulingana na kipato chake. Lakini katika kifurushi cha Dunduliza mwananchi atakua na wigo mpana wa kulipa kidogo kidogo kifurushi chake atakachoona kinafaa lakini akiwa anapewa huduma za bima ya afya kama kawaida”. Amesema Dkt. Ndugulile.

Katika kuboresha huduma za afya nchini, Dkt. Ndugulile amesema serikali ina mkakati wa kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na bima ya afya ifikapo mwaka 2020. Na itakua ni lazima na siyo jambo la hiyari kwa sababu magonjwa huwa hayana hodi yanapompata mtu, hivyo kupelekea wananchi wengi kushindwa kugharamia matibabu kwa sababu wanakua hawajajiandaa kukabili changamoto za kugharamia matibabu.

Pamoja na hayo Naibu waziri huyo alionekana kutoridhishwa na hali ya utoaji huduma  kituo cha afya cha Magugu huku ujenzi wa wodi, maabara na nyumba za watumishi ukichelewa pamoja na kwamba serikali ilipeleka Shilingi Milioni 400 za ukarabati na ujenzi wa majengo mapya.

Aidha, Dkt. Ndugulile alionekana kuchukizwa na baadhi ya watoa huduma za afya kituoni hapo kuwaandikia wagonjwa kununua dawa katika maduka binafsi wakati dawa hizo zikiwepo katika stoo ya kuhifadhia dawa.

Kufuatia hali hiyo, Dkt. Ndugulile alimuagiza mganga mfawidhi wa kituo hicho Dkt. Eliaremisa Palangyo kumrudishia mgonjwa aliyenunua dawa katika duka binafsi Bw. Onesphory Mfugale kurudishiwa hela yake kiasi cha Shilingi 27,000.
.
Naibu waziri huyo yupo katika ziara ya siku tatu katika mkoa wa Manyara ambapo atatembelea Hospitali ya Hydom iliyopo wilaya ya Hanang kisha kuelekea Simanjiro ambapo atakagua kazi mbadala za wasichana wa kimasai za ujasiriamali pia atatembelea kituo cha afya cha Orkesumet.

0 on: "WANANCHI SASA KUANZA KUJICHAGULIA VIFURUSHI VYA HUDUMA YA BIMA YA AFYA NCHINI"