NA WAMJW- DODOMA
TANZANIA ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika kutoa huduma za chanjo kwa magonjwa yanayohitaji huduma hiyo kwa asilimia 98 Afrika Mashariki.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Afya) Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati wa ufunguzi wa Mkutano mkuu wa mwaka wa kujadili masuala mbalimbali ya afya uliofanyika jijini Dodoma.
"Tanzania tumepiga hatua katika kutoa huduma za chanjo kwa asilimia 98 ambapo tumetanguliwa na wenzetu wa Rwanda kwa asilimia 99 ila tunaamini mpaka kufikia mwakani tutakua mbele zaidi" alisema Dkt. Ulisubisya.
Aidha, Dkt. Ulisubisya amesema kuwa mpaka hivi sasa Tanzania inatoa chanjo ya Surua na Rubella kwa asilimia 78 ambapo bado lengo halijatimia.
Dkt. Ulisubisya amesema kuwa mpaka sasa Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanikiwa kutibu wagonjwa wa Kifua Kikuu kwa asilimia 99 kwa wote waliogundulika wana vimelea vya ugonjwa huo.
Dkt. Ulisubisya amesema kuwa pia katika mkutano huo wanajadili na kutoka na mikakati mbalimbali ya kuibua maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi nchini ili kuweza kufikia lengo la 90 90 90 .
Mbali na hayo Dkt. Ulisubisya amesema kuwa licha ya changamoto zilizopo katika jamii kutekeleza afua za kupambana na ugonjwa wa Malaria katika mkutano huo watahakikisha wanatoka na afua za kufikia malengo ya kutokomeza ugonjwa huo nchini.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Dkt. Zainabu Chaula amesema kuwa mpaka hivi sasa Serikali imepata fedha ya kukarabati vituo 350 na kuweka vifaa na vifaa tiba kwa ajili ya matibabu ya kibingwa ya huduma za mama na mtoto.
Naye Mwakilishi wa watoa huduma za Afya binafsi Dkt. Josephine Balati amesema kuwa mpaka sasa zaidi ya vituo vya afya binafsi 190 vimeweza kuingia mkataba na Serikali katika kutoa huduma za afya nchini .
"Katika vituo binafsi vya afya 190 vilivyoingia mkataba na Serikali vituo 84 ni vya mashirika ya dini na 106 ni vya watu binafsi" alisema Dkt. Balati .
Mkutano huo wa kila mwaka unaokutanisha wataalam na wadau mbalimbali wa afya una lengo la kupitia changamoto na mafanikio sera ya afya inayotumika katika kuboresha afya za Watanzania.
0 on: "TANZANIA INATOA HUDUMA ZA CHANJO KWA ASILIMIA 98. "