Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiangalia sampuli za mbu katika maabara ya Taasisi ya Nimr Muheza, Tanga
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (kulia) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mhandisi Mwanasha Tumbo (kushoto) alipotembelea kituo cha utafiti wa magonjwa ya binadamu Nirmr.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiangalia vifaa vya zamani vilivyotumika kufanya tafiti katika kituo cha utafiti wa magonjwa ya binadamu Nirmr Amani Muheza.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiangalia lililokuwa jengo la posta ya zamani kabka ya uhuru ambalo lipo katika ofisi za Nimri Amani, Muheza.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisoma kitabu cha tafiti za zamani katika kituo cha tafiti Nimr Amani, Muheza.
Na WAMJW- Muheza, Tanga.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) kwa kufanya tafiti nzuri zinazoisaidia serikali katika mabadiliko ya sera ya afya kwenye matibabu ya ugonjwa wa Malaria.
Dkt. Ndugulile ametoa pongezi hizo mara baada ya kutembelea katika kituo cha tafiti cha ya ugonjwa wa Malaria Nirmi kilichopo katika Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga. “Serikali tunajivunia kuwa na taasisi hii, katika udhibiti wa ugonjwa wa Malaria tumepiga hatua kubwa, tumepunguza maambukizi ya Malaria kwa zaidi ya asilimia 50, tulikuwa na asilimia 14 sasa hivi tuna asilimia 7. Kwa juhudi ambazo tunaenda nazo katika tafiti hizi naamini kiwango cha maambukizi kitaendelea kushuka.” Alisema Dkt Ndugulile.
Licha ya kunufaika na tafiti hizo, Serikali imejiwekea malengo ya kutokomeza kabisa ugonjwa wa Malaria nchini, Dkt Ndugulile amesema kuwa Serikali imejiwekea mikakati mbalimbali ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria kwa kutoa vyandarua, dawa za kuuwa vimelea vya Malaria, kila mgonjwa kupimwa ugonjwa wa Malaria pamoja na kunyunyizia dawa katika makazi ili kuuwa mazalia ya mbu.
Aidha Dkt. Ndugulile ameipongeza taasisi hiyo ya Nimr kwa kutambulika na mashirika ya kimataifa kutokana na tafiti inazozifanya kuwa na ubora wa hali ya juu. “Niwapongeze kwa tafiti zetu kutambulika kimataifa, siyo tuu kwa kutusaidia katika mabadiliko ya sera bali pia
“Tafiti zetu zinatambulika kimataifa, hivi sasa kituo hiki kinatambulika na Shirika la Afya Duniani (WHO) kutokana na tafiti mbalimbali kuhusiana na ugonjwa wa Malaria, kwa hiyo nawapongeza wote kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya” alisema Dkt Ndugulile.
Awali kabla ya kufika katika Kituo hicho, Dkt Ndugulile alifika katika kituo cha tafiti cha Amani kilichopo umbali wa Kilometa 40 nje ya mji wa muheza ambapo amekuta kituo hicho chenye majengo zaidi ya 100 kutofanya kazi za kitafiti. Kituo hicho cha kale ambacho kimeanza kufanya tafiti mbalimbali tangu kabla ya uhuru kimebaki kuwa maktaba ya tafiti za kale ambapo wataalam hufika na kujisomea tafiti za zamani.
Mkuu wa kituo cha tafiti Nimr Muheza, Dkt William Kisinza alisema kuwa tafiti zote za Nimr zilihamishiwa katika majengo mapya yaliyopo Bombo na muheza mjini tangu mwaka 2005. Dkt. Kisinza amesema kuwa taasisi ya Nimr kwa kushirikiana na vyuo vya kimataifa wamekuja na mpango wa kuanzisha chuo cha utafiti wa magonjwa mbalimbali katika kituo cha amani ambapo hadi sasa hivi wamekwisha wasilisha mpango huo ngazi za juu kwa ajili ya utekelezaji.
Baada ya kutembelea majengo hayo Dkt. Ndugulile amesema kuwa ni jambo linalosikitisha kuona rasilimali zilizopo kutotumika vizuri huku akishauri vyuo vya sayansi nchi kutumia fursa hiyo kuanzisha chuo shirikishi kinachotoa elimu ya utafiti wa wagonjwa ya binadamu katika majengo hayo au katika kipindi cha muda mfupi Taasisi iangalie uwezekano wa kuanzisha kozi za muda mfupi katika maeneo ya kipaumbele ili tuweze kuzitumia vizuri rasilimali tulizonazo.
Katika hatua nyingine Dkt. Ndugulile amezitaka taasisi za Serikali kusaidiana katika kazi pale inapobidi ili kuokoa gharama na muda unaotumika katika kazi. Akiwa Jijini baada ya kutembelea hospitali ya rufaa ya Bombo na kituo cha utafiti Nimr, Dkt. Ndugulile amebain vipimo kutoka hospitali ya Bombo hupelekwa Moshi Kilimanjaro huku kituo cha Nimr chenye vifaa vya kisasa kikiwa jirani na hospitali hiyo ambacho kingetumika kufanyia vipimo.
“Tuna maabara nzuri sana pale tanga yenye mashine za kisasa lakini baada ya tafiti hazitumiki, huku vipimo vya hospitali vikipelekwa moshi. Maabara ingeweza kutusaidia kutoa huduma” Alisema Dkt. Ndugulile na kuzitaka taasisi za serikali kuacha ukiritimba na kuboresha mahusiano kwa manufaa ya taifa.
Mwisho.
0 on: "DKT. NDUGULILE AIPONGEZA TAASISI YA NIMR KWA KUFANYA TAFITI ZENYE TIJA KWA TAIFA."