JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TAARIFA KWA
UMMA
UFAFANUZI KUHUSU KAMPENI YA UMEZESHAJI WA DAWA ZA
KINGATIBA
DHIDI YA KICHOCHO NA MINYOO TUMBO NCHINI
Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Napenda kuwataarifu kuwa
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na OR -TAMISEMI imekuwa
ikitekeleza zoezi la umezeshaji wa dawa za kingatiba dhidi ya magonjwa ya Kichocho
na Minyoo ya tumbo kwa watoto walio na umri wa kwenda shule. Zoezi hili lilianza
tangu mwaka 2005 kwa baadhi ya Halmashauri zenye maambukizi mengi na makubwa Zaidi
ya magonjwa haya na baadae mwaka 2015, Serikali iliweza kuzifikia Halmashauri zote
184 nchini baada ya tafiti kuonyesha kuwa maambukizi yapo kila Halmashauri.
Ni vyema tukakumbuka
kwamba nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania ikiwa ni
mojawapo zimeridhia azimio Namba 66.12 la mwaka 2013 ambalo utekelezaji wake ni
pamoja na udhibiti wa magonjwa ya kichocho na minyoo.
Ndugu
Wananchi na Wanahabari,
Waathirika wakuu wa ugonjwa wa Kichocho na
Minyoo ya tumbo ni watoto wenye umri wa kwenda shule, yaani watoto wenye umri
kati ya miaka 5 na 14, ambao wanakuwa katika shule za msingi.
Hivyo, kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Afya, inayohimiza
kinga dhidi ya magonjwa mbali mbali, Serikali hutoa dawa hizi za kingatiba ya
kichocho na minyoo ya tumbo (Vidonge)
walau mara moja kwa kila mwaka katika Halmashauri zote zilizoathirika. Kwa vile
magonjwa haya yapo katika jamii na mazingira yetu, zoezi hili limekuwa ni
endelevu kwa takribani miaka 13 sasa. Kwa mwaka 2018, Halmashauri zote nchini zimetekeleza
zoezi hili kwa mafanikio makubwa, na kwa Mkoa wa Dar es salaam ndio
unahitimisha zoezi hili kwa mwaka huu. (Jedwali
la zoezi la ugawaji dawa shuleni 2018)
Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Hivi
karibuni kumekuwa na taarifa mbalimbali zinazosambaa kupitia vyombo vya habari
kama magazeti na mitandao ya kijamii inayozungumzia zoezi hilo la umezeshaji wa
dawa hizi za kingatiba shuleni. Napenda kutoa ufafanuzi kwamba tunachotoa ni KINGATIBA na sio CHANJO. Aidha dawa hizi za kingatiba ni salama na zimethibitishwa
ubora wake na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania( TFDA) pamoja na Shirika la
Afya Duniani (WHO). Aidha, dawa hizi (Praziquantel
na Albendazole) pia zimesajiliwa kulingana na taratibu za nchi na mamlaka
husika. Vile vile, dawa hizi zinazotumika katika zoezi hili zinatumika
katika
Hospitali na vituo mbali mbali nchini na hupatikana katika maduka ya dawa nchi
nzima kwa maelekezo ya Madaktari.
Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Napenda kutoa maelezo kuhusu magojwa ya Kichocho
na Minyoo ya tumbo kama ifuatavyo:
Minyoo
ya Tumbo: Ipo ya aina tatu (3); Minyoo Mviringo (Round worms), Minyoo
Mjeledi (Flat worms) na Minyoo safura (Hookworms). Maambukizi ya minyoo hii hutokea
pale mtu anapokula mayai ya minyoo hiyo kutoka katika udongo (kupitia mbogamboga,
matunda, au vyakula vingine vibichi ambavyo havijaandiliwa vizuri kwa kufuata
kanuni za afya) au kwa mtu kuambukizwa minyoo hii kwa kupenya kwenye ngozi.
Dalili za ugonjwa wa minyoo ya tumbo ni pamoja na tumbo kuuma, upungufu wa
damu, udumavu, utumbo kujifunga, kukosa hamu ya kula, mwili kuchoka na hivyo kupelekea
mahudhurio hafifu shuleni na mtoto kuwa na uelewa mdogo wa masomo.
Ugonjwa wa Kichocho: Husababishwa na minyoo jamii ya Schistosoma. Kuna aina
mbili (2) za kichocho; kichocho cha kibofu cha mkojo (husababishwa na minyoo ya
Schistosoma haematobium) na kichocho
cha tumbo (husababishwa na minyoo ya Schistosoma
mansoni). Maambukizi ya vimelea hivi hutokana na mtu kugusa maji
yaliyotuama yenye vimelea hivyo. Vimelea hivi hujificha na kukua katika mwili wa
konokono waishio katika maji yaliyotuama. Baadhi ya dalili za ugonjwa huu ni
damu kutoka kwenye mkojo na choo, kuvimba tumbo, na baadae inaweza kusababisha
saratani ya kibofu cha mkojo, shinikizo la damu kwenye ini, kutapika damu, n.k.
Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Zipo njia mbalimbali za
kudhibiti maambukizi ya minyoo ya tumbo na kichocho ikiwemo utoaji wa
elimu ya afya, utoaji wa dawa za
kukinga na kutibu magonjwa haya,
utumiaji sahihi wa vyoo, kuweka maeneo katika hali ya usafi na
kula vyakula vilivyopikwa na kuiva vizuri.
Dawa za vidonge za
Praziquantel ambayo ni kingatiba ya ugonjwa wa kichocho, na dawa ya Albendazole
hutolewa ili kudhibiti ugonjwa wa Minyoo ya Tumbo. Dawa
hizi hutolewa kwa watoto kwa kufuata kipimo cha urefu. Kipimo hiki kimehakikiwa
na kinashabihiana na uzito wa mtoto husika na hutoa makadirio sahihi ya dozi
inayohitajika. Zipo tafiti nyingi zilizohakiki kipimo hicho na kuonyesha kuwa
ni kipimo sahihi kinachofaa kwa zoezi la kingatiba kwa watu wengi (Mass Drug
Administration - MDA).
Zipo
faida nyingi wanazopata watoto wetu kwa kumeza dawa hizi na baadhi ya
faida hizo ni:
·
Kuua kabisa minyoo ya kichocho na minyoo ya
tumbo
·
Kuboresha ukuaji wa mtoto
·
Kuongeza uelewa wa mtoto awapo shuleni
·
Kupunguza upungufu wa damu na unyemelezi wa
magonjwa kama Malaria
·
Kuepusha athari zote za Minyoo na Kichocho
mfano Kansa ya kibofu, presha ya ini n.k
Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Napenda kuwafahamisha kwamba, kabla ya kuanza zoezi
hili kuanza kutekelezwa, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana
na OR-TAMISEMI kupitia kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Halmashauri
husika walitoa mafunzo kwa
waratibu wa afya na wa elimu wa Halmashauri zote. Aidha, uraghabishi (advocacy)
kwa kupitia Kamati za Afya za Mkoa na Wilaya (PHC) pia ulifanyika.
Aidha, Halmashauri
zote pia ziliandaa mafunzo rasmi kwa walimu wa shule za msingi na wataalamu wa
afya wanaohusika na undeshaji wa zoezi hili.
Wanajamii
pia wameendelea kuhamasishwa kushiriki kwa wingi katika zoezi hili kwa kupitia
njia mbalimbali zinazofaa kwa sehemu husika. Masuala makuu ya hamasa yanahusisha
kuandaa chakula ili watoto wapewe mlo kabla ya kumeza dawa na kushiba na kumeza
dawa hizo ndani ya masaa 2 baada ya kupata chakula.
Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Kama
ilivyo kawaida kwa dawa nyingine yapo
maudhi madogo madogo yanayoweza kujitokeza pale mtoto atakapomeza dawa hizo,
hasa iwapo atameza bila ya kuwa na kitu
chochote tumboni. Maudhi hayo ni kama yafuatayo:
·
kutapika,
·
kupata kizunguzungu,
·
kuharisha,
·
mwili kukosa nguvu.
Maudhi
haya yatokanayo na dawa hizi yanaisha kwa muda mfupi na yanakabiliwa kwa
kumpumzisha mtu sehemu tulivu na kumpatia maji. Maudhi haya
yakiendelea baada ya
masaa 24 tunashauri mtoto apelekwe kituo cha afya cha karibu yake.
Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Napenda kuwathibitishia Watanzania kwamba tangu
afua hii ianze kutumika hapa nchini kuanzia mwaka 2005 tumekuwa na mafanikio
makubwa, ambayo ni pamoja na kushuka kwa kiwango cha maambukizi (Prevalence) ya ugonjwa wa kichocho na
minyoo tumbo kutoka wastani wa asilimia 80
% (2005) hadi 30% (2018) katika maeneo mengi nchini, pia wingi wa
maambukizi ya minyoo kwa mtoto mmoja mmoja umepungua sana ambapo hivi sasa ni
chini ya asilimia 10 ya watoto walio na umri wa kwenda shule nchini ndio
wanamaambuki makubwa ya kichocho na minyoo ya tumbo (High intensity).
Aidha, nia yetu ni kuendelea na afua hii ili
hatimaye tuweze kuyatokemeza kabisa magonjwa haya nchini kwetu.
Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Kwa kuhitimisha napenda kutoa wito kwa Wazazi
na Wananchi kwa ujumla kushiriki katika mazoezi haya ya utoaji wa dawa za
kingatiba. Mazoezi haya ni muhimu na endelelevu kwani magonjwa haya yanaathiri
sana jamii yetu.
Nanyi wanahabari tunaomba muendelee kuelimisha
umma kuhusu magonjwa haya na umuhimu wa kingatiba. Dawa hizi huimarisha afya ya
mtoto na hivyo kujenga taifa lenye afya bora na lenye nguvu ya kutosha ili
kuleta maendeleo.
Aidha Ratiba ya Ugawaji dawa shuleni Mwaka
2018 ilikuwa kama ifuatavyo
Namba
|
Tarehe
|
Mikoa husika
|
1
|
APRIL,
2018
|
Arusha,
Kilimanjaro, Dodoma, Geita, Rukwa, Katavi, Manyara, Singida, Pwani, Lindi,
Mtwara, Tabora, Njombe, Iringa (14)
|
2
|
JULAI,
2018
|
Tanga,
Ruvuma, Morogoro, Mbeya, Songwe (5)
|
3
|
AGOSTI
2018
|
Shinyanga,
Mwanza, Mara, Kigoma, Simiyu, Kagera na Dar Es Salaam (7)
|
Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Aidha, Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inawataka wananchi kuzipuuza taarifa za upotoshaji zinazolenga
kuharibu huduma za chanjo zilizotolewa hivi karibuni kwa njia ya Mitandao
ya Kijamii kuwa chanjo zinazotolewa zina lengo la kuleta ugumba na kutozaa, na kwamba
ni mpango mahususi wa nchi za Ulaya katika kupunguza idadi ya Waafrika duniani.
Tunapenda kueleza kuwa taarifa kama hizi zilishawahi kutolewa tena huko nyuma
na watu wasio na utaalamu wa masuala ya chanjo na wenye lengo chafu dhidi ya
mafanikio ya chanjo nchini na duniani. Aidha ufafanuzi umekuwa ukitolewa mara
kwa mara kuhusu upotofu wa dhana hii mbaya.
Wizara inawahakikishia
wananchi kuwa Chanjo zinazotolewa nchini ni salama na zinathibitishwa na
mamlaka zetu hapa nchini na Shirika la Afya Duniani na zina lengo la kuwakinga
binadamu dhidi ya magonjwa hatari ya kuambukiza na si kuzuia mimba au kuleta
ugumba.
Ndugu Wanahabari na Wananchi,
Faida za chanjo
zinafahamika na mafanikio yake sote tumeyaona. Tunayo mifano mingi sana. Mmojawapo ni kwamba kwa kupitia afua ya
utoaji chanjo Tanzania imefanikiwa kutokomeza na kuondoa magonjwa kama vile ndui,
ugonjwa wa kupooza (Polio), Surua, na Ugonjwa wa pepopunda wa watoto wachanga.
Sote tumeshuhudia kufungwa kwa wodi za wagonjwa wa Surua katika Hospitali zote;
kupungua kwa kiasi kikubwa kwa ugonjwa wa Kuhara kwa watoto n.k. Lengo la kutoa
chanjo ni kuundaa mwili kupambana na magonjwa kwa kuuamushia kinga na ni
mojawapo ya kinga mahususi dhidi ya magonjwa husika inayoaminika Duniani kote. Aidha,
wote tumeshuhudia kupungua sana kwa vifo vya watoto chini ya miaka mitano hadi
kufikia vifo 54 kwa kila vizazi hai 1000 na hivyo kufikia lengo la Maendeleo ya
Milenia Namba 4 mwaka 2015.
Ndugu Wanahabari na Ndugu Wananchi,
Wizara inawataka
wananchi kupata Taarifa sahihi kutoka Wizara ya Afya, na kuacha mara moja
kutumia mitandao ya kijamii vibaya na kupotosha jamii. Aidha, niwaombe Waganga Wakuu
wa Mikoa na Halmashauri kote nchini kuendelea kuelimisha wananchi juu ya faida
za chanjo. Pia Wizara inaviomba vyombo
vinavyohusika kuchukua hatua dhidi ya watu wanaopotosha jamii na kuhatarisha
usalama na afya za watanzania.
Imetolewa na:
Ummy A. Mwalimu (Mb)
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto
04/09/2018
0 on: "TAARIFA KWA UMMA"