Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akionesha bango lenye ujumbe kuhusu Ugonjwa wa homa ya Ebola uliojitokeza katika nchi ya jirani ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akijibu maswali ya Waandishi wa Habari (Hawapo kwenye picha) wakati waTamko kuhusu Tahadhari ya Ugonjwa wa homa ya Ebola
uliojitokeza katika nchi ya jirani ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.
Waandishi wa Habari waliojitokeza kumsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati akitoa Tamko kuhusu Tahadhari ya Ugonjwa wa homa ya Ebola uliojitokeza katika nchi ya jirani ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.
TAMKO KUHUSU TAHADHARI YA UGONJWA WA HOMA YA EBOLA ULIOTOKEA KATIKA NCHI JIRANI YA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO
Ndugu Wanahabari,
Manamo
tarehe 10/08/2018 Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto ilitoa taarifa kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika nchi
jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) uliotangazwa na shirika
la Afya Duniani mnamo tarehe 1/08/2018. Katika taarifa hiyo ilielezwa
kwamba jumla ya wagonjwa 26 na vifo 10 (CFR = 38.5%) vilitokea katika
Nchi ya DRC.
Hata hivyo tangu tulivyotoa tamko hadi tarehe 18/08/2018,
hali ya ugonjwa imeendelea kwa kasi sana na kufikia wagonjwa 91 na vifo
50 (CFR = 54.9%). Aidha wagonjwa hawa wanatokea maeneo matano ya afya
(Health zones) katika jimbo la Kivu Kaskazini na eneo jingine moja la
Ituri. Huu ni mlipuko wa 10 wa ugonjwa wa Ebola kutokea nchini DRC, na
umetokea wiki moja tu baada ya nchi hiyo kutangaza kumalizika kwa
mlipuko mwingine uliotokea mwezi Mei 2018.
Ndugu Wanahabari
Sambamba
na takwimu za hizi zilizotolewa na WHO, Wafanyakazi tisa (9) wa Afya
wamethibitishwa kuugua ugonjwa huu, huku ikifanya jumla yao kufikia 10
(9 wamethibitika na 1 anafuatiliwa); na hadi sasa mfanyakazi mmoja
amepoteza maisha. Wafanyakazi hawa wa Afya inaaminika kwamba wamepata
ugonjwa huu wakati wakiwahudumia wagonjwa katika Kliniki zao za kawaida
na sio zile za kutibia wagonjwa wa Ebola (Ebola Treatment Centres
(ETCs), na wengi wao wameambukizwa kabla ya Shirika la Afya Ulimwenguni
(WHO) kutangaza mlipuko huu.
Ndugu Wanahabari
Tumeona
ipo haja ya kuongea nanyi leo kutokana na ukweli kuwa Shirika la Afya
Duniani (WHO) limefanya tena tathmini ya hatari ya kusambaa kwa ugonjwa
wa Ebola nchini DRC na katika nchi zinazopakana na DRC na kubaini kuwa
hatari ya kusambaa kwa ugonjwa huu kwa nchi zilizo jirani na DRC,
ikiwemo Tanzania, imeongezeka maradufu na ni “kubwa” (yaani High risk)
kutokana na kwamba; eneo lililoathirika la Kivu Kaskazini linapakana na
nchi jirani ya Uganda, uwepo wa uhusiano wa wasafiri na wakimbizi wa DRC
wanaoingia nchi jiarani za Uganda na Rwanda, na pia machafuko ya
kijamii ambayo yameendelea kuchukua muda mrefukwenye majimbo ya Kivu
kaskazini na Ituri na hivyo kutatiza kwa kiwango kikubwa makabiliano
dhidi ya ugonjwa huu.
Aidha, eneo hili la sasa ni
la karibu na nchi yetu kuliko eneo lingine lolote ambako ugonjwa huu
umeshawahi kutokea kwenye nchi ya DRC. Hivyo nchi yetu ipo katika hatari
ya kuambukizwa ugonjwa huu kutokana na ukaribu na mwingiliano wa watu,
hasa wasafiri wanaotoka na kuingia DRC kuja hapa nchini.
Ndugu Wanahabari
HADI
SASA HAKUNA MGONJWA YEYOTE ALIYEHISIWA AU KUTHIBITISHWA KUWA NA VIRUSI
VYA EBOLA HAPA NCHINI. Hata hivyo kutokana na ukweli kwamba kuna
mwingiliano mkubwa wa wananchi kati ya nchi hizi mbili na ugonjwa huu
kugunduliwa kwenye jimbo la Kivu Kaskazini ambalo linapakana na nchi ya
Uganda ni ukweli unaotuweka kwenye hali ya wasiwasi mkubwa.
Hivyo
tunasistiza kwamba wanajamii wote ikiwemo wafanyakazi wa sekta ya Afya
kuelewa vyema dalili za ugonjwa huu pamoja na kuongeza nguvu katika
kufuata kanuni za kuzuia maambukizi katika vituo vya Afya yaani
Infection Prevention and Control (IPC) measures.
Wizara
inapenda kutoa tahadhari kubwa ya ugonjwa huu kwa Wananchi wote, na
katika mikoa yote hasa ile inayopakana na nchi jirani ya DRC ambayo ni
Mwanza, Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa na Songwe. Aidha, hii haiondoi
ukweli kwamba, viwanja vya ndege vya Julius Nyerere (JNIA) cha Dar es
Salaam, Kilimajaro (KIA) na Songwe cha Mbeya kuwa vipo katika hatari ya
kuweza kuingiza mgonjwa wakati wowote ule.
Kutokana
na hali hii, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, kwa kushirikiana na Washirika mbali mbali, ikiwemo WHO,
wanafanya juhudi mbalimbali ili kuhakikisha kwamba tunaimarisha
ufuatiliaji wa wasafiri wanaopita katika mipaka yetu yote ili kuzuia
kuingia kwa ugonjwa huu hapa nchini.
Ndugu Wanahabari
Ugonjwa
wa Ebola husababishwa na virusi vya Ebola na mlipuko wa ugonjwa wa Homa
ya Ebola hutokea pale binadamu anapogusana na mnyama aliyeathirika na
ugonjwa huu kama vile Nyani, Sokwe au Popo. Aidha ugonjwa huu huenezwa
kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa binadamu mwingine kwa njia
zifuatazo;
Kugusa damu au majimaji kutoka kwa mtu aliyeambukizwa Virusi vya Ebola
Kugusa vitu vya mgonjwa wa Ebola, kama vile nguo, shuka au godoro
Kugusa au kutumia vifaa vilivotumika kwa mgonjwa wa Homa ya Ebola kama sindano
Kugusa au kuosha maiti ya mtu aliyefariki kwa Ebola
Kugusa wanyama (mizoga au wanyama hai) walioambukizwa kama vile sokwe na nyani wa msituni
Kukutana kimwili na binadamu mwenye maambukizi ya virusi vya Ebola.
Aidha tunasisitiza kwamba ugonjwa wa Homa ya Ebola hauenezwi kwa njia ya hewa, maji au chakula.
Dalili za Ugonjwa
Dalili
za Ugonjwa huanza kuonekana kwa mtu aliyeambukizwa kutoka siku 2 hadi
21 tangu kupata maambukizi ya ugonjwa huu. Dalili hizo ni pamoja na;
Homa kali ya ghafla,
Kulegea kwa mwili,
Maumivu ya misuli,
Kuumwa kichwa na vidonda kooni.
Mara nyingi dalili hizo hufuatiwa na kutapika, kuharisha, vipele vya ngozi na pia figo na Ini kushindwa kufanya kazi.
Kwa baadhi ya wagonjwa kutokwa na damu nyingi ndani na nje ya mwili.
Namna ya Kujikinga na ugonjwa wa Ebola:
Ugonjwa wa Ebola unaweza kuzuilika. Njia kuu za kujikinga na ugonjwa huu ni kama ifuatavyo:-
Epuka
kugusa damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji mengine
yanayotoka mwilini mwa mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola
Epuka
kushughulikia maiti ya mtu aliyefariki kwa dalili za ugonjwa wa Ebola;
Aidha unatakiwa kutoa taarifa kwa uongozi wa kituo cha kutolea huduma za
Afya kwa ushauri.
Epuka mila na desturi zinazoweza kuchelewesha mgonjwa kupatiwa huduma muhimu za Afya na kupelekea kueneza ugonjwa wa Ebola.
Kuzingatia kanuni za Afya na usafi wa mwili
Kutoa
taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na kwa wahudumu wa Afya katika
ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.
Kuwahi katika vituo vya huduma za Afya pale mtu anapoona dalili za ugonjwa huu.
Ndugu Wanahabari
Wizara
yangu imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuimarisha uwezo wetu wa
utayari katika kukabiliana na ugonjwa huu kwa kuzuia usiingie, na hatua
za kuchkua iwapo utaingia hapa nchini.
Hadi sasa Wizara imefanya yafuatayo;
Kufanya
tathmini ya utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa homa ya Ebola hapa
nchini (Operational readiness assessment). Tayari tathmini hiyo
imefanyika kwa kushirikiana na WHO kwenye mikoa minane ambayo ni Rukwa,
Katavi, Songwe, Mbeya, Kigoma, Kagera, Arusha na Kilimanjaro na kuanisha
uwezo uliopo na mapungufu ambayo yanafanyiwa kazi.
Aidha,
WAMJW imeajiri wataalamu wapya 33 ili kuongeza nguvu katika mipaka yetu
na tayari wamesambazwa kwenye vituo vya mipakani.
Tunaendelea
kuimarisha ufuatiliaji wa wasafiri mipakani (Travellers entry
screening) kwa kutumia vifaa vya kupima joto (thermo scaners) na fomu
maalum za wasafiri wanaoingia nchini, ambapo tayari kupitia MSD imepokea
vifaa vyenye thamani ya Bilioni 5 kutoka WHO na vimeshapelekwa kwenye
maeneo husika ikiwa ni pamoja na kupeleka vifaa kinga kwa watumishi wa
afya (Personal Protective Equipment, PPE’s) kwenye maeneo yote nchini.
WAMJW
kwa kushirikiana na Taasisi ya Udhibiti wa Magonjwa ya Kuambukiza ya
Marekani (Centres for Diseases Control, CDC) na Water Reed imenunua
“kits” nne za kupima Ebola zenye uwezo wa kupima wagonjwa zaidi ya 400
na hivyo kuiwezesha Maabara ya Taifa na hile ya kanda ya Mbeya kuwa na
uwezo mzuri.
Hadi sasa WAMJW ina uwezo wa kupima
ugonjwa huu Nchini kwa kutumia maabara ya Taifa Dar es Salaam, Hospitali
ya kanda ya MBEYA na KCRI katika Hospitali ya KCMC, Kilimanjaro
Mafunzo
ya usimamizi wa sampuli yamefanyika kwa Mikoa ya Mwanza, Arusha,
Ruvuma, Kilimanjaro, Kigoma na Kagera kwa wiki iliyopita na kupatiwa
jumla ya Triple packaging materials 18.
Uelimishaji
wa umma unaendelea kufanyika kupitia matamko pamoja na matumizi ya
vyombo vya habari ikiwemo vile vya kitaifa, vya binafsi, mitandao ya
kijamii, vipeperushi na mabango.
WAMJW tayari
imeshatoa tahadhari kwa wadau na sekta muhimu wakiwemo TAMISEMI pamoja
na mamlaka ya viwanja vya ndege ili kuongeza utayari wa maeneo husika
Vilevile Wizara yangu imepanga kufanya yafuatayo
Kuendelea
kutoa mafunzo dhidi ya ugonjwa wa Ebola ikiwemo kuwaongezea wataalamu
wapatao 80 wa mipakani uwezo wa ufuatliaji na utambuzi wa ugonjwa huu.
Mafunzo haya yanaendelea mjini Morogoro
Kutoa
mafunzo kwa Timu za dharura na maafa (Rapid Respond Teams) ambayo
yanategemewa kuanza mnamo tarehe 27 Agosti 2018 jijini Mwanza. Lengo
likiwa ni kuwajengea uwezo wa jinsi ya kuratibu na kukabiliana na
ugonjwa huu endapo utatokea hapa Nchini. Idadi ya wataalam watakao pata
mafunzo hayo ni kama ifuatavyo; Mkoa wa Mwanza (15), Kagera (15) na
Kigoma (15) ili kujaza nafasi ya mapungufu katika wilaya ambazo ziko
katika hatari na bado hazijapata mafunzo haya.
Timu
ya Wakurugenzi wa Wizara ikiongozwa na Mganga Mkuu wa serikali
itatembelea mikoa ya Kigoma, Kagera na Mwanza. Lengo la ziara hii ni
kufuatilia kwa ukaribu utayari wa mikoa hii katika kukabiliana na
ugonjwa huu endapo utatokea
Kituo chetu cha uratibu
wa milipuko ya magonjwa na majanga yaani Public Health Emergency
Operation Center (PHEOC) kipo katika utahadhari wa juu (level 1 - High
Alert) ili kufuatilia kwa ukaribu ugonjwa huu nchini DRC pamoja na
kuratibu utayari wetu Kitaifa na katika ngazi ya Mikoa
Hitimisho
Wananchi
wanatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari na kujikinga na ugonjwa huu,
pamoja na kwamba hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyeripotiwa kuugua
ugonjwa huu hapa nchini.
Hivyo naelekeza yafuatayo:-
Wakuu
wa Mikoa yote, waitishe kikao cha Afya ya msingi (PHC) na kujadili
jinsi mikoa yao ilivyojiandaa kukabiliana na ugonjwa huo endapo utaingia
kwenye maeneo yao
Wananchi wanatakiwa kutoa
taarifa katika ofisi za serikali za mitaa au kijiji au kituo cha kutolea
huduma za Afya endapo kutatokea mtu yeyote mwenye dalilil za ugonjwa
wa Ebola
Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya, na
hasa wale walioko katika mikoa iliyo katika hatari kubwa zaidi ya
maambukizi, wawe macho na makini zaidi katika kusimamia jitihada hizi za
Wizara.
Aidha Wizara itaendelea kushirikiana na
sekta mbalimbali, zikiwemo taasisi za kimataifa katika kuimarisha
ufuatiliaji na kutekeleza mikakati ya kudhibiti iugonjwa huu ili
usiingie hapa nchini.
.
Ahsanteni kwa kunisikiliza