JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TAARIFA KWA UMMA JUU YA TUHUMA YA UWEPO WA VITENDO
VYA RUSHWA KATIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA, DODOMA KAMA ILIVYORIPOTIWA KWENYE
MTANDAO WA KIJAMII WA JAMII FORUM TAREHE 28/10/2017
Uongozi
wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma umepokea kwa masikitiko taarifa
iliyotolewa kwenye mtandao tajwa hapo juu kwamba, “Serikali na Takukuru
muimulike Hospitali ya Mkapa Dodoma” kwamba, “imekuwa kawaida kabisa kwa
mgonjwa kutopata huduma ya aina yoyote bila kutoa chochote na kuna mgonjwa ana
wiki matokeo ya vipimo hayajatoka na hajapewa huduma yoyote zaidi ya dawa za
kuondoa maumivu”.
Uongozi
wa Hospitali unapenda kuwahakikishia watumiaji wa huduma za hospitali hii
kwamba, madai husika hayana ukweli wowote. Mara baada ya kupokea malalamiko na
tuhuma tajwa hapo juu, siku hiyo hiyo ya tarehe 28/10/2017 uongozi wa hospitali
ulichukua hatua ya kufanya ufuatiliaji kwa kuwatembelea wagonjwa wote waliokuwa
wamelazwa wodini na kuzungumza nao pamoja na ndugu zao ili kubaini kero
walizonazo kuhusu huduma za Hospitali.
Ufuatiliaji
huu ulizingatia kubaini tarehe ya kulazwa, ugonjwa alio nao, vipimo
alivyoandikiwa, vipimo ambavyo havijafanyika na sababu za kutofanyika. Aidha, kila mgonjwa/ndugu aliridhia na kutoa
ushirikiano mkubwa ili kubaini ukweli na pia wote walitoa mawasiliano yao ya
simu ya mkononi iwapo ufuatiliaji zaidi ungehitajika.
Yatokanayo na ufuatiliaji huo ni;
Jumla
ya wagonjwa 34 ndio walikuwemo wodini siku ya tarehe 28/10/2017. Tarehe za
kulazwa kwao zilikuwa kati ya 20/9/2017 na 28/10/2017. Kati ya hao, wanawake
watu wazima walikuwa 20 na wanaume 14 ambapo kati yao 2 walikuwa watoto
wachanga.
Wagonjwa
24 tu ndiyo matibabu yao yalikuwa yanahitaji vipimo mbalimbali na wengine hawakuhitaji
kutokana na asili ya magonjwa waliyokuwa wanaugua.
Wagonjwa
waliombwa kutoa maoni yao kuhusu hali ya huduma kwa ujumla pia kuhusu upatikanaji
wa vipimo vya uchunguzi wa maabara na mionzi na kama kuna ucheleweshaji wa
vipimo husika na dalili za kuombwa rushwa. Jumla ya wagonjwa 18 kati ya 24
waliohitaji vipimo, walikuwa wamepimwa na kupewa majibu. Wagonjwa sita (6)
waliobakia; wawili (2) kati yao walikuwa wamelazwa tarehe 27/10/2017 na tayari
walikuwa wameshaanzishiwa matibabu na kupangiwa kupimwa ECHO na ECG tarehe
30/10/2017. Aidha, wagonjwa wengine wawili (2) walikuwa wamepimwa tarehe
27/10/2017 na walikuwa wanasubiri majibu na waliobakia 2 ndiyo kwanza walikuwa
wamelazwa siku hiyo ya tarehe 28/10/2017.
Hakukuwa
na mgonjwa yeyote aliyelalamikia kusumbuliwa kuhusu vipimo wala kuona dalili za
rushwa na badala yake, wote walishukuru kwa juhudi zinazofanywa na watumishi wa
hospitali katika kuwapatia huduma.
Hata
hivyo, tangu awali hospitali hii imeweka mifumo mbalimbali ya kuhakikisha
inabaini vitendo vinavyo athiri utoaji wa huduma bora na salama vikiwemo
vitendo vya rushwa. Mifumo hii ni pamoja na:-
1.
Utoaji wa
elimu kwa wateja maeneo ya mapokezi,
maabara na kliniki.
2.
Uwepo wa
Sanduku la Maoni
3.
Uwepo wa namba
za simu za kutolea malalamiko ya wateja.
4.
Viongozi wa
hospitali kutembelea sehemu mbalimbali za kutolea huduma na kuongea na wateja.
5.
Wateja
kujaza dodoso la kutoa maoni baada ya huduma (client exit interview).
Elimu inayotolewa
huelekeza juu ya haki za wateja, huduma zinazopatikana, mfumo wa malipo, kujiepusha
na kutoa au kupokea rushwa, na jinsi ya kutoa maoni na malalamiko juu ya huduma
wanazopata kwa kutumia sanduku la maoni, kupiga namba za simu zilizobandikwa
sehemu mbalimbali na kuwaelekeza mahala palipo na dawati la malalamiko na jinsi
ya ujazaji wa dodoso la mteja baada ya huduma (Client Exit Interview). Elimu
hii hutolewa na Idara ya Ustawi wa Jamii iliyopo hapa hospitalini.
Aidha,
tangu awali, hospitali iliweka Sanduku la Maoni maeneo ya mapokezi ili wateja waweze kuweka maoni yao wakati wowote wanapohitaji. Tangu
sanduku la maoni lianze kufunguliwa, hakuna aliyelalamikia uwepo wa vitendo vya
rushwa au viashiria vyake.
Vilevile,
hospitali imebandika namba Nne (4) tofauti za Simu mkononi za Viongozi katika sehemu
mbalimbali za kutolea huduma ili kuwarahisishia wananchi/wateja kuwasilisha
maoni yao kuhusu huduma. Namba ya kwanza kwenye orodha ni ya Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji, ikifuatiwa na ya Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi, Kaimu Mkurugenzi
wa Utawala na Katibu wa Hospitali. Tangu Wananchi waanze kutumia namba hizi
hakuna aliyewahi kulalamikia uwepo wa rushwa ndani ya hospitali hii.
Uongozi
wa Hospitali umejiwekea utaratibu wa kutoka ofisini na kupita sehemu mbalimbali
za kutolea huduma na kuongea na wagonjwa ili kubaini kama kuna changamoto
wanazozikabili wakati wa kupokea huduma. Maeneo hayo ni pamoja na mapokezi,
eneo la wagonjwa wa nje (OPD), Kliniki mbalimbali, maabara, eneo la kutolea
huduma za mionzi, na mawodini. Zoezi hili huongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
wa Hospitali na hufanyika angalau mara tatu kwa wiki zikiwemo siku za mapunziko
za Jumamosi na Jumapili. Tangu zoezi hili lianze, hakuna mwananchi/mteja aliyewahi
kulalamikia uwepo au viashiria vya rushwa.
Hospitali
pia ilianzisha Dodoso Maalumu la Mteja (Client
Exit Interview) linalojazwa na mteja baada ya kupewa huduma ili kubaini
sehemu zenye changamoto. Tangu madodoso haya yaanze kujazwa, hakuna mteja/mgonjwa
aliyelalamikia uwepo au viashiria vya rushwa.
Uongozi
wa Hospitali unatoa Shukrani za pekee kwa watumiaji wa huduma za hospitali hii
na wote wanaotoa maoni kwa ajili ya kuboresha zaidi huduma. Tunapenda
kuwahakikishia kuwa, tutaendelea kusimamia maadili ya tiba na kuhakikisha wateja
wote wanafurahia huduma zetu. Hata hivyo, hatutasita kuchukua hatua stahiki za
kisheria endapo tutabaini kwamba taarifa iliyotolewa ni ya upotoshaji na / au
imetolewa kwa lengo la kuichafua hospitali, wizara au Serikali.
Uongozi
wa hospitali unatoa wito kama kuna ambaye hajatendewa haki ajitokeze na kutumia
fursa za mawasiliano zilizoainishwa hapo juu ili kero yake iweze kufanyiwa kazi
au afuate utaratibu rasmi wa kuripoti tukio husika la vitendo vya rushwa kwenye
vyombo husika vya kisheria ili taratibu za kisheria zichukuliwe.
Aidha,
milango ya hospitali iko wazi wakati wowote kwa ajili ya kupokea kero na maoni
toka kwa wateja wake ili kuboresha zaidi huduma.
AHSANTENI SANA.
30/10/2017.