DKT.
NDUGULILE ASISITIZA KUOKOA MAISHA YA
MAMA MJAMZITO NA MTOTO.
NA
WAMJW-MWANZA
NAIBU Waziri wa Afya,Maendeleo ya
Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa wadau wa
sekta ya afya na watoa huduma za afya hasa wauguzi na wakunga wanatakiwa
kujikita zaidi kwenye kuokoa na kuboresha afya ya mama mjamzito na mtoto ili
kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Akizungumza hayo wakati wa uzinduzi wa
mradi wa Ukunga salama (More and Better Midwives) uliofanyika leo katika Chuo
cha Uuguzi na Ukunga Bukumbi kilichopo Wilayani Misungwi mkoani Mwanza.
“Sisi sote tunafahamu umuhimu wa
wauguzi na wakunga katika kuimarisha afya ya mama na mtoto hivyo Serikali ya
awamu ya tano tumejipanga kuhakikisha kuwa tunapunguza kwa kiasi kikubwa vifo
vya mama na mtoto” alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha Dkt. Ndugulile alisema kuwa
Serikali inafahamu kuna changamoto ya upungufu wa watumishi katika kada
mbalimbali za afya pamoja na nyinginezo na wanaendelea kuzifanyia kazi ikiwa
kutoa kipaumbele cha ajira za wauguzi na wakunga.
Mbali na hayo Dkt. Ndugulile amewaonya
wakunga na wauguzi wenye tabia ya
kutumia lugha chafu kwa wagonjwa pamoja na kuacha vitendo vya kuwaomba rushwa
kwani fani hiyo inaendeshwa kwa taaluma na maadili.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya
Misungwi Bw. Juma Sweda amesema kuwa wananchi wa Wilaya hiyo wanatakiwa wawe
mstari wa mbele katika kukata bima za afya kwani husaidia kuokoa gharama nyingi
pindi wanapopata maradhi na mpaka hivi sasa wananchi wenye bima ta afya
inakadiriwa ni 9100.
Naye Mkurugenzi wa Mradi wa Ukunga
Salama nchini Dkt. Julius Masanika amesema kuwa mradi huo utafadhili wanafunzi
wa kanda ya ziwa na kanda ya magharibi wanaojiunga na vyuo vya Uuguzi na Ukunga
wasio na uwezo kwa kuwalipia ada pamoja na mahitaji mengine.
Kwa upande wake Mwanafunzi wa Uuguzi
na Ukunga katika Chuo cha Bukumbi ambaye
anafadhiliwa na mradi huo Rose Julius amesema kuwa anawasihi wanafunzi wafanye
bidii kwenye masomo ya sayansi na hatimae wachukue fani ya uuguzi na ukunga
katika kukabiliana na changamoto za vifo vitokanavyo na uzazi.
Mbali na ufunguzi huo wa mradi wa Ukunga
salama unaojulikana kama “More and Better Midwives” ambao umeshirikisha taasisi isiyo ya Kiserikali JHPIEGO
,wawakilishi kutoka Chama cha wakungwa
Canada(CMA) na Chama cha wakungwa Tanzania TAMA pia alitembelea Zahanati ya
Kambi ya wazee Bukumbi,Bohari ya Dawa (MSD) na Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa
Mwanza Sekou Toure ili kujua hali ya upatikanaji wa dawa .
0 on: "DKT. NDUGULILE ASISITIZA KUOKOA MAISHA YA MAMA MJAMZITO NA MTOTO."