Na
WAMJW-DODOMA
UTAALAMU wa huduma ya kupandikiza figo
kwa wagonjwa wenye magonjwa hayo upewe kipaumbele hapa nchini ili kuweza kuokoa
watanzania wengi wenye matatizo hayo kwa muda mfupi na kupunguza gharama kubwa
ya rufaa za kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa
Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati
wa uzinduzi wa mkutano wan ne wa chama cha wataalamu wa figo nchini uliofanyika
leo mjini Dodoma.
“Serikali imekuwa ikipeleka wastani wa
wagonjwa 35 kwa mwaka nje ya nchi ikiwa
ni pamoja na India kwa ajili ya kupandikiza figo ambapo inagharimu takribani
shilingi milioni 75 hadi 77 kwa mtu mmoja ikiwa ni gharama za malazi na kupandikiza
figo” alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha Dkt. Ndugulile amesema kuwa
ikiwa Tanzania itazalisha wataalamu
wengi wa kupandikiza na kusafisha figo itafanikiwa kupunguza gharama hizo na
kufanya huduma hiyo ipatikane kwa shilingi milioni 20.3 ikiwa huduma hiyo
itapatikana hapa nchini.
Mbali na hayo Dkt. Ndugulile amesema
kuwa katika kuwekeza huduma ya kupandikiza figo Serikali imefunga mashine
katika maeneo yafuatayo, UDOM 10, 5Hospitali ya Taifa ya Muhimbili 42, Hospitali ya Rufaa Mbeya 5, Hospitali ya
Rufaa Bugando 10, KCMC 10, Hospitali ya Misheni Serian 10, Hospitali ya NSK Arusha 5, TMK 10,Regency
15, Hurbert Kairuki 5, Aga Khan 10 na Access 10 ambapo takwimu zinaonyesha
mashine hizi zina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 783 kupitia huduma ya NHIF na 391
kwa huduma malipo ya papo kwa papo.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa
chama cha Wataalam wa Figo Tanzania Dkt. Paschal Rugajjo amesema kuwa wamepiga
hatua kubwa katika kuongeza madaktari wa figo hapa nchini kwani mpaka sasa wapo
madaktari 12 kutoka daktari mmoja miaka kumi iliyopita.
Mbali na hayo Dkt. Rugajjo amesema
kuwa ushirikiano unahitajika kati ya chama hicho pamoja na Serikali kutoa
kipaumbele kwenye elimu juu ya ugonjwa huo ili kuweza kupambana na tatizo hilo
kuanzia ngazi ya wananchi mpaka kwenye taasisi za afya nchini.
0 on: "UTAALAMU WA KUPANDIKIZA FIGO UPEWE KIPAUMBELE NCHINI, ASEMA DKT. NDUGULILE"