Ndugu wanahabari,
Tanzania
ni mojawapo ya nchi za kusini mwa Afrika zinazokadiriwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa na vifo vingi
vitokanavyo na Saratani. Takribani wagonjwa
wapya 50,000 kila mwaka wanagundulika kuwa na Saratani, na idadi hii
inakadiriwa kuongezeka kwa asilimia hamsini (50%) ifikapo mwaka 2020.
Taarifa kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean
Road kwa kipindi cha mwaka 2006 hadi 2015 zinaonyesha kwamba aina za Saratani
zinazoongoza hapa nchini ni kama ifuatavyo; Saratani ya mlango wa kizazi
(34%),Saratani ya Ngozi (kaporsis Sarcoma)(13%), Saratani ya matiti (12%),
Saratani ya mfumo wa njia ya chakula (10%), Saratani ya Kichwa na shingo (7%),
Saratani ya Matezi (6%), Saeatani ya Damu (4%), Saratani ya Kibofu cha mkojo
(3%),Saratani ya ngozi (3%), Saratani ya Macho (2%), na saratani ya tezi dume
(2%). Mbaya zaidi, asilimia 80 ya wagonjwa wote hao wanafika Ocean Road wakiwa
katika hatua za mwisho za ugonjwa na
kufanya matokeo ya matibabu kutokuwa mazuri.
Ndugu wanahabari,
Kupitia
takwimu hizi ni dhahiri kuwa Saratani ya Mlango wa Kizazi husababisha vifo
vingi kwa wanawake, ikifuatiwa na saratani ya matiti. Na kama ilivyo kwa
saratani nyingine, asilimia 80 ya
wanawake wanaougua saratani hiiwanafika katika vituo vya kutolea huduma za afya
kwa ajili ya tiba wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa, ambapo hufanya matibabu kutokuwa na matokeo mazuri. Aidha Serikali
imekuwa ikitumia fedha nyingi kutibu wagonjwa
hawa. Saratani ya Mlango wa
kizazi inatibika endapo itagundulika mapema sambamba na kusaidia kupunguza
gharama za matibabu ambazo Serikali, familia na mgonjwa wamekuwa wakikabiliana
nazo.
Tangu
mwaka 2008, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilianza
kutoahuduma ya uchunguzi kwa kutumia
siki(acetic acid) na matibabu ya mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango
wa kizazi kwa kutumia tiba mgando
(cryotherapy).Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, Wizara imeshaanzisha vituo 459 (vituo 343 vya serikali na 116 vya mashirika
na watu binafsi) vinavyotoa huduma ya uchunguzi na matibabu ya mabadiliko
ya awali ya Saratani ya Mlango wa Kizazi. Wizara inawapongeza na kuwashukuru
wadauwote wanaoshiriki katika kuimarisha upatikanaji wa huduma hizi. Kipekee
tungependa kutambau mchango wa Jhpiego, ICAP, EGPAF, THPS, Marie Stope, PSI,
Umati, MEWATA, T Marc na WAMA.
Tunawashukuru sana!
Ndugu wanahabari,
Katika
kuhakikisha tunaongeza upatikanaji wa huduma za uchunguzi na matibabu ya awali
ya Saratani ya Mlango wa Kizazi, Wizara ya Afya imekuja na mkakati wa kuboresha
huduma hizi kwakununuamashine 100 za tiba mgando
(cryotherapy) na mashine 9 za
upasuaji mdogo (LEEP) ambazo zitatumika kwa ajili ya matibabu ya awali ya
saratani kwa wanawake watakaofanyiwa uchunguzi na kukutwa na mabadiliko ya
awali ya saratani ya mlango wa kizazi. Pia tumenunua
mitungi 173 ya gesi ya ‘’carbon dioxide‘’ itakayowezesha mashine hizo
kufanya kazi. Vilevile, tumeshatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watoa huduma ili
kuweza kutoa huduma hizi bila vikwazo. Vifaa hivi vimekwishawasili nchini na
vinaanza kusambazwa katika vituo vya Tiba 100 nchini kuanzia kesho. Vifaa hivyo
vitasambazwa katika mikoa 10, halmashauri 31 ambazo tumebaini zina vituo
vichache vya kutolea huduma hizi ukilinganisha
na Mikoa mingine. Mikoa hii ni Mara, Singida, Geita, Dodoma, Tanga, Arusha,
Manyara, Ruvuma, Lindi na Mtwara.
Ndugu wanahabari,
Kupitia
hatua hii, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais, Mhe Dr. John Pombe
Magufuli inaongeza idadi ya vituo vinavyotoa
huduma za uchunguzi na matibabu ya awali ya saratani kutoka vituo 343 (2015) hadi vituo 443 (2017).
Huduma hizi zinapatikana katika Hospitali zote za Rufaa za Kanda na Mikoa,
Hospitali zote za Wilaya, na baadhi ya Vituo vya Afya na Zahanati.
Ndugu wanahabari,
Kupitia
kwenu, napenda kuwahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kupata huduma za
uchunguzi na matibabu ya awali ya Saratani ya Mlango wa Kizazi katika vituo
hivi. Huduma hizi zinatolewa katika
kliniki ya afya ya mama na mtoto kila siku na bila malipo yoyote. Aidha
ninavielekeza vituo vyote vya umma nchinikutenga
siku maalumu katika kila mwezi ambayo kituo kitahamasisha wanawake kuja kwa
wingi kupata huduma hizi. Na kwa kuwa mwezi wa Octoba kila mwaka ni mwezi
wa uhamasishaji wa upimaji wa saratani ya matiti duniani kote, nitumie fursa hii kutoa rai kwa wananchi hasa
wanawake wenzangu kuhudhuria vituoni kupata huduma za uchunguzi mapema.
Wananchi wengi wamekuwa wakipoteza maisha aidha kwa kutofahamu au uelewa mdogo
kuhusu saratani.
Ndugu wananchi,
Aidha,
katika kuhakikisha huduma hizi zinakuwa endelevu, nazielekeza halmashauri zote
kutenga fedha za kutosha kuhakikisha huduma hizi zinaingizwa kwenye mipango yao
ya bajeti ya vituo na halmashauri. Pia ni lazima wahakikishe mashine hizi
zinatunzwa na kufanyiwa ukarabati inapobidi.Kwa upande wetu Wizara ya Afya,
tutaendelea kusimamia ubora wa huduma zinazotolewa kulingana na miongozi,
kujenga uwezo wa watoa huduma. Vilevile, tutahakikisha mafundi sanifu tiba
wanapatiwa uelewa na nyezo za kufanya matengenezo madogo na ukarabati wa
mashine hizi kwa kushirikiana na Halmashauri husika.
Kwa
ujumla, Serikali itaendelea kuhakikisha
vituo zaidi vinaanzishiwa huduma hii ili ipatikane karibu zaidi na wananchi
hasa wa vijijini. Vilevile, tutahakikisha tunapanua huduma za Rufaa za Matibabu
ya saratani nchini kwa kuhakikisha
huduma za Tiba kwa kutumia dawa (Chemotherapy ) na Mionzi (Radiotherapy)
zinapatikana katika Hospitali za Rufaa
za Kanda- Mbeya, Bugando na KCMC ili kupunguza msongano wa wagonjwa katika
Hospitali ya Ocean Road, Dar es salaam.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
0 on: "SERIKALI YAONGEZA VITUO 100 KWA AJILI YA KUTOA HUDUMA ZA UCHUNGUZI NA MATIBABU YA AWALI YA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI NCHINI"