MUHTASARI WA HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA,
MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019
A:
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, kufuatia
taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na
Maendeleo ya Jamii ndani ya Bunge lako Tukufu, ambayo imechambua Bajeti ya
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ninaomba
kutoa hoja sasa Bunge lako likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji
wa Kazi za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
kwa mwaka 2017/18 na Vipaumbele vya Wizara kwa mwaka 2018/19. Aidha, ninaliomba
Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Kawaida
pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka 2018/19.
2.
Mheshimiwa Spika, kwanza
napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako
Tukufu na kuwasilisha hotuba yangu siku ya leo. Aidha, ninapenda kutumia fursa
hii kwa heshima na unyenyekevu mkubwa kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt.
John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi
wake imara kwa nchi yetu na maelekezo yake ambayo yamekuwa dira sahihi katika
utendaji wangu na katika kuimarisha huduma za Afya na Maendeleo ya Jamii
nchini. Aidha, ninampongeza Mheshimiwa
Rais kwa kuendelea kuipa kipaumbele Sekta ya Afya kwa kutoa msukumo mkubwa
katika uanzishwaji wa viwanda vya kutengeneza Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba na
Vitendanishi hapa nchini. Msukumo huo utaboresha huduma za afya kwa Watanzania
kama nyenzo muhimu ili kufikia Uchumi wa Kati.
3.
Mheshimiwa Spika, ninapenda
kutoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika
jitihada za kuboresha huduma za afya kwa Watanzania hasa katika mapambano dhidi
ya ugonjwa wa Kifua Kikuu, Afya ya Mama na Mtoto, Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza
pamoja na Afya ya Vijana. Wizara yangu itaendelea kutumia ushauri, nasaha,
ushawishi na uzoefu wake ili kuhakikisha Watanzania wanaweza kujikinga na
maradhi na kujenga jamii ya Watanzania wenye Afya Bora.
4.
Mheshimiwa Spika, ninaomba
kuchukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa (Mb),
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri
unaosaidia kuleta tija na ufanisi katika utendaji na kuimarisha huduma
zinazotolewa katika Sekta ya Afya. Aidha, ninampongeza kwa hotuba yake
aliyoiwasilisha kwenye Bunge lako tukufu ambayo imetoa dira ya jinsi Serikali
itakavyotekeleza majukumu yake katika mwaka 2018/19.
5.
Mheshimiwa Spika,
ninapenda kukupongeza wewe binafsi kwa kuendelea kutekeleza majukumu yako kwa
weledi katika kuliongoza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha,
ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mb) katika utekelezaji wa majukumu yake. Vilevile, nitumie fursa hii
kuwapongeza Wenyeviti wa Bunge kwa kusimamia vyema mijadala ndani ya Bunge.
6.
Mheshimiwa Spika, kipekee
ninapenda kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii,
chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Peter Serukamba (Mb), na Makamu
Mwenyekiti, Mheshimiwa Juma Nkamia (Mb)
kwa ushauri na maelekezo waliyoyatoa wakati wa maandalizi ya Bajeti hii. Aidha
ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano mzuri wanaonipatia
ikiwemo kutoa ushauri na maoni mbalimbali yenye lengo la kuboresha huduma za
afya na maendeleo ya jamii nchini. Ninawaahidi kwamba, Wizara yangu itazingatia
ushauri wao na kuendelea kuwapa ushirikiano katika kutekeleza majukumu na kazi
zetu za kuwatumikia wananchi ndani na nje ya Bunge.
7.
Mheshimiwa Spika, ninatoa pole kwa
Watanzania wote, waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki zao kutokana na sababu
mbalimbali ikiwa ni pamoja na magonjwa, ajali na majanga. Aidha, ninatoa pole
kwa wagonjwa na majeruhi wa ajali waliopo hospitalini na majumbani pamoja na
wahanga wa vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia. Ninamuomba Mwenyezi
Mungu awaponye haraka ili waweze kuendelea na ujenzi wa Tanzania ya Viwanda.
8.
Mheshimiwa Spika, Baada
ya kusema hayo, ninapenda sasa kutoa maelezo kuhusu utekelezaji wa shughuli za
Wizara kwa mwaka 2017/18, Vipaumbele vya Wizara kwa mwaka 2018/19 pamoja na
maombi ya fedha ambazo zitaiwezesha Wizara yangu kutekeleza majukumu yake.
B: MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA
BAJETI NA MPANGO WA MAENDELEO KWA MWAKA WA FEDHA 2017/18
9.
Mheshimiwa Spika, katika
kutekeleza majukumu yake, Wizara imeendelea kuzingatia Sera, Mipango Mikakati
pamoja na makubaliano ya Kitaifa na Kimataifa yenye lengo la kuimarisha utoaji
wa huduma za afya nchini. Maeneo haya ya vipaumbele yameainishwa katika Dira ya
Taifa ya Maendeleo (2025), Mpango wa Maendeleo wa Muda wa Kati 2016/17 –
2020/21, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya 2015-2020, na
Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s 2030). Aidha, Wizara imezingatia
vipaumbele vilivyoainishwa katika Sera ya Afya (2007) na Mpango Mkakati wa IV
wa Sekta ya Afya (2015 – 2020); Sera ya Maendeleo ya Jamii (1996); Sera ya
Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000); Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali (2001); Sera ya Wazee (2003); na Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008).
10. Mheshimiwa
Spika, Katika mwaka wa fedha 2017/18, kupitia Fungu 52, Wizara yangu ilipanga
kutekeleza afua mbalimbali zenye lengo la kuboresha utoaji huduma za Afya
katika maeneo yafuatayo;
a) Kuimarisha
Huduma za Kinga, Tiba, na kuongeza usawa katika kutoa huduma za afya,
b) Kuimarisha
huduma za afya ya uzazi na mtoto ili kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na
watoto,
c) Kuimarisha
upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba, vitendanishi na chanjo katika vituo vya
kutolea huduma za afya,
d) Kuimarisha
miundombinu kwenye vyuo vya mafunzo ya afya kwa lengo la kuongeza udahili na
upatikanaji wa rasilimali watu,
e) Kuimarisha
matibabu ya kibingwa nchini kwa kuendeleza ujenzi, upanuzi, ukarabati wa
miundombinu na kufunga mitambo ya kisasa ya kutolea huduma za afya katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Benjamini Mkapa - Dodoma, Taasisi ya
Saratani Ocean Road, Hospitali Maalum za Mirembe na Kibong’oto; pia Hospitali
za Rufaa za Kanda; Kanda ya ziwa (Bugando), Kanda ya Kaskazini (KCMC),
Hospitali ya Rufaa ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya) na Kanda ya Kusini (Mtwara),
f) Kuimarisha
mazingira ya ubia na ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi (PPP) katika
utoaji wa huduma za afya,
g) Kuimarisha
huduma za lishe na upatikanaji wake katika jamii na vituo vya kutolea Huduma za
Afya,
h) Uimarishaji
wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuboresha
huduma za afya,
i) Kuhamasisha
wananchi kujiunga na Mifuko ya Bima za Afya kwa lengo la kuhakikisha wananchi wote
wanapata huduma za afya zenye uhakika.
11.
Mheshimiwa Spika, kupitia Fungu 53,
Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ilipanga kutekeleza kazi zifuatazo:
a)
Kuratibu utekelezaji na ufuatiliaji wa Mpango wa
Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/18 –
2021/22;
b) Kuimarisha upatikanaji wa
haki, maendeleo na ustawi watoto ikiwemo kwa watoto walio katika mkinzano wa
Sheria;
c)
Kuwezesha wazee wasiojiweza na watoto walio katika
mazingira hatarishi kupata huduma za msingi;
d)
Kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli za
kujiletea maendeleo kwa kuzingatia rasilimali walizonazo;
e)
Kuelimisha jamii hususan wanawake na katika ngazi
ya Halmashauri kujiunga na VICOBA na SACCOS kwa ajili ya kuwawesha kiuchumi;
f)
Kuwezesha utoaji wa huduma za ustawi wa jamii
katika makazi ya wazee, Makao ya Taifa ya Watoto Kurasini, mahabusu za watoto
na Shule ya Maadilisho; na
g) Kuboresha
mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika vyuo na Taasisi za Maendeleo na
Ustawi wa Jamii.
Mapato na Matumizi ya Fedha –
Fungu 52
12.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Fungu 52 (Afya), hukusanya mapato yake
kupitia huduma za tiba zitolewazo na hospitali zilizo chini yake, tozo za
huduma katika Taasisi mbalimbali, Bodi na Mabaraza, ada za uchangiaji wa gharama
za mafunzo, marejesho ya masurufu, malipo ya ununuzi wa vitabu vya maombi ya
zabuni, pamoja na makusanyo yatokanayo na utoaji wa huduma katika Taasisi na
Mashirika yaliyo chini ya Wizara. Hadi kufikia mwezi Machi 2018, Wizara pamoja
na Taasisi zake imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi 162,891,572,942 sawa na asilimia 72 ya lengo la mwaka la kukusanya kiasi cha Shilingi 227,041,160,573 kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato.
Mafanikio haya yametokana na utaratibu wa kulipia huduma kupitia benki,
uhamasishaji kuhusu kulipa maduhuli ya serikali, udhibiti wa makusanyo,
kuongezeka kwa ari ya utendaji kazi, uboreshwaji wa Huduma za Bima na
Kuimarishwa kwa mfumo wa malipo kwa njia ya Ki-elektroniki.
13. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Wizara iliidhinishiwa na
Bunge lako Tukufu kupokea na kutumia jumla ya Shilingi 1,077,701,892,000. Kati ya fedha hizo kiasi cha Shilingi 291,895,940,000 sawa na asilimia
27 ya bajeti yote ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, na Shilingi ni Shilingi 785, 805, 952,000 sawa na asilimia 72.9 kwa ajili ya utekelezaji
wa Miradi ya Maendeleo.
14. Mheshimiwa
Spika, Hadi kufikia Machi 2018, Wizara imepokea jumla ya Shilingi
617,507,623,167 sawa na asilimia 57 ya
bajeti iliyoidhinishwa ya Shilingi
1,077,701,892,000 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Aidha,
fedha zilizopokelewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida katika kipindi cha Julai
hadi Machi, 2018 ni Shilingi 216,736,325,825,824 sawa na asilimia
74 ya fedha zote zilizotengwa kwa
ajili ya matumizi ya kawaida kwa mwaka. Kati ya fedha hizo, Shilingi
68,814,900,939 zilitumika katika
Matumizi Mengineyo (OC) ikiwa ni sawa na asilimia 73.3 ya kiasi kilichotengwa na
Shilingi 147,921,424,885 zilitumika kulipia mishahara (Fungu 52) sawa na asilimia 65 ya kiasi cha fedha kilichotengwa.
Kwa upande wa Miradi ya Maendeleo, hadi kufikia Machi, 2018 kiasi cha Shilingi 400,771,297,343 kilipokelewa, sawa na asilimia 51 ya fedha
zilizoidhinishwa kutekeleza Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, kiasi cha Shilingi 79,756,079,206 ni fedha za ndani sawa asilimia 24 ya fedha
iliyoidhinishwa. Fedha za nje zilizopokelewa ni Shilingi 321,015,218,137.12 sawa na asilimia 71 ya fedha zilizoidhinishwa. Aidha Wizara ilipokea kiasi
cha Shilingi 82,515,009,463.82 na
kuzipeleka OR–TAMISEMI kwa ajili ya
ukarabati wa vituo vya afya ili viweze kutoa huduma za dharura ikiwa ni pamoja
na upasuaji wa akinamama wajawazito (CEmONC) ili kumtoa mtoto tumboni pindi
wanapokabiliwa na uzazi pingamizi. Kati ya fedha hizo Shilingi 63,015,009,462.82 ni kutoka Benki ya Dunia na Shilingi 19,500,000,000.00 kutoka Mfuko
wa Afya wa Pamoja (Health Basket Fund).
Mapato
na Matumizi - Fungu 53
15.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2017/18, Wizara kupitia
Fungu 53 (Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto), ilitarajia kukusanya kiasi cha Shilingi 2,101,874,000 kutokana na ada za wanafunzi kutoka katika
Vyuo nane vya Maendeleo ya Jamii vya Buhare, Uyole, Rungemba, Mlale, Misungwi,
Ruaha, Mabughai na Monduli; uuzaji nyaraka za zabuni na ada mbalimbali za
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2018 jumla ya Shilingi 1,775,466,155 sawa na asilimia 84 zilikusanywa.
16.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/18, Wizara
kupitia Fungu 53 ilitengewa jumla ya Shilingi 37,909,880,000. Kati ya fedha hizo, Shilingi 19,142,252,240 ni bajeti ya Mishahara, Shilingi 16,161,349,760 ni Matumizi Mengineyo na
Shilingi 2,606,278,000 ni kwa Miradi
ya Maendeleo. Hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2018, jumla ya Shilingi 18,352,527,400 sawa na asilimia 48 zilipokelewa. Kati ya fedha hizo, Shilingi 8,848,331,727 sawa na asilimia 55 ni Matumizi Mengineyo; Shilingi 8,470,927,127 sawa na asilimia 44 ni Mishahara ya Idara pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara;
na Shilingi 1,033,268,546 sawa na asilimia 40 fedha za Miradi ya
Maendeleo.
17.
Mheshimiwa
Spika, Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara kwa kipindi
cha Julai 2017 hadi Machi 2018 ulikuwa kama ifuatavyo:
UTEKELEZAJI
WA MAJUKUMU CHINI YA IDARA KUU YA AFYA
Chanjo
18. Mheshimiwa
Spika,
Katika kipindi cha Mwaka 2017/2018, Wizara ilisimamia shughuli za utoaji wa
chanjo kwa watoto ili kuhakikisha kuwa
malengo yaliyowekwa kitaifa na kimataifa yanafikiwa. Takwimu za Januari hadi
Desemba 2017 zinaonyesha kuwa asilimia
101.2 ya Watoto waliolengwa nchini walipatiwa chanjo zote muhimu ili
kuwakinga na magonjwa. Mnamo mwezi Desemba 2017, Serikali ya
Tanzania ilipongezwa Shirika la Afya Duniani na wadau wa Kimataifa wa
Chanjo kwa kufikia kiwango cha juu cha
chanjo kwa asilimia 97 ya uchanjaji watoto kwa chanjo ya pentavalent kwa
takwimu za mwaka 2016. Lengo la Mkakati wa Dunia kupitia Shirika la Afya
Duniani ni nchi kufikia kiwango cha uchanjaji wa asilimia 90. Mikakati ya Wizara imewezesha nchi yetu kufikia
kiwango hicho ambapo inakuwa nchi ya Tatu barani Afrika ikitanguliwa na Zambia yenye kiwango cha asilimia 99 ikifuatiwa na Rwanda yenye asilimia 98.
19. Mheshimiwa
Spika, Saratani
ya mlango wa kizazi ndio inayoongoza nchini kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa
na pia kusababisha vifo vya wanawake wengi.
Kwa mujibu wa Takwimu za Taasisi ya Saratani Ocean Road za mwaka 2016/17
Asimilia 32.8 ya wagonjwa wa saratani nchini ni wa saratani ya mlango wa kizazi
ikifuatiwa na saratani ya matiti yenye
asilimia 12.9. kwa bahati nzuri, saratani ya mlango wa kizazi inazuilika kwa
kuwapatia chanjo wasichana kuanzia miaka 9 hadi 14. Katika kukabiliana na
saratani hiyo, mwaka 2017/18 Serikali
imeanza kutoa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV Vacacine). Kutokana
na upatikanaji wa dozi kutoka kwa wazalishaji, kwa mwaka 2018 chanjo hiyo
imeanza kutolewa kwa wasichana wenye miaka 14, ambapo, hadi Desemba 2018,
Wizara imelenga kuwafikia wasichana 616,734
wa umri huo. Chanjo hiyo ni salama na inatumika katika nchi mbalimbali za
Afrika ikiwemo Rwanda, Uganda, Afrika ya Kusini, Zambia na Lesotho. Kupitia
Bunge lako Tukufu, nawasihi wazazi na
walezi wenye watoto kuhakikisha binti zetu wanapata chanjo hiyo muhimu ili
kuwakinga dhini ya saratani ya mlango wa kizazi.
Afya
na Usafi wa Mazingira
20. Mheshimiwa Spika,
Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa Kampeni ya Taifa ya Usafi wa
Mazingira inayotekelezwa katika Halmashauri zote nchini pamoja na kudhibiti
magonjwa ya mlipuko hususan kipindupindu. Shughuli zilizotekelezwa zimeainishwa
katika aya 22 mpaka 24 ya Hotuba
21. Mheshimiwa
Spika,
Hali ya ugonjwa wa Kipindupindu nchini inaendelea kudhibitiwa. Katika kipindi
cha Julai 2017 hadi Machi 2018 jumla ya wagonjwa wa kipindupindu 4,508 na vifo
92 viliripotiwa katika Mikoa ya Songwe, Dodoma, Ruvuma na Mbeya. Nitoe rai kwa
viongozi katika mikoa yote nchini kulifanya suala la kupambana na ugonjwa wa
kipindupindu kuwa ni agenda ya kudumu katika vipaumbele vyao.
22.
Mheshimiwa Spika,
Katika kuimarisha huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto nchini, Wizara
imeendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa miaka 5 wa mwaka 2016 hadi 2020
unaolenga kuboresha afya ya uzazi, mama, watoto na vijana pamoja na kupunguza
vifo vitokanavyo na uzazi kufikia 292 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka
2020. Katika kutekeleza mkakati huo, Wizara imezingatia maeneo makuu matatu
ambayo ni: huduma ya uzazi wa mpango,
huduma wakati wa ujauzito na huduma wakati wa kujifungua.
23.
Mheshimiwa Spika, huduma za uzazi wa mpango ni muhimu
katika kuimarisha afya ya mama na mtoto pamoja na kupunguza vifo vitokanavyo na
uzazi. Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, Wizara
imenunua na kusambaza dawa za uzazi wa mpango katika vituo vya huduma za afya
nchini. Aidha, jumla ya wateja 519,817 walifikiwa na huduma ya
uzazi wa Mpango kupitia utaratibu wa mkoba (out reach services) na 424,595 walipata huduma kutoka katika
vituo vya kutolea huduma za afya.
24.
Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa huduma ya afya wakati wa ujauzito ni afua
muhimu katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, kwani matatizo mengi yanaweza kuzuilika, kugundulika na
kutibiwa kama wanawake wajawazito watahudhuria kliniki ya wajawazito na kupimwa
na wahudumu wenye ujuzi ndani ya wiki 12 tangu wanapokuwa wamejigundua kuwa
wanaujauzito. Katika kipindi cha 2017/18, Wizara iliendelea kuhakikisha kwamba
huduma kwa wanawake wajawazito zinapatikana sambamba na kuelimisha wajawazito
kuhudhuria kliniki. Aidha, kulingana na taarifa kutoka vituo vya kutolea huduma
ya afya, hadi kufikia mwezi Februari 2018 asilimia
81.7 walihudhuria angalau mara moja, lengo likiwa ni kufikisha asilimia 70 ya
wanawake wajawazito kuhudhuria kliniki angalau mara 4 katika kipindi cha
ujauzito ifikapo mwaka 2020. Nitumie
fursa hii kuwahimiza wajawazito wote kuhudhuria kliniki kama inavyoshauriwa.
25.
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2017/18, Wizara kwa kushirikiana na wadau
imeendelea kuhamasisha na kuhimiza wanawake wajawazito kujifungulia kwenye
vituo vya kutolea huduma. Mwelekeo ni kwamba Idadi ya akinamama wanaojifungulia
katika vituo vya kutolea huduma inaendelea kuongezeka hadi kufikia asilimia 68.5 mwezi Machi 2018 katoka asilimia 64
mwaka 2015/16. Napenda kutoa wito
kwa wanawake wajawazito wote nchini, wajifungulie kwenye vituo vya kutolea
huduma ya afya ili kupunguza vifo na changamoto za uzazi kwa mama na mtoto.
26. Mheshimiwa
Spika, kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano
ni moja ya kipaumbele cha Wizara. Kulingana na Mpango Mkakati wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa 2016-2020, Serikali
imedhamiria kuwa ifikapo 2020 vifo vya watoto wa chini ya mwezi mmoja vipungue
kutoka 21 hadi 16 katika kila vizazi hai 1,000; vifo vya watoto wa chini ya
umri wa mwaka mmoja kutoka 45 hadi 25 katika kila vizazi hai 1,000 na vifo vya
watoto wa chini ya umri wa miaka mitano kutoka 54 hadi 40 katika kila vizazi
hai.
27.
Mheshimiwa
Spika, Wizara kwa
kushirikiana na Wadau wa Maendeleo imeendelea kuboresha miundombinu ya kutolea
huduma za afya katika ngazi ya Vituo vya Afya ili viweze kutoa huduma za
dharura za upasuaji ikiwa ni pamoja na upasuaji wa kutoa mtoto tumboni (CEmONC)
pindi mama mjamzito anapohitajika. Wizara kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI
inaboresha vituo vya afya takribani 208 (kama ilivyoainishwa katika hotuba ya
Ofisi ya Rais – TAMISEMI) ili kuviwezesha kutoa huduma za CEmONC. Hadi Machi
2018, maboresho ya vituo hivyo yalikuwa yapo
katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji. Maboresho haya yanahusu ujenzi wa
vyumba vya upasuaji (Theatres), wodi ya wakinamama wajawazito (Martenity/Labour
wards), vyumba vya maabara na nyumba za watumishi. Kukamilika kwa maboresho
haya kutaongeza idadi ya vituo vinavyomilikiwa na Serikali vyenye uwezo wa
kutoa huduma hiyo ya CEmONC kufikia 283 kati ya Vituo vya Afya 527. Hii itakuwa
sawa na asilimia 53.7 ya vituo vya afya vya umma vitakavyoweza kutoa huduma za
upasuaji wa dharura kutoka asilimia 21 mwezi Juni 2016.
28. Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu
imeendelea na juhudi za kudhibiti saratani za via vya uzazi (Reproductive cancers) ikiwemo saratani
ya mlango wa kizazi, saratani ya matiti na saratani ya Tezidume. Aidha, katika
kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kupima na matibabu ya Mabadiliko ya awali
ya Saratani ya Mlango wa kizazi na saratani ya matiti ambazo ndizo zinazoongoza
nchini, Wizara
kwa kushirikiana na wadau imeanzisha vituo
vipya 100 vya uchunguzi na tiba ya mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango wa
kizazi katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Songwe, Geita, Dodoma, Singida,
Manyara, Arusha, Tanga, Lindi, Mtwara, Simiyu, Mara na Ruvuma.
Udhibiti wa UKIMWI
29. Mheshimiwa
Spika,
katika kipindi cha Julai 2017 hadi Desemba 2017, jumla ya watu wapatao 5,164,297 walipimwa
VVU na kupewa majibu ya hali zao za afya, ambapo watu 145,104 (sawa na asilimia 2.8)
kati yao waligundulika kuwa na maambukizi na kuanzishiwa dawa za kufubaza
virusi vya UKIMWI. Aidha, takwimu za hadi Desemba, 2017 zinaonesha kuwa jumla
ya watu wanaoishi na VVU wapatao 965,081
walikuwa wanatumia dawa za kufubaza VVU, ikiwa ni sawa na asilimia 69 ya watu 1,400,000
wanaokadiriwa kuishi na virusi vya UKIMWI nchini na kati yao watoto walikuwa 55,304 ambao ni sawa na asilimia 5.7. Kutokana na takwimu hizo
Tanzania tumebakiza asilimia 21
kufikia lengo la dunia la asilimia 90
ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kuanzishiwa dawa za kufubaza VVU ifikapo
mwaka 2020. Wizara imeweka mikakati mbalimbali ili kufikia lengo hilo.
30. Mheshimiwa
Spika, Huduma
za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT),
zimeendelea kutolewa, ambapo, jumla ya akina mama wajawazito 1,967,260 sawa na asilimia 98.7% ya akina mama 1,993,639 walipatiwa huduma za ushauri
nasaha na upimaji wa VVU. Kati yao akina mama 79,242 sawa na asilimia 4 waligundulika kuwa wanaishi na VVU. Akina
mama 79,240 sawa na asilimia 99.9 ya akina mama wenye maambukizi ya
VVU walipatiwa dawa (ARV) kwa ajili ya kufubaza virusi vya UKIMWI. Hivi sasa,
maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ni asilimia 4.9 kutoka asilimia
12 mwaka 2011.
Huduma
za Udhibiti wa Kifua Kikuu na Ukoma
31.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea na mkakati wake wa
Udhibiti wa ugonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma ambapo katika kipindi cha Julai
hadi Machi 2017, Serikali ilinunua na kusambaza dawa za Kifua Kikuu na Ukoma. Katika kuhakikisha Serikali inaboresha matibabu ya
ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa watoto, mwezi Machi 2018, Wizara yangu ilizindua
matumizi ya dawa mpya za kifua kikuu kwa
watoto. Dawa hizi mpya ni za mseto (RHZ/RH) ulioboreshwa, zina ladha nzuri
ya matunda, zinayeyuka kwa urahisi zikiwekwa kwenye maji na hivyo hazihitaji
kukatwakatwa ili kupata dozi sahihi.
32.
Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu imeongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za ugunduzi wa ugonjwa wa kifua
kikuu kwa kutumia vipimo vya vinasaba (gene-xpert) katika wilaya zote
nchini ili kuongeza kazi ya kuwagundua wagonjwa wengi wa TB na kuwatibu. Kwa
mwaka 2017/18, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo ilinunua na
kusambaza mashine za “genexpert” 189 ikilinganishwa na mashine 66 zilizokuwepo
mwaka 2015. Mashine hizi zimesambazwa kwenye hospitali zote za rufaa
za kanda, mikoa, wilaya na baadhi ya vituo vikubwa vya afya. Teknolojia
ya mashine hizi inatuwezesha kupata majibu ndani ya masaa 2 badala ya kusubiri
kwa zaidi ya masaa 24 kama ilivyo kwa njia za kawaida za hadubini (Microscopes). Aidha, mashine hizi zina
uwezo wa kupima usugu wa dawa za kifua kikuu wakati huo huo wa upimaji wa
makohozi, na hivyo kugundua kifua kikuu sugu kwa urahisi zaidi.
33.
Mheshimiwa
Spika, Katika kudhihirisha nia ya serikali ya kushirikiana na
Sekta binafsi katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu hasa kuongeza
idadi ya wagonjwa wa TB wanaogunduliwa kutoka asilimia 40 hadi asilimia 70
mwaka 2020, Wizara yangu imekabidhi mashine za gene-xpert tano (5) kwa
hospitali binafsi za jijini Dar es Salaam. Hospitali
zilizopokea mashine hizi ambayo kila moja ina thamani ya Shilingi milioni 38 ni
Aga Khan, Hubert Kairuki, Regency Medical Center, TMJ na Hindul Mandal.
Tumeanza na hospitali hizi zenye viwango vikubwa vya wagonjwa wanaohudumiwa na
pia kwa kuzingatia utayari wa hospitali hizi katika kutoa huduma za kifua kikuu
sanjari na malengo ya Serikali yetu ya awamu ya tano ya Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha
huduma za afya zinawafikia wananchi wote. Kadhalika, ushirikishwaji huu wa Sekta Binafsi katika kutambua
wagonjwa wa kifua kikuu umeonesha ongezeko la wagonjwa wa TB wanaoibuliwa na
sekta binafsi kutoka wagonjwa 3,476 mnamo mwaka 2014 hadi wagonjwa 7,281 katika
mwaka 2017 ambao ni sawa na 10.4% ya wagonjwa wa TB waligunduliwa na sekta
binafsi. Nitumie fursa hii kuwashukuru
na kuwapongeza sekta binafsi kwa ushiriki wao katika kutokomeza TB nchini.
34.
Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu imeendelea kuongeza wigo wa huduma za matibabu ya wagonjwa wa kifua
kikuu sugu nchini. Katika kipindi cha mwaka 2017 hadi Machi 2018 Wizara
iliongeza vituo 41 na kufanya jumla ya vitu vinavyotoa huduma hiyo kufikia
vituo 63 ikilingalishwa na kituo kimoja cha hospitali Maalum ya Kibong’oto
mwaka 2015. Mikoa yenye vituo hivyo vilivyoweza kuanzisha matibabu ya
wagonjwa chini ya ugatuzi ni Dar es salaam, Kagera, Geita, Mtwara, Lindi,
Mbeya, Pwani, Morogoro, Tanga, Unguja, Tabora, Kigoma, Mwanza, Arusha, Rukwa na
Simiyu. Vile vile, Wizara imeanzisha matibabu ya muda mfupi kwa wagonjwa wa kifua kikuu sugu kufupisha
tiba hiyo kutoka miezi ishirini ya hapo awali mpaka miezi tisa kwa wagonjwa
wanoakidhi vigezo.
35. Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa ugonjwa
wa Ukoma,
Wizara ilifanya uchunguzi wa vimelea vya Ukoma katika ngazi ya jamii kwenye
Wilaya 6 zenye maambukizi makubwa katika mikoa ya Geita (Chato), Lindi
(Liwale), Mtwara (Nanyumbu), Morogoro (Kilombero) na Tanga (Mkinga na Muheza).
Katika zoezi hilo takriban watu 500
wamefanyiwa uchunguzi, ambapo watu 54
sawa na asilimia 10.8 waligundulika
kuwa na vimelea vya ugonjwa wa ukoma na kuanzishiwa matibabu, takriban watu 300 wamepatiwa tiba kinga.
Udhibiti wa Malaria
36.
Mheshimiwa Spika,
Malaria imeendelea kuwa sababu ya vifo vya wananchi wengi ambapo kwa takwimu za
Januari – Desemba 2017, jumla ya watu 5,592,844 wameugua ugonjwa huu, kati yao wagonjwa 4,421 walifariki kutokana na ugonjwa wa
Malaria. Katika kuendeleza juhudi za kupunguza maambukizi ya malaria nchini;
Wizara yangu imeendelea kutekeleza shughuli mbalimbali za udhibiti wa malaria
ikiwa ni pamoja na kununua dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi na kusambaza
katika vituo vya huduma za afya nchini. Ili kuendelea kuwakinga wananchi dhidi
ya malaria, na hasa kulenga makundi maalum; wajawazito na watoto chini ya mwaka
mmoja, Serikali imesambaza jumla ya vyandarua
4,726,763 kwa jamii bila malipo kupitia wanafunzi shuleni na kupitia
kliniki za wajawazito na watoto (Chandarua Kliniki).
37.
Mheshimiwa Spika, Katika kutekeleza Agizo la Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, kuhusu Afua
ya kuangamiza viluwiluwi vya mbu katika mazalia (larviciding), Wizara kwa
kushirikiana na OR-TAMISEMI imeratibu zoezi la usambazaji wa viuadudu vya kibailojia (biolarviciding) jumla ya lita 236,420 katika Halmashauri zote
nchini, na Halmashauri zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa afua katika
maeneo yao.
Udhibiti wa Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele
38.
Mheshimiwa
Spika, Kutokana na utekelezaji wa afua mbalimbali za kudhibiti
magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele zikiwemo zilizoainishwa katika aya 48
na 49 ya Hotuba, jumla ya Halmashauri 93
zimefanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa matende na
mabusha na hivyo kuondolewa kwenye
orodha ya Halmashauri zenye maambukizi
makubwa zinazoshiriki katika zoezi la Kingatiba kulingana na vigezo vya
Shirika la Afya Duniani (WHO). Haya ni mafanikio makubwa kwani Watanzania
wapatao 20,446,532 wanaoishi katika
halmashauri hizi hawapo tena katika hatari ya maambukizi ya magonjwa haya.
Huduma za Lishe
39.
Mheshimiwa Spika, Katika kupambana na utapiamlo nchini,
Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau wa Lishe imetoa matone ya nyongeza ya vitamin A kwa watoto wa kati ya
miezi sita na miaka mitano sambamba na dawa za minyoo kwa watoto wa umri kati
ya mwaka mmoja na miaka mitano. Aidha, Wizara
yangu imeendelea kutoa huduma za matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto
kupitia; kuongeza idadi yaHospitali zinazotoa matibabu ya utapiamlo, kuboresha
miundombinu ya hospitali kwenye wodi za kulaza watoto, kuimarisha mfumo wa
upatikanaji wa chakula dawa na vifaa vya kupimia hali ya Lishe pamoja na
kujengea uwezo wa watoa huduma.
Elimu ya Afya kwa Umma
40. Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii kutunza afya zao
dhidi ya magonjwa, kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kujenga tabia
inayozingatia kanuni za afya. Wizara kupitia mpango wa Elimu ya Afya kwa Umma
imeandaa mkakati wa mawasiliano utakaowezesha namna ya kuwasiliana kwa haraka
wakati wa majanga na milipuko ya magonjwa, tayari timu za mikoa ya mipakani
zimeelimishwa juu ya mkakati huo. Aidha, Wizara imekamilisha ujenzi wa studio
ya radio na
televisheni ambavyo vimeanza kurekodi vipindi vitakavyorushwa nchi nzima kwa
ajili ya kuelimisha jamii ya Watanzania kuhusu masuala mbalimbali ya afya.
HUDUMA ZA TIBA
41. Mheshimiwa
Spika, Wizara imeendelea kusimamia upatikanaji wa huduma za
afya kupitia vituo vya kutolea huduma nchini vikiwemo vya Serikali, binafsi na
mashirika ya dini. Hadi kufika Machi 2018, huduma za afya zimeendelea kutolewa
katika vituo vya kutolea huduma za afya 7,437
ikilinganishwa na vituo 7,284 mwezi
Juni 2017. Aidha, katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, jumla ya Vituo
binafsi 153 vya kutolea huduma za Afya vilisajiliwa.
Uimarishaji wa Huduma za Matibabu ya Kibingwa
42. Mheshimiwa
Spika, Katika mwaka 2017/18, moja ya jukumu la kipaumbele kwa
Wizara ilikuwa ni kuendelea kuboresha na kuimarisha huduma za matibabu ya
kibingwa yatolewayo nchini. Maboresho hayo, yanalenga katika kupunguza idadi ya
wagonjwa wanaopewa rufaa ya matibabu nje ya nchi ili kupunguza gharama kubwa
kwa Serikali katika kupeleka wagonjwa nje ya nchi. Hadi kufikia mwezi Machi
2018, idadi ya Wagonjwa waliopewa rufaa ya Matibabu nje ya nchi ilipungua na
kufikia Wagonjwa 103 ikilinganishwa
na wagonjwa 304 mwaka 2016/17.
Mafanikio haya ni kutokana na maboresho yaliyofanyika katika Hospitali zilizo
chini ya Wizara ambapo kwa hivi sasa zimeongezewa uwezo wa kutoa huduma za
Kibingwa ambazo awali hazikuwa zikitolewa hapa nchini na hivyo kulazimu
wagonjwa kupatiwa rufaa nje ya nchi. Jumla
ya wagonjwa 1,090,863 walihudumiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH), Taasisi ya Mifupa (MOI), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI),
Taasisi ya Saratani Ocean Road, Hospitali ya Benjamin Mkapa, Hospitali ya
Magonjwa ya Akili Mirembe, Hospitali ya Magonjwa ya Kifua Kikuu Kibon’goto na
Hospitali za Rufaa za Kanda za Mbeya, KCKM na Bugando. Mchanganuo wa idadi
ya wagonjwa kwa kila Hospitali umeoneshwa katika Kiambatisho Namba 2 cha Hotuba yangu.
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
43.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2017/18, Hospitali ilifanya
ukarabati wa jengo la kutolea huduma za upandikizaji wa Figo na ununuzi wa
vifaa Tiba kwa ajili huduma za
upandikizaji wa figo iliyoanza kutolewa Mwezi Novemba 2017 ambapo Mgonjwa
mmoja (1) alipatiwa huduma hiyo na kwa sasa wagonjwa watano (5) wamepangwa
kupatiwa huduma hii mwishoni mwa Mwezi Aprili 2018. Hatua hii imepunguza gharama za kupandikiza figo kwa mgonjwa mmoja
nje ya nchi kutoka wastani wa Shilingi
milioni mia 100 hadi milioni 20.
44.
Mheshimiwa Spika, Hospitali imeanzisha huduma za upandikizaji wa vifaa vya kusaidia kusikia (Cochlea implant),
hadi kufikia mwezi Machi 2018, wagonjwa sita (6) walipata huduma ya kuwekewa
vifaa vya usikivu. Huduma ya kupandikiza vifaa vya kusaidia kusikia inatolewa
kwa wastani wa Shilingi milioni 36
kulinganisha na Shilingi milioni 80 hadi 100 ambazo zingetumika endapo mgonjwa
angepelekwa nje ya nchi.
45. Mheshimiwa
Spika, ukusanyaji wa mapato ya Hospitali kwa kipindi cha Julai 2017 hadi
Machi, 2018 umeongezeka na kufikia kiasi cha Shilingi bilioni 46.51 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 31.91
zilizokusanywa katika kipindi kama hicho 2016/17. Hii ni sawa na ongezeko
la asilimia 45.7. Mafanikio haya yamewezesha hospitali kukamilisha miradi
yake mbalimbali iliyoainishwa katika aya 59 ya Hotuba.
Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI)
46. Mheshimiwa
Spika, Mnamo mwezi Februari 2018, Taasisi kwa mara ya kwanza imeweza kufanya upasuaji wa mgongo kwa njia
ya matundu (Laparascopy) kwa kushirikiana na madaktari wa Hospitali ya BLK ya
India. Upasuaji huo ulifanyika kwa mafanikio makubwa, lengo mahsusi ikiwa
ni kuwapatia weledi madaktari wa MOI ili waweze kufanya upasuaji huo.
Aidha,katika mwaka 2017/18, Taasisi ilikamilisha jengo la MOI awamu ya III
pamoja na ununuzi wa Vifaa tiba mbalimbali kutokana na fedha Shilingi Bilioni 16.5 zilizopokelewa
mwishoni mwa mwaka wa fedha 2016/2017. Kazi zilizofanyika zimeainishwa katika
aya 64 ya Hotuba. Makusanyo katika Hospitali hadi mwezi Februari, 2018 yamefikia kiasi cha Shilingi 10,807,695,141.93 ukilinganisha na kiasi
cha Shilingi 6,707,172,559.43 zilizokusanywa
kuanzia mwezi Julai 2016 hadi mwezi
Februari, 2017.
Taasisi ya Moyo - Jakaya Kikwete (JKCI)
47.
Mheshimiwa
Spika, Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete ilihudumia jumla ya wagonkwa wenye matatizo ya moyo 42,029. Kati ya
hao, wagonjwa 111 walifanyiwa upasuaji ambao watu wazima walikuwa 52 na watoto
walikuwa 59. Aidha wagonjwa 157 walipatiwa matibabu kwa njia ya upasuaji wa moyo kupitia mishipa ya damy (cardiac
catheterization). Hivi sasa Taasisi ina
uwezo wa kutoa huduma za upasuaji za ubingwa wa hali ya juu kwa asilimia 85 kwa
huduma za awali ambazo awali zilikuwa zikipatikana nje ya nchi. Hali hii
imesaidia kupunguza rufaa za wagonjwa wa moyo nje ya nchi na kuipunguzia
Serikali gharama ambapo hadi kufikia March 2018 wagonjwa wa mouo waliopeleela
India ni 12 kutoka wagonjwa 43 kwa mwaka 2016/17. Taasisi kwa kushirikiana na Madaktari
rafiki wa nchi za Marekani, India, Italy, Israel na Australia walifanya kambi
maalum za matibabu ya kibingwa ya moyo kwa watoto na watu wazima nchini kwa
mafanikio makubwa kama ilivyoainishwa katika aya 66 mpaka 68 ya Hotuba. Aidha,
Taasisi imeweza kukusanya mapato ya jumla ya Shilingi 8,462,092,000 Katika kipindi cha hadi Machi 2018
ikilinganishwa na kiasi cha Shilingi
4,105,000,000.00 kilichokusanywa katika kipindi hicho mwaka 2016.
Taasisi
ya Saratani Ocean Road (ORCI)
48. Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu imeendelea kuboresha huduma kwa wagonjwa wa
Saratani ambapo hadi kufikia mwezi Machi 2018, Taasisi imeboresha tiba za
mionzi ya nje kwa kufunga kifaa kiitwacho 'multi-leaf
collimator' katika mashine ya EQ80 ambacho kimenunuliwa kwa kushirikiana na
Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA). Aidha, Taasisi imenunua vyanzo
vipya vya mionzi kupitia Bohari ya Dawa kwa gharama ya Shilingi 473,363,437.50. Hatua hii imeboresha utoaji wa tiba ya
mionzi ya ndani kwa kutibu wagonjwa 70
kutoka wagonjwa 30 kwa siku. Vile
vile, Taasisi inaendelea kufunga mashine
za tiba mpya na za kisasa za mionzi aina ya “Linear
Accelerator”, (LINAC) 2 na ‘CT
Simulator’ (1) ambazo zimenunuliwa kwa gharama ya Shilingi 9,500,000,000. Mashine hizo zitaiwezesha Taasisi kutoa
huduma ya matibabu ya mionzi na kupunguza muda wa wagonjwa kusubiria tiba
kutoka wiki 6 sasa kufikia wiki 2 na kuongeza ufanisi katika tiba
inayotolewa. Vilevile, Taasisi tayari imewapeleka mafunzoni nje ya nchi
watumishi 7 kwa ajili ya kuongeza ujuzi wa kutumia mashine hizo ambao ni
Madaktari bingwa 2, Wataalamu wa tiba ya mionzi 2, Medical physicist 2 na Bio-engineer
1.
49. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2017/18, Taasisi imeanzisha huduma za wodi
za binafsi ambayo ina vitanda 4 vya VIP na vitanda 20 vya binafsi. Hatua
hii imesaidia kuboresha huduma kwa wagonjwa wenye uhitaji huo na pia kuongeza
mapato. Lengo la huduma hizi ni kuhakikisha kuwa wananchi wenye uwezo wa
kuchangia gharama wanakaa katika wodi binafsi. Kukamilika kwa wadi binafsi kumechangia
kuongezeka kwa makusanyo ya Taasisi, ambapo katika kipindi Julai 2017 hadi
Machi 2018, jumla ya Shilingi 86,622,300
zilikusanywa ikilinganishwa na kiasi cha Shilingi
40,320,000 kilichokusanywa kwa kipindi cha mwaka 2016/17. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 53.
Hospitali ya Benjamin Mkapa –Dodoma
50.
Mheshimiwa Spika, Katika
kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa, mnamo tarehe 22/3/2018, Hospitali
kwa kushirikiana na TOKUSHIKAI Medical group kutoka nchini Japan, ilifanikiwa kufanya upandikizaji figo kwa mara ya
kwanza kwa mgonjwa mmoja mwenye umri wa miaka 51. Hali ya mgonjwa
inaendelea vizuri na amepewa ruhusa kwenda nyumbani. Aidha, Matayarisho ya kuanzisha huduma za upasuaji wa moyo
yapo katika hatua za mwisho za ukamilishwaji. Vile vile, Hospitali iko katika
hatua za mwisho za kuanzisha huduma ya
kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo kwa kutumia mashine maalum (Hemodialysis). Pia, hospitali
imefanikiwa kuanzisha huduma za chumba cha wagonjwa mahututi (ICU). Upatikanaji
wa dawa katika hospitali ilikuwa kwa asilimia
95.2 kwa kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018. Uwezo wa hospitali
kukusanya mapato umeendelea kuimarika ambapo jumla ya Shilingi 1,892,978,585 kimekusanywa hadi Machi 2018 ukilinganisha
na Shilingi 794,162,415
zilizokusanywa katika kipindi cha Julai 2016 hadi Februari 2017 kwa mwaka 2016/17.
Hospitali
ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe
51. Mheshimiwa
Spika, Hospitali ya Mirembe na Tasisi ya Isanga imeendelea
kutoa huduma kwa wagonjwa wa afya ya akili ambapo hali ya upatikanaji wa dawa
imeendelea kuimarika na kufikia zaidi ya asilimia
90 kwa dawa muhimu za magonjwa ya akili. Aidha, hospitali imeendelea kutoa
huduma za kibingwa kwa wagonjwa wa akili wa kawaida na wagonjwa wa akili walio
na tuhuma za uvunjaji wa sheria kwa kuwafanyia uchunguzi, kutoa ushauri kwa
mahakama, Tiba kwa umeme, Tiba kwa vikundi, Tiba kwa familia, Tiba kwa maongezi
na Tiba kwa kazi (Occupational Therapy) kwa wataalamu wa kada mbalimbali
ikiwemo madaktari bingwa wa afya ya Akili (Psychiatrist), Saikolojia (Clinical
Psychologist), Mishipa ya fahamu (Clinical Neurologist) na wengine. Vile vile,
katika mwaka 2017/18, hospitali imeendelea na ujenzi wa Jengo la kuhudumia
waathirika wa Dawa za kulevya lililopo chini ya Hospitali ya Mirembe katika
eneo la Itega ambapo mkandarasi yupo katika eneo husika anaendelea na
kukamilisha ujenzi ili huduma zianze kutolewa mapema.
Hospitali ya Rufaa ya Magonjwa ya Kifua
Kikuu- Kibong'oto
52. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2017/18, Hospitali iliendelea kutoa huduma za utambuzi na matibabu ya Kifua kikuu, Kifua kikuu sugu,
VVU na magonjwa mengine ya kuambukiza. Aidha, Hospitali imeweza kutoa elimu kwa
wataalamu 239 (Madaktari, wauguzi, wataalam wa maabara pamoja na wafamasia)
kutoka mikoa mbalimbali nchini kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kuanzisha
matibabu ya kifua kikuu sugu (Multi-Drug
Resistant TB, MDR TB). Pia Hospitali imeweza kuanzisha jengo la kutolea
huduma kwa waathirika mahala pa kazi (Occupational
Health Services). Aidha, Wizara kwa
kushirikiana na Southern African
Development Community (SADC) imeanzisha huduma za afya kwa wachimbaji
Madini na familia za Wachimbaji Madini katika Hospitali hii.
Hospitali ya Rufaa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mbeya
53.
Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha 2017/18, Hospitali imeendelea
kuboresha huduma za kibingwa kwa kuongeza miundombinu ya kutolea huduma kama
ilivyoainishwa katika aya 82 ya
Hotuba. Upatikanaji wa dawa katika hospitali umekuwa katika kiwango cha asilimia 95 hivyo wananchi wameondolewa
usumbufu wa kufuata dawa nje ya hospitali. Ukusanyaji wa mapato katika kipindi
cha Julai 2017 hadi Machi 2018 ulikuwa Shilingi
9,931,439,974.57 ukilinganisha na Shilingi
5,607,223,511.78 kwa mwaka 2016/17.
Hospitali
ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando
54. Mheshimiwa
Spika, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa, Bugando imeendelea
kutoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa kutoka mikoa 8 ya Kanda ya Magharibi na
Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Geita, Mara, Kagera, Simiyu, Kigoma, Shinyanga
na Tabora. Kwa kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, hospitali ilifanya
upasuaji kwa wagonjwa 72 wenye
matatizo ya Saratani ya Utumbo mpana, saratani za tumbo, magonjwa ya pua na koo
pia uti wa mgongo. Upasuaji huu ulifanywa na Madaktari wazalendo kwa
kushirikiana na madaktari kutoka Marekani (Mending Kids). Pia, Hospitali
imenunua Mashine ya kutibu mionzi ya ndani (Brachytherapy)
kwa kushirikiana na Shirika la nguvu la Atomiki Duniani (IAEA). Kuhusu Huduma
ya tiba ya saratani, jumla ya wagonjwa 131
wa saratani ya mlango wa kizazi walipatiwa huduma ya tiba ya saratani kwa
njia ya mionzi (Radiotherapy). Vilevile, Hospitali imenunua mashine 2 za vipimo
vya moyo na 1 ya ultrasound, pamoja na mashine ya CT Scan (128 slice) kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.7 kutokana na mapato ya ndani.
Hospitali ya Rufaa ya Kanda Kaskazini (KCMC)
55. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2017/18, Hospitali imeendelea kuboresha na
kutoa huduma kwa wananchi wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Tanga
ambapo Hospitali imeweza kuhudumia wagonjwa 1,123 wa saratani ambapo wagonjwa 47 walipatiwa huduma shufaa
(Palliative care). Aidha, kwa kuzingatia umuhimu wa elimu kwa jamii juu ya
maradhi ya saratani, Hospitali kwa kushirikiana na Taasisi ya “Mission Eine
Welt” ya nchini Ujerumani, imeanzisha kampeni maalum mwezi Oktoba 2017
ijulikanayo kama PrevACamp yaani Prevention
and Awareness Campaign yenye lengo la kutoa elimu juu ya saratani,
kuainisha mila na imani potofu na kufanya uchunguzi wa viashiria vya awali vya
saratani.
Hospitali za Rufaa za Mikoa
56.
Mheshimiwa Spika, Uendeshaji wa
Hospitali za Rufaa za Mikoa ulikuwa unasimamiwa na kuratibiwa na OR-TAMISEMI.
Hata hivyo, baada ya maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa tarehe 25 Novemba 2017, usimamizi na
uendeshaji wa Hospitali hizi sasa upo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Hospitali za Rufaa za Mikoa zilizopo ni 28. Katika
kipindi cha Julai 2017 hadi 2018, jumla ya wagonjwa 1,637,835 walihudumiwa
katika Hospitali ya Rufaa za Mikoa ya Mount Meru (Arusha), Dodoma General
(Dodoma), Kitete (Tabora), Shinyanga, Geita, Singida, Mpanda (Katavi), Mawenzi
(Kilimanjaro), Bombo (Tanga), Morogoro, Ligula (Mtwara), Sokoine (Lindi),
Maweni (Kigoma), Sekou Toure (Mwanza), Mwananyamala, Amana, Temeke (Dar es
Salaam), Songwe, Kibena (Njombe), Iringa, Tumbi (Pwani), Sumbawanga ( Rukwa),
Bariadi (Simiyu), Musoma (Mara), Songea (Ruvuma), Mbeya, Babati (Manyara) na
Bukoba (Kagera).
57.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeweka mikakati ya muda
mfupi, muda wa kati na mrefu ili kuhakikisha kwamba huduma muhimu za kibingwa
za Upasuaji (General Surgery), Magonjwa ya Wanawake na Uzazi
(Obstetrics & Gynaecology), Magonjwa ya Watoto (Paediatrics & Child
Health), Magonjwa ya ndani (Internal Medicine), Magonjwa ya Kinywa na Meno
(Dentistry) na Radiolojia (Radiology) zinazotolewa katika Hospitali hizo
zinaboreshwa. Mikakati hiyo ni pamoja na kuboresha
miundombinu ya kutoa huduma, kuongeza idadi ya madaktari bingwa, kuboresha
upatikanaji wa dawa, kupanga kwa uwiano watumishi wa Hospitali za
Rufaa za Mikoa kwa kuzingatia huduma na uzito wa kazi zinazotolewa na hospitali
hizo, kuanzisha na kuboresha huduma za afya kwa njia ya masafa (telemedicine) kwa kila Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa na kufanya huduma hiyo kutumika kama kiunganishi kati ya
Hospitali hizo na Hospitali za Rufaa za Kanda na Taifa, kuboresha utoaji wa
huduma za uchunguzi wa maabara na radiolojia kwa kupanua na kuimarisha
miundombinu ya huduma za uchunguzi ikiwa ni pamoja na kununua na kuweka vifaa
vya kisasa vya maabara na radiolojia.
Udhibiti wa
Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (NCDs)
58. Mheshimiwa
Spika, Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba kumekuwa na
ongezeko la Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza hapa nchini. Utafiti wa viashiria vya
magonjwa yasiyo ya kuambukiza uliofanywa na Wataalam wa Wizara kwa kushirikiana
na Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) mwaka 2012, ulionesha kuwa
kuna ongezeko kubwa la viashiria vinavyosababisha magonjwa yasiyo ya
kuambukiza. Utafiti huo ulionesha kuwa asilimia 15.9 ya wananchi wanavuta
sigara, asilimia 29.3 wanakunywa pombe, asilimia 97.2 wanakula mboga mboga na
matunda chini ya mara tano kwa wiki. Aidha, utafiti ulionesha kuwa, asilimia 26
ya wananchi ni wanene kupita kiasi, asilimia 26 wana lehemu nyingi mwilini,
asilimia 33.8 wana mafuta mengi mwilini, asilimia 9.1 wana kisukari na asilimia
25.9 wana shinikizo kubwa la damu. Utafiti pia ulionesha kwamba, asilimia 25 ya
wananchi waliohojiwa hawajishughulishi na kazi zinazotumia nguvu na hawafanyi
mazoezi yeyote.
59. Mheshimiwa
Spika, mapambano dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza
yamekuwa yakiendelea ndani ya Wizara yangu na yamejikita zaidi katika masuala
ya Kinga, kama tunavyofahamu kuwa Kinga
ni bora kuliko Tiba. Tangu kuanzishwa kwa kampeni ya “Afya Yangu Mtaji Wangu” iliyozinduliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara
imeendelea kuhimiza jamii kuhusu umuhimu wa kufanya mazoezi mara kwa mara
sambamba na kujiepusha na visababishi vingine vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza
ikiwemo ulevi kupita kiasi na uvutaji wa sigara na tumbaku. Aidha, Wizara
imeendelea kushirikiana na Wadau kufanya Kampeni za uchunguzi wa magonjwa
yasiyo ya kuambukiza katika Mikoa yote. Nitumie
fursa hii kulipongeza Bunge lako tukufu kwa kuanzisha Jukwaa la Waheshimiwa
Wabunge la Kupambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza ili waweze kupata elimu juu
ya namna ya kujikinga na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza na kuwaelimisha wananchi
juu ya magonjwa hayo.
Upatikanaji
wa Damu Salama
60. Mheshimiwa Spika, Katika kuhakikisha
upatikanaji wa uhakika wa damu salama, Mpango wa Taifa wa Damu Salama
umeendelea kukusanya, kuhifadhi na kusambaza damu salama katika vituo vya
kutolea huduma za afya. Katika kipindi cha kuanzia Julai 2017 hadi Machi 2018
Mpango ulifanikiwa kukusanya idadi ya chupa za damu 233,953 ambazo ni sawa na asilimia
101 ya lengo la makusanyo kwa mwaka ambalo lilikuwa ni kukusanya chupa za
damu 230,000. Nitumie
Bunge lako Tukufu kuwashukuru wananchi wote wanaojitolea kuchanga damu. Aidha,
nitoe rai kwa watanzania kuchangia damu mara kwa mara ili kuokoa maisha ya
wagonjwa hasa wanawake wajawazito na watoto wa umri chini ya miaka 5.
Upatikanaji
wa Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba
na Vitendanishi
61. Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, Wizara yangu imeendelea
kuhakikisha kwamba hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na
vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya vya umma inaendelea
kuimarika. Hali ya upatikanaji wa dawa,
vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika Bohari ya Dawa (MSD) imeendelea
kuimarika hadi kufikia wastani wa asilimia
81 kwa Dawa muhimu 135. Aidha, katika kipindi hicho, hali ya upatikanaji wa
dawa, vifaa, vifaa tiba, vitendanishi na chanjo ilifikia asilimia 92 kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Vilevile, kutokana na kuendelea kuwasili kwa dawa, vifaa, vifaa tiba,
vitendanishi na chanjo nchini, na kwa mujibu wa mikataba iliyopo kati ya
wazalishaji na Bohari ya Dawa, hali ya upatikanaji wa dawa kwenye hospitali
inatarajiwa kuimarika na kufikia asilimia 89 ifikapo mwishoni mwa mwezi Aprili
2018.
62. Mheshimiwa Spika, Katika kutekeleza maagizo ya
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuanzisha viwanda vya
dawa Nchini ili kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, Wizara yangu kwa
kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji iliweza kuandaa
mkutano mkubwa kwa lengo la kuwaleta pamoja wawekezaji wenye nia ya kuwekeza
katika viwanda vya dawa na vifaa tiba. Jumla ya wadau mia nne thelathini (430) walihudhuria mkutano huo na wawekezaji
thelathini na nane (38) walijitokeza
kwa nia ya kuwekeza katika uzalishaji wa dripu (infusion), uzalishaji wa bomba za sindano, uzalishaji wa
vifungashio vya dawa, uzalishaji wa bidhaa za pamba zinazotumika hospitalini na
uzalishaji wa dawa za kuhifadhi maiti. Uwepo wa Viwanda hivyo utawezesha Serikali kuokoa fedha nyingi za kigeni
zinazotumika kuagiza dawa toka nje ya nchi. Jitihada hizi zitasaidia kuongeza
uzalishaji wa ndani ambao kwa sasa hivi ni asilimia
6 hivyo na kupunguza kiwango cha uagizaji wa dawa nje ya nchi
ambao kwa sasa ni asilimia 94.
UHAKIKI UBORA WA HUDUMA ZA AFYA
63.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kufanya Uhakiki na Ukaguzi kwa vituo vya kutolea huduma
za Afya. Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, Wizara ilifanya zoezi la tathmini ya mara ya pili
(re-assessment) ya kutoa nyota kulingana na ubora kwa Vituo vya Kutolea Huduma
za Afya ya Msingi (Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali katika
Halmashauri/Wilaya) katika mikoa 14 ya Dar es Salaam, Iringa, Geita, Kagera,
Katavi, Kigoma, Mara, Mwanza, Pwani, Tanga, Tabora, Singida, Simiyu na
Shinyanga. Matokeo yanaonesha vituo 180 sawa na asilimia 4.7 tu ndivyo vimepata nyota sifuri na Vituo 749 sawa na
asilimia 19.4 vilipata nyota 3 na zaidi ukilinganisha na matokeo ya tathmini ya awali ya mwaka 2016 ambapo jumla
ya vituo 1,244 sawa na asilimia 33 ya vituo vyote 3,713
vilivyofanyiwa tathmini ya ubora katika mikoa vilipata nyota sifuri na vituo 62
sawa na asilimia 2 vilipata
nyota 3 au zaidi. Matokea haya yanaonyesha kuimarika kwa ubora wa huduma za
afya katika vituo hivyo ambako ndiko wananchi wengi wanapata huduma za afya.
RASILIMALI
WATU KATIKA SEKTA YA AFYA
64.
Mheshimiwa Spika, Katika kuongeza idadi ya wataalamu wa Afya nchini,
Wizara imeendelea kushirikiana na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi NACTE
katika kusimamia ubora wa mafunzo ya kada za Afya zisizo katika kiwango cha
shahada.Katika kipindi cha kuanzia Julai 2017 hadi Machi 2018, jumla ya
wanafunzi 16,214 walichaguliwa
kujiunga na vyuo vya Afya. Kati ya hao wanafunzi 6,564 walichaguliwa kwenye vyuo vya Serikali na 9,650 kwenye vyuo binafsi katika
programu za Uuguzi na Ukunga, Sayansi Shirikishi za Afya na wahudumu Afya ya
Jamii. Aidha, Jumla ya wanafunzi 23,098
walifanya mitihani ya kuhitimu katika kipindi hiki, kati yao 10,669 ni wa Sayansi Shirikishi za
Afya, 7,300 wa Uuguzi na Ukunga na
wa Wahudumu Afya ya Jamii 5,129.
65.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa
Maendeleo katika kutoa ufadhili wa mafunzo ya kibingwa ya muda mfupi na muda
mrefu yanayolenga kuwajengea uwezo wa kiutendaji watumishi wa sekta ya Afya.
Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018 jumla ya Watumishi 376 wameendelea kulipiwa gharama za masomo yao ndani na
nje ya nchi katika ngazi ya shahada ya Uzamili hususan Madaktari Bingwa katika
fani za kipaumbele za upasuaji, magonjwa ya wanawake na uzazi, magonjwa ya
watoto, magonjwa ya ndani na radiolojia.
66.
Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka 2017/18 ,Wizara yangu,
ilipokea kibali cha ajira ya watumishi 3,152
wa kada za afya kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora. Kibali hicho kilikuwa na nafasi za Madaktari Daraja la II 45, Madaktari Bingwa (Medical
Specialist) 24, Madaktari Washauri
(Medical Consultant) – 2, Wauguzi
Daraja la II 137 na kada nyingine za
Afya 3,081 ambapo mchakato mzima wa
kujaza nafasi za ajira ambazo Wizara ilipewa ulikamilika na Watumishi wote
walipatikana isipokuwa Madaktari Washauri. Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya
Rais, TAMISEMI ilishawapangia Vituo vya kazi Watumishi hao. Aidha Katika
kipindi hiki jumla ya Wataalam wa kigeni 35
walipata ajira katika taasisi mbalimbali za Serikali.
67.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu, imeendelea kuboresha mazingira ya
kufanyia kazi kwa watumishi ambao wanafanya kazi katika maeneo yenye mazingira
magumu ili kuwapatia motisha ili kuendelea kutoa huduma za afya katika maeneo
hayo. Katika kipindi cha Julai hadi Machi 2018 jumla ya nyumba 30 zimejengwa na
kukamilika katika Halmashauri tatu (3) za mkoa wa Manyara, ambazo ni ;
Halmashauri za Kiteto 10, Simanjiro 10 na Hanang nyumba 10. Kukamilika kwa nyumba hizo kumeongeza idadi
ya nyumba za watumishi zilizojengwa kupitia mradi huu wa ‘Global Fund’ na
kufika nyumba 480 katika maeneo yenye mazingira magumu.
UGHARAMIAJI WA HUDUMA ZA AFYA
68.
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa
kushirikiana na OR-TAMISEMI pamoja na Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya inaendelea na utekelezaji wa mpango wa Mfuko wa Afya
ya Jamii (CHF). Hadi kufikia Machi 2018, Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF)
ulikuwa na jumla ya kaya 2,096,692
zilizojiunga ukilinganisha na kaya 2,030,666
zilizokuwa zimejiunga mwaka 2016/17. Aidha, wanufaika wameongezeka kutoka 12,183,996 mwaka 2016/17 hadi kufikia
wanufaika 12,580,149 Machi 2018 sawa
na asilimia 25 ya Watanzania wote. Vilevile, katika kuchangia juhudi za wananchi
wanaochangia CHF na kuboresha huduma zitolewazo, Serikali hutoa malipo ya tele kwa tele kwenye Halmashauri
kulingana na kiwango cha makusanyo ya CHF.
Malipo yaliyofanyika kwa Halmashauri kwa kipindi cha kuanzia Julai 2017
hadi Machi 2018 ni Shilingi bilioni 1.4. na hivyo kuwezesha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kulipa malipo ya Tele kwa Tele
yenye jumla ya Shilingi bilioni 15.8
kwa Halmashauri mbalimbali nchini tangu Mfuko ulipokabidhiwa jukumu hili mwezi
Julai 2009.
69.
Mheshimiwa Spika, Serikali ipo katika hatua za kuhakikisha inafikia
malengo ya afya kwa wote (Universal Health Coverage) ambapo kila mwananchi
atakuwa na uhakika wa upatikanaji wa huduma bora za afya bila kuwa na kikwazo
cha kifedha. Lengo ni kuwa ifikapo mwaka 2020 asilimia 70 ya wananchi wawe wamejiunga na mifuko ya Bima ya Afya.
Hali iliyopo sasa kuwa ni takribani asilimia
32 ya watu wote ndiyo waliopo katika mfumo wa Bima za Afya nchini. Nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge, kwa nafasi zao na
ushawishi mkubwa walionao katika jamii tunayoishi, kuendelea kuwaelimisha
wananchi wote umuhimu wa kujiunga na kuchangia katika mfuko huo wa bima ya afya
ili waweze kupata huduma za tiba bila kikwazo cha fedha.
70.
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa
kushirikiana na OR-TAMISEMI imeanza utekelezaji wa azimio la kupeleka fedha
moja kwa moja katika Vituo vya kutolea huduma za Afya nchini (Direct Health
Facility Financing (DHFF) badala ya kuzipeleka kwenye Halmashauri zao. Hatua
hii imelenga kuongeza ufanisi wa matumizi ya fedha za afya na kusogeza huduma
karibu zaidi na wananchi. Utekelezaji wa azimio hili umeanza katika kipindi cha
2017/2018 ambapo fedha za Mfuko wa Pamoja wa Afya zilizotengwa kwa ajili ya
matumizi ya vituo vya kutolea huduma za Afya zilipelekwa moja kwa moja kutoka
Hazina kwenda katika Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati. Jumla ya Shilingi 45,751,004,800 zimetolewa na
kupelekwa katika vituo 5,170. Hatua
hii imechangia kuboresha upatikanaji wa fedha katika vituo kwa wakati na
kusaidia vituo kupanga mikakati ya kuboresha huduma na kuleta ufanisi.
TEKNOLOJIA
YA HABARI NA MAWASILIANO
71.
Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa eHealth strategy 2013-2018. Katika mwaka
2017/18, Wizara kwa
kushirikiana na OR-TAMISEMI na Taasisi ya Bill and Melinda Gates Foundation
kupitia mdau wa maendeleo PATH ilizindua Mpango wa Uwekezaji (Digital Health
Investment Recommendation Roadmap). Mpango huu umeainisha vipaumbele
vinavyohitajika vya matumizi ya mifumo ya kielektroniki ili kuboresha huduma za
afya katika ngazi zote, pamoja na umuhimu wa kukusanya taarifa na matumizi sahihi ya takwimu za sekta ya Afya kwa
ujumla. Aidha, Wizara
imefunga mfumo wa kieletroniki wa ukusanyaji wa taarifa za chanjo katika vituo
vya Afya. Hadi kufikia Machi 2018, jumla ya vituo 1,303 vya mikoa ya
Arusha, Kilimanjaro Tanga, Manyara na Dodoma vilifungiwa mfumo na kupewa vifaa
vya komputa. Vilevile
jumla ya watumishi 3,258 walipewa mafunzo ya jinsi ya
kutumia mfumo huu.
UTEKELEZAJI
WA MIRADI YA MAENDELEO INAYOPATA RUZUKU TOKA SERIKALI KUU KWA MWAKA 2017/18
72.
Mheshimiwa Spika,
Katika mwaka 2017/18, Wizara ilitenga kiasi cha Shilingi 785,805,952,000 kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya
Maendeleo. Kati ya fedha hizi, Shilingi,
336,300,000,000 ni fedha kutoka vyanzo vya ndani na Shilingi 449,505,952,000 ni fedha kutoka vyanzo vya nje.
Miradi
iliyotekelezwa kwa fedha za Ndani
73.
Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, Wizara ilipokea Shilingi 74,756,079,206.00 (Fedha za
Ndani) ambazo zilitumika kutekeleza miradi iliyoainishwa kwenye aya 128 ya
Hotuba yangu.
Miradi iliyotekelezwa kwa fedha za Nje
74.
Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, Wizara ilipokea fedha, dawa,
vifaa na vitendanishi vyenye thamani ya Shilingi
403,530,227,600.94kutoka katika Vyanzo vya Nje kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli
mbalimbali za kuboresha huduma za afya nchini kwa mchanganuo ufuatao:
Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Basket
Fund)
Kazi
zilizotekelezwa kupitia fedha za Mfuko wa Afya wa Pamoja zimeainishwa katika
aya 129 ya Hotuba.
Mpango wa malipo kwa ufanisi (RBF)
75.
Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha Julai hadi Machi 2018, Wizara yangu kwa kushirikiana na OR–
TAMISEMI ilikarabati miundombinu ya kutolea huduma za afya katika Vituo 1,325 vya Serikali vya kutolea
huduma za afya katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Pwani, Tabora, Simiyu,
Kigoma, Kagera na Geita. Aidha, jumla ya Shilingi
3,425,162,919 zilipelekwa katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na
kulipwa kama motisha kwa Timu za Uendeshaji wa shughuli za Afya za Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Uimarishaji wa huduma za dharura za mama
na mtoto (CEmONC)
76.
Mheshimiwa Spika, moja
ya vipaumbele vya Serikali katika mwaka wa fedha 2017/18 ni kupunguza vifo vya
akina mama na watoto vitokanavyo na uzazi. Katika kutekeleza azma hiyo serikali
kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeanza kufanya ukarabati/ ujenzi wa
miundombinu ya kutolea huduma ikiwemo chumba cha upasuaji, maabara, wodi ya
wazazi na wodi ya watoto utakaowezesha upatikanaji wa huduma kamili za uzazi
ikiwa ni pamoja na upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni, ili kupunguza vifo vya
mama na watoto. Kupitia mpango huo, jumla ya vituo vya Afya 208 vinaboreshwa.
Katika kutekeleza mradi huu, jumla ya Shilingi
40,000,000,000 kutoka Banki ya Dunia kwa ajili ya kuboresha Vituo vya Afya
100 na Shilingi 19,500,000,000.00
kutoka Denmark kwa ajili ya vituo vya Afya zimepelekwa katika Halmashauri
mbalimbali nchini kukamilisha kazi ya ukarabati na ujenzi ambao upo katika
hatua mbalimbali chini ya uangalizi wa OR-TAMISEMI na Wizara ya Afya. Aidha,
Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI inakamilisha mchanganuo wa vituo vya afya
21 vitakavyoboreshwa kwa kutumia fedha za Mfuko wa Afya wa Pamoja.
Mfuko
wa Dunia (Global Fund):
77.
Mheshimiwa Spika, Katika
kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, Wizara ilipokea fedha, dawa, vifaa tiba
na vitendanishi vyenye thamani ya Shilingi
303,238,541,795.37 kwa ajili ya kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu, na
Malaria.
UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA TAASISI CHINI YA IDARA KUU YA AFYA
Bohari Kuu ya Dawa (MSD)
78.
Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka wa Fedha 2017/18, Bohari ya
Dawa (MSD) imeendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali kuhusu kununua dawa moja
kwa moja kutoka kwa wazalishaji kwa kuingia makubaliano ya muda mrefu (Framework Agreement) na viwanda vya
uzalishaji dawa. Jumla ya wazalishaji 110 tayari wana mikataba na MSD na kati
ya hao wazalishaji 10 ni viwanda vya ndani. Mpango huu umewezesha MSD
kufanikiwa kupunguza bei ya dawa 109 kwa
wastani wa asilimia 40. Hali
hiyo imesaidia vituo vya afya kuweza kununua dawa kwa bei nafuu na hivyo
kuongeza kiasi cha dawa. Aidha, Bohari
Kuu ya Dawa inaendelea kuimarisha mfumo wake wa usambazaji wa dawa ili
kuhahikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma
za afya vya umma unafikia asilimia 100. Katika kufanikisha hili jumla ya magari
181 yamenunuliwa na Serikali kwa kushirikiana na Global Fund, Magari hayo yalizinduliwa na Mhe. Rais tarehe 26 Machi, 2018. Hali hiyo imewezesha
vituo vya kutolea huduma za afya kuwa na dawa muhimu kwa asilimia 89.6. Vilevile, upatikanaji wa dawa za ARVs
umeimarika na kuwa kati ya asilimia 92 hadi 100
MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA (NHIF)
79.
Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umeendelea kubuni na
kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuongeza wigo wa wanufaika wa bima ya
afya.kufuatia utekelezaji wa mikakati hiyo, katika kipindi cha Julai 2017 hadi
kufikia Machi 2018, Mfuko umeweza kusajili idadi ya wanachama wapya wapatao
167,791 kutoka katika Sekta ya Umma na Binafsi sawa na asilimia 97 ya lengo.
Hivyo idadi ya wanachama wachangiaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
imeongezeka kutoka wanachama 753,992 waliokuwa wameandikishwa mwaka 2016/17
hadi kufikia wanachama 763,068 mwezi Machi 2018. Aidha, idadi ya wanufaika nayo
iliongezeka kutoka 3,491,400 mwaka 2016/17 hadi kufikia wanufaika 3,619,697
mwezi Machi 2018 sawa na asilimia 7 ya Watanzania wote. Hii inaonyesha kuwa
wanachama wa Mfuko wameongezeka kwa wastani wa asilimia 10 na wanufaika
asilimia 7 katika kipindi cha miaka mitano.
80.
Mheshimiwa
Spika, Wizara kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI pamoja na Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya inaendelea na
utekelezaji wa mpango wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF). Katika kipindi
cha Julai 2017 hadi Machi 2018 kaya mpya zilizoandikishwa kwenye Mfuko wa Afya
ya Jamii (CHF) zilikuwa 66,026 na kufanya jumla ya kaya 2,096,692 zilizojiunga
ukilinganisha na kaya 2,030,666 zilizokuwa zimejiunga mwaka 2016/17. Aidha,
wanufaika wameongezeka kutoka 12,183,996 mwaka 2016/17 hadi kufikia wanufaika
12,580,149 Machi 2018 sawa na asilimia 25 ya Watanzania wote. Aidha, mafanikio
hayo yametokana na juhudi zinazofanywa
na Mfuko za kuelimisha wananchi pamoja na kubuni mbinu mbalimbali za kuongeza
wigo wa wanachama, kama kuanzishwa kwa mpango wa KIKOA (unaojumuisha kundi la
wajasiriamali, vikundi vya vikoba, saccos na wavuvi), TOTO AFYA KADI
(unaojumuisha watoto chini ya miaka 18), Wanafunzi wa vyuo vya Elimu ya Juu,
Wastaafu na wanachama binafsi.
81.
Mheshimiwa
Spika, Serikali kupitia NHIF na kwa kushirikiana na Benki ya
Ujerumani (KfW) Ilianza kutekeleza Mpango wa NHIF/CHF kwa Wanawake Wajawazito
na Watoto ujulikanao kama Tumaini la
Mama mwaka 2012 ambapo kina mama wajawazito hulipiwa kadi za NHIF/CHF na
kuwa na uhakika wa kupata matibabu
katika kipindi chote cha ujauzito na miezi sita baada ya kujifungua kwa mama na
mtoto. Mpango huu una lengo la kupunguza vifo vya kina mama na watoto ili
kwenda sambamba na utekelezaji wa malengo ya kimataifa ya maendeleo endelevu
(SDGs). Katika kipindi cha kuanzia Julai 2017 mpaka Machi 2018, akina mama 199,954 na watoto 20,998
walikuwa wamesajiliwa na kunufaika na mpango huu. Tangu kuanzishwa kwa mpango,
tayari wanawake wapatao 875,375 wamenufaika katika mikoa ya Mbeya, Tanga,
Lindi, Mtwara na Songwe. Aidha, shughuli nyingine zinazofanywa na NHIF katika
kuboresha huduma za afya zimeainishwa katika aya 141 mpaka 144 ya Hotuba.
82.
Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu
kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa, inatekeleza Mpango Mkakati mpya wa miaka
mitano (5) wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (2017/18 - 2021/22). Mamlaka
ilifanya tathmini ya maombi ya usajili wa vyakula na kukagua viwanda vya dawa
na viwanda vya vyakula nje ya nchi ambapo matokeo yalikuwa kama ilivyoainishwa
kwenye aya 146 na 147 ya Hotuba. Aidha, Mamlaka imeendelea na utoaji wa elimu kwa
umma kwa makundi mbalimbali ya wananchi kuhusu
madhara ya dawa, vipodozi hatarishi na usalama wa chakula pamoja na
jumbe fupi zilirushwa kupitia redio, runinga, magazeti na mitandao mbalimbali
ya kijamii.
83.
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha wa
2017/18, mfumo wa kupokea taarifa za usajili wa vitendanishi kwa njia ya
mtandao umetengenezwa na kuanza kutumika na hivyo kupungua kwa muda wa
kushughulikia maombi yanayowasilishwa na wateja. Mamlaka imeweza kuweka taarifa
za bidhaa zote zilizosajiliwa nchini kwenye mtandao ambao umeunganishwa na
mfumo wa kielektroniki wa ndani (www.tfda.go.tz/portal/registered-products). Taarifa hizi zinasaidia
wananchi na wateja kwa ujumla kuona bidhaa zilizosajiliwa na tarehe za kuisha
muda wa usajili.
MAMLAKA
YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI
84.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha wa 2017/18, Taasisi iliyokuwa Wakala
wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ilibadilishwa rasmi na kuwa Mamlaka ya
Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa sheria Na. 8 ya mwaka 2016. Katika
kuhakikisha kwamba Mamlaka inafanya kazi kwa ufanisi, mamlaka imesaini mikataba
mitatu (3) ya ununuzi wa mitambo na vifaa vya maabara vyenye thamani ya Shilingi bilioni 1.4, vifaa hivyo
vinatarajiwa kupokelewa kabla ya mwezi Juni, 2018. Aidha, ukarabati wa Maabara
ya DNA Makao Makuu Dar es Salaam umeanza na unategemewa kumalizika mwezi Juni
2018.
TAASISI YA CHAKULA NA LISHE (TFNC)
85.
Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Chakula na Lishe imeendelea kutekeleza
majukumu mbalimbali katika kuimarisha utoaji wa huduma za Lishe nchini. Katika
kutekeleza azma ya Serikali ya kupunguza
vifo vya watoto wadogo na wachanga nchini, Taasisi imeendelea kuratibu zoezi la
kitaifa la utoaji wa vitamini A ya nyongeza kwa watoto wenye umri kati ya miezi
6 hadi 59 na dawa za kutibu minyoo kwa watoto wenye umri wa miezi 12 hadi 59. Msisitizo
katik kipindi hiki ulikuwa ni kufuatilia
na kutoa usaidizi katika mikoa na Halmshauri ambao zilibainika kutofikia asilimia 90 inayopendendwawa na
Shirika la Afya Dunia.
TAASISI
YA UTAFITI WA MAGONJWA YA BINADAMU (NIMR)
86.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Taasisi ya Uchunguzi
wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imeendelea kutekeleza majukumu yake ya Utafiti. Taasisi
imefanya tafiti mbalimbali ikiwemo tafiti za Majaribio ya Chanjo ya UKIMWI,
Tiba Mbadala, Afya ya mama na mtoto, Malaria na TB. Matokeo ya tafiti hizi
yamesaidia kuandaa afua mbalimbali za kuboresha huduma kwa waathirika wa
magonjwa hayo. Aidha, tafiti kwenye afya ya mama na mtoto zinalenga kuboresha
mfumo wa afya hasa upatikanaji wa huduma ikiwemo chanjo, elimu ya lishe na hatua
za kupunguza vifo vya mama na watoto chini ya miaka 5. Taasisi kwa kushirikiana
na Wizara na wadau wa Afya imefanya tathmini ya uwepo wa maji salama na usafi
wa mazingira (WASH) katika vituo vya afya mbalimbali vinavyotoa huduma za
kujifungua. Taarifa zilizopatikana kutokana na utafiti huo ni kwamba, pamoja na
Serikali kupitia Sekta ya Afya kusisitiza wananchi kwenda kujifungulia katika
vituo vya kutolea huduma za Afya, bado yapo mapungufu makubwa ikiwa ni pamoja
na yafuatayo; Asilimia 19 ya vituo hutumia maji toka vyanzo visivyoboreshwa
vikiwemo vyanzo wazi kama mito na mabwawa na visima visivyoboreshwa; Asilimia
46.5 ya sampuli za maji zilizopimwa zilionekana kuwa na vimelea vya maambukizi
ya magonjwa mbalimbali; Asilimia 42 ya vyumba vya kuzalia havikuwa na sehemu za
kunawia mikono; Asilimia 10 ya vituo hasa zahanati vilikuwa na vyoo duni
visivyoboreshwa na kuleta hatari ya maambukizi.
87.
Mheshimiwa Spika,
Wizara imejipanga kufanyia kazi matokeo yaliyobainishwa na utafiti huo kwa
kuelekeza msukumo mkubwa katika eneo la afya Kinga ikiwa ni pamoja na
kushirikiana na OR-TAMISEMI kuhakikisha kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa
zinatenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya kuondoa changamoto
zilizobainishwa na utafiti huo.
UTEKELEZAJI
WA MAJUKUMU CHINI YA IDARA KUU YA MAENDELEO YA JAMII
88.
Mheshimiwa
Spika, Wizara imeendelea kutekeleza afua kwa kushirikiana wadau
mbalimbali katika maeneo muhimu yafuatayo:
Uwezeshaji Wanawake
89.
Mheshimiwa
Spika, katika kuwawezesha wanawake kiuchumi, Wizara yangu iliendelea kuratibu na kusimamia
Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF). Katika
kipindi cha Julai hadi Disemba 2017, Halmashauri 130 kati ya 185 zilichangia
Shilingi bilioni 7.3 katika Mfuko ikilinganishwa na Shilingi bilioni 8.9
zilizochangiwa na Halmashauri kwa mwaka 2016/17. Fedha zilizochangiwa ni sawa
na asilimia 26 ya Shilingi bilioni 28.3 zilizopaswa kuchangiwa kwa mwaka
2017/18. Fedha hizo zilitolewa kama mikopo kwa vikundi 4,365 vyenye wanawake wajasiriamali
39,449.
90.
Mheshimiwa
Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali wakiwemo SIDO, Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote(EOTF) na Baraza la Taifa
la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi iliendelea kuwezesha ushiriki wa wanawake katika
Maonesho ya Biashara ya Kitaifa na Kimataifa. Katika mwaka 2017/18, wanawake wajasiriamali 1,183 kutoka mikoa 26 ya
Tanzania Bara waliwezeshwa kushiriki katika Maonesho ya Sabasaba, Juakali,
Nanenane na VICOBA.
91.
Mheshimiwa Spika, Katika
mwaka 2017/18, wajasiriamali 6,237 (Ke 5,097 na Me 1,140) walipatiwa mikopo na Benki
ya Wanawake Tanzania ikilinganishwa na
wajasiriamali 6,267 (Ke 4,596 na Me 1,671) mwaka 2016/17. Juhudi hizi zimewesha
wajasiriamali 87,063 (Ke 71,744 na Me 15,319) kupata mikopo tangu mwaka 2010. Kwa
upande wa thamani ya mikopo iliyotolewa mwaka 2017/18, benki ilitoa mikopo ya Shilingi
bilioni 10.1 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 13.3 mwaka 2016. Tthamani ya
mikopo iliyotolewa tangu mwaka 2010 mpaka Machi, 2018 ni Shilingi bilioni
131.9.
92.
Mheshimiwa
Spika, Benki ya Wanawake Tanzania imefungua vituo 244 vya
kutolea mikopo na mafunzo kwa wanawake wajasiriamali katika mikoa ya Dar es
Salaam (115), Mwanza (46), Dodoma (27), Mbeya (5), Iringa (9), Ruvuma (24) na
Njombe (18) katika mwaka 2017/18 ikilinganishwa na vituo 88 mwaka 2016/17 sawa
na ongezeko la asilimia 177.
93.
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2017/18, jumla ya akaunti 10,415 (Ke
7,811 na Me 2,604) zilifunguliwa hadi kufikia akaunti 88,397 Machi, 2018 katika
matawi mawili ya Benki ya Wanawake Tanzania (tawi la Mkwepu na Mjasiriamali)
kutoka mwaka 2009. Kati ya akaunti hizo, akaunti 65,419 ni za wateja wanawake
sawa na asilimia 74, akaunti 20,961 za wanaume na akaunti 2,017 za makampuni.
Maendeleo ya Jamiii
94.
Mheshimiwa Spika,
Wizara, inaendelea kuamsha ari ya
Wananchi kushiriki katika Miradi ya Maendeleo. Katika kipindi cha Julai
hadi Machi 2018, Wizara imefanya uhamasishaji katika Mikoa 11 ya Iringa,
Dodoma, Mwanza, Pwani, Kigoma, Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Kagera na
Shinyanga. Uhamasishaji huu umewezesha
ujenzi wa majengo ya Kituo cha Afya Mondo, Wilaya ya Misungwi (Mwanza); ujenzi
wa bwawa la maji Maghangu Mpwapwa (Dodoma); ujenzi wa Zahanati Ufyambe
(Iringa); ujenzi wa shule ya sekondari na kituo cha afya – Uvinza (Kigoma);
ujenzi wa shule ya sekondari na kituo cha afya – Mpanda (Katavi); ujenzi wa
kituo cha afya – Sumbawanga (Rukwa);
ujenzi wa kituo cha afya – Mbozi (Songwe); ujenzi wa shule ya sekondari –
Manispaa ya Mbeya (Mbeya); kuchangia fedha na vifaa kwa ajili ya ujenzi wa
nyumba ya mtumishi wa Makazi ya wazee (Kagera); kuzindua Kituo cha Mkono kwa
Mkono (One Stop Centre) cha wahanga wa ukatili wa kijinsia na ukatili wa watoto
Wilaya ya Kahama (Shinyanga) na ujenzi wa madarasa mawili katika Kijiji cha
Chambasi, Kisarawe (Pwani).
95.
Mheshimiwa
Spika, Wizara
imeendelea kusimamia na kuratibu uzalishaji
wa wataalam wa Maendeleo ya Jamii
kutoka katika vyuo 8 vya maendeleo ya jamii vya Buhare, Mlale, Misungwi,
Rungemba, Mabughai, Ruaha, Uyole na Monduli. Vyuo hivyo hutoa mafunzo ya
Maendeleo ya jamii katika ngazi ya Cheti na Stashahada. Katika mwaka 2017/18, jumla ya wanafunzi 1,588 (Ke 984 na Me 604) walidahiliwa ikilinganishwa na 3,248 (Ke 1,987 na Me 1,261) mwaka
2016/17. Aidha, katika mwaka 2017/18, jumla ya wanafunzi 3,320 (Ke 1,947 na Me 1,373) walihitimu katika Vyuo 8 vya Maendeleo ya Jamii ikilinganishwa na wahitimu 3,694 (Ke 2,228 na Me 1,466)
mwaka, 2016/17.
Mashirika
Yasiyo ya Kiserikali
96.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali kwa kuweka mazingira wezeshi ya kuchangia katika kuleta maendeleo ya
Taifa. Kwa kipindi cha Julai hadi Machi, 2018, jumla ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 192
yalisajiliwa. Kati ya mashirika yaliyosajiliwa, mashirika 21 yalisajiliwa katika ngazi ya Kimataifa,162 katika ngazi ya Kitaifa na Mashirika 9 ngazi ya Wilaya. Usajili
huu umewezesha jumla ya mashirika 8,211
kusajiliwa nchini kuanzia mwaka 2005 hadi Machi, 2018 (Kiambatisho Na.5).
97.
Mheshimiwa Spika, Wizara ilihakiki mashirika na hadi kufikia Machi, 2018, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 4,868 yalikuwa yamehakikiwa. Aidha, katika uhakiki huo, wizara
imebaini jumla ya mashirika 513
yenye sifa za mashirika ambayo yaliyokuwa yamesajiliwa chini ya Sheria nyingine
na kuyajumuisha chini ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na.24 ya
mwaka 2002. Hatua hii imesaidia kuimarisha uratibu na usimamizi mzuri wa
mashirika haya katika misingi ya uwazi, utoaji taarifa na uwajibikaji kwa
jamii.
Haki na Maendeleo ya Mtoto
98.
Mheshimiwa Spika, ukatili
dhidi ya watoto bado ni tatizo kubwa katika nchi yetu. Kwa mujibu wa Takwimu za
Jeshi la Polisi za mwaka 2017, matukio ya ukatili dhidi ya watoto yalikuwa
13,457 ikilinganishwa na matukio 10,551 mwaka 2016. Katika kukabiliana na tatizo hilo, Wizara kwa
kushirikiana na wadau imeendelea kutekeleza Mpango Kazi wa
Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/18 – 2021/22). Katika
mwaka 2017/18, Kazi zilizofanyika chini ya mpango huu ni kutoa elimu kuhusu athari za
mila na desturi zenye madhara kwa jamii ikiwemo ukeketaji, mimba na ndoa za
utotoni kwa makundi mbalimbali katika jamii. Jumla ya wananchi 13,020
walipatiwa elimu wakiwemo wanafunzi 8,546, walimu 476, wazee wa mila 56,
viongozi wa dini 64, ngariba 38, waendesha bodaboda 168, wazazi/walezi 3,600 na
watendaji 72 kutoka mikoa ya Shinyanga, Mara, Tabora, Lindi, Dodoma, Tanga, Dar
es Salaam na Katavi.
99.
Mheshimiwa
Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau imeendelea
kuwapatia huduma watoto waliofanyiwa ukatili kupitia Huduma ya Simu kwa Watoto (Child Help Line). Katika mwaka 2017/18,
simu 18,464 zilipokelewa kuhusu ukatili dhidi ya watoto. Kati ya simu hizo,
simu za watoto 1,072 (Ke 621 na Me 451) ziliwezeshwa kupata huduma (chakula,
vifaa vya shule na huduma za sheria na afya) ikilinganishwa na simu za watoto 441 (Ke 325 na Me 96) waliopata huduma
mwaka 2016/17 sawa na ongezeko la asilimia 143.
100.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha watoto wanashiriki katika maendeleo yao na kujitambua, kwa mwaka
2017/18 Wizara imeendelea kuwezesha ushiriki wa watoto katika mabaraza na klabu
za wasichana za Kujikinga na mimba za utotoni. Jumla ya mabaraza ya watoto 13 na klabu 600 katika shule za msingi na
sekondari zimeanzishwa kwa kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018 na kufikia
idadi ya mabaraza 1,669 na Klabu 2,000.
Huduma ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Watoto
101.
Mheshimiwa
Spika, Wizara imeendelea kusimamia utoaji wa
huduma ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto walio chini ya miaka
mitano walio katika vituo vya kulelea watoto wadogo mchana (Day Care Centres)
vya Serikali na Binafsi. Kwa kipindi cha
Julai, 2017 hadi Machi, 2018, vituo 139
vilipatiwa usajili ikilinganishwa na
vituo 270 vilivyopatiwa usajili
mwaka 2016/17 na hivyo kufikia vituo
1,046 vilivyosajiliwa nchi nzima. Aidha, watoto 6,075 (Ke 4,018 na Me
2,057) waliandikishwa katika vituo vya kulelea watoto wadogo mchana 2016/17 ikilinganishwa
na watoto 4,450 (Ke 3,097, Me 1,353) mwaka 2015/16.
102.
Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2017/18, Wizara imeendelea kuzalisha wataalamu wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto
katika Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara. Jumla ya wanafunzi 83 (Ke 58 na Me
25) walidahiliwa kwa mwaka 2017/18 ikilinganishwa na wanafunzi 56 (Ke 39 na Me
17) waliodahiliwa mwaka 2016/17. Aidha,
wanafunzi 52 (Ke 35 na Me 17) wahitimu katika mwaka 2017/18 ikilinganishwa na
wahitimu 8 wote wanawake mwaka 2016/17.
103.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2017/18, Wizara
imeendelea kuzalisha wataalamu wa
malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika Chuo cha Ustawi wa
Jamii Kisangara. Jumla ya wanafunzi 83 (Ke 58 na Me 25) walidahiliwa kwa mwaka
2017/18 ikilinganishwa na wanafunzi 56 (Ke 39 na Me 17) waliodahiliwa mwaka
2016/17. Aidha, wanafunzi 52 (Ke 35 na Me 17)
wahitimu katika mwaka 2017/18 ikilinganishwa na wahitimu 8 wote wanawake mwaka 2016/17.
Huduma za Ustawi kwa Watoto
104.
Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2017/18, Wizara kwa kushirikiana na Asasi Zisizo za Kiserikali imeendelea
kuhakikisha upatikanaji wa huduma za msingi za malezi, matunzo na ulinzi kwa watoto walio katika mazingira hatarishi
nchini. Jumla ya watoto 6,132 (Ke
2,972 na Me 3,160) walio katika mazingira hatarishi walipatiwa huduma za
msingi katika makao ya watoto 157
yanayoendeshwa na Taasisi za dini, Mashirika ya watu binafsi na Serikali
ikilinganishwa na watoto 4,515 (Ke 2519
na Me 1,996) mwaka 2016/17. Kati ya watoto hao, watoto 78 (Ke 43 na Me 35) wanaishi katika Makao ya Taifa ya Watoto
Kurasini ambayo yanamilikiwa na Serikali.
105.
Mheshimiwa
Spika, kwa kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi,
2018, jumla ya leseni 14 za usajili wa
Makao ya watoto zimetolewa ikilinganishwa na leseni 50 kwa mwaka 2016/17 na
kufikia idadi ya makao 157 nchi nzima. Kati ya makao hayo, moja ni la Serikali na 156 yanamilikiwa na kuendeshwa na watu
binafsi, Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya kijamii au Taasisi za kidini. Nitumie
fursa hii kuwataka watu/Taasisi zote zinazotoa huduma za malezi kwa watoto
wanaoishi katika mazingira magumu kujisajili katika Halmashauri zao mara moja.
106.
Mheshimiwa Spika,
Wizara imeendelea kuhakikisha kuwa watoto
walio katika
mkinzano na Sheria wanapata haki za msingi ikiwa ni pamoja na huduma
za sheria na elimu katika mahabusu tano za watoto za Mbeya, Moshi, Tanga,
Arusha na Dar es Salaam. Katika mwaka 2017/18, jumla ya watoto 291 (Ke 13 na Me
278) walio katika mkinzano na sheria waliwezeshwa kupata huduma za msingi
(chakula, malazi, mavazi, huduma za matibabu na elimu) ikiwa ni pamoja na
huduma za msaada wa kisheria ikilinganishwa na watoto 255 (Ke 18 na Me 237)
mwaka 2016/17 sawa na ongezeko la asilimia 14.
107.
Mheshimiwa
Spika, Wizara kwa
kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria imewachepusha watoto 126 (Ke 24 na
Me 102) kutoka katika mfumo rasmi wa haki jinai kwa kuwarekebisha tabia na
kuwaunganisha na familia zao ikilinganishwa na watoto 72 (Ke 8 na Me 64)
waliochepushwa mwaka 2016/17 sawa na ongezeko la asilimia 67. Aidha, katika mwaka 2017/18, Wizara imeendelea kuwezesha huduma za msingi
(chakula, malazi, mavazi na huduma za matibabu) ikiwa ni pamoja na marekebisho
ya tabia, elimu na mafunzo kwa watoto wa
kiume 35 waliobainika na makosa ya jinai waliopo katika Shule ya Maadilisho
Irambo Mbeya ikilinganishwa na watoto 72 mwaka 2016/17.
108.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2017/18, Wizara kwa kushirikiana na OR - TAMISEMI imeendelea na juhudi ya
kuhakikisha kuwa watoto wanalelewa katika ngazi ya familia kulingana na Sheria
ya Mtoto Na.21 ya mwaka 2009 kwa kutoa huduma za malezi ya kambo na uasili. Wizara imewezesha watoto 44 (Ke 24 na Me 20) kuwekwa chini ya malezi
ya kambo ikilinganishwa na watoto 54 (Ke 21 na Me 33) mwaka 2016/17. Aidha,
watoto 17 (Me 8 na Ke 9) waliasiliwa mwaka 2017/18 ikilinganishwa na watoto 21
(Ke 11 na Me 10) mwaka 2016/17.
109.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuwatambua Watu wa Kuaminika (Fit
Persons) ili kulea watoto walio katika mazingira hatarishi. Juhudi
hii imewezesha Watu wa Kuaminika 187 kutambuliwa katika Halmashauri 19 mwaka
2017/18. Hadi kufikia Machi, 2018, jumla ya watoto 243 wamepitia kwenye familia
za watu wa kuaminika katika Halmashauri 19 za Magu DC, Kasulu DC, Kasulu TC,
Musoma Dc, Iringa MC, Iringa DC, Mufindi DC,
Njombe DC, Makete DC, Mbeya Jiji, Mbeya DC, Mbarali DC, Hai DC, Temeke
DC, Arusha DC, Kakonko DC, Kibondo DC, Misenyi DC na Chunya DC.
Huduma za Ustawi kwa Wazee
110.
Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kuratibu upatikanaji wa huduma
za msingi kwa wazee wasiojiweza. Katika mwaka 2017/18, jumla ya wazee wasiojiweza 517 (Ke 250 na Me
267) wanaoishi
katika makazi 17 ya Serikali walipatiwa huduma za msingi - chakula, malazi,
mavazi na matibab ikilinganishwa na wazee 465 (Ke 221 na Me 244) mwaka 2016/17 sawa
na ongezeko la asilimia 11.
111.
Mheshimiwa Spika, Wizara
kwa kushirikiana OR - TAMISEMI iliwezesha
wazee 506,943 (Ke 220,312 na Me 286,631) kupata vitambulisho vya matibabu bure
katika kipindi cha Julai hadi Machi, 2018 ikilinganishwa na wazee 74,590 waliopata vitambulisho vya
matibabu bure mwaka 2016/17. Juhudi hizi zimewezesha kufikia idadi ya wazee
581,533 (Ke 254,793 na Me 326,740) waliopata vitambulisho ikiwa ni asilimia 35
ya wazee 1,657,206 waliotambuliwa katika Halmashauri
zote.
Huduma za Usuluhisho wa
Migogoro ya Ndoa na mashauri ya matunzo kwa watoto
112.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Wizara kupitia Baraza la
Usuluhishi wa Ndoa lililopo chini ya usimamizi wa Kamishna wa Ustawi wa Jamii
na Ofisi za Ustawi wa Jamii za Halmashauri zimeendelea kutoa huduma za
usuluhishi wa migogoro ya ndoa kwa familia. Kwa kipindi cha Julai, 2017 hadi
Machi, 2018, jumla ya mashauri ya
migogoro ya ndoa 13,382 yalipokelewa na kufanyiwa usuluhishi ikilinganishwa
na mashauri ya migogoro ya ndoa
8,454 mwaka 2016/17. Kati ya mashauri hayo, mashauri 11,326 sawa na asilimia 85
yamesuluhishwa na yamekamilika, mashauri 1,397 sawa na asilimia 10 yamepelekwa
mahakamani na mashauri 659 sawa na asilimia 5 yanaendelea na usuluhishi.
113.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa, watoto wanapata matunzo
kutoka kwa wazazi, Wizara imeendelea kufanyia kazi mashauri ya matunzo ya
watoto nchini. Kwa kipindi cha
mwezi Julai, 2017 hadi Machi, 2018 jumla ya mashauri ya matunzo ya watoto 11,815 yalipokelewa. Kati ya mashauri
hayo, 4,965 yalihusu matunzo ya watoto walio ndani ya migogoro ya ndoa na 5,708
watoto waliozaliwa nje ya ndoa Kati ya
mashauri yaliyopokelewa, 10,673 yalikamilika kuwezesha huduma kwa watoto na
mashauri 1,142 yaliyopewa rufaa
kwenda mahakamani ikilinganishwa mashauri ya matunzo ya watoto 12,406
yaliyokamilika mwaka 2016/17 (matunzo ya watoto walio kwenye migogoro ya ndoa
6,557, matunzo ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa 4,133 na mashauri 1,716
yaliyopewa rufaa kwenda mahakamani).
UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA
TAASISI CHINI YA IDARA KUU YA MAENDELEO YA JAMII
Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru
114.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18,
Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru ilidahili jumla ya wanafunzi 1,169 katika
fani ya Maendeleo ya Jamii ikiwa ni ongezeko la asilimia 86 ya udahili wa
wanafunzi 628 mwaka 2016/17. Kati ya wanafunzi waliodahiliwa, wanafunzi 486
walidahiliwa katika ngazi ya cheti, wanafunzi 83 Stashahada na wanafunzi 600
ngazi ya Shahada. Aidha, wanafunzi 684 walihitimu mwaka 2017/18 ikilinganishwa
na wahitimu 609 mwaka 2016/17 ikiwa ni ongezeko la asilimia 12.
115.
Mheshimiwa Spika,
Taasisi pia imefanya tafiti tatu ambazo ni Tathmini ya mahitaji ya Ushiriki wa
Jamii katika kijiji cha Kikwe wilaya ya Arumeru, tafiti kuhusu watoto walio katika
mazingira hatarishi katika sekta isiyo rasmi katika Wilaya ya Arumeru (utafiti
kuhusu watoto katika masoko ya jamii) na Tathmini ya changamoto inayowakabili
Maafisa Maendeleo ya Jamii Tanzania katika Halmashauri. Matokeo
ya tafiti hizi yatawezesha Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na Wizara
kuboresha utoaji wa mafunzo na utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya jamii.
Taasisi ya Ustawi wa Jamii – Kijitonyama
116.
Mheshimiwa
Spika, Taasisi ya Ustawi wa Jamii -
Kijitonyama imeendelea kutoa mafunzo katika ngazi ya Cheti, Diploma, Shahada,
Stashahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamili. Katika mwaka 2017/18, Taasisi ilidahili
wanafunzi 1,185 (Ke 811 na Me 374) katika fani zitolewazo katika ngazi
mbalimbali ikiwa upungufu wa asilimia 6.91 ya wanafunzi 1,273 waliodahiliwa
mwaka 2016/17. Aidha, wanafunzi 1,122 (Ke 722 na Me 400) walihitimu mwaka
2016/17 katika fani na ngazi mbalimbali ikilinganishwa na wanafunzi 1,172 (Ke
789, Me 383) waliohitimu mwaka 2015/16 sawa na ongezeko la asilimia 4.
C:
VIPAUMBELE VYA WIZARA KWA MWAKA 2018/19
117.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2018/19, Wizara kupitia fungu 52
(Idara kuu ya Afya) imejiwekea vipaumbele vifuatavyo ili kuboresha utoaji wa
huduma za afya nchini;
i)
Kuimarisha huduma za chanjo kwa watoto ili
kuendelea kubaki katika viwango vya juu vya utoaji wa huduma za chanjo ili
kuwaepusha watoto na magonjwa yanayoweze kuepukika kwa chanjo.
ii)
Kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa
yanayotokana na kutozingatia kanuni za usafi na usafi wa mazingira kama
magonjwa ya kuhara, kuhara damu na kipindupindu kwa kuongeza uhamasishaji na
usimamizi wa usafi na usafi wa mazingira
iii)
Kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa
yasiyoambukiza kama magonjwa ya moyo, kisukari na saratani kwa kuhamasisha
jamii kuepukana na tabia hatarishi na kujijengea tabia ya kufanya mazoezi mara
kwa mara na kuzingatia ulaji wa vyakula unaofaa ili kujiepusha na hatari ya
kupata magonjwa hayo.
iv)
Kuimarisha huduma za afya ya uzazi na mtoto
nchini ili kupunguza idadi ya vifo vya wanawake na watoto vinavyotokana na
Uzazi kwa kukarabati
na kujenga Wodi Maalum kwa ajili ya Watoto wachanga (Neonatal Care Units)
katika Hospitali za Rufaa za Mikoa 7 na Wodi za Wazazi na kujenga vyumba vya
wagonjwa mahututi (ICU) wanaotokana na uzazi katika Hospitali za Rufaa za Mikoa
(5) mitano yenye viwango vikubwa vya vifo vitokanavyo na uzazi.
v)
Kupunguza maambukizi ya Malaria, TB na
VVU/UKIMWI;
vi)
Kuimarisha upatikanaji wa damu salama nchini
ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya kukusanyia Damu Salama (Satellite Blood Banks)
vii)
Kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa
tiba na vitendanishi katika vituo vyote vya umma vya kutolea huduma za za afya
nckiahini
viii) Kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa
nchini katika Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Rufaa za Kanda,
Hospitali Maaluma na za Kitaifa ili kusogeza huduma hizi karibu zaidi na
wananchi na kupunguza rufaa za nje ya nchi zisizo na ulazima
ix)
Kuimarisha ubora wa huduma zinazotolewa katika
vituo vya afya vinavyomilikiwa na Serikali
x)
Kuboresha vyuo vya mafunzo ya afya ili
kuendelea kuzalisha wataalam wenye ubora kwa kufanya upanuzi na ujenzi wa
majengo na ukarabati kwenye Vyuo vya Mafunzo ya Afya vya Uuguzi vya Nachingwea,
Kibondo, Kagemu, Kondoa, Same na Kiomboi; Vyuo vya Mafunzo ya Maafisa Afya vya
Bombo Tanga, Mpwapwa na Ngudu Mwanza; vyuo vya Maafisa Tabibu vya Kibaha, Tanga
na katika Chuo cha Maabara cha Singida
xi)
Kuimarisha Mifumo ya Habari, Takwimu na
Teknolojia ili kurahisisha upatikanaji wa Takwimu katika sekta ya Afya.
xii)
Kuimarisha mfumo wa ugharimiaji wa
huduma za afya nchini kwa kuongeza wigo wa huduma za bima ya afya kwa wananchi
ili kufikia malengo ya kuwa na bima kwa wananchi wote na kufikia lengo la afya
kwa wote (Universal Health Coverage – UHC)
118.
Mheshimiwa Spika, ili
kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika Fungu 52 kwa mwaka 2018/19, kazi
zitakazotekelezwa zimeainishwa kwenye aya ya 199 mpaka 205 vya hotuba ya
bajeti. Hata hivyo ningependa kutaja kazi muhimu na za kipaumbele zifuatazo:-
i.
Kununua na
kusambaza chanjo za watoto na chanjo
ya kwa wasichana wenye miaka kati ya 9 – 14 ambapo jumla ya shilingi bilioni 30 zimetengwa.
ii.
Kukarabati
na kujenga Wodi Maalum kwa ajili ya Watoto wachanga (Neonatal Care Units)
katika Hospitali za Rufaa za Mikoa 7 ya Dar es Salaam, Katavi, Geita, Rukwa,
Kilimanjaro, Iringa na Kigoma ambapo shilingi
milioni 900 zimetengwa.
iii.
Kupanua
Wodi za Wazazi na kutenga vyumba vya wagonjwa mahututi wanaotokana na uzazi
katika Hospitali za Rufaa za Mikoa (5) ya Mbeya, Shinyanga, Morogoro, Pwani na
Kigoma mitano ya ambapo, shilingi bilioni 1 zimetengwa.
iv.
Kuimarisha
upatikanaji wa huduma ya damu salama kwa kujenga vituo vya kukusanyia Damu
Salama (Satellite Blood Banks) katika mikoa 12 ya Manyara, Katavi,
Rukwa, Ruvuma, Njombe, Tanga, Arusha, Pwani, Singida, Songwe, Geita na Simiyu ambapo kiasi cha shilingi bilioni 4.3 kimetengwa
v.
Kununua
dawa za malaria kwa ajili ya kinamama wajawazito (Sulphadoxine +pyrimethamine),
dawa za kuokoa maisha ya mama wajawazito ambapo shilingi bilioni 8.5 zimetengwa.
vi.
Kununua na
kusambaza vitanda, magodoro, mashuka na vitanda vya kuzalia mama wajawazito
ambapo kiasi cha shilingi bilioni 4.9
kimetengwa
vii.
Kuimarisha
hali ya upatikanaji wa Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba na Vitendanishi nchini kwa
kununua na kuvisambaza katika vituo vya kutolea huduma za afya. Jumla ya shilingi bilioni 270 zimetengwa.
viii.
Kuendelea na huduma za kupandikiza figo (renal
transplant) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Benjami Mkapa
ix.
Kuendelea kutoa huduma za upandikizaji wa vifaa
vya kusaidia kusikia kwa kuweka cochlear implants
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
x.
Kununua na kusimika vifaa vya kisasa vya
uchunguzi na matibabu ya Saratani katika Taasisi ya Saratani Ocean Road ambapo kiasi cha shilingi bilioni 14.5
zimetengwa.
xi.
Kuendelea na ujenzi wa jengo na kusimikia vifaa vya
uchunguzi (X-Ray Building), pamoja na kununua vifaa vya tiba ya mionzi, katika
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya ambapo kiasi cha shilingi bilioni 5 zimetengwa.
xii.
Wizara imepanga kununua na kusambaza Ambulances 27 kwa ajili ya kuimarisha
mfumo wa rufaa Nchini
xiii.
Kufanya
ukarabati katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ambapo kiasi cha shilingi bilioni 20 zimetengwa
xiv.
Kuendelea
na ujenzi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa ambayo haina hospitali hizo katika
mikoa ya Simiyu, Geita, Katavi, Songwe Mara, Njombe ambapo shilingi bilioni 10 zimetengwa
xv.
Kufanya ukarabati na upanuzi wa vyuo afya ambapo
jumla ya shilingi bilioni 8
zimetengwa
119.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2018/19, Wizara kupitia fungu 53
(Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii) imejiwekea vipaumbele vifuatavyo ili
kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini;
(i)
Kukuza usawa wa jinsia na
uwezeshaji wa wanawake kiuchumi;
(ii)
Kuimarisha upatikanaji wa haki na
huduma za ustawi wa jamii kwa wazee na watoto;
(iii)
Kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa
Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/18 –
2021/22 ili kupunguza ukatili dhidi yao kwa asilimia 50;
(iv)
Kuboresha mazingira ya kufundishia na
kujifunzia katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na Taasisi ya Ustawi wa
Jamii – Kijitonyama;
(v)
Kuboresha majengo na miundombinu
katika makazi ya wazee, Makao ya Taifa ya Watoto Kurasini, mahabusu za watoto
na Shule ya Maadilisho
(vi)
Kuweka mazingira wezeshi ili
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa; na
(vii)
Kuamsha ari ya wananchi kushiriki
katika shughuli za maendeleo.
120.
Mheshimiwa Spika, ili
kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika Fungu 53 kwa mwaka 2018/19, kazi zitakazotekelezwa
zimeainishwa kwenye aya ya 206 mpaka 213 vya hotuba ya bajeti. Hata hivyo
ningependa kutaja kazi muhimu zitakazotekelezwa kwa muhtasari ambazo ni:
(i)
Kukuza usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake ambapo shilingi milioni 413 zimetengwa;
(ii)
Kukarabati majengo katika vyuo vya maendeleo ya jamii vya
Uyole, Mlale na Misungwi ambapo kiasi cha shilingi
milioni 550 kimetengwa;
(iii) Kukarabati
makazi ya wazee Bukumbi, Mwanzage na Mizufini ambapo shilingi milioni 450
zimetengwa;
(iv) Kukamilisha
ujenzi wa mahabusu ya watoto Mtwara ambapo kiasi cha shilingi milioni 500
kimetengwa;
(v)
Kuimarisha ulinzi
wa mtoto ambapo shilingi bilioni 1.8 zimetengwa; na
(vi) Kuimarisha hali
ya upatikanaji wa huduma za msingi kwa wazee wasiojiweza na watoto walio katika mazingira
hatarishi na watoto walio katika mkinzano na sheria ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1 kimetengwa.
D: SHUKRANI
121.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii ya kipekee kuzishukuru nchi wahisani
za Denmark, Canada, Ireland, Uswisi na Korea ya Kusini pamoja na Mashirika ya
Maendeleo ya Kimataifa ya UNICEF na Benki ya Dunia kwa kutoa misaada katika
Mfuko wa Pamoja wa Sekta ya Afya ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha
huduma za afya nchini. Pia shukrani ziende kwa WHO, GAVI na Global Fund kwa
mchango wao katika kutekeleza mikakati ya Sekta ya afya. Aidha, napenda
kuzishukuru nchi za China, Cuba, Hispania, India, Italia, Japan, Marekani,
Misri, Sweden, Uingereza, Ujerumani na Ufaransa na ambazo zimeendelea kuisaidia
Sekta ya Afya kwa njia mbalimbali.
122.
Mheshimiwa Spika, vilevile nayashukuru mashirika mengine ya Kimataifa kwa
ushirikiano wao waliotoa kwa Wizara pamoja na Wadau wa Maendeleo ambao kwa
pamoja wamewezesha wizara yangu kutekeleza mikakati ya kisekta na hivyo
kuboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini Wadau wote hawa wameainishwa
kwenye Hotuba yangu kuanzia aya ya 214 mpaka ya 216.
123.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki cha utendaji wangu wa kazi nikiwa
Waziri, nimepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi na wafanyakazi wa
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Napenda kumshukuru
Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile (Mb.), Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto kwa ushirikiano anaonipa katika kutekeleza majukumu
yangu. Aidha, naomba kuwashukuru Dkt. Mpoki M. Ulisubisya Katibu Mkuu
(Afya) na Bibi Sihaba Nkinga Katibu Mkuu (Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto) kwa mchango wao katika kuwezesha utekelezaji wa majukumu
yangu. Vilevile, nawashukuru Prof. Muhammad
Bakari Kambi, Mganga Mkuu wa Serikali, Makamishna, Wakurugenzi na
Wakuu wa Vitengo vya Wizara. Nawashukuru pia, Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa
Muhimbili Prof. Lawrence Museru, Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (
MOI) Dr. Respicious Boniface Rwezimula; Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI), Prof. Mohamed Janabi; Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya
Ocean Road (ORCI); Dr. Julius Mwaiselage; na Mkurugenzi wa Hospitali ya
Benjamin Mkapa (BMH) Dkt. Alphonce Chandika; Mkurugenzi wa Hospitali Maalum ya
Kibong’oto Dkt. Riziki Kisonga, Mkurugenzi wa Hospitali ya Afya ya Akili
Mirembe Dkt. Erasmus Mndeme, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya
Dkt. Godlove Mbwanji; Mkurugenzi wa Hopsitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Dkt
Abel Makubi; Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC Dkt Gilead
Masenga. Aidha, nichukue fursa hii pia
kuzishukuru Taasisi zilizo chini ya
Wizara pamoja na Waganga Wakuu wa Mikoa
na Wilaya, Waganga Wafawidhi wa Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati, Wakuu wa
Vyuo vya Mafunzo vilivyo chini ya Wizara na wafanyakazi wote wa Wizara na
Mashirika ya Dini (FBOs), ya kujitolea na Binafsi. Natoa shukrani kwa sekta
zote ambazo tunashirikiana nazo katika kutoa huduma za afya, maendeleo ya jamii
na ustawi wa jamii pamoja na wananchi wote kwa ushirikiano wao. Nawaasa
waendelee kuzingatia misingi ya huduma bora na kufanya kazi kwa bidii kwa
manufaa ya taifa letu.
124.
Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii kuishukuru familia yangu, kwa upendo na uvumilivu na
kunitia moyo katika kutekeleza majukumu yangu ya Kitaifa. Aidha, Napenda
kuwashukuru wananchi wote wa Mkoa wa
Tanga kwa ushirikiano wanaoendelea
kunipatia katika kuendeleza Mkoa wetu. Naahidi kuwa nitaendelea kuwatumikia kwa akili na nguvu zangu zote ili
kuleta Maendeleo katika Mkoa wetu.
E:
MAOMBI YA FEDHA KWA KAZI ZILIZOPANGWA KUTEKELEZWA KATIKA MWAKA WA FEDHA 2018/19
Fungu 52 - Afya
Mapato
125.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2018/19 Wizara imekadiria kukusanya mapato ya Shilingi
bilioni mia mbili arobaini, milioni arobaini na mbili, mia tano na nane elfu,
mia moja hamsini na saba (240,042,508,157.00) Kati ya fedha hizo Shilingi
bilioni mia mbili ishirini, milioni mia mbili sitini na saba, elfu kumi na
hamsini na saba (220,267,010,057.00) zitakusanywa katika mashirika na taasisi zilizo chini ya Wizara na
Shilingi bilioni kumi na tisa, milioni mia saba sabini na tano, mia nne tisini
na nane elfu, mia moja (19,775,498,100.00) ni kutoka makao makuu.
Matumizi ya Kawaida
126.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2018/19, Wizara inakadiria kutumia kiasi cha Shilingi
bilioni mia tatu nne, milioni mia nne sabini na tatu, mia nne sabini na sita elfu
(304,473,476,000.00) kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. Kati ya fedha hizo, Shilingi
bilioni themanini na nane, milioni mia nne sitini na tano, mia saba hamsini na
sita elfu (88,465,756,000.00) zitatumika kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi bilioni
mia mbili kumi na sita, milioni saba, mia saba ishirini elfu (216,007,720,000.00)
zitatumika kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi.
Miradi ya Maendeleo
127.
Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa shughuli za maendeleo, Wizara inakadiria kutumia Shilingi
bilioni mia tano sitini na moja, milioni mia saba hamsini na tisa, mia tisa
tisini na tisa elfu (561,759,999,000) kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo.
Kati ya hizo, fedha za ndani ni Shilingi
bilioni mia moja themanini na nne, milioni mia tisa hamsini na tisa, mia tisa
tisini na tisa elfu (184,959,999,000) na fedha za nje ni Shilingi
bilioni mia tatu sabini na sita, milioni mia nane (376,800,000,000.00.) Jumla
ya Makadirio ya Bajeti kwa 2018/19 kwa Fungu 52 ni Shilingi
bilioni mia nane themanini na sita, milioni mia mbili thelathini na tatu, mia
nne sabini na tano elfu (866,233,475,000.00).
Fungu
53 – Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Mapato
128.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara imekadiria
kukusanya Shilingi bilioni tatu, milioni tisini, mia saba tisini na
sita elfu (3,090,796,000)
kutokana na ada za wanafunzi kutoka Vyuo 8 vya Maendeleo ya Jamii na Chuo cha
Ustawi wa Jamii Kisangara, ada ya usajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na
mauzo ya vitabu vya zabuni.
Matumizi Kwa mwaka 2018/19
129.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2018/19 inakadiriwa kuwa Shilingi bilioni thelathini na mbili, milioni mia moja arobaini, mia
sita arobaini na tisa elfu (32,140,649,000). Kati ya makadirio hayo, Matumizi
ya Kawaida ni Shilingi bilioni ishirini na saba, milioni mia mbili ishirini
na sita, mia nane na nne elfu (27,226,804,000) na Miradi ya Maendeleo ni Shilingi bilioni nne, milioni mia tisa kumi
na tatu, mia nane arobaini na tano elfu
(4,913,845,000).
Matumizi ya
Kawaida
130.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara inakadiria
kutumia kiasi cha Shilingi bilioni ishirini na saba,
milioni mia mbili ishirini na sita, mia nane na nne elfu (27,226,804,000) kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida.
Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni
kumi na tano, milioni mia moja kumi na sita, mia tisa sitini na mbili elfu (15,116,962,000)
ni Mishahara ya watumishi na Shilingi
bilioni kumi na mbili, milioni mia moja na tisa, mia nane arobaini na mbili
elfu (12,109,842,000) ni Matumizi Mengineyo.
Miradi ya
Maendeleo
131.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa shughuli za maendeleo,
Wizara inakadiria kutumia Shilingi bilioni
nne, milioni mia tisa kumi na tatu, mia nane arobaini na tano elfu (4,913,845,000) kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo.
Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni
moja, milioni mia tano (1,500,000,000) ni fedha za ndani na Shilingi bilioni tatu, milioni mia nne na
kumi na tatu, mia nane arobaini na tano elfu (3,413,845,000) ni fedha za
nje.
132.
Mheshimiwa Spika, Jumla kuu ya fedha inayoombwa kwa mwaka
2018/19, kwa Fungu 53 ni Shilingi bilioni thelathini na
mbili, milioni mia moja arobaini, mia sita arobaini na tisa elfu (32,140,649,000).
133.
Mheshimiwa Spika, Jumla kuu ya
fedha inayoombwa kwa mwaka 2018/19, Shilingi bilioni mia nane tisini na nane,
milioni mia tatu sabini na nne, mia moja ishirini na nne elfu (898,374,124,000).
134.
Mheshimiwa
Spika, Hotuba kamili
inapatikana katika tovuti za Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto www.moh.go.tz. na www.mcdgc.go.tz.
135.
Mheshimiwa Spika,
naomba kutoa hoja.
0 on: "HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII MHE. UMMY MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019"