Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatatu, 9 Aprili 2018

TAARIFA KWA UMMA


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO


TAARIFA KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI KWA KIPINDI CHA JANUARI HADI MACHI 2018 ILIYOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU (MB); WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, TAREHE 9 APRILI, 2018.

Ndugu Wanahabari,
Serikali kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imekuwa ikitoa taarifa ya mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu na hatua zinazochukuliwa kudhibiti ugonjwa huu Kuanzia Januari hadi kufikia tarehe 31 Machi 2018, jumla ya wagonjwa 1448, wametolewa taarifa, na kati ya hao 27 wamepoteza maisha.

Kwa kipindi cha Januari wagonjwa 365 na vifo 9 walitolewa taarifa, Februari wagonjwa 996 na vifo 18 na Machi wagonjwa 87 bila kifo. Mwenendo wa takwimu hizi za ugonjwa wa Kipindupindu zinaonyesha kuwa idadi ya wagonjwa na vifo imepungua kwa kiasi kikubwa. Aidha, Mkoa wa Dodoma umeongoza kwa kipindi cha Januari hadi Machi kwa kuripoti jumla ya wagonjwa 583 kati ya 1,448 walioripotiwa nchi nzima sawa na asilimia 40.3%, ikifuatiwa na Ruvuma 374 (25.8%), Rukwa 276 (19.1%), Iringa 88 (6.1%), Morogoro 56 (3.9%), Songwe 37 (2.6%), Kigoma 25 (1.7%) na Manyara 9 (0.6%).

Kwa mwezi Machi 2018, jumla ya wagonjwa 87 bila kifo wametolewa taarifa, ambapo ni pungufu kubwa sawa na asilimia 91.3% ukilinganisha na mwezi Februari 2018 ambapo kulikuwa na jumla ya wagonjwa 996 na vifo 18. Kwa mwezi Machi mikoa na halmashauri ambazo zimeendelea kutoa taarifa ya ugonjwa wa Kipindupindu nchini ni Dodoma (Mpwapwa-35, Chamwino-15, Dodoma Mjini-6, Kongwa-5), Ruvuma (Nyasa-18, Mbinga-5), Rukwa (Sumbawanga Vijijini-5), na Iringa (Kilolo-2).

Ukilinganisha idadi ya wagonjwa waliotolewa taarifa mwezi Februari na ule wa mwezi Machi, mikoa imeweza kufanikiwa kudhibiti ugonjwa huu kwa kiasi kikubwa. Mfano mkoa wa Morogoro umefanikiwa kudhibiti kikamilifu kutoka wagonjwa 56 mwezi Februari na kutokuwa na wagonjwa wowote mwezi Machi. Mikoa mingine iliyofanikiwa kupunguza idadi ya wagonjwa kwa sehemu kubwa katika kipindi cha mwezi mmoja ni Iringa (punguzo la asilimia 97.7%), Rukwa (punguzo la asilimia 96.1%) na Ruvuma (punguzo la asilimia 92.7%). Mkoa wa Dodoma pia umefanikiwa kupunguza idadi ya wagonjwa kwa takribani asilimia 83% katika kipindi cha mwezi mmoja.

Wizara inatoa pongezi kwa Mikoa kwa jitihada mbalimbali walizozichukuwa kudhibiti ugonjwa huo ambayo imepelekea kupunguza kwa sehemu kubwa kuenea kwa ugonjwa huu katika kipindi cha mwezi wa Machi.

Ndugu Wanahabari,
Ingawa takwimu hizi zinaonyesha kuwa ugonjwa umepungua, bado uwezekano wa kuenea kwa ugonjwa wa Kipindupindu na kupata maambukizi mapya ni tishio hata kama ni Halmashauri moja tu itakuwa na wagonjwa wa Kipindupindu. Tishio hili inaongezeka katika msimu huu wa mvua ambapo inaweza kuongeza kasi ya kuenea kwa maambukizi ya Kipindupindu. Hivyo tunahitaji kuzidisha juhudi za kuzuia ugonjwa huu, kwa kusimamia kikamilifu maelekezo na miongozo stahiki inayotolewa. 

Ni dhahiri kuwa ushirikishwaji wa sekta zote kwa ngazi mbalimbali na jamii kwa ujumla ni muhimu sana katika kukabiliana na ugonjwa wa Kipindupindu.  Wizara inasisitiza kuwa wadau wote wapewe nafasi katika mapambano haya kupitia vikao mbalimbali za kujadili udhibiti wa ugonjwa wa Kipindupindu kwenye Halmashauri na Mikoa. Viongozi wa dini, watu mashuhuri na waganga wa tiba mbadala pia wasaidie kuhamasisha jamii zao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu.

Ndugu Wanahabari,
Wizara inaendelea kuwasihi wananchi kuungana na Halmashauri, Mikoa, hasa iliyotoa taarifa kipindi cha Januari hadi Machi, pamoja na Wizara katika juhudi za kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa Kipindupindu.  Jamii izingatie kanuni za usafi binafsi na usafi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na:
1.   Kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo tunayoishi.
2.   Kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni kabla ya kula, baada ya kutumia choo, na baada ya kumsafisha mtoto aliyejisaidia.
3.   Kunywa maji safi na salama yaliyotakaswa kwa dawa (kama vile water guard) au yaliyochemshwa na kupoa.
4.   Kuzingatia ushauri na elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa Kipindupindu, ili jamii iondokane na imani potofu kuhusu Kipindupindu.
5.   Kufikisha wagonjwa wa Kipindupindu mapema katika vituo vya kutolea huduma ili wawahi kupata matibabu.
6.   Kutotiririsha maji   taka   ovyo

Vile vile, Wizara inasisitiza yafuatayo yasimamiwe kwenye Halmashauri na Mikoa yote nchini,
1.   Utoaji wa taarifa sahihi za ugonjwa wa Kipindupindu na kwa wakati kwa kufuata miongozo iliyopo.
2.   Usimamizi wa utekelezaji wa miongozo katika kuzuia na kudhibiti ugonjwa ni pamoja na;
o   Usimamizi wa utekelezaji wa sheria ndogondodo za usafi wa mazingira ili kuimarisha matumizi ya vyoo.
o   Usafi wa mazingira pamoja na udhibiti wa biashara za chakula na pombe za kienyeji katika mitaa.
o   Kuzingatia agizo la Mheshimiwa Rais la kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
3.   Kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yote mijini na vijijini hasa wakati wa mlipuko wa Kipindupindu. Hii ni pamoja na:
o   Mamlaka za maji katika ngazi zote ziweke mkazo wa kuwepo kwa vyanzo mbadala vya maji.
o   Utakasaji wa maji ya bomba kwa njia ya kutumia klorini ufanyike kama miongozo inavyotaka na ufuatiliaji wa ubora wa maji ufanyike kulingana na miongozo.

Hitimisho
Wizara kwa ukaribu itaendelea kufuatilia mwenendo wa ugonjwa wa Kipindupindu nchi nzima. Aidha, Wizara inawashukuru wadau wote wa sekta mbalimbali, wataalamu na watumishi, waandishi wa habari na wananchi kwa michango yao mbalimbali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kipindupindu nchini.  


Asanteni sana

0 on: "TAARIFA KWA UMMA"