NA WAMJW-DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto
Mhe. Ummy Mwalimu amewashauri wananchi kwenda vituo vya tiba haraka mara baada
ya kugundua kuwa wana dalili za ugonjwa wa dengue.
Hayo ameyasema wakati alipotoa tamko juu ya kuingia
kwa ugonjwa wa dengue hapa nchini mara baada ya kufunga Mkutano wa 65 wa Jumuiya ya Mawaziri
wa Afya wa Nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini ECSA leo jijini Dar es
salaam.
“Kuna dalili za Ugonjwa Dengue zikiwemo homa ya ghafla, kuumwa kichwa
hususan sehemu za macho, maumivu ya viungo na uchovu. Dalili hizi huanza kujitokeza
kati ya siku 3 hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa virusi vya homa ya Dengue hivyo
Wizara inashauri kuwa wananchi
wasiwe na hofu, bali mara tu wanapoona dalili za
ugonjwa waende katika vituo vya tiba alisema Waziri Ummy.
Aidha Waziri Ummy amesema kuwa Wakati mwingine dalili za
ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za malaria hivyo basi wananchi
wanaaswa kuwa, wakipata homa wahakikishe kuwa wanapima ili kugundua kama wana
vimelea vya malaria au Dengue, au sababu nyingine, ili hatua stahiki
zichukuliwe.
Waziri Ummy amesema kuwa ili
kujikinga na ugonjwa huo ni lazima Kuangamiza
mazalio ya mbu kwa kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama au nyunyuzia dawa ya
kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo pamoja na Kujikinga na kuumwa na mbu kwa kuvaa nguo
ndefu muda wote hasa nyakati za mchana.
Aidha Waziri Ummy amesema kuwa Wizara itaendelea Kuimarisha ufuatiliaji wa
magonjwa nchi nzima kwa kutumia mfumo uliopo wa ukusanyaji wa taarifa (IDSR),
ambapo tunaendelea kupata taarifa za kila siku juu ya mwenendo wa ugonjwa huu
na Kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari.
Mbali na hayo Waziri
Ummy amesisitiza kuwa hakuna vikwazo
vyovyote vilivyowekwa kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na wanaotoka nchini na Wizara itaendelea kushirikiana na wadau na sekta mbalimbali katika kufuatilia
na kudhibiti ugonjwa huo.
Homa ya Dengue ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyoenezwa
na mbu wa aina ya Aedes ambao ni
weusi wenye madoa madoa meupe yenye kung’aa.
0 on: "WAZIRI UMMY AWASHAURI WANANCHI KWENDA VITUO VYA TIBA HARAKA PINDI WANAPOGUNDUA DALILI ZA UGONJWA WA DENGUE."