Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumapili, 25 Machi 2018

SIKU YA KIFUA KIKUU DUNIANI (World TB Day) 24 March 2018SIKU YA KIFUA KIKUU DUNIANI (World TB Day) 24 March 2018

Kifua Kikuu (TB) bado ni tatizo nchini kwetu.  Jumla ya watu 160,000 wanakadiriwa kuwa na ugonjwa huu nchini Tanzania. Mwaka 2016, jumla ya watu 65,908 waligundulika na kuwekwa kwenye matibabu ya TB. Asilimia 90 ya waliopata matibabu walipona kabisa.

Hata hivyo, takwimu pia zinaonyesha kuwa, wagonjwa wapatao 94,000 (59%) nchini hawakuweza kugundulika na hivyo kukosa kupewa matibabu ya TB. Na hivyo kuweka hatarini maisha yao na ya watu wengine kwa kuwa ugonjwa huu unaambukiza kwa njia ya hewa.

Katika kuadhimisha Siku ya TB Duniani, natoa wito kwa kila mmoja wetu na jamii kushiriki katika kutokomeza TB. Tunahitaji kumfikia kila mhitaji wa huduma za kupima na matibabu ya TB popote Tanzania. Tuhimize watu wote wenye dalili za TB kwenda kwenye Vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya kupima TB na kupata matibabu. Dalili za TB ni pamoja na kukohoa zaidi ya wiki 2, homa ya zaidi ya wiki 2, kutoka jasho sana, kupungua uzito na kukosa hamu ya kula. TB inatibika na kupona kabisa, dawa za TB zinatolewa bila malipo. 

Stop TB Tanzania!

Ummy Mwalimu, Mb
WAMJW
24 March 2018.
————-

# Kifua Kikuu (TB) ni ugonjwa wa kuambukiza unaoongoza kwa kusababisha vifo vingi Duniani. Ugonjwa huu unaambukiza kwa njia ya hewa.

# Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani(WHO) inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 10.4 huugua Kifua Kikuu kila mwaka Duniani na Milioni Moja kati ya hao ni watoto wenye umri chini ya miaka 15.

# Nchini Tanzania kila mwaka jumla ya watu 160,000 wanakadiriwa kuwa na ugonjwa wa Kifua Kikuu.

# Kwa mwaka 2016 jumla ya watu 65,908 waligundulika na kuwekwa kwenye matibabu ya kifua kikuu. Asilimia 90 ya waliopata matibabu ya TB wamepona kabisa. Hata hivyo, takwimu pia zinaonyesha kuwa, wagonjwa wapatao 94,000 (59%) nchini Tanzania hawakuweza kugundulika na hivyo kukosa kupewa matibabu ya TB. 

# Kauli mbiu ya Siku ya TB Duniani 2018 ni “Viongozi Tuwe Mstari wa Mbele Kuongoza Mapambano ya Kutokomeza TB."

# Nitoe wito kwa viongozi wa ngazi zote kuifanya vita dhidi ya TB kuwa agenda muhimu na ya kipaumbele. Wakati ni sasa!Viongozi wenzangu wa kisiasa, taasisi na kijamii yatupasa kuyasimamia mapambano haya na kuwa mstari wa mbele ili kuleta mabadiliko na tija katika vita hii na kulielekeza taifa letu katika hatua ya kutokomeza TB.
 
# Napenda kuwakumbusha watanzania kuwa *TB inatibika na kupona kabisa, dawa zake zinatolewa bure na zinapatikana sehemu zote nchini katika vituo vya Umma na Binafsi.*

# Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na tatizo la Kifua Kikuu nchini ikiwemo kuimarisha Huduma za uchunguzi na ugunduzi wa Kifua Kikuu katika Vituo vya Afya. Katika kupambana na TB, Serikali ya Awamu ya 5 inayoongozwa na Mhe Rais, Dr John Pombe Magufuli imefanya yafuatayo:-

i. Kuboresha Mfumo wa uchunguzi na ugunduzi wa TB katika vituo vyetu “Quality Improvement in TB case detection” ili kuhakikisha kila mgonjwa au mtu anayefika katika kituo cha huduma kupata matibabu yoyote anafanyiwa uchunguzi ili kubaini kama ana TB au la.
 
Kwa mwaka 2017 tulianza kutumia mfumo huu mpya katika mikoa 16 ambapo karibu yote imepata ongezeko katika uibuaji wa wagonjwa wa TB kati ya asilimia 13 hadi 42. Ongezeko hili limetuwezesha kufikia wagonjwa wapya wa TB wapatao 69,819 mwaka 2017 ikilinganishwa na 62,180 mwaka 2015. 

ii. Huduma ya ugunduzi wa TB kwa kupima makohozi imeboreshwa na kuanza kutumia teknolojia mpya ya gene-Xpert badala ya hadubini.  Mashine hii sasa (Gene-Xpert) ndiyo kipimo cha awali cha kuchunguza makohozi ya wahisiwa wote wa TB.

Wizara imeweza kuongeza mashine hizi kutoka mashine 66 mwaka 2014 hadi kufikia 189 mwezi Machi, 2018. Teknolojia ya mashine hizi inatuwezesha kupata majibu ndani ya masaa 2 badala ya kusubiri kwa zaidi ya masaa 24 kama ilivyo kwa njia za kawaida za hadubini. Mashine hizi pia zina uwezo wa kupima usugu wa dawa za TB wakati huo huo wa ugunduzi wa vimelea vya TB; na hivyo kugundua TB sugu kwa urahisi zaidi. Mashine hizi zimesambazwa kwenye hospitali zote za rufaa za kanda, mikoa, wilaya na baadhi ya vituo vikubwa vya afya.
Napenda kusisitiza na kuvitaka vituo vyote ambavyo vimepata teknolojia hii vitumie njia hii ya gene-Xpert kupima makohozi ya wahisiwa wote wa TB na siyo hadubini kama ilivyozoeleka. *Huduma za kupima TB kwa kutumia gene-Xpert ni bure*
 
Wiki hii, ikiwa ni mojawapo ya shughuli ya maadhimisho haya, tumetoa mashine za gene-Xpert tano (5) kwa hospitali binafsi za jijini Dar es Salaam ili kudhihirisha nia ya serikali ya kutaka kila mtoa huduma kushiriki kikamilifu na kumfikia kila Mtanzania mwenye uhitaji wa huduma za TB. Hospitali hizi ni Aga khan, Kairuki, Regency Medical center, TMJ na Hindul Mandal. Mashine hizi tulizotoa kila moja ina thamani ya Tshs. milioni 38. 
 
iii. Tarehe 20 March 2018, Serikali imezindua dawa mpya za TB za watoto ili kuhakikisha tunakidhi matakwa ya shirika la Afya Duniani (WHO) yaliyotolewa mwaka 2017 kwa nchi wanachama. Dawa hizi mpya za watoto ni za mseto (RHZ/RH) ulioboreshwa, zina ladha nzuri ya matunda, zinayeyuka kwa urahisi zikiwekwa kwenye maji na hivyo hazihitaji kukatwa katwa ili kupata dozi sahihi.  
 
iv. Mwaka 2017 tulikamilisha tahmini ya awali ya hali ya TB mashuleni, na kubaini ya kuwa kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaougua TB na Wizara yangu ikishirikiana na OR-TAMISEMI na Wizara ya Elimu tulitoa maagizo kwa ma-Katibu Tawala wa mikoa kuhakikisha wanafunzi wote hasa wa Shule za Bweni wanachunguzwa TB kabla ya kuanza shule. Nichukue fursa hii pia, kurudia kuwaagiza waganga wafawidhi wote  wa hospitali na vituo vya huduma kuhakikisha watoto wote wanaoanza shule za Bweni wafanyiwa uchunguzi wa TB kikamilifu kabla ya kuanza masomo hasa wale wa shule za bweni. Ni marufuku kujaza fomu za uchunguzi wa Afya tu bila kumpima mwanafunzi husika, hii ni kuliangamiza taifa kwa makusudi na uzembe ambao hauwezi kuendelea kuvumiliwa. 
 
v. Ushirikishwaji wa sekta binafsi katika kuibua wagonjwa wa TB umeonyesha ongezeko katika miaka ya hivi karibuni. Kwa mwaka 2017, takribani wagonjwa 7,281 ambao ni sawa na 10.4% waligunduliwa na sekta binafsi ikilinganishwa na wagonjwa 3,476 ( 5.5%) mnamo mwaka 2014.
 
vi. Serikali na wadau mbali mbali tunaendelea na utekelezaji wa kampeni za uhamasishaji na upimaji wa wananchi katika maeneo ya migodi, makazi duni kwenye miji mikubwa, magerezani na shule za bweni.
 
vii. Kwa kuzingatia kwamba wahisiwa wengi wa kifua kikuu hutafuta huduma za afya kwa waganga wa jadi, serikali imejipanga mwaka huu wa fedha kujenga uwezo kwa waganga hao ili watambue mapema na kuwapa rufaa wahisiwa wote wa kifua kikuu wanaofika kwenye maeneo yao. Ushirikishwaji huu utafanyika katika wilaya zote katika mikoa ya Simiyu, Mara, Tanga, Shinyanga, Mbeya, Kagera, Dodoma na Ruvuma.
 
viii. Ugatuzi wa huduma za Kifua kikuu sugu unaendelea na hadi kufikia Februari 2018, vituo 60 vinatoa matibabu haya ikilingalishwa na kituo kimoja cha hospitali ya Kibong’oto (Kilimanjaro) miaka mitatu iliyopita. Mafanikio haya yamewawezesha wagonjwa wa TB sugu kutibiwa katika hospitali karibu wakitokea majumbani kwao badala ya Kibong’oto wilayani Siha, Kilimanjaro ambako pia walikuwa wanakaa kwa muda mrefu.
 
# Bado kuna changamoto ambazo zinatukabili katika kukabiliana na TB kama vile Idadi kubwa ya watu wenye TB kutoweza kufikiwa na kuwekwa kwenye matibabu kila mwaka, Wagonjwa wa TB kuchelewa kujitokeza katika vituo vya huduma ili kuweza kuchunguzwa na kupatiwa matibabu kwa wakati na Ushiriki mdogo wa watoa huduma kutoka sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali.

 # Serikali itaendelea kuchukua hatua za haraka na za makusudi ili kukabiliana na changamoto hizi kwa lengo la kutokomeza TB nchini.

# Tunawashukuru wadau wetu wa maendeleo kwa kutuunga mkono na kuboresha huduma za Afya nchini zikiwemo huduma za TB. Wadau hawa ni pamoja na Global Fund, USAID, CDC/PEPFAR, Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la UNITAID, Global Drug Facility (GDF) na wengine wengi wa hapa nchini na nje pia.  

# Pia nazishukuru asasi zisizo za serikali na sekta binafsi kwa kutuunga mkono katika mapambano dhidi ya kifua kikuu. Kwa umuhimu huo huo mkubwa, napenda kuwashukuru wanahabari kwa kazi kubwa wanayofanya kuhakikisha wananchi wanapata taarifa muhimu na elimu juu ya magonjwa mbali mbali ikiwemo TB.
 
“VIONGOZI TUWE MSTARI WA MBELE KUONGOZA MAPAMBANO YA KUTOKOMEZA TB”

0 on: " SIKU YA KIFUA KIKUU DUNIANI (World TB Day) 24 March 2018"