Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Ijumaa, 29 Machi 2019

CHANJO YA MLANGO WA KIZAZI NI SALAMA

- Hakuna maoni
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jengo na mashine za tiba ya saratani.

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kushoto) wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jengo na mashine za tiba ya saratani katika taasisi ya Saratani Ocean Road

 Baadhi ya Wakurugenzi na viongozi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakifuatilia kwa makini ujumbe kutoka kwa Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jengo na mashine za tiba ya saratani katika taasisi ya Saratani Ocean Road.
 Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akikata utepe, ishara ya uzinduzi rasmi wa mashine mpya za tiba ya mionzi, Wakwanza kushoto ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akipata maelezo juu ya mashine ya kisasa ya tiba ya saratani kwa mionzi kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji  wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt. Julius Maiselage wakati hafla ya uzinduzi wa Jengo na mashine za tiba ya saratani. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

Mashine mpya za kisasa za tiba ya saratani za Linac ( Linear Accelerator) ambazo zimezinduliwa leo katika Taasisi ya Saratani Ocean Road. 

Picha ya pamoja ikiongozwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jengo na mashine za tiba ya saratani katika taasisi ya Saratani Ocean Road


Na WAMJW - DSM
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewaasa wananchi wote hususan Wazazi kuwapeleka mabinti  wao kupata chanjo ya mlango wa kizazi (HPV) ili kuwakinga dhidi ya Saratani ya hiyo.

Ameyasema hayo leo wakati wa uzinduzi wa mashine mpya za tiba ya mionzi (linear accelerators) katika Taasisi ya Saratani Ocean Road Jijini Dar es salaam.

Mhe. Samia amesema kuwa Chanjo ya mlango wa kizazi ni salama  na inatumika katika nchi mbali mbali Afrika ikiwemo nchi za Uganda, Rwanda,Afrika Kusini, Zambia na Lesotho, hivyo kuwataka wazazi na walezi kuwapeleka mabinti wao kupata chanjo hiyo inayopatikana bila malipo.

"Kwa maelezo ya Wataalamu wametuhakikishia chanjo hii haina madhara, hivyo basi nawasihi Wazazi na Walezi wenye watoto kuhakikisha binti zetu ambao wengi wapo mashuleni, wanapata chanjo hii " alisema Mhe Samia.

Aidha, Mhe Samia amesema kuwa takribani wasichana 507,720 hapa nchini, wamepatiwa chanjo hii ya mlango wa kizazi, huku lengo likiwa ni kuwafikia wasichana 616,734 hadi Disemba 2018,

Mhe. Samia amesema kuwa nchi ya Tanzania inaripotiwa kuwa na Wagonjwa wa Saratani takribani 42,060, huku wagonjwa 28,610 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na ugonjwa huo.

Mhe. Samia aliendelea kusema kuwa takwimu za 2018 za hospitali zinazotibu ugonjwa wa Saratani hapa nchini zinaonesha kuwa ni wagonjwa 14,000 sawa na 33.4% ndio wanaofika katika Hospitali ya Ocean road kupata huduma, ambao ni takribani wagonjwa 7600 kwa mwaka.

"Takwimu za hospitali zinazotibu ugonjwa wa Saratani hapa nchini za 2018, zinaonesha wagonjwa 14,000 sawa na asilimia 33.4 ndio wanaofika katika Hospitali yetu ya Ocean kupata huduma , ambao kwa mwaka ni 7600, Bugando ni wagonjwa 2790, KCMC 1050, Muhimbili 1321 na Mbeya Rufaa ni 218" alisema Mhe Samia Suluhu.

Aidha, Mhe Samia amesema kuwa inakadiriwa wagonjwa 1000 wanapata huduma katika Hospitali binafsi nchini,  huku 75% ya wagonjwa wengi wanafika katika hatua ya mwisho ya ugonjwa hali inayopelekea ugumu kuutibu ugonjwa huu.

Naye, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa idadi ya wagonjwa wanaopata ugonjwa huu, inaendelea kuongezeka nchini na Duniani huku ripoti ya 2018 ya Shirika la Umoja wa taifa la utafiti wa Saratani ikionesha kwamba takribani wagonjwa 28,610 hufariki katika wagonjwa wapya 42,060, huku vifo hivyo vikitarajia kufika Milioni 24 ifikapo 2035

Mbali na hayo, Waziri Ummy amesema kuwa kwa wanawake Saratani ya matiti inaongoza kwa kuwa na wagonjwa 24.2%, ikifuatiwa na Saratani ya utumbo mpana 9.6%, huku Saratani ya mapafu ni 8.4% na Saratani ya mlango wa kizazi ikiwa ni 6.6%

Aliendelea kusema kuwa kwa wanaume Saratani ya mapafu inaongoza kwa asilimia 14.5% ikifuatiwa na Saratani ya tezi dume ambayo ni asilimia 13.5%, Saratani ya utumbo mpana asilimia 10.9% na Saratani ya tumbo ni 7.2%.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt. Julius Mwaiselage amesema kuwa taasisi imefanikiwa kupunguza muda wa kuwahudumia wagonjwa tangu kufungwa kwa mashine hizo kutoka wiki sita mpaka kufikia wiki tatu,  na ifikapo mwezi Mei itafikia wiki mbili tu.

Naye, Shuhuda aliewahi kupata matibabu kupitia mashine hizo katika taasisi ya Saratani Ocean Road Bw. Frank  Ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Rais wake Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa juhudi wanazofanya za kuboresha Sekta ya Afya hususan katika huduma za kibingwa.

Mwisho.

Alhamisi, 28 Machi 2019

SERIKALI YAOKOA BILIONI KUMI ZA CHANJO

- Hakuna maoni




Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu (wakatikati) akikagua chumba cha kuhifadhia chanjo pindi alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa jengo la chanjo, katika   eneo la Mabibo Jijini Dar es salaam. Kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Zainab Chaula na Wakwanza kushoto ni Meneja mpango wa taifa wa chanjo Bi Dafrosa Lyimo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akiongozana na Katibu mkuu wa Wizara hiyo Dkt Zainab Chaula wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa maabara ya Afya ya Jamii iliyo katika eneo la Mabibo Jijini Dar es salaam.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akikagua ujenzi wa maabara ya Afya ya Jamii ulio katika hatua za Mwisho.



Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara kuu ya Afya Dkt Zainab Chaula katika picha pamoja na Meneja mpango wa taifa wa chanjo Bi Dafrosa Lyimo katika gari la kusafirishia chanjo lenye thamani ya zaidi ya Milioni 391.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt Zainab Chaula (Watatu kushoto) akiongozana na Meneja mpango wa taifa wa chanjo Bi Dafrosa Lyimo (wapili kushoto) pamoja na Mkandarasi wa jengo la maabara ya Afya ya Jamii (Wakwanza kushoto) wakati wa ziara ya ukaguzi wa maabara hiyo iliyo katika eneo la Mabibo Jijini Dar es salaam.



Muonekano wa Jengo la Maabara ya Afya ya Jamii lililo katika hatua za Mwisho ili kuanza kutoa huduma, jengo hilo lipo katika eneo la Mabibo Jijini Dar es salaam.

BILIONI KUMI ZAOKOLEWA KILA MWAKA - CHANJO

Na WAMJW - DSM

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imefanikiwa kuokoa takribani kiasi cha shilingi Bilion 10 kwa mwaka ambazo zingetumika katika kuhifadhi chanjo za watoto pamoja na vifaa, kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa bohari ya taifa ya chanjo iliyogharimu kiasi cha shilingi bilion 1.2.

Ameyasema hayo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu pindi alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la bohari ya Taifa ya Chanjo, akiongozana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt .Zainab Chaula.

Kwa kiasi kikubwa Waziri Ummy ameridhishwa na hali ya ujenzi huo, hususan katika ujenzi wa vyumba vya kuhifadhia chanjo (stoo), jambo litalosaidia wananchi hususan Wazazi wenye watoto wadogo kupata Chanjo kwa wakati.

Pia,  Waziri Ummy amempongeza Meneja Mpango wa taifa wa chanjo Dkt.Dafrosa Lyimo kwa kushirikiana na Mkandarasi kwa usimamizi mzuri wa jengo hilo hadi kufikia hatua ya mwisho.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara kuu ya Afya Dkt Zainab Chaula ameahidi kuendelea kusimamia vizuri shughuli zote ili kuendelea kuboresha Sekta ya Afya kwa kasi ili wananchi wa hali zote wanufaike.

Kwa upande mwingine Dkt. Zainab Chaula amesisitiza juu ya ushirikiano baina ya Watumishi katika Sekta ya Afya ili kurahisisha utendaji kazi kwa urahisi katika ngazi zote, hali itayosaidia wananchi kupata huduma bora.

Kwa upande wake Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo Dkt.Dafrosa Lyimo amesisitiza kwamba jengo hilo litakapokamilika  litaleta faida nyingi katika kutoa huduma kwa wananchi ikiwemo kurahisisha usambazaji wa chanjo katika ngazi ya Mkoa, na kurahisisha upatikanaji wa chanjo hizo katika ngazi zote kwa wakati wowote.

Dkt.Lyimo ameahidi kuendelea kusimamia kwa ukaribu shughuli zote za mpango huo ikiwemo upatikanaji wa Chanjo kwa wakati wote na mahali popote ili wananchi waendelee kupata huduma hiyo.

Mwisho.

Jumatano, 27 Machi 2019

SERIKALI YAZINDUA MFUMO WA MATIBABU KWA MTANDAO

- Hakuna maoni
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akibofya batani, ikiwa ni ishara ya kuzindua Mfumo mpya wa utoaji huduma za afya kwa njia ya mtandao,  katika Mkutano wa 27 wa masuala ya Sayansi na Afya uliowakutanisha mawaziri wa afya kutoka nchi za Afrika Mashariki katika Kituo cha mikutano ya Kimataifa cha J.K Nyerere Jijini Dar es salaam.

Wadau wa masuala ya Afya, kutoka nchi mbali mbali wakifuatilia ufunguzi wa wa mkutano wa 7 wa masuala ya sayansi na Afya uliowakutanisha mawaziri wa Afya kutoka nchi za Afrika Mashariki, mkutano huo ulifunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (Hayupo kwenye picha).

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, akinyanyua juu kitabu cha Mwongozo wa Mfumo mpya wa utoaji huduma za afya kwa njia ya mtandao utaosaidia kurahisisha utoaji wa huduma za Afya kwa wananchi. Wakwanza kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje, Palamagamba Kabudi na Watatu kushoto ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.
 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Wakulia) akipata maelekezo, wakati alipita katika mabanda ya maonesho baada ya kumaliza Mkutano wa Kimataifa wa 7 wa masuala ya Sayansi na Afya uliowakutanisha mawaziri wa afya kutoka nchi za Afrika Mashariki, mkutano huo umefanyika katika Kituo cha mikutano cha Kimataifa cha J.K Nyerere Jijini Dar es salaam.




SERIKALI YAZINDUA MFUMO WA MATIBABU KWA MTANDAO

Na WAMJW - DOM

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto leo imezindua Mfumo mpya wa utoaji huduma za afya kwa njia ya mtandao utakaosaidia kurahisisha utoaji  huduma za Afya ikiwemo  matibabu ya kibingwa kwa wananchi.

Uzinduzi huo umefanyika  na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 7 wa masuala ya Sayansi na Afya uliowakutanisha mawaziri wa afya kutoka nchi za Afrika Mashariki kujadili kwa pamoja juu ya njia ya kufanikisha malengo ya Afya ya Umoja wa Mataifa.

Mhe. Samia amesema kuwa nchi za Afrika Mashariki zikijikita katika utoaji huduma kwa mfumo huo kwa ushirikiano wa pamoja, itakuwa ni njia sahihi kwa nchi hizo kufikia malengo ya milenia na huduma za afya kwa wote.

“Tunapaswa kufikia malengo tuliyojiwekea kama bara la Afrika na nchi za Afrika mashariki, mkutano huu si tu wa watafiti kutoka Afrika Mashariki bali ni muhimu kwa wadau wote katika sekta ya afya tufanye kazi kwa pamoja kukamilisha malengo haya,” alisema Mhe. Samia.

Mhe. Samia aliendelea kusema kuwa tiba mtandao itawezesha na kuongeza ufanisi katika kufanya uchunguzi, utoaji wa tiba na dawa kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali, hivyo kurahisisha utoaji huduma za Afya kwa Wananchi.

Aidha, Mhe. Samia aliongeza kuwa tiba mtandao itapunguza gharama za wagonjwa na wanaowahudumia kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za matibabu katika Vituo vya kutolea huduma na Hospitali.

Naye,Waziri wa Afya na mapambano dhidi ya VVU kutoka Burundi Dkt. Thaddee Ndikumana alisema programu hiyo itakuwa ikitumika kwa nchi za Afrika Mashariki itakuwa chachu katika kuleta Mapinduzi ya utoaji huduma za Afya kwa Wananchi wa Afrika Mashariki.

 “Wananchi wa Burundi watakuwa wanaweza kupatiwa matibabu na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili wakiwa nchini kwao bila kuja Dar es Salaam hiyo ni kitu muhimu tutakuwa tunabadilishana uzoefu raia wa Burundi walikuwa wanakuja kila siku sasa safari zitapungua, watabaki Bunjumbura na huduma watapata.” Amesema Dkt. Thaddee Ndikumana

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa daktari atakuwa na uwezo wa kuwasiliana na madaktari wenzake katika mtandao na madaktari bingwa wa nchi nzima wanaona lile tatizo jambo litalosaidia katika kutoa huduma bora kwa Wananchi wa nchi za Afrika Mashariki.

Waziri Ummy Mwalimu, aliendelea kusema kuwa tayari Tanzania ilishaingia katika mfumo wa matumizi ya kidijitali katika utoaji wa huduma kwenye maeneo mengi, na umekuwa na msaada mkubwa sana katika Sekta ya Afya.

“Nchini Tanzania miezi mitatu iliyopita madaktari walianzisha mfumo mawasiliano kupitia dijitali ambao unawawezesha madaktari bingwa kuwasiliana moja kwa moja na madaktari waliopo pembezoni na umeweza kuokoa maisha ya kinamama sita ambao walikuwa wanajifungua,” amesema Ummy.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Nimr Profesa Yunus Mgaya alisema kuwa mfumo huo utapunguza gharama za utoaji wa huduma za afya na itaongeza ufanisi katika utendaji wa kazi wa wahudumu wa afya.

“Italeta utaalamu wa hali ya juu wa kibingwa katika maeneo ambayo hauwezi kufikika kwa mfano wataalamu wanaweza kuwepo Muhimbili na mgonjwa akawa mbali ambako hapafikiki kirahisi na hiyo ni msaada mkubwa sana kwa kuwa hizi huduma kama ingetakiwa wataalamu wawepo kule gharama yake ingekuwa kubwa sana,” alisema Prof. Mgaya.

Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje na afrika Mashariki, Palamagamba Kabudi amesema kuwa nchi ya Tanzania itanufaika zaidi katika mfumo huo katika kulifikia lengo namba tatu la malengo ya milenia, pia itasaidia kufanikisha lengo la afya kwa wote ifikapo 2030.

MWISHO

Jumamosi, 23 Machi 2019

SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA KIFUA KIKUU (TB)

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kushoto) akitoa dawa za Kifua Kikuu kwa Bw. Abbas Sudi alipotembelea Hospitali ya Mbagala Jijini Dar Es Salaam kujionea hali ya utoaji huduma za matibabu ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu na kutoa Tamko la Serikali katikabkuadhimisha Siku ya Kifua Kikuu Duniani amnayo huadhimishwa Tarehe 24 Machi kila Mwaka.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kushoto) akitoa dawa za Kifua Kikuu kwa Bi. Aisha Rashid alipotembelea Hospitali ya Mbagala Jijini Dar Es Salaam kujionea hali ya utoaji huduma za matibabu ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu na kutoa Tamko la Serikali katikabkuadhimisha Siku ya Kifua Kikuu Duniani amnayo huadhimishwa Tarehe 24 Machi kila Mwaka.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kushoto) akiangalia zawadi ya nguo aliyopewa na Taasisi ya Mukukite inayojishughulisha kutoa huduma za matibabu ya ugonjwa wa kifua kikuu.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wa kati kati) akipokea maelezo kutoka kwa mtaalam kuhusu uchugnguzi wa ugonjwa wa Kifua Kikuu alipotembelea Hospitali ya Mbagala Jijini Dar Es Salaam


Wananchi waliojitokeza kumsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo pichani) alipotembelea Hospitali ya Mbagala Jijini Dar Es Salaam na kutoa Tamko la Siku ya Kifua Kikuu Duniani.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisema jambo na wananchi (hawapo pichani) alipotembea Hospitali ya Mbagala Jijini Dar Es Salaam na kutoa tamko la Siku ya Kifua Kikuu duniani.





Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Felix Lyaviva pindi alipofanya ziara na kujionea huduma za matibabu ya ugonjwa wa Kifua Kikuu katika  Hospitali ya Mbagala Jijini Dar Es Salaam


Na WAMJW - DSM 


SERIKALI imeendelea kuboresha huduma za matibabu ya kifua Kikuu kwa kuongeza vituo vya kutolea huduma za matibabu sambamba na kuongeza vifaa tiba, ikiwa ni jitihada za Serikali kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu  leo wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za kifua Kikuu na kutoa tamko kuhusiana na ugonjwa huo katika Hospitali ya Mbagala Jijini Dar es salaam. 

"Huduma za matibabu ya Kifua Kikuu (TB) sugu zimesogezwa karibu kwa wananchi, ambapo kwa sasa tunazo hospitali 93 za kutibu Kifua Kikuu sugu ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo, huduma za matibabu zilikuwa zinapatikana katika Hospitali ya Kibong'oto pekee " amesema Waziri Ummy. 

Pia, Waziri Ummy amesema katika kila Watanzania 100,000 Watanzania 269 wanahisiwa kuwa na ugonjwa wa Kifua Kikuu, huku watu 70 wanafariki kila siku kutokana ugonjwa wa Kifua Kikuu ambapo ni sawa na watu watatu hufariki kila saa. 

"watu 70 kila siku kutokana na ugonjwa wa Kifua Kikuu, kwahiyo kila saa ni sawa na watu watatu wanafariki kutokana na ugonjwa wa Kifua Kikuu ambao unatibika " alisema Waziri Ummy. 

Waziri Ummy amesema takribani wagonjwa 154,000 wanaokadiriwa kuugua ugonjwa wa Kifua Kikuu wanapaswa kufikiwa na kuingizwa katika mpango wa matibabu kila mwaka ili kuutokomeza ugonjwa huu nchini. 

Waziri Ummy ameendelea kusema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 Duniani zenye kiwango kikubwa cha wagonjwa wa Kifua Kikuu, inakadiriwa kuwa wapo wagonjwa takribani 154,000 ambao huugua ugonjwa wa kifua Kikuu kila mwaka. 

Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa Mgonjwa wa Kifua Kikuu ambae hajaanza matibabu anaweza kuambkiza Kati ya watu kumi hadi watu 20 kwa mwaka, hivyo jitihada za makusudi zinatakiwa kuendelea kuchukuliwa ili kutokomeza ugonjwa huu nchini. 

"ifahamike kuwa mgonjwa wa kifua Kikuu ambae hajaanza matibabu anaweza kuambukiza kati ya watu kumi hadi watu ishirini kwa mwaka, hivyo tunalojukumu kubwa lakuhakikisha tunawafikia wote wanaougua ili tuweze kuzuia maambukizi mapya ya Kifua Kikuu" amesemaWaziri Ummy 

Mbali na hayo, Waziri Ummy amesema kuwa kitaifa tunakadiliwa kuwa wapo wagonjwa wa Kifua Kikuu sugu takribani 200 na kati yao, wagonjwa 167 sawa na 84% walianzishiwa matibabu, huku akitoa wito kwa wagonjwa wengine kujitokeza kupata matibabu. 

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaviva amemuomba Waziri Ummy kuona ulazima wa kuipanua Hospitali ya Mbagala, ili kurahisisha utoaji huduma za Afya, kwani takribani wanawake 67 mpaka 70  hujifungua kwa siku.

"Wakina mama wanaojifungua hapa ni wengi sana, kwa Mfano jana tu wakina mama 67 wamejifungua, siku nyingine wanafika 70 mpaka 80, hivyo tunahitaji ipanuliwe hospitali hiyo " alisema Mhe. Felix Lyaviva 

Nae Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Mbagala Dkt. Dk Ally Mussa amesema kuwa kutokana na maboresho makubwa ya hospitali kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa hadi kufikia wagonjwa 1700 kwa siku,  kumekuwa na maboresho makubwa ya huduma za mama na mtoto, maboresho ya huduma za uchunguzi wa magonjwa (maabara za kisasa) 

"kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa baada ya maboresho mengi katika huduma za Afya za hospitali, kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa hadi kufikia wagonjwa 1700 kwa siku" alisema Dkt. Dk Ally Mussa

VIFO VYA WAMAMA WAJAWAZITO VYAPUNGUA KWA ZAIDI YA 40%

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akikata utepe kuashiria ufunguzi wa jengo la wagonjwa wa kulipia hospitali ya CCBRT Jijini Dar es salaam.Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa CCBRT Brenda Msangi

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akihoji kupata ufafanuzi wa kina kutoka kwa mtaalamu wa Maabara ya macho CCBRT wakati wa ufunguzi wa jengo la jengo la wagonjwa wa kulipia hospitali ya CCBRT Jijini Dar es salaam.

Baadhi ya wageni waliohudhuria hafla ya ufunguzi wa jengo la wagonjwa wa kulipia hospitali ya CCBRT Jijini Dar es salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Hayupo kwenye picha)

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa jengo la jengo la wagonjwa wa kulipia hospitali ya CCBRT Jijini Dar es salaam.

Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na Viongozi wa CCBRT na wajumbe wa bodi ya CCBRT baada ya ufunguzi wa jengo la wagonjwa wa kulipia hospitali ya CCBRT Jijini Dar es salaam.


VIFO VYA WAMAMA WAJAWAZITO VYAPUNGUA KWA ZAIDI YA 40%

Na WAMJW - DSM

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Wadau wa masuala ya Afya imefanikiwa kupunguza Vifo vya wamama wajawazito kwa zaidi ya 40% , hali inayotokana na uboreshwaji wa huduma za Afya kwa wananchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu leo wakati wa ufunguzi wa jengo la wagonjwa wa kulipia hospitali ya CCBRT Jijini Dar es salaam.

Waziri Ummy amesema kuwa Serikali imejenga na kuboresha zaidi ya vituo vya kutolea huduma za afya zaidi ya 350 ambavyo vinatoa huduma za dharura ikiwemo huduma ya upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni.

"Tumepunguza vifo vyakina mama wajawazito kwa zaidi ya 40% ndani ya miaka sita (2012-2018), na kazi hii haijafanywa na Serikali tu,  kwahiyo hongereni sana CCBRT " alisema Mhe. Ummy Mwalimu.

Pia, Waziri Ummy amesema kuwa sote tunatambua umuhimu wa mtu kuwa na afya njema ili kuweza kumudu kushiriki katika shughuli za kijamii na kiuchumi kuanzia ngazi ya kaya hadi taifa, hivyo hatuwezi kuendelea kutegemea watu wengine kushughulikia afya za Watanzania.

Aidha, Waziri Ummy alisema kuwa Serikali imekuwa ikitoa huduma za matibabu kwa gharama nafuu sana au bila malipo kwa baadhi ya magonjwa kama Fistula, Mdomo Wazi na watoto chini ya miaka mitano.

Mbali na hayo, Waziri Ummy amesema kuwa katika miaka ya hivi karibuni uchumi wa dunia umeyumba na kupelekea kupungua kwa wafadhali. Kujengwa kwa kliniki hii ambayo itasaidia kuziba pengo la kiasi kinachopungua kutoka kwa wafadhili ambao ni jambo la msingi na la kuigwa.

Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau kama CCBRT imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye Sekta ya Afya yenye lengo la kuboresha utoaji wa huduma za afya na kuimarisha afya za wananchi.

KAMATI YA BUNGE YAKUDUMU YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII YAFANYA ZIARA HOSPITALI YA TUMBI-PWANI

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akijibu hoja za baadhi ya Wabunge ambao ni wanakamati ya Bunge ya kudumu ya huduma na Maendeleo ya Jamii wakati wa ziara yao ya ukaguzi wa ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Peter Selukamba akihoji jambo lililokwenye taarifa ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje wakati Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na Maendeleo ya Jamii ilipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiongozana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula baada ya kumaliza ziara Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na Maendeleo ya Jamii ilipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiteta jambo  na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula wakati wa kujibu hoja Wabunge wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na Maendeleo ya Jamii walipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Peter Selukamba akipitia kwa kina taarifa ya ujenzi wa jengo la uchunguzi na jengo la vyumba vya upasuaji ambalo limekamilika kwa 100%,  jengo la wagonjwa wa nje, wakati Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na Maendeleo ya Jamii ilipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi.

Wabunge na Wajumbe wa kamati ya Bunge ya huduma na Maendeleo ya Jamii wakifuatilia uwasilishwaji wa taarifa za ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje, jengo la uchunguzi na jengo la vyumba vya upasuaji.


Na WAMJW-PWANI

Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na Maendeleo ya Jamii imefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi ikiwa ni mwendelezo wa ziara yao ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya.

Kwa kiasi kikubwa kamati hiyo imeridhishwa na ujenzi wa jengo la uchunguzi, jengo la vyumba vya upasuaji ambalo limekamilika kwa 100%, huku ikionekana kutoridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje,

Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Peter Selukamba amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula kupitia mkataba wa ujenzi wa jengo hilo ili kurekebisha baadhi ya mapungufu ili ujenzi umalizike mapema na huduma zianze kutolewa.

Nae Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amekiri uwepo wa mapungufu na kuahidi kutatua mara moja na huduma zitaanza kutolewa.

Alhamisi, 21 Machi 2019

HOSPITALI ZA MIKOA ZATAKIWA KUONGEZA UBUNIFU ILI KUWEZA KUJIENDESHA

- Hakuna maoni
Kaimu Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii ambae pia ni Mbunge wa Biharamulo  Mhe. Oscar Mukasa akiteta jambo na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati kamati hiyo ilipotembelea hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mwananyamala katika kujionea hali ya utoaji huduma za afya.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula akijibu hbaadhi ya hoja za Wabunge wa kamati ya Bunge ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii wakati kamati hiyo ilipotembelea hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mwananyamala katika kujionea hali ya utoaji huduma za afya.

Mbunge wa Nzega mjini Hussein Bashe akisisitiza jambo wakati wa kikao cha kamati ya Bunge ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii pindi ilipotembelea hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mwananyamala katika kujionea hali ya utoaji huduma za afya.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akijibu hoja mbele ya Wabunge wa kamati ya Bunge ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii pindi kamati hiyo hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mwananyamala katika kujionea hali ya utoaji huduma za afya.

Kaimu Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii ambae pia ni Mbunge wa Biharamulo  Mhe. Oscar Mukasa (Watatu kushoto) akiongozana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (wapili kushoto) pamoja na Wabunge wengine kutoka kamati ya Bunge ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii pindi kamati hiyo hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mwananyamala katika kujionea hali ya utoaji huduma za afya.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akieleza kuhusiana na unyanyasaji wa kijinsia, pindi alipotembelea wodi ya wagonjwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala wakati kamati ya Bunge ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii pindi ilipotembelea hospitali hiyo kujionea hali ya utoaji huduma za afya.

Picha ya pamoja ikiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii ambae pia ni Mbunge wa Biharamulo  Mhe. Oscar Mukasa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula na Wabunge wengine kutoka kamati ya Bunge ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii pindi kamati hiyo hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mwananyamala katika kujionea hali ya utoaji huduma za afya.


HOSPITALI ZA MIKOA ZATAKIWA KUONGEZA UBUNIFU ILI KUWEZA KUJIENDESHA

Na WAMJW - DSM

Matumizi ya fedha za ndani katika Hospitali za umma yanaweza  kutumika katika kutatua uhaba wa watumishi katika ngazi zote na kuacha tabia ya kuisubiri Serikali kufanya kila kitu.

Hayo yamesemwa leo na Kaimu Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii ambae pia ni Mbunge wa Biharamulo  Mhe. Oscar Mukasa wakati kamati hiyo ilipotembelea hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mwananyamala katika kujionea hali ya utoaji huduma za afya.

Aidha,Mhe.Mukasa ameziasa Hospitali hizo kuwa wabunifu ili ziweze  kujiendesha katika kutoa huduma bora  kwa wananchi. 

"Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya ni moja ya maeneo ambayo nimewahi kushuhudia matumizi bora ya fedha za ndani katika kutatua ikama ya watumishi hata ngazi ya Madaktari na Wauguzi " alisema Mhe. Oscar Mukasa.

Akijibu hoja za baadhi ya Wabunge Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha vituo vya Afya na kujenga Hospitali za Wilaya ili kupunguza msongamano katika Hospitali za Rufaa za mikoa.

"Serikali kwa kushirikiana na mamlaka nyingine tumeamua kuboresha vituo vya Afya ili kupunguza mzigo mkubwa kwa Hospitali za Rufaa, na katika Wilaya ya Kinondoni kuna vituo vya afya viwili vinavyojengwa" alisema Dkt Ndugulile 

Dkt. Ndugulile aliendelea kusema kuwa Serikali inatambua kuwa zaidi ya 60% ya watu wanaoenda kupata huduma za Afya ni watu wa misamaha, hivyo kupoteza zaidi ya Bilioni mbili kwa mwezi na hiyo ni kutoka Julai 2018 mpaka mwezi Februari 2019, hali inayorudisha nyuma shughuli za utoaji huduma bora za Afya. 

Aidha,  Dkt Ndugulile amesema kuwa Serikali ipo katika hatua ya  kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na Bima ya Afya, ikiwa ni moja ya njia ya kuondokana na tatizo la misamaha kwa matibabu kwa wananchi. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula ameahidi kuendelea kuboresha Sera na miongozo ya Sekta ya Afya ili hali ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi iwe ya kuridhisha na stahili kwa wananchi. 

Mwisho.

Jumanne, 19 Machi 2019

TANZANIA YATOA MSAADA KWA MSUMBIJI, ZIMBABWE NA MALAWI

- Hakuna maoni
Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa Kimataifa Prof. Palamagamba Kabudi akimkabidhi boksi la dawa Balozi wa Malawi nchini Tanzania Mhe. Glad Chembe Munthali (Wakwanza kushoto), Watatu kushoto ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula wakati wakikabidhi msaada wa vyakula na madawa kwa nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe zilizopata janga la mafuriko. Tukio limefanyika leo katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Wakwanza kulia) akionesha maboksi ya Dawa zinazotaraji kupelekwa katika nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe zilizopata janga la mafuriko.

Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa Kimataifa Prof. Palamagamba Kabudi akiongozana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakiwa ndani ya ndege itayotumika kubeba dawa vyakula kwaajili ya msaada kwa nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe zilizopata janga la mafuriko.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wa kulia) akiongozana na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt Zainab Chaula baada yakujionea dawa zilizoingizwa ndani ya ndege yakijeshi itayopeleka misaada hiyo.


Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa Kimataifa Prof. Palamagamba Kabudi (Wakwanza kushoto)  akiongozana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wapili kutoka kushoto)  wakati wakikabidhi msaada wa vyakula na madawa kwa nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe zilizopata janga la mafuriko. Tukio limefanyika leo katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.





Shughuli yakupakia Dawa na Vyakula katika ndege ikiwa tayari kuelekea katika nchi zilizopata majanga ya mafuriko (Zimbabwe,Malawi na Msumbiji).


TANZANIA YATOA MSAADA KWA MSUMBIJI, ZIMBABWE NA MALAWI 

Na WAMJW - DSM

Nchi ya Tanzania kupitia Rais wake Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli imedhihirisha ule msemo wa "undugu ni kufaana na si kufanana" baada kujitolea  msaada wa vyakula na madawa ili kuwasaidia wananchi walioathirika na mafuriko  ikiwa ni sehemu ya kudumisha umoja na ushirikiano baina ya nchi hizi.

Hayo yamejiri leo baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Prof. Palamagamba Kabudi kwa kushirikiana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kutoa msaada wa vyakula na madawa kwa nchi za Msumbiji na Malawi baada yakupata janga la mafuriko.

"Hawa ni ndugu zetu, jirani zetu,  tupo pamoja katika jumuia ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC), kwahiyo Tanzania imeona ni vyema katika undugu wetu, umoja wetu na ujirani wetu tuweze kuwapelekea nchi hizi msaada wa madawa na chakula ikiwa ni sehemu ya kuwapa pole kwa maafa haya" alisema Prof.  Kabudi. 

Prof. Kabudi amesema kuwa Kimbunga hicho cha Idai kimepelekea mafuriko ambayo yameleta maafa makubwa sana, huku nchi ya Msumbiji jumla ya watu 221 wamepoteza maisha,  huku watu 88 kutoka Beira, watu 68 Manika, watu 51 Zambezi, na watu 19 kutoka Tete, huku zaidi ya watu 1000 hawana mahali pa kuishi.

Prof. Kabudi aliendelea kusema kuwa,  kwa upande wa Zimbabwe watu 98 kutoka mji wa Manipaland wamefariki,  huku watu 122 wakiwa wamefariki katika nchi ya Malawi, huku wengine wakiachwa katika hali ngumu. 

Aidha, Prof. Kabudi amewaasa Wafanya biashara na wananchi wengine walioguswa na maafa haya wasisite kutoa msaada kwa nchi jirani ambazo zimepata majanga Hayo kadiri ya uwezo wao.

Pia,  Prof. Kabudi aliendelea kuyaasa mashirika, makampuni na watu binafsi ambao wameguswa na hali ambayo imezikuta nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe waweze kuchanga na kuvikabidhisha vitu hivyo katika Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Afya ili viweze kupelekwa mahala husika. 

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa Wizara ya Afya imeandaa tani 24, ambazo ni sawa na tani (8) kwa kila nchi ambazo zitasaidia wananchi waliopata janga hilo kukabiliana dhidi magonjwa.

Mbali na hayo,  Waziri Ummy amesema kuwa kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Mawaziri wa Afya kutoka nchi za Zimbabwe na Malawi dawa kubwa zinazohitajika ni dawa za kuzuia maambukizi ya bakteria (antibiotics) na dawa kwa ajili ya magonjwa ya matumbo, (ORS) na dripu.

"tumeweka takribani aina tano za dawa za kuzuia maambukizi ya bakteria, tumeweka dawa kwa ajili ya magonjwa ya matumbo, Kama vile kuhara (ORS), tumeweka dawa kwa  ajili ya kutibu kwa kutumia maji (dripu), pia mashuka, magodoro, vyandarua, blanket na dawa za maumivu " alisema Waziri Ummy. 

Hata hivyo,  Waziri Ummy amesema kuwa kila nchi itapata tani  saba (7) za mchele kwa ajili ya Msumbiji na Zimbabwe na Malawi watapata tani 200 za mahindi ambayo yatatoka katika mkoa wa Mbeya ambayo upo karibu na nchi hiyo. 

Kwa upande wa Balozi wa Malawi nchini Tanzania Mhe. Glad Chembe Munthali ameishukuru nchi ya Tanzania kwa upendo na msaada waliouonesha kwa Malawi na kuahidi kufikisha salam hizo za upendo kwa rais wa Malawi huku akisisitiza kuwa Serikali ya Tanzania na ya Malawi zitaendelea kuwa marafiki milele. 

Mwisho