Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa Kimataifa Prof. Palamagamba
Kabudi akimkabidhi boksi la dawa Balozi wa Malawi nchini Tanzania Mhe.
Glad Chembe Munthali (Wakwanza kushoto), Watatu kushoto ni Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula wakati
wakikabidhi msaada wa vyakula na madawa kwa nchi za Msumbiji, Malawi na
Zimbabwe zilizopata janga la mafuriko. Tukio limefanyika leo katika
uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy
Mwalimu (Wakwanza kulia) akionesha maboksi ya Dawa zinazotaraji
kupelekwa katika nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe zilizopata janga
la mafuriko.
Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa Kimataifa Prof. Palamagamba
Kabudi akiongozana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakiwa ndani ya ndege itayotumika kubeba
dawa vyakula kwaajili ya msaada kwa nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe
zilizopata janga la mafuriko.
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
(wa kulia) akiongozana na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt Zainab Chaula
baada yakujionea dawa zilizoingizwa ndani ya ndege yakijeshi itayopeleka
misaada hiyo.
Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa Kimataifa Prof. Palamagamba
Kabudi (Wakwanza kushoto) akiongozana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wapili kutoka
kushoto) wakati wakikabidhi msaada wa vyakula na madawa kwa nchi za
Msumbiji, Malawi na Zimbabwe zilizopata janga la mafuriko. Tukio
limefanyika leo katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini
Dar es salaam.
Shughuli yakupakia Dawa na Vyakula katika ndege ikiwa tayari kuelekea katika nchi zilizopata majanga ya mafuriko (Zimbabwe,Malawi na Msumbiji).
TANZANIA YATOA MSAADA KWA MSUMBIJI, ZIMBABWE NA MALAWI
Na WAMJW - DSM
Nchi ya Tanzania kupitia Rais wake Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli imedhihirisha ule msemo wa "undugu ni kufaana na si kufanana"
baada kujitolea msaada wa vyakula na madawa ili kuwasaidia wananchi
walioathirika na mafuriko ikiwa ni sehemu ya kudumisha umoja na
ushirikiano baina ya nchi hizi.
Hayo yamejiri leo baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa Prof. Palamagamba Kabudi kwa kushirikiana na
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy
Mwalimu kutoa msaada wa vyakula na madawa kwa nchi za Msumbiji na Malawi
baada yakupata janga la mafuriko.
"Hawa ni ndugu zetu, jirani zetu, tupo pamoja katika
jumuia ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC), kwahiyo Tanzania imeona
ni vyema katika undugu wetu, umoja wetu na ujirani wetu tuweze
kuwapelekea nchi hizi msaada wa madawa na chakula ikiwa ni sehemu ya
kuwapa pole kwa maafa haya" alisema Prof. Kabudi.
Prof. Kabudi amesema kuwa Kimbunga hicho cha Idai
kimepelekea mafuriko ambayo yameleta maafa makubwa sana, huku nchi ya
Msumbiji jumla ya watu 221 wamepoteza maisha, huku watu 88 kutoka
Beira, watu 68 Manika, watu 51 Zambezi, na watu 19 kutoka Tete, huku
zaidi ya watu 1000 hawana mahali pa kuishi.
Prof. Kabudi aliendelea kusema kuwa, kwa upande wa
Zimbabwe watu 98 kutoka mji wa Manipaland wamefariki, huku watu 122
wakiwa wamefariki katika nchi ya Malawi, huku wengine wakiachwa katika
hali ngumu.
Aidha, Prof. Kabudi amewaasa Wafanya biashara na wananchi
wengine walioguswa na maafa haya wasisite kutoa msaada kwa nchi jirani
ambazo zimepata majanga Hayo kadiri ya uwezo wao.
Pia, Prof. Kabudi aliendelea kuyaasa mashirika, makampuni
na watu binafsi ambao wameguswa na hali ambayo imezikuta nchi za
Msumbiji, Malawi na Zimbabwe waweze kuchanga na kuvikabidhisha vitu
hivyo katika Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Afya ili viweze kupelekwa
mahala husika.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa Wizara ya Afya imeandaa
tani 24, ambazo ni sawa na tani (8) kwa kila nchi ambazo zitasaidia
wananchi waliopata janga hilo kukabiliana dhidi magonjwa.
Mbali na hayo, Waziri Ummy amesema kuwa kwa mujibu wa
taarifa kutoka kwa Mawaziri wa Afya kutoka nchi za Zimbabwe na Malawi
dawa kubwa zinazohitajika ni dawa za kuzuia maambukizi ya bakteria
(antibiotics) na dawa kwa ajili ya magonjwa ya matumbo, (ORS) na dripu.
"tumeweka takribani aina tano za dawa za kuzuia maambukizi
ya bakteria, tumeweka dawa kwa ajili ya magonjwa ya matumbo, Kama vile
kuhara (ORS), tumeweka dawa kwa ajili ya kutibu kwa kutumia maji
(dripu), pia mashuka, magodoro, vyandarua, blanket na dawa za maumivu "
alisema Waziri Ummy.
Hata hivyo, Waziri Ummy amesema kuwa kila nchi itapata
tani saba (7) za mchele kwa ajili ya Msumbiji na Zimbabwe na Malawi
watapata tani 200 za mahindi ambayo yatatoka katika mkoa wa Mbeya ambayo
upo karibu na nchi hiyo.
Kwa upande wa Balozi wa Malawi nchini Tanzania Mhe. Glad
Chembe Munthali ameishukuru nchi ya Tanzania kwa upendo na msaada
waliouonesha kwa Malawi na kuahidi kufikisha salam hizo za upendo kwa
rais wa Malawi huku akisisitiza kuwa Serikali ya Tanzania na ya Malawi
zitaendelea kuwa marafiki milele.
Mwisho
0 on: "TANZANIA YATOA MSAADA KWA MSUMBIJI, ZIMBABWE NA MALAWI"