Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akisema jambo wakati wa kikao na watendaji wa Hospitali ya Wilaya ya Kilosa (hawapo pichani)
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu (kushoto) akichunguza hali ya utoaji huduma katika duka la dawa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu ( kulia) akiwasalimia mama na mtoto katika wodi ya mama na mtoto katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akisoma nyaraka za dawa katika chumba cha dawa cha Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu (kushoto) akiteta jambo na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Dkt Halima Mangiri.
Na Englibert Kayombo, WAMJW - Kilosa, MOROGORO.
Wananchi wametakiwa kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya ili kuwa na
uhakika wa kupata matibabu wanapofika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya
nchini.
Waziri Ummy Mwalimu ameyasema hayo leo alipokuwa ziarani Wilaya ya
Kilosa Mkoa wa Morogoro akikagua hali ya utoaji wa huduma za afya katika
Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.
“Ni muhimu kwa wananchi kuwa na bima ya afya ili waweze kuwa na uhakika
wa kupata matibabu ikiwemo dawa bila ya kikwazo cha fedha” amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema kuwa matarajio ya wananchi mara baada ya kujiunga na
bima ya afya ni kupata huduma bora za afya bila usumbufu huku wakiwa na uhakika
wa kupata dawa kwa makundi yote ikihusishwa wale wa Bima ya Afya pamoja na
Mfuko wa Bima ya Afya Ngazi ya Jamii (CHF) iliyoboreshwa.
“Mwananchi yeyote ambaye amekuja na bima ya afya, CHF iliyoboreshwa
wanapaswa kupata huduma zote, kumwona daktari bure, vipimo bure, na dawa bure”
amesema Waziri Ummy na kuongezea “Bila ya kufanya hivyo hakuna umuhimu wa
kuwaambia wananchi kukata bima za afya.
Kwa upande mwingine, Waziri Ummy amewataka watoa huduma za afya nchini
kutoa huduma bora kwa kuzingatia Mwogozo wa Taifa wa Matibabu na orodha ya dawa
muhimu huku akiwataka kutoa huduma bora za matibabu kwa kutoa dawa kulingana na
mwogonzo unavyobainisha.
“Badala ya kumwandikia unayoitaka wewe au mgonjwa, tumeweka utaratibu
weka dawa ambayo ipo kwa mujibu wa mwongozo” alisema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha wananchi
wanapata dawa katika vituo vya kutolea huduma kwani kumekuwa na malalamiko hapo
zamani wagonjwa wakisema madaktari walikuwa waki waambia dawa hakuna huku ili
hali dawa zipo.
“Hatutaki kuona wananchi wanalalamika dawa hakuna na kutuona
tunadanganya wakati dawa zipo, na mwongozo unasema wazi kama hakuna dawa A mpe
dawa B. Alisikika akisema Waziri Ummy.
Kwa upande mwingine Waziri Ummy ameupongeza Uongozi wa Hospitali ya
Wilaya ya Kilosa kwa kuhakikisha dawa zinapatikana kwa ufanisi muda wote na
kuwataka mafanikio ambayo wameyapata wahakikishe waharudi chini.
“Serikali itaendela kuhakikisha inaboresha Sekta ya afya ili Taifa
liweze kuwa na nguvu kazi yenye afya bora kazi yenu nyinyi ni kuhakikisha
mnaendelea kutoa huduma bora na kuhakikisha dawa zinapatikana muda wote”
amesema Waziri Ummy.
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Dkt. Halima Mangiri ameishukuru
Serikali kwa kuuongeza bajeti ya dawa wilayani humo.
Dkt. Mangiri amesema kuwa bajeti ya dawa imekuwa ikiongezeka maradufu
mwaka hadi mwaka huku akitolea mfano wa mwaka 2017/18 hali ya upatikanaji wa
dawa ilikuwa ni asilimia 86, huku kwa mwaka 2018/19 hali ya upatikanaji dawa
ikiongezeka na kufikia asilimia 96.
“Tunaishukuru Serikali, Kwa kweli hali sasa sii kama zamani, tunapata
dawa na hali inaridhisha” alisema Dkt Mangiri.
Mwisho
0 on: "“BIMA YA AFYA NDIYO SULUHISHO LA UHAKIKA WA MATIBABU”-WAZIRI UMMY MWALIMU"