Moja ya maduka yaliyofungwa na wataalam kutoka Sekretarieti ya Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala baada ya kukaguliwa na kubainika kukosa vigezo vya kuendesha biashara hiyo. |
Na WAMJW-DSM
Watoa huduma
za tiba asili na tiba mbadala wametakiwa kufuata taratibu zilizowekwa na
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
ili kulinda afya ya watumiaji wa dawa na huduma hizo.
Hayo yamebainika
baada ya timu ya wataalam kutoka Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala lililo
chini ya Wizara ya Afya kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika maduka yanayouza
dawa za asili na kutoa huduma za tiba mbadala katika maeneo mbalimbali jijini
Dar Es Salaam.
Katika ukaguzi
huo imebainika baadhi ya maduka kufanya shughuli hiyo bila ya kuwa na vibali
vikiwemo kibali cha mtoa huduma, Kibali cha duka pamoja na kibali cha usajili
wa dawa, ambapo vibali hivyo vinatolewa na Baraza la Tiba Asili na Tiba
Mbadala.
Dkt. Ruth
Suza msajili wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala amewataka watoa huduma
hizo kufuata taratibu zilizowekwa na Wizara ili kuepuka usumbufu wa kufungiwa
na kulipa faini kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa na Baraza la Tiba Asili na
Tiba Mbadala.
“Ninawataka
watoa huduma za Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini kote kuhakikisha wanafuata
taratibu zilizowekwa na Baraza ili kuweza kuendesha biashara zao, vinginevyo
tukipita kukagua na tukikuta duka lina kasoro kwa kukosa vibali basi tutapiga
faini na ikishindikana kulipa faini tutalifunga duka hilo mpaka muhusika afuate
utaratibu unaotakiwa wa kufanya biashara hiyo”. Amesema Dkt. Ruth.
Katika ukaguzi
huo uliochukua takribani wiki mbili katika wilaya zote za Jiji la Dar Es
Salaam, jumla ya maduka 70 yamekaguliwa, maduka 10 yamefungwa kutokana na
sababu mbalimbali ikiwemo maduka na wauzaji wa dawa kutokua na vibali kutoka
baraza la tiba asili na tiba mbadala.
Zoezi hili
lenye lengo la kulinda afya ya watumiaji wa dawa za asili na tiba mbadala ni
endelevu ambapo linategemea kuendelea katika mikoa yote nchini kukagua uhalali
wa usajili wa dawa za asili, vibali vya maduka na watoa huduma pamoja kuhakikisha
ubora wa dawa zinazotolewa.
0 on: "WATOA HUDUMA ZA TIBA ASILI NA TIBA MBADALA WATAKIWA KUFUATA UTARATIBU WA KUTOA HUDUMA HIYO"