Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatano, 6 Machi 2019

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AZITAKA TAASISI ZA UMMA KUTOINGILIANA MAJUKUMU.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) akisema jambo na watendaji wa ofisi ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) hawapo pichani alipotembelea ofisi hizo kuona utendaji kazi wao.

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa wa (wa tatu kutoka kushoto) akiongozana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wa pili kushoto) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaj Mhe. Angellah Kairuki (kushoto) kuelekea maabara za Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa ameshika  dawa ya malaria aina ya DUO -COTECXIN,  halisi kulia na bandia kushoto zilizopimwa na  Maabara ya Mamlaka ya Chakula  na Dawa (TFDA)  wakati alipotembelea ofisi za  TFDA,  wa pili kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, Angela Kairuki na wa tatu kulia ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

 Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akionyeshwa sampuli na mtaalam katika maabara ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) mapema leo alipotembelea ofisi hizo kujionea utendaji kazi wao.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kushoto) akiteta jambo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki (kulia)  wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa katika Ofisi za Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Jijini Dar Es Salaam.


Na WAMJW - Dar Es Salaam
Serikali imedhamiria kushughulikia malalamiko yaliyotolewa na  wafanyabiashara kuhusu mkanganyiko wa majukumu baina ya Taasisi za Serikali zinazoingiliana majukumu na kuzitaka kila taasisi kama hizo ziwe na mipaka yake ya kazi na kupunguza urasimu.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa alipokuwa akizungumza na watendaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa TFDA mapema leo alipotembelea ofisi hizo kujionea utendaji wao wa kazi.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema Taasisi za Serikali ambazo zimekuwa zikiingiliana majukumu na zimekuwa zikisababisha adha kwa wananchi na kuongeza urasimu na upotevu wa muda mwingi katika kuwahudumia wateja.

“Serikali imedhamiria kutafuta ufumbuzi wa malalamiko ya mwingiliano wa majukumu baina ya taasisi za Serikali ili kumwondolea usumbufu mwananchi” amesema Waziri Mkuu Majaliwa na kuendelea kusema kuwa mkanganyiko huo unapelekea watu kutokujua majukumu yao aidha kwa kutokujua sheria au kwa makusudi.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kumekuwa na malalamiko mengi ya utendaji usiyo sahihi wa mwingiliano wa majukumu hasa kwenye eneo la ukaguzi na uchukaji wa sampuli baina ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na kuzitaka taasisi hizo kujiridhisha na kuyafahamu vizuri majukumu yao.

Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Viongozi wa Wizara ya Afya, Wizara ya Kilimo, Mifugo,Wizara ya Viwanda na Uwekezaji kuwasilisha ofisini kwake ripoti ya utekelezaji wa “Blueprint” ifikapo Machi 30 mwaka huu.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa ameitaka TFDA kujiimarisha zaidi kwenye ukaguzi wa vyakula na dawa na kuhakikisha bidhaa zisizokuwa na usajili haziingii sokoni na kuitaka TFDA kuongeza wataalam katika Mikoa na Wilaya ili kudhibiti mapito ya magendo ya bidhaa za chakula na dawa.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika maabara za uchunguzi wa vyakula na dawa na hivi sasa taasisi hiyo imefikia ngazi ya tatu ya ubora wa udhibiti wa dawa kimataifa hivyo kuaminika na mataaifa mbalimbali na kuvutia wafanyabiashara wengi zaidi kuja kuingiza bidhaa zao nchini.

Waziri Ummy amesema kuwa TFDA imepewa dhamana ya kulinda afya za watanzania kwa kuhakikisha vyakula na dawa zinazozitumia kila siku ni salama kwa afya za wananchi na kukiri kuwa kweli changamoto zipo na kupitia wizara yake atahakikisha changamoto hizo zinatatuliwa ndani ya muda mfupi.

Naye ,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Angellah Kairuki amesema kuwa Serikali imeanzisha huduma ya mahali pamoja iliyopo katika kituo cha uwekezaji (TIC) ambapo mpaka sasa zipo taasisi 16 ikiwemo TFDA huku akiomba Wizara husika kuongeza watumishi katika kitengo hicho ili kuweza kushughulikia kwa uharaka masuala ya uwekezaji katika vyakula na dawa.

Aidha,Waziri Kairuki amekiri kuwepo mkakanganyiko wa majukumu baina ya taasisi za Serikali huku akiitaka TFDA kutowahudumia wawekezaji wanaofika nchini wakiwa na Vyeti vya Usajili wa Vivutio kwani wanatakiwa kuhudumiwa na TIC.

"Naomba kuweka msisitizo, mara anapokuja mwekezaji, swali lenu la kwanza liwe ni kuuliza kama anacho Cheti cha usajili wa vivutio kutoka TIC au la, na endapo anayo basi nyinyi mwelekezeni TIC".Alisisitiza Waziri Kairuki

Mwisho.

0 on: "WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AZITAKA TAASISI ZA UMMA KUTOINGILIANA MAJUKUMU."