Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Alhamisi, 14 Machi 2019

TAMKO LA NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, DKT. FAUSTINE NDUGULILE (MB) KWENYE MAADHIMISHO YA WIKI YA KUONGEZA UELEWA KUHUSU UGONJWA WA SHINIKIZO LA MACHO “GLAUCOMA”


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (MB)

 

TAMKO LA NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, DKT. FAUSTINE NDUGULILE (MB) KWENYE MAADHIMISHO YA WIKI YA KUONGEZA UELEWA KUHUSU UGONJWA WA SHINIKIZO LA MACHO “GLAUCOMA”

TAREHE 10-16 MARCH 2019
Ndugu wananchi,
Maadhimisho ya wiki ya elimu juu ya ugonjwa wa Shinikizo la Macho huadhimishwa duniani kote ikiwa ni Mpango ulioanzishwa na Chama cha Wagonjwa wa Shinikizo la Macho na Chama cha Wataalamu wa Afya wa Shinikizo la Macho kwa lengo kuu la kuongeza uelewa na kujenga ufahamu wa wananchi juu ya ugonjwa huu hatari wa Shinikizo la Macho, ujulikanao kwa kitaalam “Glaucoma” au Presha ya Macho, katika azma nzima ya kuzuia ulemavu wa kutokuona.  Tanzania, inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha wiki hii muhimu kwa Afya ya Macho.
Maadhimisho haya yaliyoungwa mkono na wadau wa Afya ya Macho duniani, kwa mwaka huu, yanafanyika wiki ya tarehe 11 mpaka 17 mwezi wa Machi.
Ndugu wananchi,
Asilimia 2.8 ya watu wote wenye upungufu wa kutokuona vizuri, sawa na watu milioni 7 duniani wana Ugonjwa wa Shinikizo la Macho, kati yao, milioni 4.5 hawaoni kabisa.
Shinikizo la Macho ni kati ya vyanzo vinayoongoza kwa idadi ya watu wasioona duniani. Kwa Afrika, ugonjwa wa Shinikizo la Macho unachangia asilimia 15 ya watu wasioona. Ugonjwa wa Shinikizo la macho unaathiri zaidi watu wenye umri kuanzia miaka 40. Kwa Tanzania, inakadiriwa kuwa asilimia 4.2 ya watu wenye umri zaidi ya miaka 40 wana ugonjwa huu, sawa na watu 440,000. Kwa bahati mbaya, 70-90% ya watu wenye ugonjwa huu hawajijui iwapo wanao ugonjwa huu. Hii inatokana na watu kutokuwa na tabia ya kuchunguzwa Afya ya Macho kama inavyoshauriwa na wataalamu. Kwa kuwa ugonjwa huu huleta ulemavu wa kutokuona katika umri mdogo, Taifa hupoteza nguvu kazi.
Kwa mwaka 2018, ni watu 18,000 tu waliohudhuria kwenye vituo vyetu vya tiba wakiwa na tatizo la Shinikizo la Macho kulingana na vituo vilivyowasilisha taarifa zao. Idadi hii ni ndogo ikilinganishwa na watu walio kwenye hatari ya kuwa na ugonjwa huu ambao wapo kwenye jamii yetu na hawajagunduliwa.
Ndugu wananchi,
Ugonjwa huu wa Shinikizo la Macho ni moja kati ya kundi la Magonjwa ya Macho yanayoshambuliwa mshipa wa fahamu unaopeleka mawasiliano ya uoni kwenye ubongo (Neva ya Optiki) ili kuweza kutafsiri kile unachokiona. Ugonjwa huu husababisha upofu kwa taratibu sana kwa siku hadi siku bila dalili yoyote katika hatua ya awali na hivyo umepewa jina la Mwizi wa kimya kimya wa uwezo wa Macho kuona. Ili kugungua iwapo mtu ana ugonjwa huu, kuna umuhimu sana wa kupima macho angalau mara moja kila mwaka haswa kwa makundi yaliyo hatarini hata kama mtu haoni tatizo lolote kwenye macho.

Ndugu wananchi,
Maadhimisho ya Wiki ya Shinikizo la Macho kwa mwaka 2019 yamebeba kauli mbiu isemayo:
OKOA UONI WA MACHO YAKO
Sambamba na kauli mbiu hii, ujumbe mahususi kwa jamii na wadau wa huduma za macho na afya kwa ujumla ni:
“TAA YA KIJANI, NENDA KAPIME IWAPO UNA SHINIKIZO LA MACHO!
Kauli mbiu hii inatuhimiza wana jamii kwenda kwenye Vituo vya Tiba kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi iwapo una tatizo la Shinikizo la Macho. Kila mwana jamii anapaswa kupimwa Afya ya Macho yake angalao mara moja kwa mwaka.
Ndugu wananchi,
Aina ya Shinikizo la Macho linalopatikana zaidi kwa Waafrika ikiwemo Tanzania huwa na tabia zifuatazo; haina dalili kama maumivu katika hatua za mwanzo za ugonjwa, huwapata zaidi watu wenye umri wa miaka 40 na kuendelea, huambatana na tatizo la kutokuona mbali (myopia) na kuna uwezekano wa hadi asilimia 20 kuwepo katika familia. Ugonjwa huu husababisha upofu katika muda mfupi kutokana na kuanza kujitokeza katika umri mdogo na wagonjwa huwa na viwango vya juu sana vya presha ya maji ya macho.  Pamoja na kuwa ugonjwa huu mara nyingi hujitokeza kuanzia umri wa miaka 40, watu wengi zaidi hudhurika kadri umri wa kuishi unapokuwa mkubwa.
Ndugu wananchi,
Matibabu ya ugonjwa huu wa Shinikizo la Macho yanapatikana hapa nchini katika vituo vyetu vya tiba vyenye wataalamu wa Macho. Kuna Tiba ya dawa za kushusha Presha ya jicho lakini pia tiba kwa njia ya Upasuaji kwa wale ambao tiba ya dawa haitashusha presha kufikia kiwango cha presha kilicho salama. Iwapo Ugonjwa wa Shinikizo la Macho utagundulika mapema kabla ya mtu amepoteza uwezo wa kuona, tiba ya mapema itawezesha kuzuia hali ya upofu kwa asilimia kubwa.
Ndugu wananchi,
Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea kuboresha miundombinu pamoja na kuongeza wataalamu wa afya ya macho, Vifaa na Vifaa Tiba ili kusogeza huduma za uchunguzi na Tiba kwa Matatizo ya Macho ikiwemo Shinikizo la Macho karibu zaidi na wananchi. Aidha, kwa kupitia Mwongozo wa Tiba na Orodha ya Dawa Muhimu, Serikali itasimamia na kuhakikisha hali ya upatikanaji wa Dawa za Macho katika vituo vyetu vya tiba inazidi kuimarika.

Ndugu wananchi,
Kama sehemu ya Maadhimisho ya Juma hili, kutakuwa na shughuli za Elimu ya Afya ya Macho pamoja na upimaji wa Afya ya Macho kwenye hospitali mbalimbali hapa nchini kwa wiki nzima ya kuanzia tarehe 10 hadi 16 Machi kwa wale wote watakaojitokeza kwenye kliniki za macho. Iwapo wewe au mmoja kwenye familia yako ana umri wa miaka 40 na kuendelea au kuna ndugu mwenye tatizo hili, mnahimizwa kufika katika hospitali iliyo karibu na wewe ili uweze kupimwa presha ya macho na vipimo vingine vya kuchunguza hali ya mshipa fahamu wa ndani ya jicho.  Aidha, pamoja na elimu kwa wagonjwa wote watakaojitokeza kwenye kliniki za macho, elimu kuhusu Shinikizo la Macho itaendelea kutolewa kupitia vyombo mbalimbali vya kuelimisha jamii.

Ndugu wananchi,
Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa kila mmoja wetu kutumua Maadhimisho haya kwa kupima Macho. Ikumbukwe uwezo wa kuona uliopotea kutokana na Shinikizo la Macho hauwezi kurejeshwa tena hata baada ya tiba. Lengo kuu la matibabu ni kuzuia uharibifu usiendelee kutokea kwa kupunguza presha ya macho tu. Hivyo kupima mapema ni bora zaidi kuliko kusubiri ugundulike wakati madhara ya ugonjwa yameshajitokeza. Endapo utashindwa kupima kwa kipindi cha Juma hili la Maadhimisho, unaaswa kufika kwa ajili ya huduma ya upimaji katika hospitali zetu zote hapa nchini mara upatapo fursa hiyo.

“Tushirikiane kutokomeza ulemavu wa kutokuona”


ASANTENI KWA KUNISIKILIZA

1 on: "TAMKO LA NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, DKT. FAUSTINE NDUGULILE (MB) KWENYE MAADHIMISHO YA WIKI YA KUONGEZA UELEWA KUHUSU UGONJWA WA SHINIKIZO LA MACHO “GLAUCOMA”"
  1. In conclusion, you will discover all kinds of payment methods in an internet on line casino. Besides cryptocurrency, on-line casinos also present the choice of using e-wallets. These e-wallets are a better choice 토토사이트 than traditional banking methods as they are much quicker and extra environment friendly. Ignition has operated since 2016 and has grown into a full-blown on-line on line casino with rock-solid model recognition and buyer satisfaction ever since.

    JibuFuta