JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA MHE.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO DKT. FAUSTINE NDUGULILE ZIKISISITIZA
JUU YA WAJIBU WA WATOA HUDUMA ZA AFYA NA MABARAZA YA KITAALUMA PAMOJA NA HAKI
ZA WANANCHI KUPATA HUDUMA BORA ZA AFYA.
Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii kuungana nanyi nyote kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha salama siku hii ya leo tunapoanza mwaka mpya
2018. Hii ni neema pekee ambayo Mwenyezi Mungu
ametujaalia kwani kuna wengi
walitamani kuifikia siku hii lakini hawakubahatika. Hivyo, nawatakieni nyote
kheri na fanaka katika mwaka huu mpya.
Napenda
kutumia fursa hii pia kuwashukuru na kuwapongeza Wanataaluma na Watoa huduma za
afya wote kwa kuendelea kutoa huduma kwa ari, juhudi, uaminifu na uadilifu
licha ya changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika utendaji kazi wa kila
siku. Nami nawatia shime na hamasa ili
muendelee na moyo huo wa kuwahudumia na kuwatumikia Wananchi.
Natambua kuwa Sera
yetu ya Afya inataka tuijenge jamii yenye afya bora na ustawi ambayo itachangia
kikamilifu katika maendeleo ya mtu binafsi pamoja na yale ya Taifa. Aidha, Sera na Sheria zetu mbali mbali
zinatambua umuhimu na nafasi ya Mabaraza ya kitaaluma katika kuboresha na
kusimamia viwango vya maadili ya wanataaluma walio chini ya Wizara yangu. Jambo
hili ni muhimu sana hususan tukizingatia ongezeko la minong’ono, manung’uniko
na hata malalamiko kutoka kwa wananchi dhidi ya baadhi ya watoa huduma ambao wanakiuka taratibu au
miiko ya kazi zao na hivyo kuathiri ubora wa utoaji huduma.
Nimeona
kama sehemu ya salamu zangu za mwaka mpya wa 2018, nitoe maelekezo yatakayoweza
kutusaidia kuboresha utoaji huduma katika sekta ya afya kupitia Watoa Huduma za
Afya na Mabaraza ya Kitaaluma na pia kuwakumbusha wananchi juu ya haki yao ya
msingi ya kupata huduma bora za afya na wajibu wao wa kuhakikisha hilo
linatokea.
i.
Wanataaluma
wa Afya:
Nawakumbusha
Wanataaluma wote katika Sekta ya afya, yaani Madaktari, Wauguzi, Wakunga,
Wafamasia, Wataalam wa Maabara, Madaktari na Wataalam wa Afya ya Kinywa na
Meno, Wataalam wa Mionzi, Wataalam wa viungo bandia na Wafiziotherapia, kwamba taaluma
hizi ni za Kuheshimika sana (Noble), na hivyo kazi na majukumu mnayoyatekeleza
yamejengwa katika misingi ya kuaminiwa (Trust) na Jamii, na
kwamba kuaminiwa huko ndio kiini cha heshima ya taaluma hizi.
Hivyo, ni wajibu wa kila mwanataaluma kutekeleza majukumu yake akiongozwa na
msingi huu mkuu, pamoja na misingi mingine ya kimaadili ambayo ni: HURUMA, UKWELI, FARAGHA, USIRI, UAMINIFU,
USAWA, HAKI, UTU na MAHUSIANO MEMA.
Aidha, naendelea kuwakumbusha kuwa,
utekelezaji wa majukumu yenu siku zote ni lazima uzingatie matakwa ya Katiba ya
Nchi ambayo ndiyo Sheria Mama. Mkumbuke kuwa Dira Kuu katika utekelezaji wa wajibu wenu kama wanataaluma
ni uzingatiaji wa haki, heshima, usawa na utu kwa wote wanaokuja mbele yenu
kupata huduma za kitaaluma. Vile vile mkumbuke kuwa siku zote mnao wajibu wa
kutekeleza majukumu yenu ya kitaaluma kwa kuzingatia Sheria nyingine za
nchi, Kanuni, Sera, pamoja na Miongozo iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria za
Nchi, pamoja na Miongozo na Matamko ya
Kimataifa ambayo tumeridhia kuyatekeleza na kuyazingatia.
Aidha,
nawakumbusha Wanataaluma wote Waandamizi na Viongozi katika Sekta ya Afya
kwamba ni wajibu wao kuhakikisha kuwa Wanataaluma na watoa huduma wote walio
chini yao wanazingatia na kufuata Sheria, Kanuni, Weledi (Professionalism)
pamoja na Maadili (Ethics) ya taaluma au kazi zao na kuchukua hatua stahiki za
nidhamu, kwa mujibu wa Sheria, kunapotokea ukiukwaji. Pia kila Mwanataaluma ana
wajibu wa kuhakikisha kuwa Wanataaluma wanaomzunguka wanatekeleza majukumu yao
kwa misingi hii iliyotajwa na ana wajibu wa kutoa taarifa kwa Mamlaka husika
pindi panapotokea ukiukwaji au kuonekana viashiria vyake. Jambo hili ni muhimu
sana ili kama Wanataaluma msikubali kazi nzuri inayofanywa na wengi iharibiwe
na wakorofi wachache miongoni mwenu.
ii.
Mabaraza
ya Taaluma
Natumia
fursa hii pia kuyakumbusha Mabaraza yote ya Kitaaluma yaliyo chini ya Wizara
yangu kuhakikisha kuwa wanasimamia kikamilifu Sheria zinazosimamia Wanataaluma
wao. Hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa
mtu yeyoye anayetaka kutoa huduma za kitaaluma ni lazima awe na elimu na
ujuzi unaokubalika, na atambulike kwa
kupewa usajili na leseni ya kufanya kazi za kitaaluma. Dhima ya Wizara ni kuona
kuwa jamii inapata huduma zilizo sahihi, salama na zenye ubora unaokubalika.
Hivyo, Mabaraza yana wajibu wa kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayebainika
kukiuka Sheria na taratibu zilizowekwa.
iii.
Wanajamii
Napenda
kuwajulisha wanajamii wote kuwa mnayo haki ya kupata huduma za afya zilizo
salama, bora na ambazo zinazingatia misingi ya usawa, haki na zinazozingatia
heshima na utu wa binadamu. Pia, mnayo
haki ya kupata taarifa sahihi kuhusu hali ya afya au ugonjwa, na kupata ushauri
au tiba kwa wakati na kwa gharama zinazokubalika. Hivyo, wanajamii mnao wajibu
wa kutoa taarifa wakati wowote mnapobaini kuwepo kwa viashiria au vitendo vya
ukiukwaji wa maadili, sheria na taratibu zilizowekwa kwa misingi ya Sheria za
Nchi. Kati ya vitendo visivyo kubalika
ni pamoja na rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, wizi, lugha chafu, matusi,
dharau, mavazi yasiyo na heshima, ulevi, matumizi ya madawa ya kulevya,
uropokaji wa siri za wagonjwa, unyanyasaji wa kijinsia, matumizi mabaya ya simu
za mkononi na tabia nyingine zote zinazofanana na hizi.
Hitimisho na Maagizo,
Nahitimisha
salamu zangu kwa kutoa maagizo yafuatayo:
a) Wanataaluma na Watoa Huduma,
i.
Kila Mwanataaluma na mtoa huduma
anapaswa kuvaa kitambulisho chenye jina lake kamili wakati wote awapo eneo la kazi. Hii ni pamoja
na uvaaji wa sare nadhifu za kazi.
ii.
Viongozi wa kila kituo cha kutolea
huduma za afya wahakikishe kuwa kuna Masanduku ya kutolea maoni yanayoonekana
kwa uwazi na urahisi, na kwamba maoni yanayotolewa yanafanyiwa
kazi ipasavyo.
iii.
Viongozi wa kila kituo cha kutolea
huduma za afya wahakikishe kuwa kuna Ofisi za kuwasilisha malalamiko zilizo
karibu ili kufikiwa na wateja wote wenye uhitaji.
iv.
Viongozi wa vituo vya kutolea
huduma za afya wanapaswa kuweka wazi namba zao rasmi za simu kwenye mbao za
matangazo ambazo mwananchi atazitumia kutoa taarifa au kuwasilisha maoni au
malalamiko.
v.
Mganga Mkuu wa Kituo, Mganga
Mkuu wa Wilaya, Mganga Mkuu wa Mkoa au Kiongozi mwenye mamlaka katika utoaji wa
huduma za afya ana wajibu wa kuwasilisha malalamiko dhidi ya mwanataaluma
anayetuhumiwa katika Baraza la Taaluma husika pindi panapotokea vitendo vya
ukiukwaji wa weledi (Professionalism) na maadili (Ethics).
b) Mabaraza ya Taaluma
Kila Baraza la taaluma pamoja na Wawakilishi wao waliopo katika
Wilaya, Mikoa na ngazi ya Taifa waweke wazi utaratibu wa kisheria wa
uwasilishwaji wa malalamiko na taratibu za Uchunguzi wa vitendo viovu dhidi ya
wanataaluma. Hii ni pamoja na kuweka wazi namba za simu na anuani za barua pepe
(e-mails).
c) Wanajamii kwa ujumla:
i.
Nawasihi Wanajamii kuwaheshimu
na kuwathamini Watoa huduma za Afya nchini
ii.
Nawasihi wanajamii wote kutoa
taarifa, maoni au malalamiko dhidi ya wanataaluma au watoa huduma wanaokiuka
misingi ya Taaluma zao, au wanaotoa huduma kinyume na Taratibu zilizopo kwa:
a. Uongozi
wa kituo husika,
b. Mganga
Mkuu wa Wilaya,
c. Mganga
Mkuu wa Mkoa,
d. Ofisa
wa TAKUKURU,
e. Baraza
la Taaluma Husika,
f. Katibu
Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, au
g. Katibu
Mkuu OR-TAMISEMI, au kwa
h. Kiongozi
yeyote wa Serikali, ili awasilishe taarifa hizo kunakostahili.
Aidha ni vema taarifa itolewe kwa kumtaja
mhusika ili kurahishisha ufuatiliaji.
Nawatakieni nyote Kheri na Afya Njema kwa mwaka mpya wa 2018.
Ahsanteni sana.
Dkt. Faustine Ndugulile (Mb)
NAIBU WAZIRI WIZARA YA AFYA,
MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO