Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumanne, 26 Juni 2018

WAZIRI UMMY ATEMBELEA TAASISI YA SARATANI YA OCEAN ROAD NA KUWATAKA WAKAMILISHE HARAKA UFUNGAJI WA MASHINE MPYA ZA MIONZI ILI KUHAKIKISHA HUDUMA BORA ZAIDI KWA WAGONJWA WA SARATANI NCHINI

- Hakuna maoni
 Mkurugenzi wa taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt Julius Mwaiselage akitoa maelezo kwa Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu juu ya ufanisi wa mashine mpya na yakisasa ya mionzi iliyopo katika taasisi hiyo.

Mtaalamu wa masuala ya mionzi kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt. Hemed Myanza akitoa majibu ya moja ya swali lililoulizwa na Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu pindi alipofanya ziara katika taasisi hiyo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akimsililiza ndugu wa moja kati ya wagonjwa waliofika Hospitalini hapo kupata huduma za matibabu ya Saratani.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisikiliza malalamiko ya mama aliekuwa akisubiri matibabu ya ugonjwa wa kansa katika taasisi hiyo ya Ocean Road. Wa katikati ni Mkurugenzi wa taasisi hiyo Dkt. Julius Mwaiselage.

Mashine ya Kisasa ya Linear Accelerator iliyounganishwa na CT simulator zote mbili zikiwa na gharama ya shilingi Bilion9.5 iliyojumuishwa  na mafunzo ya Wataalamu na matengenezo kinga ya miaka miwili.


WAZIRI UMMY ATEMBELEA TAASISI YA SARATANI YA OCEAN ROAD NA KUWATAKA WAKAMILISHE HARAKA UFUNGAJI WA MASHINE MPYA ZA MIONZI ILI KUHAKIKISHA HUDUMA BORA ZAIDI KWA WAGONJWA WA SARATANI NCHINI

Na WAMJW-Dar Es Salaam.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe.Ummy Mwalimu (Mb), amefanya ziara ya kikazi katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ili kukagua utoaji wa huduma za Matibabu katika Hospitali hiyo. 

Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri alifahamishwa kwamba mashine zote za tiba ya mionzi ya nje inafanya kazi vizuri na huduma zinaendelea kutolewa kwa wagonjwa.

Pia wakati wa ziara hiyo, Mhe.Ummy alitumia fursa hiyo kuzungumza na wagonjwa mbalimbali waliokuwa wakipata huduma za tiba ya mionzi  hospitalini hapo, huku baadhi ya wagonjwa walitoa malalamiko kwa Waziri kuwa, wamekuwa wakitumia muda mrefu kusubiri kupata huduma hususani  huduma za mionzi ya nje. 

Kufuatia hali hiyo, mhe. Ummy alitoa maelekezo kwa uongozi wa Hospitali kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri ambao utapunguza muda kwa wagonjwa kusubiri huduma za mionzi ikiwemo kuwepo na ratiba ambayo kila mgonjwa atajua anafika saa ngapi kupata tiba hiyo.

Vile vile, mhe. Ummy alitembelea  kitengo cha utoaji wa huduma za mionzi ya ndani ambapo alijionea changamoto ya kutokufanya kazi kwa mashine hizo za utoaji wa mionzi ya ndani kutokana na kukosekana kwa vifaa vya 'transfer tubes' na 'gyn applicators'.

Kufuatia hali hiyo mhe.Ummy alitoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Ocean Road, Dkt.Julius Mwaiselage kuhakikisha kuwa mashine hizo zinafanya ndani ya siku 2 kwa kuazima hivyo vifaa hivyo kutoka Hospitali ya Bugando ili kurudisha huduma hizo kwa wagonjwa ambao wengi ni wanawake wenye tatizo la Saratani ya Mlango wa Kizazi.
 "Naelekeza kuwa fanyeni utaratibu wa kupata kifaa kilichoharibika mapema iwezekanavyo" alisema mhe.Ummy.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road , Dkt.Julius Mwaiselage alimhakikishia mhe.Waziri kuwa atajitahidi ili vifaa vilivyoharibika vinapatikana ndani ya siku mbili kutoka Hospitali Bugando na pia wameagiza vifaa hvyo kutoka kiwandani nje ya nchi kwa gharama ya Euro 43,200.00

Jumatatu, 25 Juni 2018

SERIKALI YATOA TAADHARI KWA WANANCHI JUU YA UWEPO WA UGONJWA WA CHIKUNGUNYA NCHINI

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akieleza jambo mbele ya Waandishi wa Habari (Hawapo kwenye picha) wakati akitoa tamko kuhusu ugonjwa wa Chikungunya, Dengue na Ebola katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es salaam. Kushoto kwake ni Katibu mkuu wa Wizara ya Afya Idara Kuu ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya na Kulia ni Mkurugenzi Mkazi kutoka shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Adiele Onyeze.

Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbali mbali wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu kuhusu ugonjwa wa Chikungunya, Dengue na Ebola katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es salaam.


SERIKALI YATOA TAADHARI KWA WANANCHI JUU YA UWEPO WA UGONJWA WA CHIKUNGUNYA NCHINI.
Na WAMJW - DSM
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa tahadhari kwa wananchi juu ya kuingia kwa ugonjwa wa Chikungunya nchini baada ya watu wanne waliotokea  nchini Kenya kubainika kuwa na dalili zinazofanana na ugonjwa  huo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu mapema leo jijini katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es salaam wakati akiongea na waandishi wa Habari.
“Mnamo tarehe 20, Mwezi Juni, 2018 wasafiri wanne wa familia moja waliotokea tena Mombasa nchini Kenya walishukiwa kuwa na ugonjwa huu baada ya kuwa na dalili zinazofanana na ugonjwa wa homa ya Chikungunya kwenye kutuo cha mpakani cha Holili kilichopo wilayani Rombo mkoani Kiliamanjaro”, alisema Mhe. Ummy
Waziri Ummy aliwatoa hofu wananchi kuwa Ugonjwa huu si mpya katika nchi yetu kwani hapa nchini  uligundulika katika maeneo ya Kusini mwa Tanzania, sehemu za Makonde katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji mnamo mwaka 1952 huku  Jina la ugonjwa likiwa na asili ya Kimakonde lenye maana ya “kilichopinda” yaani  hali ya kupinda mwili inayotokana na maumivu makali ya viungo kunakosababishwa na ugonjwa huu.
Kwa upande mwingine Mhe. Ummy alithibitisha juu ya kuwepo kwa ugonjwa wa Dengue nchini hususani katika jiji la Dar es salaam huku idadi ya wagonjwa ambao wamethibishwa kwa kipindi cha Januari hadi Mei ni 226 ambao wanatoka katika mkoa wa Dar es Salaam.
‘Dengue ulithibitishwa kuwepo hapa nchini hususani jijini Dar es Salaam kuanzia mwishoni mwa mwezi wa Januari 2018. Hadi kufikia sasa idadi ya wagonjwa ambao wamethibishwa kuwa na ugonjwa huu kwa kipindi cha Januari hadi Mei ni 226 ambao wanatoka katika mkoa wa Dar es Salaam.  Vilevile ugonjwa huu si mpya hapa nchini kwani umewahi kuripotiwa katika miaka ya 2010, 2013 na 2014” alisema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy ameeleza dalili za ugonjwa wa Dengue zinashabihiana amabazo ni pamoja na homa ya ghafla, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu. Dalili hizi huanza kujitokeza siku ya 3 hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa virusi vya magonjwa haya. Wakati mwingine dalili za magonjwa haya yanaweza kufanana sana na dalili za ugonjwa wa malaria. Vilele mara nyingine magonjwa haya yanaambatana na kutokwa na damu sehemu za fizi, mdomoni, puani, kwenye macho na pia kwenye njia ya haja kubwa au ndogo.
Kwa upande mwingine Waziri Ummy amethibitisha kuwa hadi sasa nchini Tanzania hakuna mgonjwa yoyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya Ebola, huku kwa tathmini ilifanyika na Shirika la Afya Duniani (Regional Risk Assessment) imesema kuwa Tanzania ipo kwenye uwezekano wa kupata ugonjwa wa Ebola na imewekwa katika kundi la pili miongoni mwa nchi 6 zilizo katika hatari ya kupata maambukizi zaidi, kutokana na kupakana na nchi ya DRC pamoja na mwingiliano mkubwa wa watu wake.

Pia Mhe. Waziri amewatoa hofu Wananchi na kuwataka kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huu kwani mpaka sasa hakuna mtu aliyethibitishwa kuugua ugonjwa huu hapa nchini, huku akiwaonya wanaosambaza taarifa za uzushi juu ya uwepo wa ugonjwa huu na kuwataka waache haraka.

Aidha, Wizara itaendelea kushirikiana na Sekta mbalimbali katika kuimarisha ufuatiliaji na kuendelea kutekeleza mikakati ya kudhibiti ili ugonjwa huu usiingie nchini na kuendelea kutoa taarifa pamoja na Elimu kwa Jamii kadri itakavyohitajika.




Jumamosi, 23 Juni 2018

PICHA ZA MATUKIO KATIKA MATEMBEZI YA SIKOSELI KATIKA VIWANJA VYA MWEMBE YANGA.

- Hakuna maoni
Wadau wa sikoseli wakiongozwa na Waziri wa Afya,  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kunyoosha viungo baada yakumaliza matembezi ya Km 3 ambayo yalikomea katika viwanja vya Mwembeyanga.

Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la vyama vya Sikoseli Tanzania Dkt. Deo Soka akimweleza jambo Waziri wa Afya,  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu baada ya matembezi ya siku ya sikoseli katika viwanja vya Mwembeyanga.

Waziri wa Afya,  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wakatikati) akiwa katika matembezi ya siku ya Sikoseli, kushoto kwake ni mwakilishi wa WHO na kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Felix Lyaviva 

Wadau wa sikoseli wakiongozwa na Waziri wa Afya,  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kunyoosha viungo baada yakumaliza matembezi ya Km 3 ambayo yalikomea katika viwanja vya Mwembeyanga.

 Mama mzazi wa Feisal, mtoto mwenye Sikoseli akiongea na Waziri wa Afya,  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo kwenye picha).

Waziri wa Afya,  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisisitiza jambo mbele ya Wananchi waliojitokeza katika viwanja vya Mwembeyanga na Wadau wa Sikoseli wakati wa matembezi ya siku ya Sikoseli ambayo kauli mbiu ni Kuwa mjanja, Ijue Sikoseli.


Ijumaa, 22 Juni 2018

MAGONJWA YASIYO YA KUAMBUKIZA YAONGEZEKA

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia,Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu katikati akikagua vifaa vipya vilivyowekwa kwenye chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Benjami Mkapa wakati wa uzinduzi wa Bodi ya udhamini na chumba cha uchujaji damu Hospitalini hapo leo jijini Dodoma.

Waziri wa Afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia,Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu kushoto akikagua chumba cha kusafishia maji ya wagonjwa wa figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa wakati wa uzinduzi wa Chumba cha uchujaji damu kwa wagonjwa wa figo leo jijini Dodoma, Kulia mwenye koti jeupe ni Daktari Bingwa wa Figo Dkt. Kessy Shija.

Waziri wa Afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia,Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu kushoto akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kulia Dkt. Alponce Chandika  kuhusu kengere za kuitia wauguzi katika wodi ya wagonjwa wa figo wanaochujwa damu kwenye Hospitali hiyo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya udhamini na chumba cha uchujaji damu leo jijini Dodoma.

Waziri wa Afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia,Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu akikata utepe kuashiria kuzindua rasmi miongozo ya Bodi ya udhamini katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyozinduliwa leo jijini Dodoma.

Waziri wa Afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia,Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu akikata utepe kuashiria kuzindua rasmi jengo la kuchuja damu kwa wenye matatizo ya figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma leo.


Waziri wa Afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia,Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu kulia akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya Hospitali ya  Benjamin Mkapa Dkt. Deodatus Mtasiwa kushoto baada ya kuzinduliwa rasmi kwa bodi hiyo leo jijini Dodoma.

Na WAMJW-Dodoma
Magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kama moyo,figo na mengineyo yanaongezeka kwa kasi duniani kote na hapa nchini yamekua yakigharimu Serikali  kiasi cha shilingi Bilioni 36.6 kwa mwaka.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa bodi ya wadhamini ya Hospitali ya Benjamin Mkapa leo Jijini Dodoma.
Waziri Ummy amesema hapa nchini kwa takwimu za Julai 2013 hadi Juni 2016 magonjwa ya Moyo na Figo ndiyo yalikuwa yakiongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa   kutibiwa nje ya nchi na kugharimu  Serikali kiasi hicho cha fedha.
“Kati ya wagonjwa 560 waliosafirishwa na Serikali  wagonjwa 430 walienda kutibiwa moyo na wagonjwa 160 walienda kupandikizwa figo ”alisema Mhe.Ummy.
Aidha, Waziri Ummy alisema kuwa kwa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) magonjwa yasiyoambukiza yanachangia vifo kati ya watu mia moja  watu sitini hufa kwa magonjwa hayo na kati ya wagonjwa 100 watu 47 wanaugua magonjwa yasiyoambukiza
Waziri Ummy aliongeza kuwa kwa kuanzishwa hospitali ya Benjamin Mkapa kutaokoa kiasi kikubwa cha fedha na kuipunguzia Serikali mzigo mkubwa  wa gharama na badala yake fedha hizo zitatumika kuimarisha miundombinu ya hospitali za hapa nchini.
Hata hivyo aliitaka bodi hiyo ya wadhamini kuongeza kasi  ya utekelezaji wa mikakati ya kuboresha huduma za afya ili kuvutia wagonjwa wengi zaidi kutibiwa hospitalini hapo na kupunguza rufaa za wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa matibabu.
“Nawaomba mkachape kazi  bila kuchoka ili hospitali hii ikawe na tija katika kuwahudumia watanzania na hata ndugu zetu wa nchi jirani hasa za  Jumuiya ya Afrika Mashariki katika huduma za matibabu ya Kibingwa”,Alisisitiza Waziri Ummy.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Dkt. Alponce Chandika alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa hospitali hiyo ni kutoa huduma za afya maalum za Kibingwa ikiwemo uchunguzi wa magonjwa ya Moyo,Figo,Macho,Damu, Saratani pamoja na kutoa  huduma za upasuaji kwa kutumia matundu madogo(endoscope).
“Mbali na huduma hizo hospitali yetu inatumika kwa ajili ya kufundisha wataalamu wa kada za afya,kufanya tafiti na huduma za kliniki tembezi” alisema Dkt.Chandika.
Dkt.Chandika alisema kuwa wanatarajia mwezi Agosti kufanya tena upandikizaji  wa figo kwa wagonjwa watatu pia wanatarajia kufanya upasuaji wa matundu madogo kuanzia mwezi Julai mwaka huu
Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt.Deodatus Mtasiwa alisema kuwa Serikali na wananchi wanatarajia huduma nzuri katika hospitali hiyo hivyo hawanabudi kushirikiana na hospitali mbalimbali zinazotoa huduma za Kibingwa ili kutoa huduma stahili hapa nchini.
Sambamba na uzinduzi wa bodi hiyo yenye wajumbe sita Waziri Ummy  alizindua kitengo cha kuchuja damu katika hospitali ya Benjamin Mkapa.


Alhamisi, 21 Juni 2018

SERIKALI ITAENDELEA KUTOA KIPAUMBELE KWA WATAALAM WA AFYA

- Hakuna maoni

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa  wa Tatu kulia akizindua majengo ya Taasisi ya Elimu ya Afya Mvumi yaliyojengwa kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Maralia (Global Fund) uliofanyika leo jijini Dodoma, wa pili kulia ni Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.
 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa  wa nne kulia akikata utepe kuzindua majengo ya Taasisi ya Elimu ya Afya Mvumi yaliyojengwa kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Maralia (Global Fund) uliofanyika leo jijini Dodoma na wanne kutoka kushoto ni Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.
 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kulia akipokea cheti cha umalizaji wa ujenzi wa majengo ya Taasisi ya Elimu ya Afya Mvumi kutoka kwa Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa majengo hayo uliofanyika leo jijini Dodoma.
 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa mwenye suti ya bluu akikagua baadhi ya sehemu za majengo ya Taasisi ya Elimu ya Afya Mvumi baada ya kuzindua majengo hayo yaliyojengwa kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Maralia (Global Fund) yaliyozinduliwa leo jijini Dodoma.
 
 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kulia akipata ufafanuzi wa kina kutoka kwa Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa majengo majengo ya Taasisi ya Elimu ya Afya Mvumi yaliyojengwa kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Maralia (Global Fund) uliofanyika leo jijini Dodoma.
 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa katikati waliokaa akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Taasisi ya Elimu ya Afya Mvumi wakati wa uzinduzi wa majengo ya Taasisi hiyo yaliyojengwa kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Maralia (Global Fund) uliofanyika leo jijini Dodoma, wa tatu kutoka kushoto ni Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.
 
 Baadhi ya viongozi na wananchi  wa Mvumi wilayani Chamwino waliojitokeza kumsikiliza na kushuhudia uzinduzi wa Majengo ya Taasisi ya Elimu ya Afya Mvumi yaliyojengwa kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Maralia (Global Fund) uliofanya na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa leo jijini Dodoma.
 
 
NA WAMJW-DODOMA
SERIKALI itaendelea kutoa kipaumbele kwenye sekta ya  afya hususan swala la kuajiri wataalam wa kada mbalimbali za afya nchini kwa kuzingatia maeneo yenye uhaba mkubwa wa watumishi hasa maeneo ya vijijini.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa kuzindua majengo ya Taasisi ya Elimu ya Afya Mvumi yaliyojengwa kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Maralia (Global Fund) uliofanyika leo jijini Dodoma.
Mhe. Majaliwa aliendelea kusema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kutekeleza Malengo Endelevu ya Milenia hususan lengo nambari tatu linalohusu kuboresha afya za watu pamoja na ustawi wao.
“Miongoni mwa hatua hizo ni kuhakikisha tunashirikiana na wadau wote ili kuongeza idada ya wataalam wa afya nchini kwa kuvijengea uwezo wa kimiundombinu vyuo vya elimu ya afya nchini ili viweze kuongeza udahili na kuzalisha wataalam bora wa afya” alisema Mhe. Majaliwa.
Aidha, Mhe. Majaliwa aliwataka wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza idadi ya watumishi wa afya nchini watakaotekeleza majukumu yao kwa uadilifu na weredi mkubwa kwani Taifa bora linajengwa na wananchi wenye afya bora na afya bora kwa wananchi itapatikana iwapo watahudumiwa ipasavyo.
Mbali na hayo Mhe. Majaliwa alisema kuwa nchi bado inakabiliwa na changamoto  ya magonjwa ya Kifua kikuu na Malaria ,hata hivyo Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya nchini imeongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za ugunduzi wa magonjwa hayo kwa kutumia vipimo vya vina saba (gene -expert).
“Tumefanikiwa kusambaza mashine za “gene expert” 191 kwenye Hospitali zote za Rufaa za Kanda ,Mikoa,Wilaya na baadhi ya vituo vikubwa vya afya ili kuwezeza kupata majibu ya vipimo vya utambuzi wa kifua kikuu ndani ya masaa mawili badala ya kipimo cha hadumini kinachotoa majibu baada ya masaa 24” alisema Mhe. Majaliwa
Aidha , Mhe. Majaliwa amewataka wananchi kujikinga na maambukizi ya Malaria kwa kuzuia mazalia ya mbu kupitia usafi wa mazingira wanayoishi na kutumia vyandarua kwa usahihi ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Kwa uapnde Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto mhe. Ummy Mwalimu  ametoa shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendelea kutoa kipaumbele kikubwa katika masuala ya afya za Watanzania.
“Serikali kupitia Wizara yangu itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta ya afya yenye lengo la kuboresha huduma za afya na  vyuo vya kutolea mafunzo ya kada za afya ili kuimarisha afya za wananchi” alisema waziri Ummy.
Naye Mkurugenzi wa Tume ya Kikristo ya Huduma za jamii Bw. Peter Maduki amesema kuwa mradi wa ukarabati ,upanuzi na ujenzi wa majengo mapya pamoja na vifaa tiba na tahama ulioanza April 2015  katika chuo hicho umegharimu shilingi Bilioni 5.2 ikiwa na malengo ya kuongeza uzalishaji wa wataalam wa afya nchini.



Jumatano, 20 Juni 2018

UMMY MWALIMU AWEKA JIWE LA MSINGI KITUO CHA AFYA MUNDEMU

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kushoto akiweka jiwe la msingi Mradi wa ukarabati na uboreshwaji katika Kituo Cha Afya Mundemu kilichopo Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma leo.kulia ni Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Mzee na Mbunge wa Bahi Bw. Omari Baduel.



Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kushoto akiweka jiwe la msingi Mradi wa ukarabati na uboreshwaji katika Kituo Cha Afya Mundemu kilichopo Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma leo.kulia ni Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Mzee na Mbunge wa Bahi Bw. Omari Baduel.


Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiwasalimia wanakijiji waliojitokeza  wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika kituo cha Afya Mundemu kilichopo wilayani Bahi mkoa wa Dodoma .

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiongea na wanakijiji wa kata ya Mundemu hawapo pichani wakati wa uwekaji jiwe la msingi katika kituo cha Afya Mdemu wilayani Bahi  jijini Dodoma.

Mbunge wa Jimbo la Bahi Bw. Omari Baduel akiongea na wanakijiji wa kata ya Mdemu hawapo pichani wakati wa uwekaji jiwe la msingi katika kituo cha Afya Mundemu wilayani Bahi  jijini Dodoma, kushoto waliokaa ni Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu na anayefuata ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi Bi. Elizabeth Kitundu 


Baadhi ya wanakijiji waliojitokeza kumsikiliza na kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi katika Kituo cha afya Mundemu uliofanywa na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu hayupo pichani wilayani Bahi  jijini Dodoma.

Mafundi wakiwa katika hatua ya mwisho ya kumalizia jengo la Mochwari lilipo katika Kituo cha Afya Mundemu Wilayani Bahi Mkoa Dodoma .

NA WAMJW-DODOMA

WAZIRI wa Afya,maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameweka jiwe la msingi katika Kituo cha Afya Mdemu kilichopo Wilayani Bahi Jijini Dodoma baada ya kuridhishwa na ujenzi huo.
Akizungumza wakati wa kuweka jiwe hilo la msingi Waziri Ummy alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli imefanya kipaumbele maboresho mbalimbali hususan katika sekta ya afya nchini.
“Nilipofika hapa mwaka 2016 niliona wanawake wajawazito wanalala kwa kubanana na wengine wanafariki kwa uzazi pingamizi hivyo nikaona tuanze kujenga vyumba vya upasuaji wa dharura nchini ikiwemo  wodi ya wanawake wajawazito ili kuokoa Maisha ya mwanamke na mtoto anapojifungua ” alisisitiza Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy alisema kuwa mpaka sasa wilaya ya Bahi imefikia asilimia 98 ya wanawake wajawazito kujifungulia katika vituo vya afya amabapo Kitaifa inaonesha katika kila wanawake 100  wanawake  51 ndo hijifungilia kwenye vituo vya afya.
Vilevile Waziri Ummy amesema kuwa Juhudi za Serikali katika kuokoa vifo vya wakina mama wajawazito  Kijijini Mundemu atawapatia gari ya kubebea wagonjwa kwa ajili ya rufaa kutoka kituo kituoni hapo kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Bi. Benadertha Januari amesema kuwa wamefanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 4 mwaka 2015 mpaka vifo 3 mwaka 2017 na vifo vya watoto chini ya miaka 5 kutoka 50 mwaka 2015 mpaka kufikia vifo 12 2017.
Aidha Bi. Januari amesema kuwa wamefanikiwa kukusanya chupa za damu salama 1640 kati ya chupa 2216 ya malengo waliojiwekea ambayo ni sawa na asilimia 74 kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Juni mwaka huu.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Kata ya Mundemu Bw. Reuben Ntiruka amesema kuwa Kituo cha afya Cha Mundemu kinapokea rufaa ya kutoka Zahanati 21 za vijiji vitatu ambayo idadi ya walengwa wake ni wananchi 9103.
Mbali na hayo Bw. Ntiruka ameiomba Serikali kuijengea Kituo hicho Uzio ,nyumba za watumishi, kuongeza idadi ya watumishi  pamoja gari ya kubebea wagonjwa kwani ndio changamoto kubwa zinazoikumba Kituo hicho cha afya.

SALAMU ZA MHE. UMMY. A MWALIMU (MB) KATIKA KAMPENI YA FURAHA YANGU.

- Hakuna maoni
 
SALAMU ZA MHE. UMMY. A MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, KATIKA UZINDUZI WA KITAIFA WA KAMPENI YA KUPIMA VVU NA KUANZA DAWA MAPEMA KWA WENYE MAAMBUKIZI MKOA WA DODOMA, VIWANJA VYA JAMHURI TAREHE 19 JUNI 2018

Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 
Mheshimiwa Suleiman Jafo (Mb) - Waziri wa Nchi - Ofisi ya Rais, TAMISEMI,
Mheshimiwa Jenister Mhagama - Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu,
Waheshimiwa Mawaziri wote mliopo hapa,
Mheshimiwa Dkt. Bilinith Mahenge - Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, 
Mkurugenzi Mkazi wa USAID,
Manaibu Waziri wote mlioko hapa,
Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM - Mkoa wa Dodoma,
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,
Waheshimiwa Wabunge,
Waheshimiwa Mabalozi,
Makatibu Wakuu Wote Mlioko hapa,
Viongozi wa Madhehebu ya Dini,
Dkt. Leonard Maboko - Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, 
Ndugu Justine Mwinuka Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI,
Wadau wa Maendeleo katika Mapambano dhidi ya UKIMWI. 
Viongozi wa Vyama vya siasa,
Waandaaji wa kampeni ya Furaha Yangu,
Wanahabari,
Wageni Waalikwa, 
Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote, Napenda kumshukuru Mungu kwa kuwezesha na kutuweka salama kuifikia siku hii ya leo ambayo ni muhimu sana kwa ajili ya Afya ya watanzania katika uhamasishaji wa kupima VVU na kuanza ARV mapema maarufu kama Furaya Yangu - Pima, Jitambue, Ishi. Zaidi ya yote, napenda kukushukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiwa mgeni rasmi na balozi wa Kampeni hii. 
Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuupongeza kwa dhati, uongozi wa Mkoa wa Dodoma chini ya Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Dkt. Belinith Mahenge kwa kuwa mwenyeji wa uzinduzi huu na kwa ushirikiano mkubwa uliotuonyesha kwa kamati ya maandalizi ya Kitaifa na ile ya Mkoa, pongezi sana.

Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Kampeni hii inawalenga watanzania wote watambue hali zao za maambukizi ya VVU, hususani wanaume na makundi mengine ambayo ni Wasichana walio katika umri wa balehe, Wanawake vijana wenye umri wa miaka 15-24, akinamama wajawazito na wanaonyonyesha pamoja na watoto wao.
Napenda kutoa ufafanuzi kwa nini tunawalenga wanaume zaidi na makundi tajwa hapo juu katika kampeni hii, ni kwa sababu takwimu za utafiti wa Viashia vya VVU na UKIMWI nchini wa mwaka 2016-2017 umeonyesha kuwepo na kiwango cha chini cha upimaji wa VVU kwa wanaume ukilinganisha na wanawake. Katika utafiti huo, inakadiriwa kuwa asilimia 48 ya watu wanaoishi na VVU Tanzania hawajui kuwa wana maambukizi ya VVU. Hali hii ni hatari kwa afya ya watu hao, familia, kaya na Taifa kwa ujumla, kwa kuwa inadhoofisha mapambano dhidi ya UKIMWI nchini na kulifanya Taifa letu kutofikia malengo ya kutokomeza ugonjwa huu hivyo kuendelea kuwa kikwazo katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. 

Mheshimiwa Waziri Mkuu, 
Katika kukabiliana na VVU na UKIMWI, nchi yetu mnamo mwaka 2015 iliridhia malengo ya kidunia ya tisini tatu ifikapo mwaka 2020 ambapo asilimia 90 ya watu wanaoishi na VVU wawe wanajua hali zao za maambukizi ya VVU na asilimia 90 kati yao wawe wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU, na kati yao wanaotumia dawa asilimia 90 Virusi vya ukimwi viwe vimefubaa. 
Tanzania imekuwa kati ya nchi zinazoonyesha mafanikio katika kupambana na maambukizi ya VVU kwa kiwango kikubwa. Tunajivunia kuweza kushusha kiwangocha maambulkizi kutoka asilimia 7 mwaka 2003 kufikia asilimia 4.7 mwaka 2017/2018 (THIS report). Haya ni matokeo mazuri ya miaka 30 ya mapambano dhidi ya ugonjwa huu hatari wa UKIMWI nchini
Hali ilivyo kwa mujibu wa takwimu za Utafiti wa Viashiria vya VVU na UKIMWI THIS 2016/2017 ni kwamba kwa 

Tisini ya Kwanza: waliopimwa na kugundulika na maambukizi ya VVU ni asilimia 52.2 kati ya watu wanaokadiriwa kuwa 1,400, 000 wanaoishi na VVU nchini wenye umri wa miaka 15 - 64 ambao wanajua hali zao za maambukizi ya VVU ambapo Wanawake ni asilimia 55.9 na Wanaume ni asilimia 45.3

Kuhusu Tisini ya Pili: Wanaotumia dawa Kati ya watu wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15 - 64 ambao wanajua hali zao za maambukizi, asilimia 90.9 walitoa taarifa kuwa wanatumia ARV, Wanawake ni asilimia 92.9. na Wanaume ni asilimia 86.1. kwa takwimu hizi inaonyesha tumepiga hatua nzuri na hata kuvuka lengo kwa ujumla wake kitaifa na kwa kundi la wanawake.

Aidha kwa upande wa Tisini ya Tatu: Kushuka kwa kiwango cha VVU mwilini, inaonyesha kuwa kati ya watu wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15 - 64 ambao wametoa taarifa kuwa wanatumia ARV, asilimia 87.7 ya watu hao inaonyesha kiasi cha VVU kimeshuka mwilini. Wanawake ni asilimia 89.2 na Wanaume ni asilimia 84. Natoa wito kwa wanaotumia ARV kuzingatia masharti na kuwa na ufuasi endelevu wa kutumia ARV.

Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Kampeni hii imepewa jina la Furaha yangu - Pima, Jitambue, Ishi kutokana na ukweli kwamba Kampeni hii tofauti na kampeni zilizopita kwani inatoa ujumbe wa furaha kwa wote watakaopima na kujua hali zao za maambikizi. Kwa wale watakaokutwa na VVU sasa wanaanzishiwa matibabu mara moja tofauti na ilivyokuwa zamani walipokuwa wanalazimika kusubiri kuanza dawa mpaka CD4 zishuke au kufikia hatua fulani ya ugonjwa. Kuanza ARV mapema na kuzitumia kama inavyotakiwa, hukata makali ya VVU haraka na kumfanya mtu anayeishi na VVU kuepuka kushuka kwa kinga ya mwili na hivyo kuishi maisha ya kawaida na kupunguza uwezekano wa kuwaambukiza watu wengine. Hivyo basi, kampeni hii inaleta furaha na amani kwa watu hata kama unaishi na VVU. 

Tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na wadau wetu wa maendeleo wakiwemo PEPFAR, Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua kikuu na Malaria na Jumuiya za Umoja wa Mataifa kwa kuwezesha uwepo wa vitendanishi na dawa za kutosha kwa wote wanaohitaji huduma hizi. Wizara yangu imefanikiwa kupima VVU kwa watu milioni 7.4 hadi kufikia Disemba, 2017 ambao ni sawa na ongezeko la watu milioni 2.4 ikilinganishwa na watu waliopima mwaka 2016 ambao ni milioni 5. Aidha, vituo vya kutolea huduma za upimaji wa VVU na ushauri nasaha vimeongezeka kutoka vituo 5,700 mwaka 2015 hadi kufikia vituo 6,005 hadi Machi, 2018. Pia, hadi sasa kuna jumla ya vituo 1,868 vinayotoa huduma za CTC na vituo 4,365 vinavyotoa huduma za PMTCT. Katika kuboresha utoaji wa huduma hizi tunatarajia kuongeza vituo vya kutoa huduma za Tiba na Matunzo (CTC), hadi kufikia jumla ya vituo 4,050 ifikapo mwaka 2018/19.  

Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Napenda kuchukua fursa hii pia kuwataarifu watu wanaoishi na VVU na wanaotumia ARV na watanzania wote kwa ujumla kuwa hivi sasa tumeanza kwa majaribio kutoa ARV kwa wateja wetu kwa miezi mitatu mitatu hasa wale ambao mwenendo wao wa tiba unaridhishwa kwa kuwa kiwango cha VVU mwilini kimeshuka na wanazingatia umezaji wa ARV na mahudhurio kiliniki, Aidha utaratibu huu hautawahusu wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, walio kwenye dawa za mstari wa pili na wale ambao hawatakidhi vigezo vya kitaalamu vilivyoweka.

Mpango huu utasaidia kupunguza muda kwa walengwa kusubiri huduma vituoni hivyo kwaongezea muda wa kufanya shughuli za ujenzi wa taifa letu katika kujenga Tanzania ya Viwanda na kuelekea uchumi wa kati. Aidha nitoe wito kwa wataalamu wetu kufuatilia kwa karibu mwenendo wa huduma za tiba kwa wagonjwa na kuchukua hatua pale inapojitokeza kuna tatizo lolote la kitaalamu au kiafya.

Aidha, 2019 Wizara itaanza kutoa dawa zenye ufanisi zaidi na zenye maudhi kidogo ukilinganisha na hizi za sasa. Hii ni kutokana na tafiti za kisayansi zinazoendelea kufanyika chini ya WHO.

Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Napenda kukutaarifu kuwa Jumla ya mashine 35 zenye uwezo wa kupima Wingi wa Virusi vya UKIMWI (HIV Viral Load) Hospitali za Mikoa 17 na Hospitali za Wilaya 18 na hivi sasa tuna mashine za Genexpert 191 zinazopima wagonjwa wa TB na zina uwezo wa kupima wingi wa Virusi vya UKIMWI ambapo zimesambazwa katika Hospital za Mikoa na Wilaya ili kuboresha huduma ya upimaji wa wingi wa VVU katika vituo vya kutolea huduma za afya. Aidha hadi Mwezi Machi 2018 watu 1, 022,745 walikuwa wameandikishwa katika huduma za tiba na Matunzo, kati ya hao 1,007,026 wanatumia ARV.

Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Maambukizi ya VVU yanaenezwa kwa kiasi kikubwa na ngono zisizo salama. Aidha, watu wanaotumia dawa ya kulevya kwa kujidunga, wanawake wanaofanya biashara ya ngono, wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao, Wasichana wadogo wa umri balehe (miaka 15 -19) ,wasichana wa umri kati ya miaka 20 - 24, vijana wa kiume miaka 15 - 24 ambao ndio nguvu kazi ya taifa letu wako katika hatari zaidi ya maambuzi ya ugonjwa huu. Hivyo nitoe wito wa watanzania kujitambua na kuchukua hatua.  kwa kulitambua hilo Wizara imekuwa ikitoa huduma kwa makundi haya ambayo yapo katika hatari zaidi ya kuambukiza au kuambukizwa VVU. 

Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Pamoja na mkakati wa kupima na kuanza ARV mapema, Wizara yangu, tukishirikiana kwa karibu na TACAIDS, OR TAMISEMI na Wadau wa maendeleo, inaendelea kutekeleza mikakati mingine ikiwemo huduma za tohara kwa wanaume, Elimu ya matumizi sahihi na endelevu ya kondomu, Utoaji wa damu salama, kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na Elimu ya kubadili tabia. 

Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Katika kutekeleza mikakati mbalimbali tunaweza kufanikiwa zaidi iwapo kila mmoja wetu atachukua hatua aidha kwa kutumia huduma za afya, kubadili tabia hatarishi, kuacha unyanyapaa na kuchangia rasilimali fedha pale ambapo Serikali na wadau wameishia. Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wadau ambao baadhi yao ni: 
Serikali ya Marekani kupitia mradi wa PEPFAR,
Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua kikuu na Malaria, 
Shirika la Maendeleo la Marekani USAID kupitia mradi wa Tulonge Afya, 
Shirika la Kimataifa la Kazi Duniani (ILO),
Asasi za Kiraia za mapambano dhidi ya UKIMWI wakiwemo Jhpiego, MDH, TAYOA, WRP, Pharm Access, Benjamin Mkapa Fondation, THPS, 
Viongozi wa Dini na Vyama vya Siasa.

Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Kwa heshima nikuombe ukabidhi vyeti vya shukrani kwa mabalozi wanne wa Kampeni ya Furaha yangu, mabalozi hao ni baadhi ya watu wanaoishi na VVU ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha umma kujua hali zao za maambukizi ya VVU na kuanza dawa za ARV mapema bila uwoga wowote na hivyo kuwa mstari wa mbele katika kutokomeza unyanyapaa. 
(Majina ya watu hao yatatajwa).
FURAHA YANGU - PIMA, JITAMBUE, ISHI
Asanteni kwa kunisikiliza

PICHA ZA MATUKIO MBALI MBALI WAKATI WA UZINDUZI WA KAMPENI YA FURAHA YANGU-DODOMA

- Hakuna maoni
Waziri wa afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiongea na hadhira ya watu (hawapo kwenye picha) waliojitokeza katika kampeni ya Furaha yangu iliyofanyika katika viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma, Kampeni hiyo ilizinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kasim Majaliwa.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa (wa tatu kulia) akiwa ameambatana na viongozi wengine wakikagua mabanda ya watoa huduma za afya wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Kupima VVU na kuanza kutumia dawa mapema inayojulikana kama Furaha Yangu iliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma leo.


Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa (wa pili kushoto) akiwa ameambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe Jenista Mhagama (wa pili kushoto) wakipokea maelezo kutoka kwa mtaaalam wa Afya wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Kupima VVU na kuanza kutumia dawa mapema inayojulikana kama Furaha Yangu iliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma leo. 
 
Wakazi mbalimbali wa maeneo ya Dodoma wakiingia katika baadhi ya mabanda kupata huduma za kupima VVU pamoja na kupata ushauri nasaha katika viwanja vya Jamhuri kwenye uzinduzi wa kampeni ya Furaha yangu leo Mjini Dodoma.

Kundi la wanafunzi waliojitokeza kupata  huduma  za kupima VVU pamoja na ushauri nasaha katika viwanja vya Jamhuri kwenye uzinduzi wa kampeni ya Furaha yangu leo Mjini Dodoma.

Wakazi mbalimbali wa maeneo ya Dodoma waliojitokeza kwenye viwanja vya Jamhuri kushuhudia uzinduzi na  kupata  huduma  za kupima VVU pamoja na ushauri nasaha katika viwanja vya Jamhuri kwenye uzinduzi wa kampeni ya Furaha yangu leo Mjini Dodoma.

Waziri wa afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu kushoto akijadili jambo pamoja na Waziri wa TAMISEMI Mhe. Suleiman Jaffo  katika viwanja vya Jamhuri kwenye uzinduzi wa kampeni ya Furaha yangu leo Mjini Dodoma.
 
Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kasim Majaliwa wakati akikata utepe ikiwa ni ishara ya ufunguzi rasmi wa kampeni ya Furaha yangu aliyoifungua katika viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma.