SERIKALI kupitia Wizara ya afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee
na Watoto imerahisisha ukusanyaji wa takwimu za vifo vinavyotokea kwenye ngazi
ya jamii nchini kwa kugawa vifaa maalumu vya kukusanyia takwimu hizo kwa
Maafisa afya katika kata za mkoa wa Iringa.
Hayo yamezungumzwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendelo ya
jamii,Jinsia,Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Afya) Dkt. Mpoki Ulisubisya
wakati akikabidhi Kompyuta Kibao ( Tablets) zanye mfumo maalum wa kukusanyia
takwimu hizo kwa Maafisa Afya leo Mkoani Iringa.
“Takwimu zitakazokusanywa kuhusu vifo na Maafisa hawa wa
afya kutokana na Mifumo hii zitawasaidia madaktari kujadili changamoto
pamoja na sababu za vifo hivyo ili kupata ufumbuzi wa matatizo hayo na kuweza
kupunguza idadi ya vifo nchini” alisema Dkt. Ulisubisya.
Aidha,Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema kuwa takwimu hizo
zikikusanywa kikamilifu zitasaidia kutoa elimu kwa jamii na kupunguza imani za
kishirikina kwa wananchi kwani zitaleta picha sahihi ya kugundua vyanzo
vya vifo hivyo kwenye jamii husika.
Hata hivyo Dkt. Ulisubisya amewataka maafisa hao kutumia
vifaa hivyo kwa matumizi ya kazi ya kukusanyia takwimu na sio matumizi binafsi
na kama itatokea afisa afya yeyote atakayehama kituo cha kazi basi
arudishe ofisini kwa ajili ya mtumishi mwingine atakayekuja.
Kawa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa iringa Bw. Fikira
Kissimba amesema kuwa mfumo huo wa ukusanyaji taarifa zitasaidia pia
uandikishwaji wa mirathi ya marehemu wakati ndugu husika anapokwenda kufungua
mirathi yake mahakamani.
Naye Mratibu wa usajili wa Takwimu wa Masuala muhimu ya Binadamu
nchini kutoka wizara ya afya Dkt.
Gregory Kabadi amesema kuwa jumla ya Kompyuta kibao (Tablets) zilizogawiwa ni
106 kwa kila kata ya mkoani Iringa na thamani yake ni takribani shilingi
Milioni 61.5.
Aidha , Dkt Kabadi amesema kuwa zoezi hilo limeanza kwa
majaribio katika halmashauri tano kwenye mikoa mitatu ikiwemo Pwani,Tanga na
Morogoro na kufanya tathimini ya utekelezaji wa mifumo hiyo katika mkoa wa
Iringa kabla ya kutumika nchi nzima.
Kwa upande wake Afisa afya wa kata ya Kitwilu Bw. Wilson
Ntagondwa amesema kuwa kupitia mfumo huo waliokabidhiwa itawasaidia kukusanya
takwimu kwa urahisi hivyo kupelekea kujua sababu zinazosababisha vifo na
kusaidia kupanga maendeleo.