Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole
Sendeka kitabu cha muongozo wa utoaji huduma kwa wauguzi na wakunga nchini
wakati wa uzinduzi wa Mkakati wa wauguzi na wakunga kusogeza huduma za VVU
na UKIMWI karibu na jamii uliofanyika Kitaifa
Mkoani Njombe
NA WAMJW-NJOMBE
Serikali kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya
Jamii,Jinsia, Wazee na watoto imewataka watoa huduma za afya nchini
kutokuwasahau watoto na vijana katika
kuwakinga na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa uzinduzi wa
Mkakati wa wauguzi na wakunga kusogeza
huduma za VVU na UKIMWI karibu na jamii ikiwemo ushauri nasaha, kupima VVU na
kufuatilia maendeleo ya afya za walengwa uliofanyika mapema leo mkoani Njombe.
“Bado tuna changamoto kwa watoa huduma wetu wa
afya kwa baadhi ya maeneo ikiwemo kutokuwapima watoto hali ya maambukizi, kutoa dawa kwa watoto na
kuwapa elimu vijana hivyo natoa rai kwa wahudumu wa afya tuweze kuweka mkakati
wa kufikia makundi hayo” alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha Dkt. Ndugulile amewasisitiza Wauguzi na
Wakunga kutoa huduma kwa kuzingatia miiko na maadili hususan katika kutoa
huduma za VVU kwa jamii inayowazunguka ikiwemo kutumia lugha nzuri na kuwa
wanyenyekevu kwa wananchi.
Sambamba na hilo Dkt. Ndugulile amewaasa wanaume
nchini kuacha uoga na kujitokeza kupima VVU ili kutambua afya zao na kuanza
matibabu mara moja iwapo watakutwa na maambukizi.
“Tutawafuata wanaume popote walipo hususan waliopo
kwenye mikusanyiko yao ikiwemo kwenye
sehemu za starehe, viwanja vya mipira , Migodini na sehemu za uvuvi ili kutoa
elimu na kuwashauri wapime ili kujua afya zao” alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha Dkt. Ndugulile amesema kusudio la kufanya
hivyo ni kuhakikisha kufikia malengo ya 90 90 90 ya kutokuwa na maambukizi
mapya ifikapo mwaka 2030. Ambapo asilimia 90 ya watu wanaoishi na virusi vya
Ukimwi wawe wanajua hali zao za maambukizi.
Ili kutimiza malengo ya serikali katika kupambana
na maambukizi, Dkt Ndugulile amesema Serikali imekuja na utaratibu wa dawa
kinga ambapo dawa hizo zitatumika kwa makundi maalumu ambayo yako hatarini
kupata maambukizi.
“Lakini vile vile tumekuja na utaratibu unaoitwa
dawa-kinga ambazo kuna makundi ambayo tumebaini, ambayo yako kwenye hatari
kubwa ya kupata maambukizi ya UKIMWI. Makundi haya kuna dawa ambayo tunataka
tuwape zisaidiane na kinga nyingine ili kusaidia watu wasipate maambukizi ya
virusi vya UKIMWI lakini hatusemi kwamba tumeshapata kinga”. Dkt Ndugulile.
Sambamba na hayo Dkt. Ndugulile amewataka watoa
huduma waende wakatoe msisitizo na kuelimisha jamii katika maeneo ambayo
dawa-kinga zimeanza kufanyiwa majaribio ili kuleta matokeo chanya.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher
Ole Sendeka amesema ukanda wa nyanda za juu kusini ni ukanda ambao una
maambukizi makubwa ya VVU na serikali ya mkoa ilianza kampeni ya tohara kwa
wanaume, na sasa inaelekea kwa watoto wa sekondari na shule ya msingi ikiwa ni
njia mojawapo ya kupambana na maambukizi mapya.
“Takwimu zinaonesha sisi tuna kiwango kikubwa cha
maambukizi kuliko katika ukanda ule ambao tohara kwa wanaume inaanzia katika
umri mdogo kiwango cha maambukizi kiko chini lakini pia kuna mahusiano kati aya
tohara ya wanaume na maambukizi ya VVU kwahiyo kama mkoa kampeni hii tumeivalia
njuga chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na
TAMISEMI”. Alisema Ole Sendeka.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Waganga Wakuu wa
mikoa na Wafawidhi wa mikoa mbalimbali pamoja na wauguzi na wakunga waliopata
muongozo wa kusogeza huduma za VVU na UKIMWI karibu na jamii ikiwemo ushauri
nasaha, kupima VVU na kufuatilia maendeleo ya afya za walengwa.
|
0 on: "WATOA HUDUMA ZA AFYA WATAKIWA KUTOWASAHAU WATOTO KATIKA KUWAKINGA NA MAAMBUKIZI YA VVU."