Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (katikati) akitoa maelekezo kwa Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Rajabu Risasi (kushoto) wakati alipotembelea Hospitali ya Mahenge iliyopo wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro. Kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo Ngollo Malenya.
NA WAMJW-ULANGA
Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amewaasa watumishi wa afya nchini kote
kuzingatia maadili katika utendaji ili kutoa huduma za afya kwa wananchi kwa
kiwango kilicho bora.
Dkt. Ndugulile amesema hayo wakati alipofanya
ziara na kukagua hali ya utoaji wa huduma za afya katika Hospitali ya Mahenge
iliyopo wilaya ya Luanga mkoani Morogoro.
Katika ziara hiyo, Dkt. Ndugulile alionekana
kushangazwa na baadhi ya watoa huduma hospitalini hapo kutozingatia muda wa
kuwepo kazini muda wote.
Amebaini hilo wakati alipotembelea maabara ya
Hospitali na kukuta kumbukumbu za mnyororo wa baridi hazijaandikwa ipasavyo,
damu na vitendanishi vikiwekwa katika Friji moja na mpangilio mzima wa maabara
hiyo kuwa mbovu.
“Niwakumbushe wataalamu wa maabara, taaluma ambazo
wamezisoma hazibadiliki hata wakiwa kazini, kuna misingi ya taaluma ambayo
tunayo, vitu vidogo kama Temperature Chart vinaonesha umakini na weledi kwa
mwana taaluma ambaye tumemkabidhi jukumu lile”. Amesema Dkt. Ndugulile.
Kutokana na hali hiyo, Dkt. Ndugulile aliagiza
kuondolewa msimamizi wa maabara Donald Masamaki na kuletwa mtu mwingine
atakayezingatia taaluma na weledi katika utoaji wa huduma za maabara na afya
kwa ujumla.
Aidha, Dkt. Ndugulile alishangazwa na malalamiko
ya wananchi kuhusu wahudumu wa maabara kuwaagiza wagonjwa kwenda kupima Malaria
katika vituo vya watu binafsi huku kipimo cha MRDT kikiwepo stoo ya dawa.
Kufuatia hali hiyo Naibu Waziri huyo aliagiza Kamat ya Ulinzi na Usalama ya
Wilaya pamoja na Mkuu wa Wilaya hiyo Ngollo Malenya kufuatilia kwa ukaribu na
kubaini ukweli wa jambo hilo na wale watakaobainika wachukuliwe hatua.
“Niwakumbushe watu wa maabara, nimkumbushe mganga
mfawidhi kuhakikisha kwamba vipimo vyote vinakuwepo Hospitali. Nimepata
malalamiko kutoka kwa wananchi, mpaka vipimo vya MRDT vya Malaria watu
wanaambiwa wakapime nje”. Ameongeza Dkt. Ndugulile.
Pamoja na hayo, Naibu Waziri aliagiza kufanyiwa
marekebisho kwa baadhi ya kasoro zilizoonekana Hospitalini hapo ikiwa ni pamoja
na kuagiza kununuliwa mafaili ya kutunzia kumbukumbu za mgonjwa, kujengwa kwa
sehemu ya kuchomea taka, kurekebisha mfumo wa mapato na kuiagiza bohari ya dawa
(MSD) kuhakikisha dawa zote muhimu zinapatikana Hospitalini hapo.
Katika kuhitimisha ziara yake wilayani Ulanga,
Dkt. Ndugulile aliahidi kuipatia Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga gari la
wagonjwa (Ambulance) katika mgao unaofuata.
Naibu Waziri Dkt. Ndugulile alihitimisha ziara
yake mkoani Morogoro kwa kutembelea kituo cha afya cha Lupiro na kukagua ujenzi
wa majengo mapya ya chumba cha kuhifadhia maiti, wodi ya wanawake, maabara na
nyumba ya daktari. Huku kwa kiasi kikubwa akionekana kuridhika na ujenzi wa
kituo hicho.
|
0 on: "DKT. NDUGULILE AAGIZA WATUMISHI WA AFYA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA KATIKA UTENDAJI WAO."