Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Christina Mndeme (aliyesimama) akisema jambo katika Semina ya uraghibishaji na uhamasishaji wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele iliyojumuisha Wakuu wa Wilaya pamoja wataalam mbalimbali toka Mamlaka za Serikali za Mitaa za Mkoa wa Ruvuma (hawapo pichani)
Kaimu Meneja wa Mpango wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbe Kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bwana Oscar Kaitaba (aliyesimama) akiongea na washiriki wa Semina ya uraghibishaji na uhamasishaji wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele iliyojumuisha Wakuu wa Wilaya pamoja wataalam mbalimbali toka Mamlaka za Serikali za Mitaa za Mkoa wa Ruvuma (hawapo pichani)
Mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Mkoa wa Ruvuma Dkt. Charles Hinju (aliyesimama) akitoa mada katika Semina ya Uraghibishaji na uhamasishaji wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kwa Viongozi wa Wilaya na Wataalam toka Mamlaka za Serikali za Mitaa Mkoa wa Ruvuma.
Viongozi pamoja na wataalam toka Mamlaka za Serikali za Mitaa Mkoa wa Ruvuma wakisikiliza mada katika Semina ya Uraghibishaji na uhamasishaji wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele iliyofanyika katika Ukumbi wa Mipango Mkoani Ruvuma.
Na WAMJW - RUVUMA
Pamoja na juhudi zinazofanywa na
Serikali na wadau mbalimbali katika kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi
kipaumbele, mwamko wa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kutumia kingatiba bado upo
chini hivyo kukwamisha malengo yaliyokusudiwa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa
Ruvuma Bi. Christina Mndeme alipokuwa akifungua semina ya uraghibishaji na
uhamasishaji wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kwa Wakuu wa
Wilaya pamoja na wataalam wa Mamlaka za Serikali za Mitaa za Mkoa wa Ruvuma
iliyofanyika katika ukumbi wa mipango Oktoba 13, 2018.
Mkuu huyo wa Mkoa aliyataja
magonjwa ambayo bado yanaendelea kusumbua wananchi mkoani humo kuwa ni; Usubi,
Minyoo ya tumbo pamoja na kichocho huku akiwapongeza wataalam kwa kufanikiwa
kwa kiasi kikubwa kudhibiti magonjwa ya Vikope (trakoma), Matende pamoja na
Mabusha.
Bi. Mndeme amesema kuwa sehemu
kubwa ya jamii bado haijahamasika kumeza dawa kutokana na uelewa mdogo wa
athari za magonjwa hayo huku wananchi wengi bado wakiwa na imani potofu juu ya
dawa hizo.
“Magonjwa haya yamekuwa yakiathiri
rika zote katika jamii, tumeona Watoto wakishindwa kwenda shuleni na
kusababisha taaluma kushuka huku kwa watu wazima wakipata ulemavu wa kudumu
hivyo kushusha nguvu kazi ya Taifa” alisema Bi Mndeme.
Naye Meneja wa Mpango wa Kudhibiti
Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bwana Oscar Kaitaba, amesema kuwa lengo la
Serikali ni kuhakikisha kuwa magonjwa hayo yanadhibitiwa kikamilifu hivyo
kuwaomba wataalam walioshiriki semina hiyo kusaidia Serikali katika kuelimisha
na kuhamasiha jamii kutumia kingatiba ili kudhibiti magonjwa hayo.
“Njia bora ya kudhibiti magonjwa
haya ni kuhakikisha wananchi katika maeneo tunayotoka wanakunywa dawa zinazopatikana
katika hospitali zetu” Alisema Bwana Kaitaba.
Kwa upande wake Mratibu magonjwa
yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Mkoa wa Ruvuma Dkt. Charles Hinju amesema
shughuli ya kuhamasisha wananchi kumeza kingatiba bado inaendelea kutolewa licha
ya changamoto wanazokutana nazo.
“Kwa mwaka 2016 jumla ya watu 1,052,907 kati ya 1,420,317 walipata kingatiba sawa na asilimia 74 huku
kwa mwaka 2017 watu 1,192,390 kati ya 1,413,751
walipata kingatiba sawa na asilimia 84.3” alisema DKt. Hinju.
Dkt. Hinju amezitaja changamoto za
kuchelewa kwa dawa na rasilimali fedha kuwa zinaathiri ufanisi wa kazi huku pia
Halmashauri nyingi hazitengi fedha ili kufanikisha kazi ya kukabiliana na
magonjwa hayo.
Akifunga semina hiyo, Mkuu wa Mkoa
wa Ruvuma Bi. Christina Mndeme ameishukuru Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto kwa kuandaa Mpango huo wa kudhibiti magonjwa hayo na
kuishauri Wizara kuandaa vipindi maalum kwenye vyombo vya habari ili kuhamasisha
jamii kumeza dawa za kutibu magonjwa hayo huku akiwataka wataalam katika maeneo
wanayotoka kuelimisha jamii kuachana na imani potofu juu ya dawa hizo.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amewataka
Waganga Wakuu wa Wilaya kuwa na takwimu sahihi za idadi ya watu wanaofika
katika vituo vya afya na hospitali ili kusaidia katika maombi ya dawa toka
bohari kuu ya dawa.
MWISHO
0 on: "UMEZAJI DAWA NDIYO SULUHISHO KAMILI KATIKA KUDHIBITI MAGONJWA YALIYOKUWA HAYAPEWI KIPAUMBELE."