Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu (MB) akisisitiza jambo mbele ya
waandishi wa Habari wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wauguzi na Wakunga katika
Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar Es Salaam.
Watumishi wa Baraza la Uuguzi
na Ukunga pamoja na Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu (Hayupo kwenye Picha) wakati
wa uzinduzi wa Baraza la Wauguzi na Wakunga.
Afisa Uuguzi wa Baraza la Uuguzi
na Ukunga Tanzania Jane Mazigo akitoa maelezo mbele ya Mgeni rasmi Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu (MB) wakati
wa uzinduzi wa Baraza la Wauguzi na Wakunga.
Mwenyekiti wa Baraza la
Uuguzi na Ukunga aliyemaliza muda wake Stuart Mbelwa akipokea Cheti kutoka kwa
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu
wakati wa uzinduzi wa Baraza la Uuguzi na Wakunga, Kulia ni Msajili wa Baraza
la Uuguzi na Ukunga Tanzania Lena Mfalila
Mwenyekiti aliyeingia
kuliongoza Baraza la Uuguzi na Ukunga Abner Mathube akiahidi kuchapa kazi mbele
ya mgeni rasmi ambae ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Mh. Ummy Mwalimu (MB) wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wauguzi na
Wakunga.
Picha ya Pamoja ikiongozwa na
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu
wakati akizindua Baraza la Uuguzi na Ukunga katika Ofisi ndogo za Wizara jijini
Dar Es Salaam.
Na WAMJWW.DSM.
Serikali kupitia Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeahidi kuendelea kutatua
changamoto za zinazowakabili watumishi wa Kada ya Afya nchini ikiwemo kuboresha
miundombinu inayowazunguka.
Hayo yamesemwa na Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu (MB) mapema
leo wakati akizindua Baraza la Wauguzi na Wakunga katika Ofisi ndogo za Wizara
jijini Dar Es Salaam.
“Asilimia 80% ya Kazi zote za
kutoa huduma za Afya, zinafanywa na Wauguzi na Wakunga, kwaiyo wakati
tunazungumzia kuboresha huduma za, Serikali ya awamu ya tano itaendelea
kuzifanyika kazi changamoto hizo ikiwemo suala la watumishi” alisema Mh. Ummy
Mwalimu.
Mh. Ummy aliendelea kusema
kwamba, sambamba na changamoto Wauguzi na Wakunga wanazoendelea kukumbana nazo
Serikali itaendelea kutimiza wajibu wake wa kutatua changamoto hizo katika
kuboresha Huduma za Afya.
Kwa upande mwingine Mh. Ummy
alimwagiza Mwenyekiti mpya wa Baraza hilo Bw. Abner Mathube Kusimamia
mabadiliko ya kanuni za maadili ya Baraza hilo ambazo zimeonekana kupitwa na
wakati, hivyo kutofanya kazi kwa ufanisi unaostahili na kushindwa kuendana na
wakati huu.
“Nimeelekeza zile kanuni za
maadili za mwaka 2007 ni lazima zifanyiwe marekebisho, kwani zimepitwa na wakati, ili tuweze kusimamia
taaluma hii vizuri ya Uuguzi na Ukunga.” Alisema Mh. Ummy Mwalimu.
Pia Mh. Ummy Mwalimu
amelitaka Baraza hilo kujizatiti katika kutoa taarifa za Baraza mbele ya umma
katika kueleza shughuli za kila mara za Baraza hilo, jambo litakalosaidia
kuwafahamisha wananchi juu ya majukumu ya baraza hilo.
“Jamii haipati taarifa kuhusu
utendaji kazi wa Baraza, tunatakiwa kuliona Baraza linakuja mbele, angalau kila
robo mwaka katika kila kipindi, kukaa kimya kunafanya wananchi waone Baraza
halina meno wala maamuzi” Alisema Mh. Ummy Mwalimu.
Kwa upande mwingine Mh. Ummy
amelitaka Baraza hilo kuwachukulia hatua Waauguzi na Wakunga wanaenda kinyume
na maadili ya kazi yao, huku akikemea matumizi ya lugha chafu yanayofanywa na
baadhi ya wauguzi wachache ambao kwa kiasi kikubwa wanaitia doa kada hiyo.
Aidha, Mh. Ummy amemshukuru
mwenyekiti aliyemaliza muda wake Stuart Mbelwa kwa kazi nzuri aliyoifanya ya
kuliongoza Baraza hilo ikiwemo kusimamia wauguzi na wakunga nchini, kusimamia
vyuo na vituo vya kutolea huduma za Afya na kuweza kukamilisha jengo la
kuwaendeleza Wauguzi na Wakunga, huku akiwataka waamishe kazi zote za Baraza
hilo katika jengo hilo lililopo Kibaha.
Mwisho Waziri Ummy aliahidi
kuvifungia au kuvishusha hadhi Vituo vya Afya ambavyo havitakidhi vigezo vya
kutoa huduma kwa jamii, huku akiwataka Wakurugenzi kujenga tabia ya
kuvitembelea vituo hivyo ili kujionea mahitaji ya Vituo hivyo.
“Tutafungia au kuvishusha
hadhi Vituo vya Afya ambavyo havikidhi vigezo, kwa hili hatutooneana aibu, wala
kujali hiki ni kituo cha Afya cha serikali au chabinafsi, wakishindwa kutoa
Huduma Bora hatutasita kuvifungia” alimaliza Mh. Ummy Mwalimu.