Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa Habari (Hawapo kwenye pich) pindi akitoa taarifa ya siku ya Ukoma Duniani, tukio lililofanyika mapema leo katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es salaam.
Waandishi wa Habari wakifuatilia taarifa kutoka kwa Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile(Hayupo kwenye picha) katika siku ya Ukoma Duniani, tukio lililofanyika mapema
leo katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es salaam.
TAMKO LILILOSOMWA NA NAIBU WAZIRI WA
AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. DKT. FAUSTINE
NDUGULILE (MB) KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA UKOMA DUNIANI TAREHE
28/01/2018
Ndugu wanahabari,
Siku
ya Ukoma Duniani huadhimishwa ulimwenguni kote kila Jumapili ya mwisho
ya mwezi Januari. Kwa mwaka huu, siku hii itaadhimishwa tarehe 28
Januari, 2018. Mwaka huu imetimia miaka 64 tangu siku hii ilipoasisiwa
mnamo mwaka 1954 na mwandishi wa habari mfaransa Raoul Follereau kama
njia ya kuelimisha na kuongeza uelewa duniani kuhusu ugonjwa huu wa kale
ambao una kinga, unatibika na mgonjwa kupona kabisa.
Ndugu wanahabari,
Katika
siku hii, Tanzania inaungana na mataifa mengine ulimwenguni kufanya
maadhimisho hayo ili kuukumbusha umma na kuuelimisha juu ya uwepo wa
ugonjwa huu hatari, athari mbaya za vidonda na ulemavu vinavyotokana na
ukoma. Ni dhahiri kuwa ugonjwa wa ukoma umekuwa ukiogopwa sana na
kusababisha unyanyapaa mkubwa katika jamii zetu hasa kutokana na ukweli
kwamba unasababisha ulemavu wa kudumu na kwa kiasi kikubwa waathirika
hujikuta wakitengwa na kubaguliwa.
Pamoja
na kwamba nchi yetu ilifikia viwango vya utokomezaji wa Ukoma kitaifa
mnamo mwaka 2006 kwa kiwango cha chini ya mgonjwa 1 kati ya watu 10,000,
Ukoma bado unaendelea kuwa tatizo la kiafya miongoni mwa jamii nchini
kwetu. Kwa mujibu wa takwimu za Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua kikuu
na Ukoma za mwaka 2016, jumla ya wagonjwa wapya 2,047 waligunduliwa na
hivyo kufanya kiwango cha ugunduzi kuwa watu 4 kwa kila watu 100,000.
Takwimu hizi zinaifanya Tanzania kuendelea kuwa miongoni mwa nchi 22
zenye wagonjwa wengi wa ukoma duniani.
Takribani
mikoa yote nchini mwetu inagundua na kutibu wagonjwa wa ukoma japo kwa
viwango tofauti. Hivi sasa bado kuna mikoa kumi ambayo inagundua
wagonjwa wapya kila mwaka. Mikoa hiyo ni pamoja na: Lindi, Rukwa,
Mtwara, Morogoro, Pwani; Tanga, Geita, Dodoma, Tabora and Kigoma.
Aidha,
bado zipo wilaya 20 ambazo kiwango cha ukubwa wa tatizo la ukoma kipo
juu sana na bado hazijafikia lengo la utokomezaji, nazo ni Liwale,
Nkasi, Ruangwa, Nanyumbu, Shinyanga manispaa, Kilombero, Mafia, Pangani,
Mvomero, Masasi mjini, Lindi vijijini, Kilwa, Mpanda, Nachingwea,
Rufiji, Korogwe, Mkinga, Ulanga, Morogoro vijijini na Chato.
Ndugu wanahabari,
Takwimu
za miaka kumi iliyopita, tangu 2007 hadi 2016, zinaonyesha hapa nchini
mwetu watoto wapatao 1,456 waligunduliwa na kutibiwa ukoma. Ugonjwa wa
Ukoma miongoni mwa watoto ni dalili ya kuwa bado kuna maambikizi mapya
katika baadhi ya maeneo nchini mwetu. Miongoni mwa hawa, watoto 73
waligunduliwa wakiwa tayari wamepata ulemavu wa kudumu; yaani wakiwa
tayari wamekatika baadhi ya viungo vyao na wengine kuhitaji kutumia
viungo bandia na kiasi kikubwa kuwa tegemezi maisha yao yote.
Ndugu wanahabari,
Kauli
mbiu katika maadhimisho ya mwaka huu inasema “TOKOMEZA ULEMAVU MIONGONI
MWA VIJANA WETU”. ‘ZERO DISABILITIES IN GIRLS AND BOYS” Kila mmoja
wetu anahitajika kushiriki kikamilifu kupambana na ukoma, hususani
katika halmashauri ambazo zina wagonjwa wengi na hazijafikia viwango vya
utokomezaji. Juhudi zetu tuzielekeze katika kuwagundua wagonjwa mapema
wakiwa bado wapo katika hatua za awali za ugonjwa, ili kuzuia maabukizi
katika jamii hususan miongoni mwa watoto na vijana wetu kabla ugonjwa
haujawa mkubwa na kusababisha ulemavu.
Ndugu wanahabari,
Dalili
ya awali kabisa za ugonjwa wa Ukoma ni baka au mabaka kwenye ngozi
yasiyo na hisia na yenye rangi ya shaba. Kwa kawaida hayawashi wala
hayaumi. Mabaka haya hukosa hisia ya joto, mguso au maumivu. Dalili
nyingine za ukoma ni pamoja na vijinundu (vijifundo) kwenye ngozi hasa
usoni na masikioni, uvimbe na maumivu kwenye mishipa ya fahamu, ganzi
kwenye mikono na miguu, vidonda au kuungua moto katika mikono na miguu
bila kusikia maumivu yoyote,
Athari za Ukoma
ambazo pia watu hufikiri ni dalili ni pamoja na kukatika vidole vya
mikono na miguu na upofu; athari hizi ni matokeo ya kuchelewa kuanza
matibabu.
Ndugu wanahabari,
Zipo hatua zinazochukuliwa na serikali yetu ya awamu ya tano kudhibiti ukoma nchini. Hatua hizo ni pamoja na:
• Kuendesha
kampeni za uibuaji wa wagonjwa wapya ngazi ya jamii kwa
kuwashirikisha watoa huduma ngazi ya jamii ( Leprosy Elimination
Campaigns) hasa katika wilaya zenye kiwango kikubwa cha wagonjwa wa
Ukoma,
• Utekelezaji
wa mpango wa majaribio wa utoaji wa dawa kinga ngazi ya kaya kwa ajili
ya kuzuia maambukizi ya ukoma (Leprosy Post-Exposure Prophylaxis).
Mpango huu unafanyika katika wilaya za Nanyumbu, Liwale na Kilombero
ambapo umeonesha mafanikio makubwa katika kuzuia kuenea kwa ukoma katika
jamii,
• Utekelezaji
wa maazimio ya Bangkok (the Bangkok Declaration Special Fund (BDSF) kwa
ajili ya kuhamasisha uibuaji wa wagonjwa wa ukoma mapema na kutatua
changamoto wanazokabiliana nazo watu walioathirika na ukoma. Zoezi hili
linatekelezwa kwenye wilaya za Mkinga, Muheza – Tanga na Chato mkoani
Geita,
• Utekelezaji
wa shughuli za kuzuia ulemavu unaotokana na ukoma ikiwemo kutathmini
wagonjwa wenye vidonda, kufanya upasuaji maalumu, huduma za kitaalamu za
macho, utoaji wa viungo bandia pamoja na viatu maalum,
• Kuagiza na kusambaza dawa za kutosha za ugonjwa wa ukoma nchi nzima.
• Kutoa elimu kwa umma kuhusu dalili na tiba ya ukoma.
Ndugu wanahabari,
Pamoja
na hatua zanazochukuliwa na serikali na mafanikio zipo changamoto.
Miongoni mwa changamoto zinazotukabili ni pamoja na jamii kuendelea
kushikilia imani potofu juu ya ukoma kuwa ni ugonjwa wa kurithi au
kulogwa na wagonjwa kuchelewa kujitokeza kupata matibabu hadi wanapopata
ulemavu. Ukoma ni ugonjwa wa kuambukizwa unaosababishwa na vimelea
vinavyoshambulia mishipa ya fahamu na huambukizwa kwa njia ya hewa
pekee.
Nitoe rai kwa
jamii, wazazi na walezi kuwa sote tujenge tabia ya kuchunguza miili yetu
na ya watoto wetu. Endapo utaona mojawapo ya dalili za Ukoma,
unashauriwa kwenda kwenye kituo cha tiba kilicho karibu nawe kwa
uchunguzi bila kuchelewa. Hii itawawezesha wataalam wa afya kuchunguza
na kubainisha kama mgonjwa ana ukoma ili apate tiba sahihi mapema na
hivyo kuzuia maambukizi na ulemavu wa kudumu unaoweza kuzuilika.
Tiba
ya Ukoma inapatikana nchini kote na hutolewa bila malipo kwa wagonjwa
wote. Nirudie tena kuwa, pale tunapoona mabadiliko yoyote yanajitokeza
kwemye miili yetu twende mapema katika vituo vyetu vya huduma
kuchunguzwa ili tupate matibabu stahili.
Ndugu wanahabari,
Aidha,
napenda kuwashukuru wanahabari, watoa huduma katika vituo vya afya kwa
juhudi wanazofanya kila siku kuhakikisha ugonjwa huu si tatizo la
kiafya tena nchini.
Pia
nachukua nafasi hii kwa niaba ya serikali ya awamu ya tano ya Jamuhuri
ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
kuyashukuru mashirika mbalimbali ya ndani na nje kama vile Norvatis
Foundation ya Uswisi, Germany Leprosy and Tuberculosis Relief
Association (GLRA) ya Ujerumani, Nippon Foundation chini ya Sasakawa
Memorial Health Initiative ya Japani na Shirika la Afya Duniani (WHO)
kwa michango yao katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukoma hapa nchini
Tanzania.
“TOKOMEZA UKOMA KUZUIA ULEMAVU MIONGONI MWA VIJANA WETU”.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
0 on: "TAMKO KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA UKOMA DUNIANI TAREHE 28/01/2018"