Na.WAMJWW. KIGOMA
Serikali imeviagiza vyombo vya
usalama na kamati za Afya za vijiji kuimarisha mifumo yote ya udhibiti wa
upotevu wa Dawa nchini, kwa kusimamia na kufuatilia kwa ukaribu hali ya
upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba, ili kuondoa ubadhilifu unaofanywa na
baadhi ya watu wasio waaminifu.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine
Ndugulile (MB) katika ziara yake katika Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma ya
kukagua utoaji huduma za Afya na kufuatilia utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya
jamii ambao unasisitiza ushirikishwaji wa jamii katika maamuzi,
“Niwaombe sana ndugu zangu wananchi
tuwe walinzi, hiyo dawa ingeweza kukusaidia wewe, au ndugu yako, hivyo
kushiriki katika ubadhilifu huo ni kujiumiza mwenyewe” alisema Dkt. Ndugulile.
Katika kupunguza vifo vya kina mama
na watoto Dkt. Faustine amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya, maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewekeza kiasi cha shilingi Milioni 400
katika Halmashauri 175, kikiwemo kituo cha Afya cha Uvinza , fedha
zitakazotumika kuboresha na kujenga vyumba vya kutolea huduma ya dharura wakati
wa kujifungua, nyumba za watumishi pamoja na maabara.
Dkt. Faustine aliendelea kusema
kwamba, Serikali inaendelea kufanya vizuri barani Afrika na Dunia kwa ujumla
kwa upande wa utoaji chanjo, kwani imefikia asilimia 97 ya walengwa wote
wanaohitaji chanjo nchini jambo linalosaidia kutunza Afya za watu katika jamii.
Dkt. Ndugulile aliongeza kuwa
anatambua uhaba wa watumishi unaovikabili vituo vingi vya Afya katika Wilaya ya
Uvinza ambao umefikia asilimia 66 na kuahidi kulifanyia kazi ombi hilo ili
kupunguza changamoto katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande mwingine Dkt. Ndugulile
ameendelea kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli kwa kuongeza Bajeti ya dawa , kutoka Bilioni 30 mpaka Bilioni
270 wa mwaka huu wa fedha hali iliyosaidia kuimarisha mapambano dhidi ya
maradhi mbali mbali.
Aidha, Dkt. Ndugulile aliwapongeza
wananchi wa kata ya Kazuramimba kwa kuonesha kwa vitendo utayari wao wa
kusukuma guruduma la maendeleo ya elimu katika Kijiji hicho kwa kuamua kujenga
madarasa ya shule katika Kijiji cha Nyanganga kilicha kata ya Kazuramimba ili
kuweza kuwakomboa watoto wao na janga la ujinga na umasikini.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Bi
Mwanamvua Mlindoko ameeleza faida ya mradi wa ujenzi wa madarasa ikiwemo
ongezeko la ufaulu kutoka wanafunzi 4115 mwaka 2017 huku waliochaguliwa
kujiunga na kidato cha kwanza ni wanafunzi 1641 ambao ni sawa na asilimia 36
tu, hivyo kutokana na ujenzi wa madarasa haya utasaidia wanafunzi 2482 sawa na
asilimia 64 kuendelea na elimu.
|
0 on: "DKT. FAUSTINE AVIAGIZA VYOMBO VYA USALAMA MKOANI KIGOMA KUIMARISHA MIFUMO YA UDHIBITI WA UPOTEVU WA DAWA."