Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (aliye mbele) akizindua rasmi maabara ya uchunguzi na tiba ya magonjwa ya moyo (Cathlab) katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma walio kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula pamoja na Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt. Alphonce chandika.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akielekezwa namna magonjwa ya moyo yanavyochunguzwa katika maabara ya uchunguzi na tiba ya moyo Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma
Picha ya pamoja Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na wataalam wa uchunguzi na tiba ya magonjwa ya moyo kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Dsm.
Mashine ya uchunguzi na tiba ya moyo (Cathlab) katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Zainab Chaula akisisitiza jambo kwenye halfa ya uzinduzi wa Maabara ya uchunguzi na tiba ya magonjwa ya Moyo.
Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt. Alphonce Chandika akisisitiza jambo kwenye halfa ya uzinduzi wa Maabara ya uchunguzi na tiba ya magonjwa ya Moyo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisisitiza jambo kwenye halfa ya uzinduzi wa Maabara ya uchunguzi na tiba ya magonjwa ya Moyo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisalimiana na wananchi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma alipoenda kuzindua Maabara ya Uchunguzi na Tiba ya Magonjwa ya Moyo (Cathlab)
Na WAMJW – Dodoma.
Katika azma ya kuboresha huduma
za kibingwa za matibabu, Serikali kupitia Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini
Dodoma imeanzisha huduma za matibabu ya moyo kwenye maabara ya uchunguzi na
tiba ya magonjwa ya moyo kwa kutumia mashine maalum (Cathlab).
Maabara hiyo ya tatu nchini na
ya pili kwenye taasisi ya serikali inatarajiwa kutoa huduma za uchunguzi na
tiba ya magonjwa ya moyo ndani ya muda mfupi hivyo kuhudumia wagonjwa wengi
ndani ya muda mfupi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi
wa maabara hiyo, mgeni rasmi Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa kufunguliwa kwa
maabara hiyo ni mafanikio makubwa kwa serikali katika kusogeza huduma za
kibingwa karibu na wananchi hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa waliokuwa
wakisafiri kwenda mbali kufuata huduma za matibabu.
“Huduma za kibingwa zimepunguza
idadi ya wagonjwa waliokuwa wanasafiri au kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya
matibabu kwa asilimia 95 kutokana na uboreshaji wa huduma za afya ndani ya
nchi” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy Mwalimu amesema
kuwa Serikali imekuwa ikiwajengea uwezo wataalam wa afya nchini ili waweze
kutoa huduma bora kwa wananchi jambo ambalo limezaa matunda kwa kuwa wagonjwa
wengi hivi sasa wanapata matibabu ndani ya nchi.
Hata hivyo Waziri Ummy ametoa
ufafanuzi wa upatikanaji wa rufaa ya matibabu nje ya nchi na kusema kuwa
Serikali haijazuia rufaa za matibabu nje ya nchi bali ni lazima kujiridhisha
kwanza huduma za matibabu hazipatikani hapa nchini kabla ya kutoa rufaa.
“Hakuna daktari tuliyemkataza
kutoa rufaa nje ya nchi, sasa hivi tuna uwezo wa kutoa huduma za matibabu ya
kibingwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni lazima daktari awe
amejiridhisha na kuthibitisha kwamba matibabu hayo hayapatikani hapa nchini
kabla ya kutoa rufaa” alisema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy ameupongeza uongozi
wa Hospitali ya Benjamin Mkapa na Taasisi ya Jakaya Kikwete kwa kuwa wabunifu
na kushirikiana kutoa huduma bora za matibabu ya moyo kwa wananchi na kuzitaka
hospitali na taasisi nyingine za afya kuiga mfano wao katika kuboresha huduma za
afya nchini.
Katika hatua nyingine Waziri
Ummy amewataka wananchi kujiunga na Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya ili waweze
kupata bima ya afya ambayo itawasaidia kupata huduma za matibabu kwa uhakika.
Waziri Ummy amesema kuwa ni muhimu kwa watanzania kuwa na bima ya afya ambayo
itawapunguzia gharama za matibabu huku akiwataka wananchi kujiwekea malengo na
kukata bima ya afya ambayo gharama zake ni nafuu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu
Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa ipo haja ya kuwathamini
madaktari wazalendo ambao wamekuwa wakijitoa kuokoa maisha ya wagonjwa. Dkt
Chaula amesema kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika wataalam wa afya nchini
ili kuweza kuwa na madaktari bingwa wengi wanaotoa huduma za kibingwa hapa hapa
nchini pamoja na kuwekeza kwenye miundombinu na vifaa.
Awali akitoa salamu zake,
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Mohammed Bakari Kambi, ametoa rai kwa wananchi
kuzingatia mtindo bora wa maisha, kufanya mazoezi na kula chakula bora ili
kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo kisukari, presha na
shinikizo la damu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt. Alphonce Chandika amesema kuwa maabara hiyo
imegharimu kiasi cha Tsh Bilioni 5 na inatarajiwa kutoa huduma za uchunguzi na
matibabu ya magonjwa ya moyo hivyo kupunguza adha ya wagonjwa kusafiri umbali
mrefu kufuata huduma za matibabu ambapo awali zilikuwa zikipatikana Dar Es
Salaam kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete pamoja na Hospitali nyingine
moja isiyo ya kiserikali.
Dkt. Chandika amesema kuwa
wataendelea kushirikiana na wataalam kutoka Taasisi ya Moyo ya jakaya Kikwete
ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi huku akiiomba serikali kuongeza
wataalam ili kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma za afya.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi amesema
kuwa hadi kufikia jioni jumla ya wagonjwa 13 kutoka Dodoma na mikoa ya jirani
tayari walishakuwa wamefanyiwa uchunguzi katika maabara hiyo ambapo kati
yao wagonjwa wanne wakitakiwa kwenda JKCI kwa uchunguzi na tiba zaidi.
Aidha Prof. Janabi alitumia
nafasi hiyo kuishukuru Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kuwapa nafasi na heshima
kubwa ya kuja kushirikiana katika kutoa huduma za matibabu kwa wananchi.
Mwisho
0 on: "SERIKALI YAANZISHA HUDUMA ZA KIBINGWA MATIBABU YA MOYO DODOMA."