Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula akisema jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wataalam wa udhibiti ubora wa Mamlaka ya Chakula na Dawa TFDA na Wakala wa Chakula, Dawa na vipodozi Zanzibar (ZDFA) Jijini Dar Es Salaam.
Picha ya Pamoja wajumbe wakiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula (aliyeketi wa tatu kulia)
Na WAMJW- Dar es Salaam
TANZANIA yatajwa miongoni mwa nchi 50 kati ya 194 duniani zenye mifumo imara na madhubuti ya udhibiti wa ubora wa bidhaa za vyakula, dawa na vipodozi.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Zainab Chaula leo wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tano kwa wataalam wa udhibiti ubora wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi (ZDFA) na wenzao kutoka nchi ya Malawi.
Mafunzo hayo maalum yameandaliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO-Tanzania) kwa lengo la kuwaongezea mbinu mbalimbali zitakazowasaidia kuimarisha nchi hizo kuongeza nguvu ya udhibiti wa bidhaa hizo.
“WHO imetutambua na imetupa level (daraja) la tatu, hii ni hatua nzuri, TFDA imefanya kazi kubwa, hii inamaanisha mifumo ya udhibiti tanzania inatambulika duniani kote na kwamba misingi ya udhibiti ya mamlaka yetu imefikia ngazi ya kimataifa". Amesema Dkt. Chaula na kuongeza “Lakini pamoja na hatua hiyo lazima iendelee kujiimarisha ili ikiwezekana tupande daraja tufikie level 4 ambayo ndiyo kiwango cha juu zaidi".
“Ili tuweze kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi, mamlaka yetu inapaswa kutengeneza mifumo ya ufuatiliaji ubora na usalama wa bidhaa kuanzia viwandani hadi kwa mtumiaji, ili kuhakikisha hakuna dawa bandia zinaingia nchini mwetu”.
Akiwasilisha mada Dkt. Alireza Khadem Broojerdi kutoka WHO amesema ili kuongeza nguvu ya udhibiti nchi zinapaswa kushirikiana kwa ukaribu.
“Tunayo malengo 17 ya kidunia (SDGs), lengo namba tatu linasisitiza juu ya afya bora kwa wote, tunayo pia malengo ya mwaka 2019- 2030, mpaka sasa nchi 50 ikiwamo Tanzania sawa na asilimia 26 zimefikia daraja la tatu na nne. Nchi 45 sawa na asilimia 23 zipo daraja la pili, nchi 96 zimefikia daraja la kwanza na zingine zilizobaki bado hazijafikia viwango hivyo,” amesema Dkt. Khademu.
Awali akizungumza Kaimu Mkurugenzi wa TFDA, Dkt. Candida Shirima amesema kupitia semina hiyo iliyoandaliwa na WHO watajifunza mbinu mbalimbali zitakazowasaidia kuweza kufikia malengo waliyojiwekea katika kuendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti wa bidhaa hizo.
0 on: "TANZANIA NI MIONGONI MWA NCHI 50 ZENYE MIFUMO IMARA YA UDHIBITI UBORA BIDHAA ZA VYAKULA NA DAWA"