Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile akikagua idadi ya Wananchi waliofika kupata huduma
wakati alipofanya ziara katika Mpango wa Taifa wa Damu salama jijini Dar
es salaam.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile akikagua jokofu la kuhifadhia sampuli ya Damu pindi
alipofanya ziara katika Mpango wa Taifa wa Damu salama jijini Dar es
salaam.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile akipata maelezo kutoka kwa Afisa wa Mpango wa Taifa
wa Damu salama, wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma
na kuangalia mashine mpya za kielektroniki za kupima sampuli ya Damu.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile akipata maelezo kutoka kwa Mtaalamu wa Mashine yakupima Sampuli za Damu, Mpango wa Taifa
wa Damu salama, wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma
na kuangalia mashine mpya za kielektroniki za kupima sampuli ya Damu.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile akisisitiza jambo wakati akiongea na Watumishi wa
Mpango wa Taifa wa Damu salama, alipofanya ziara ya kukagua hali ya
utoaji huduma na kuangalia mashine mpya za kielektroniki za kupima
sampuli ya Damu katika taasisi hiyo.
Meneja Mpango wa Taifa wa Damu salama Dkt. Magdalena Lyimo, akisikiliza
maelekezo kutoka kwa Naibu Waziri wa Afya Dkt.Faustine Ndugulile (hayupo
kwenye picha) wakati wa ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma na
kuangalia mashine mpya za kielektroniki za kupima sampuli ya Damu.
Picha ya pamoja ikiongozwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile baada ya kumaliza ziara
ya kukagua hali ya utoaji huduma na kuangalia mashine mpya za
kielektroniki za kupima sampuli ya Damu.
SERIKALI YAZITAKA HOSPITALI BINAFSI KUCHANGIA GHARAMA ZA DAMU
Na WAMJW - DSM
Mpango
wa Taifa wa Damu salama imetakiwa kuhakikisha Hospitali Binafsi zote
zinaanza kuchangia gharama za huduma za afya ili kupata mgao wa damu.
Hayo
yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati alipofanya ziara ya
kukagua mashine za kupima sampuli za damu na utendaji kazi wa Mpango wa
Taifa wa Damu salama.
Katika
ziara hiyo Dkt. Ndugulile amesema kuwa ni lazima Mpango huyo uhakikishe
unajiendesha wenyewe na kuhakikisha unapunguza gharama za utegemezi kwa
Wafadhili na Serikali katika kutimiza majukumu yake.
"Ni
lazima kupunguza gharama za utegemezi kwa Wafadhili na Serikali kwa
kuanzisha mfumo wa uchangiaji gharama za huduma za Afya wakati Sera
inaelekea kukamilika, Mpango unapendekeza kurudisha gharama kutoka
Hospitali binafsi kupitia njia ya Bima" Alisema Dkt. Ndugulile
Dkt.
Ndugulile alisema kuwa Idadi kubwa ya wanaokuja kuchukua Damu katika
Taasisi hiyo ni Hospitali Binafsi ukilinganisha na Hospitali za Umma,
ambapo mfumo wake ni wakutoza huduma kwa Wananchi (Biashara)
"Wanaokuja
kuchukua Damu nyingi hapa, wengi ni Hospitali Binafsi, kuliko hata za
kwetu za umma, Damu nyingi tunawapa, lakini hawa tukiwapa Damu hizi, wao
wanaenda wanatoza pesa, kwahiyo sisi tunawatengenezea bidhaa bure
halafu wao wanaenda kutoza pesa, hata senti tano sisi hatupati, sio
sahihi" alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha,
Dkt. Ndugulile amewaagiza viongozi wa Mpango wa Taifa wa Damu salama
kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili kuangalia ni namna
gani Damu iwe ni moja ya vitu vitakavyo gharamiwa na Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya.
"Muwahusishe
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, kuangalia jinsi gani damu itakuwa
inagharamiwa na Bima ya Afya, mtuletee mapendekezo na sisi tutafanya
maamuzi" Alisema Dkt. Ndugulile.
Mbali
na hayo Dkt. Ndugulile ameagiza kufanya maboresho ya mfumo wa Takwimu
kuanzia kwenye ukusanyaji wa mapato mpaka hatua ambayo mgonjwa anapata
damu hiyo jambo litakalosaidia kuboresha huduma kwa wananchi.
Kwa
upande mwingine Dkt. Ndugulile ameagiza kuweka mikakati ya kuhakikisha
wanawabakishia wachangiaji Damu ambao wanakuja kuchangia, hii inatokana
na takwimu kuonesha Wachangiaji wa Damu wa hiari wanapungua kutoka 67%
mpaka 63% mwaka 2017-2018.
"Taarifa
yenu ya Mwaka 2017-2018 inaonesha kwamba, wachangiaji Damu wa hiari
wanapungua kutoka 67% mpaka 63% , maana yake bado kuna changamoto, na
kuna kazi tunatakiwa kufanya ikiwemo kuweka mikakati ya kuhakikisha
kwamba tunaowapata Mara ya kwanza kuendelea kuwa nao" Alisema Dkt.
Ndugulile
Naye Meneja
Mpango wa Taifa wa Damu salama Dkt. Magdalena Lyimo amesema kuwa Mpango
una mkakati wa kuboresha mfumo wa ukusanyaji taarifa na Takwimu za
kielektroniki unaunganishwa nchi nzima ili kuleta tija na ubora wa
huduma za damu salama nchini.
Kwa
upande mwingine Dkt. Lyimo amesema kuwa Mpango umefanikiwa katika
kipindi cha Mwaka 2018 kwa kushirikiana na timu za Mikoa na Halmashauri
ulikusanya jumla ya chupa 307,835 ambayo ni sawa na Chupa 6 kwa kila
watu 1000, huku Shirika la Afya Duniani linapendekeza kukusanya chupa 10
kwa kila watu 1000, makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la chupa 73,882
sawa na 32% ikilinganishwa na Takwimu za 2017.
Dkt.
Magdalena Lyimo aliendelea kusema kuwa kwa Mwaka 2018, Wastani wa chupa
25,653 zilikusanywa kila mwezi na damu zote zilipimwa magonjwa ya
HIV,Kaswende pamoja na makundi ya damu, huku matarajio ni kuongeza damu
hadi kufikia chupa 375,000 kwa Mwaka 2019.
Mwisho.
0 on: "SERIKALI YAZITAKA HOSPITALI BINAFSI KUCHANGIA GHARAMA ZA DAMU"